KIKOSI CHA KISASI

SURA YA NANE

MAUAJI YA KISHENZI

IV

Ilikuwa saa sita kamili Willy alipofika hotelini kwake na alimkuta Mwadi yuko kazini. "Habari za saa hizi?" Willy alimgutusha Mwadi aliyekuwa ameinama huku anaandika.

"Oh Willy mpenzi, habari zangu ni nzuri tu. Vipi shughuli zako?"

"Shughuli zangu zimeenda vizuri sana, nafikiri mambo yangu yatafanikiwa haraka zaidi kuliko nilivyotegemea", alijibu Willy. "Ehe nipe mipango, ningetaka kuonana na Tete jioni ili aweze kunielewesha vitu fulani fulani, kwa hivyo nitakupitia jioni tukamwone halafu ndipo tutaendelea na mambo mengine baada ya hapo."

"Tete amenipigia simu, akiuliza tuna mipango gani jioni. Mimi nimemjibu kuwa mpaka tuonane ndipo nitamjibu. Sasa mimi nitamwambia kuwa tutaenda kwake jioni atusubiri. Sawa?" Mwadi aliuliza.

"Sawa kabisa, kwani yeye anakaa wapi?" Willy aliuliza.

"Anaishi huko Ndolo, unakujua ndolo?"

"Ndiyo".

"Basi ana nyumba moja nzuri sana huko, barabara ya Kibinda nyumba nambari 16, nyumba yake inatazamana na kiwanja cha ndege cha Ndolo", alisema Mwadi kwa utulivu.

"Nyumba hiyo amepanga ama ni mali yake?", Willy aliuliza.

"Ni mali yake. Watu wengi wanasema nyumba hii alinunuliwa na rafiki yake Muteba. Kama ulivyomwona msichana mwenyewe hata wewe kama angekwambia umnunulie nyumba naamini ungefanya hivyo", Mwadi alimtania.

"Wacha mambo yako", Willy alijibu huku anaangalia saa yake. 


"Twende tukapate chakula cha mchana".

"Nenda tu mimi niko kazini mpaka baadaye." Mwadi alijibu.

"Nisubiri nyumbani nitakupitia kiasi cha saa kumi na mbili au saa moja jioni".

"Usiwe na shaka mimi nitakuwepo nikikusubiri kwa hamu sana," Mwadi alijibu.

"Willy alielekea kwenye chumba cha chakula, huku nyuma Mwadi akiwa anamwangalia hadi alipopotea. "Nitahakikisha kijana huyu anaondoka na mimi," alijisemea Mwadi. Baada ya chakula Willy aliondoka na kuelekea nyumbani kwa Robert, ili kuwahi miadi yao waliyokuwa wameipanga hapo awali. 


"Nilipoingia chumbani kwangu nilikuta chumba kimepekuliwa vibaya sana lakini kwa ujuzi wa hali ya juu kiasi kwamba mtu wa kawaida hawezi kujua kimepekuliwa. Hii inazidi kuthibitisha kuwa watu hawa si wa kawaida ila nao ni watu wenye ujuzi," alieleza Willy alipofika.

"Mimi nilikuwa ninayo mawazo kuwa, jioni ingebidi tukaangalie hii gereji iitwayo G.A.D. ili tuhakikishe kama kuna huhusiano kati yake ya Garage Papadimitriou?" Kofi alishauri.

"Hili lipo nilikuwa bado nakuja kulizungumzia. Mpango wa leo utakuwa kama ifuatavyo. Sasa hivi itabidi tupumzike mpaka jioni kwani usiku wa leo ndipo kazi itafanyika. Saa kumi na mbili jioni mimi nitaondoka kwenda kumwona Tete, maana nina miadi na Mwadi ili aweze kunipeleka huko.
      
"Shughuli zangu itabidi nizifanye katika muda wa masaa matatu ili kiasi cha saa tatu usiku niwe nimerudi hapa tayari kwa shughuli za usiku. Kama Kofi alivyosema itabidi tuitembelee Garage 'G.A.D'. Kwa hivyo sasa hivi tutapumzika kusudi tujiweke katika hali nzuri ya kuweza kukabili mambo yoyote yatakayotokea usiku". Willy aliwaeleza.

"Jambo la maana kabisa sababu usiku wa jana hatukupumzika vizuri," alijibu Ozu. Wote walikubaliana na maelezo ya Willy na kuondoka kuelekea kwenye vyumba vya kupumzika ndani ya hii nyumba ya Robert ambayo ilikuwa nyumba kubwa sana.

Wakati Willy na wenzake wakiendelea na mazungumzo. Pierre na wenzake nao walikuwa wamekusanyika ofisini kwake wakiwa na mazungumzo vile vile.

"Wale watu ni watu wenye ujuzi wa hali ya juu sana. Jinsi walivyotukwepa na kutufanya tusiwaone ni kwa namna ya ujuzi wa pekee Patron, mimi nimeridhika kabisa kuwa watu hawa kama alivyosema Papa wana ujuzi sawa sawa na sisi huenda hata na kuzidi. Hivi itabidi sasa tutumie mbinu zetu zote tukitaka kuwafutilia mbali," alikiri Muteba. Jean naye alieleza maelezo kama haya haya naye vile vile akakiri kuwa watu waliokuwa wanapambana nao hawakuwa mchezo. 


Pierre aliwasikiliza kwa utulivu sana kisha akasema; "Kwa taarifa yenu kuna mtu mwingine ambaye anaweza kuwa mmoja wa watu hawa kwa vile sababu zilizomleta ni sawa sawa na za hawa watu wawili. Yeye naye alifika mjini hapa juzi Jumatatu akitokea Lusaka akiwa katika mapumziko ya kikazi. Mtu huyu anasema yeye ni mwakilishi wa kampuni moja ya wakala ya Zambia iitwayo 'Zambia Oversea Agency'. Mtu huyu leo alikwenda kwenye ofisi za Sozidime akaonana na Max wakazungumza mambo ya kibiashara. Mtu huyu anasemekana alionana jana usiku na Tete huko Parafifi Bar, na kupeana miadi ya kufika ofisini kwao kwa mazungumzo ya kibiashara na wakuu wake, kitu ambacho ametimiza.

Muteba ambaye moyo wake ulikuwa ukipiga haraka haraka kwa kusikia jina la Tete linatajwa katika habari hii aliinua macho yake ambayo yalionana sawa sawa na Pierre, ikabidi Pierre amuulize, "Unasemaje Muteba?"

"Hizi habari umezipataje?" Muteba aliuliza.

"Kama unavyojua wakala wanafanya kazi zao kwa makini sana. Wao toka nimewapasha habari juu ya matukio ya jana mchana na usiku wako macho. Waliposkia kuwa kuna mtu wa namna hii anakuja kuwaona walitia mashaka. Na mashaka yao yalizidishwa baada ya kumwona mtu huyu, mtu huyu wanahisi lazima awe mpelelezi tu kutokana na alivyo. Hivyo walinasa mazungumzo yake kwenye utepe uliokuwa umefichwa ofisini mwa Max. Mazungumzo yote nimeyasikia kwani wamenieleza. Kwa kujibu suala lako Muteba hivi ndivyo nilipata habari hizi. Mtu huyu anajiita Willy Chitalu. Mkurugenzi amepeleka habari hizi BOSS waweze kuchunguza na kutujibu kama wanaweza kuwa na habari za mtu huyu akiwa kama ni mpelelezi. Wakati huo huo huenda itakuwa rahisi kwako Muteba kuweza kupata habari kamili za mtu huyu kutoka kwa rafiki yako Tete ambaye ndiye amemfahamisha mtu huyu huko Sozidime."

Muteba alijawa na wasiwasi kwani kujiingiza kwa Tete katika suala hili ingeweza kuwa hatari kwake, kwa kutaka kumtetea alijibu, "Mimi nina imani Tete alifanya hivi kikazi bila kujua jambo lolote kwani yeye hajui shughuli za kisiri za Sozidime. Kwa hivi alimjulisha mtu huyu kikazi kabisa. Lakini hata hivyo nitazungumza niweze kujua alimfahamufahamuje mtu huyu kiasi cha kuwekeana miadi,"

"Hata mimi naamini kuwa Tete hakumjulisha kwa nia mbaya, bali chunguza tu na ikibidi jaribu kumshawishi akujulishe kwa mtu huyu. Kazi hii jaribu kuishughulikia leo hii maana kama kweli na huyu vile vile ni mmoja wao inabidi tuwe na uhakika tuweze kujua nguvu za upinzani wetu," kisha alimgeukia Jean akamwambia, "Mtu huyu amefika toka Jumatatu, na amefikia Hoteli Memling, na mimi nilikueleza wageni wote toka juzi waorodheshwe hasa kama huyu ambaye anatoka Lusaka sijui kama yuko kwenye orodha yako?"

"Jina hilo bado halijanifikia, nashangaa kwa nini. hebu nipe simu." Jean alipiga simu ofisini kwake akazungumza na Kabeya. Wengine waliendelea na mazungumzo. Alipomaliza aliwaeleza. "Ni jambo la ajabu sana. Kabeya anasema amepata majina ya watu wote waliofika hoteli Memling kwa msichana mmoja aitwaye Mwadi ndiye anampa maelezo yote kwa muda mrefu sasa ila anashangaa kwa nini jina la mtu huyu lilisahauliwa. Amesema atachunguza kwa nini."

"Mwadi ninamfahamu sana ni rafiki yake Tete, hivyo mueleze Kabeya asifanye lolote anisubiri tutalishughulikia jambo hili pamoja," Muteba alishauri.

"Jambo zuri sana, kama utalishughulikia jambo hili, maana nahisi kuna kitu kati ya wasichana hawa na mtu huyu. Ufanye kila mbinu uweze kuonana naye", Pierre alimweleza Muteba.

Mambo ya huyu Chitalu tuyaache mikononi mwa Muteba na Kabeya wayashughulikie," Papa alikubaliana.

"Tatizo lililobaki ni kwamba hawa watu wawili Ozu na Kofi bado wanatusumbua, usiku wa leo lazima tuwe na ulinzi mkubwa huko 'Garage Papadimtriou' maana wanaweza kwenda huko na leo tena. Vile vile magereji mengine yawe katika ulinzi wa kutosha maana huwezi kujua watu hawa wanajia kiasi gani. Fikiria, kama huyu Willy ni mmoja wao vipi ameweza kuitilia mashaka Sozidime? Hivyo lazima tuwe tayari kila dakika kuwakabili watu hawa wakijitokeza. Halafu msako wa watu hawa lazima uongezwe, na mahali popote watakapoonekana tu wauawe pale pale msisubiri maana kama mnavyosema wenyewe watu hawa ni hatari. Msiogope polisi, nyinyi shughulikeni, mambo ya polisi mniachie mimi," Pierre aliwaeleza.

"Jambo la maana kabisa Patron, tokea sasa hivi ninaongoza msako huu, kwani hawa watu nina deni nao, lazima tuonane tena uso kwa uso ili ijulikane waziwazi, nani ni nani kati yetu," alijigamba Papa. Baada ya mkutano huu, watu hawa waliondoka kwenda kushughulikia kazi kila mmoja aliyoipewa.


ITAENDELEA 0784296253

Comments

  1. Duuuuh kila sura zinavyosonga ndivyo hadithi inavyozidi kua nzuri... sasa ubaya wake ni kwamba thread haziji kwa kufukuzana

    ReplyDelete
  2. Brother Nyaka hii riwaya imeisha?? tutupie muendelezo tafadhali

    ReplyDelete
  3. Huyu jamaa yuko busy sana!! Hata kufanya updates anashindwa!! Ajili MTU wa kufanya updates acha ubaili tengeneza pesa!! That's a big business!!

    ReplyDelete

Post a Comment

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU