KIKOSI CHA KISASI

SURA YA NANE

MAUAJI YA KISHENZI

Ilikuwa yapata saa kumi na mbili asubuhi, Willy alipoegesha gari lake katika maegesho ya Hoteli Memring.

"Tutaonana baadaye", Mwadi alimwambia Willy huku wakitelemka toka kwenye gari.

"Asante sana, nitatoka asubuhi hii kwenda ofisini kwa akina Tete kwa mazungumzo ya kibiashara nikirudi toka huko ndipo nitakueleza kama nitakuwa na shughuli au vipi. Kama sitakuwa na shughuli mchana nitakuja nyumbani, lakini yote hayo nitakueleza tutakapoonana mchana," Willy alieleza.

"Vizuri, mimi nitasubiri unieleze mchana," Mwadi alijibu kisha akainama akampiga busu motomoto Willy.

"Asante," Willy alishukuru, Mwadi aliondoka kwenye maegesho na kuelekea hotelini kuanza kazi yake. Willy alingojea mpaka Mwadi alipokuwa ameingia ndani ya hoteli maana hakutana watu wote wajue kuwa alikuwa amekuja na Mwadi. Ndipo akatelemka na kufunga milango ya gari na kuelekea zake hotelini. Kwa sababu alikuwa ameondoka na funguo za chumba chake, alipanda moja kwa moja mpaka chumbani kwake, Kwa sababu hawakuwa wamepata usingizi wa kutosha aliamua ajilaze kidogo hadi saa mbili hivi ambapo angeweza kwenda kwenye ofisi za 'Agence Sozidime'. Kutokana na mafikira ya Robert kuhusu Kampuni ambayo ni wakala wa Kampuni ya Afrika Kusini, Willy alikuwa ameamua kuwa lazima akaonane na watu wa kampuni hii aweze kuwapima yeye mwenyewe. Kufahamiana na Tete usiku uliokuwa umepita Willy alichukulia kama bahati kubwa kwa upande wake. "Siku zote mimi husema bila bahati huwezi kufanikiwa katika shughuli za upelelezi," Willy alijisemea moyoni na kujilaza tayari kuvuta usingizi kwa muda mfupi.

Willy aliamshwa na kengele ya simu iliyokuwa ikilia. Aliamka na kuangalia saa yake akaona ilikuwa imetimia saa moja unusu. Aliiendea simu, akaiinua, "Hallo," aliita.

"Hapa mapokezi kuna simu yako kutoka nje," 

"Asante," alijibu huku akingojea opereta amuunganishe na nje.

"Hallo," simu iliita.

"Haloo, nani mwenzangu," Willy aliuliza.

"Robert hapa, habari za asubuhi?"

"Safi yahhe, salama wewe?"

"Mimi salama, lakini naamini wewe salama zaidi", Robert alisema kwa sauti ya utani.

"Hujakosa bado, mimi salama zaidi", Willy alijibu.

"Wote tuko hapa tafadhali fika upesi iwezekanavyo kuna habari muhimu sana," Robert alimwambia. Kutokana na usemi huu Willy alitambua kuna mambo muhimu.

"Nakuja sasa hivi", alijibu Willy na kukata simu.

Willy aliondoka na kwenda maliwatoni kujimwagia maji. Alipokuwa amemaliza kuoga, alitafuta suti yake moja iliyokuwa inampendeza sana akaiweka tayari kwa kuivaa, maana alitaka aonekane nadhifu iwezekanavyo tayari kwa mazungumzo ya kibiashara na meneja wa 'Agence Sozidime'. Ghafla alikumbuka kitu akainua simu na kuzungumza na mapokezi. Nipe STK ofisi zao zilizoko kiwanja cha ndege," alimweleza opereta.

"Subiri," opereta alijibu. Aliweka simu chini akaendelea kuvaa. Baada ya muda kidogo simu ililia. "Hallo", Willy aliita.

"Zungumza na STK," opereta alijibu.

"Hallo naomba zungumza na Ntumba," alijibiwa.

"Hallo Willy hapa, sijui bado unanikumbuka?"

"Aah Mzambia we, uko wapi toka juzi? umemezwa kabisa na mji huu, mwanaume wewe!" Ntumba alilalamika.

"Nipo tu nilikuwa bado najiweka sawa," alijibu Willy. 

"Wacha uongo wako mimi najua kuna maguberi chungu mzima hapa Kinshasa ndiyo yatakuwa yamekuweka sawa."

"Ya nini nitafute maguberi na watoto wabichi kama wewe wapo mjini hapa?".

"Utajua wewe, nasikia maguberi yana fedha hivi yanawahonga vijana kama wewe." Wote wawili walicheka kisha Ntumba akaendelea.

"Ulikuwa unasemaje mwanaume wewe?"

"Nakuomba unieleze kitu fulani lakini kiwe siri yako, unasemaje?"

"Uliza tu toka juzi nimekwambia hata ukitaka kukaa nyumbani kwangu itakuwa siri yangu," Ntumba alijibu kwa kejeli.

"Jana mchana kuna gari lenu lilipatwa na ajali barabara ya Poids Lourds, unaweza kuniambia nani alikuwa amelikodi?"

Ntumba alikuwa amezoea kuulizwa maswali ya ajabu ajabu kama haya mara kwa mara. Kwa vile alikuwa ameisha mwahidi kijana huyu alijibu. "Gari hili lilikuwa limekodiwa na kijana mmoja wa Kizungu aitwaye Charles, aliacha anwani yake na tulikuwa na nambari ya leseni yake ya kuendeshea. Kitu cha ajabu ni kwamba anwani aliyotuachia na leseni vyote ni vitu vya bandia hivi tunahisi hata jina lake ni la uongo. Je una zaidi?"

Willy alipata zaidi kuliko alivyotegemea hivi alijibu.

"Sina zaidi, asante sana."

"Umefikia hoteli gani?" Ntumba aliuliza.

"Hoteli Memling".

"Mbona husemi karibu? Basi mimi nakukaribisha nyumbani kwangu."

"Asante sana. Mimi nina simu ya nyumbani kwako nitakupigia simu".

"Lini?" Aliuliza Ntumba.

"Kesho, maana leo nitakwenda Brazzavile na kurudi kesho asubuhi." Willy aliongopa.

"Haya, asubuhi nitasubiri simu yako, mimi natoka kazini saa kumi mchana".

"Vizuri, tegemea simu yangu kesho jioni. Kwa heri."

"Asante kwa heri," Walikata simu. Willy alimaliza kuvaa, akajiangalia kwenye kioo kuna kama alikuwa amejiweka katika sura ya mfanyabiashara aliyeendelea. Kusema kweli alionekana mfanyabishara wa hali ya juu kabisa kutokana na alivyoonekana. Alichukua bastola yake akaiweka ndani ya koti lake na kutelemka chini.

Ilikuwa saa mbili na nusu Willy alipofika nyumbani kwa Robert. Aliwakuta wote watatu wako mezani wanapata kifungua kinywa. "Karibu karibu", Robert alimkaribisha.

"Vipi unaenda kuoa au una miadi kwa mara ya kwanza na msichana?" Kofi aliuliza huku wote wakicheka. 

"Kwa nini?" Aliuliza Willy.

"Umevalia vizuri sana", alidakia Ozu.

"Ninaenda kwenye miadi ya kikazi," alijibu Willy huku akivuta kiti kwenye meza ili na yeye aweze kupata chochote kwani hakuwa amechukua kule hotelini. Walisalimiana huku wakiendelea na chakula. Willy alipowaangalia vizuri alitambua kuwa Ozu na Kofi walikuwa hawakupata usingizi wa kutosha na vile vile nguo zao zilikuwa zile zile za jana yake na zimechafuka, kitu kilichomuonyesha kuwa walikuwa bado hawajafika mahotelini kwao tokea jana yake.

"Ehe, leteni habari," Willy alisema.

"Nafikiri Ozu ataeleza vizuri zaidi," alisema Kofi baada ya kutazamana na Ozu nani aeleze.

"Oke mimi nitaeleza," alijibu Ozu. Ozu alimweleza Willy mambo yote tokea walipokuwa wameachana mpaka muda ule wa asubuhi. Kisha alimalizia . "Asubuhi tulipoamka tulionelea tuonane kwanza ili tuweze kuelezana tukio hili kabla hatujaendelea na mambo mengine. Kwa hivyo tulikata shauri tuje hapa ambapo tungeweza kukutana kwa urahisi". Willy aliyekuwa anasikiliza maelezo haya kwa makini alivuta pumzi ndefu na kusema. "Kazi mliyoifanya inastahili pongezi. Sasa nina imani kazi hii itafanikiwa."

"Unaona mambo yanavyokuja yenyewe Willy. Ni jana tu ulipouliza maswali mengi juu ya Papadimitriou, na sasa amejifunua mwenyewe," Robert alisema.

"Mimi nilipatwa na mashaka jinsi gari ya marehemu ilivyoweza kuwa imetegwa bomu. Sasa imedhihirisha waziwazi kuwa Papadimitriou alijua gari hilo litatumiwa na nani, kwa hivi wakalitega gari moja kwa moja kabla halijatoka gereji. Hii inaonyesha kuwa kuna mtu katika Wizara ya mambo ya nchi za nje ambaye anashirikiana na watu hawa, hivi Robert jaribu tena kutumia uhusiano wako ulio nao na CND uweze kujua ni nani hasa alishughulika na kupanga hili gari kuwa linatumiwa na marehemu. Tukishampata mtu huyu tutakuwa tumeunganisha mambo haya."

"Hata mimi nilikuwa na mawazo hayo hayo," alijibu Robert. Kisha Willy naye aliwaeleza maelezo yote aliyokuwa amepata kutoka kwa Mwadi juu ya Kabeya vile vile aliwaelezea kukutana kwake na Tete na juu ya 'Agence Sozidime'.

"Kutokana na maelezo Robert aliyokuwa ameeleza juu ya Wakala wa Makampuni ya Afrika Kusini, mimi nimeonelea nizitembelee hizi ofisi za Sozidime huenda nikabahatisha mambo fulani fulani," Willy alimalizia.

"Lo naona Mungu amekuwa upande wetu usiku wa jana maana sasa naweza kuona mwanga wa mambo haya yalivyo. Kitu kimoja kinachoonekana waziwazi ni haya magereji. Inaonekana majambazi haya yanatumia magereji kama makambi yao kutunzia na kuimarisha ujambazi wao. Mimi nitaenda kupeleleza nani mwenye hii G.A.D. gereji halafu ndipo tutaangalia habari za gereji hii zaidi," Robert alishauri.

"Mimi sidhani hawa watu ni majambazi wa kawaida. Nina imani hiki ni kikundi maalumu ambacho kimewekwa hapa kwa nia fulani ya kisiasa na ndiyo sababu wamemuua Ndugu Mongo pamoja na wanamapinduzi wengine waliokwisha uawa hapa mjini. Hivi hatuna budi kuliangalia kuliangalia suala hili katika mfumo wa namna hiyo," alisema Kofi. 

"Sawa kabisa, na hayo ndiyo mawazo ya kamati ya Ukombozi ya OAU. Je huyu Papadimitriou wewe ulimkadiria vipi?" Willy alimuuliza Kofi.

"Macho yetu yalipogongana moja kwa moja tulitambuana kitu kimoja, wote tulikuwa watu ndani ya mchezo mmoja. Huyu mtu ni hakika kabisa ni jasusina jasusi wa hali ya juu. Kitu hiki kinaonekana waziwazi katika macho yake... nadhani mnaweza kutambuana," Kofi alieleza huku wenzake wakitingisha vichwa kuonyesha kuwa wameelewa.

"Robert itabidi upeleke maelezo yote haya Lusaka. Halafu uwaambie wajaribu kutafuta habari za huyu Papadimitriou kama anaweza kuwa jasusi wa kundi gani na watuletee habari haraka sana. Nafikri itakuwa rahisi hasa kwa vile mtu huyu amewahi kukaa Lusaka." Willy alimshauri Robert.

"Sawa nitafanya hivyo," Robert alijibu.

"Sisi tutarudi mahotelini kwetu tukapumzike kidogo na kubadilisha mavazi," Ozu alisema.

"Jiangalieni sana maana inavyoonekana watu hawa wana mbinu nyingi sana. Huyu Kabeya ana uhusiano na Mahoteli karibu yote makubwa kama nilivyokwisha kuwaeleza, hivyo msipuuze kitu chochote dakika yoyote," Willy aliwashauri.

"Tuonane tena hapa wote mchana kiasi cha saa saba ili tuelezane maendeleo ya asubuhi hii, maana kama Robert kama Robert ataweza kupata hizo habari nafikiri litakuwa jambo la maana sana. Sasa mimi naondoka lakini tutaonane wakati huo," Willy alisema huku akisimama. Aliangalia saa yake ilikuwa tayari saa tatu.

"Oke, saa saba tutaonana." Walijibu wenzake,  yeye Willy akaondoka.

ITAENDELEA 0784296253

Comments

  1. safi sana mkuu kwa muendelezo wa tamthilia hii, nimeanza kuifwatlia rasmi usiikawize sana mkuu

    ReplyDelete
  2. This comment has been removed by the author.

    ReplyDelete

Post a Comment

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru