KIKOSI CHA KISASI

MAUAJI YA KISHENZI 

VI 

Ilikuwa saa tatu na dakika kumi Willy alipowasili nyumbani kwa Robert. Alipoingia ndani alikuta wenzake wote wako tayari na wanamsubiri kwa hamu. Kule kuingia tu wenzake walijua jambo kubwa lilikuwa limetokea kwani sura yake ilikuwa imebadilika kabisa na kwenye bega shati lake lilikuwa na damu. Aliondoka akiwa amevaa suti lakini sasa alikuwa hakuvaa koti na wala tai hii yote ilidhihirisha kuwa huko alikokuwa mambo yalikuwa yamechafuka. Wote walikaa kimya huku wanamwangalia. Willy alienda akaketi kwenye kochi na Robert akamletea glasi ya whisky. Willy alianza kuwasilimulia kwa kinaganaga mambo yote yaliyokuwa yametokea toka alipoondoka mpaka wakati huo alipokuwa amerudi. 

"Hii ina maana kuwa kuna chama au kikundi kinachoitwa White Power. Tukigundua kikundi hiki ni kikundi gani na kina madhumuni gani, na kwa nini kinaua ndugu zetu wapigania uhuru basi kazi yetu itakuwa imekamilika," Willy aliwaambia. Wenzake waliokuwa wanamsikiliza kwa makini, walionyesha sura ya masikitiko sana.

"Ingawa nilikuwa sijamwona Mwadi, nimehudhunishwa sana na tukio hili," alisema Kofi. Ozu na Robert nao walitingisha vichwa kuonyesha kuwa na wao walisikitishwa sana na mauaji haya ya kishenzi.

"Kama nilivyofikiria toka mwanzo baada ya kufanya upelelezi wangu kuwa kampuni yoyote iliyokuwa inawakilisha maslahi ya makaburu kiuchumi lazima itakuwa inashughulikia na maslahi mengine ya kisiasa kwa makaburu, sasa naanza kuona mwanga kabisa kwa haya magereji na hii kampuni ya wakala ya Sozidime ni ofisi za kijasusi za makaburu wanazozitumia huku wakidanganya watu kuwa zinashughulikia biashara. Kama Kofi alivyoeleza, nakubaliana naye kuwa watu wenye magereji haya na kampuni hiyo ni majasusi. Hii ndiyo sababu wameweza kufanya uhalifu mkubwa bila kujulikana kwa sababu wote hawa ni majasusi wa ujuzi wa hali ya juu kiasi cha kwamba idara ya polisi au ya upelelezi ya nchi ya Kiafrika ni vigumu kuwagundua. Hivyo hii habari ya watu hawa kuwa na gereji ni geresha tu ya kuficha shughuli zao hasa," alisema Robert kwa kirefu.

"Nafikiri ingekuwa rahisi kwetu kukikabili kikundi hiki cha 'WP' kama serikali ya Zaire ingekuwa inajua tuko hapa kwa sababu ya shughuli hiyo. Maana najua kuanzia sasa lazima tuwe macho maana tunaweza tukajikuta mikononi mwa polisi kabla hatujatekeleza shughuli yenyewe," alisema Ozu.

"Maneno yako ni sawa, lakini tatizo tulilonalo ni kwamba msimamo wa serikali ya Zaire juu ya jambo kama hili haujulikani bado. Nafikiri hii ndiyo sababu tumetumwa hapa kisiri kwa sababu ofisi inayoshughulikia jambo hili nayo haijawa na uhakika na msimamo wa serikali ya Zaire. Lakini hata hivyo inabidi itabidi Robert amwambie Chifu juu ya matatizo tunayoweza kuyakabili kama serikali ya Zaire haitakuwa na habari yoyote kuhusu sisi. Uamzi atakatoa ndiyo huo tutaufuata, kwa sasa hivi sisi tuendelee na shughuli hizi kisiri kama tulivyoagizwa," alifafanua Willy.

"Sisi tuko tayari kwenda huko "GAD GARAGE' kama tulivyokuwa tumepanga nafikiri kazi uliyoifanya kwa leo imetosha, wewe baki sisi twende," Ozu alimshauri Willy.

"Hata kidogo, kazi tunayoenda kuifanya ni ngumu, hivi lazima twende wote ila Robert itambidi abaki", Willy alieleza.

"Hapana, na mimi lazima niende, lazima na mimi nipewe nafasi ya kupambana na watu hawa." Robert alilalamika.

"Si hivyo, shughuli hii ni kubwa hivi hatuwezi kwenda wote kwa pamoja, tutakuwa tunafanya mchezo. Kwanza wewe ni mtu ambaye huwezi kukisiwa kwa jambo lolote ovu na mtu yeyote hivyo lazima ubaki kama akiba yetu kwa wakati mbaya zaidi. Vile vile itabidi ubaki ili uweze kuzungumza na ofisi yetu ya Lusaka, kusudi uweze kuwaeleza yote yaliyotokea vile vile wakueleze kama wana habari zozote," Willy alimweleza.

"Sawa kabisa, lazima Robert abaki," Ozu alikubaliana na Willy.

"Na mimi nakubaliana na nyinyi kabisa, lazima Robert abaki kwa usalama wetu baadaye," Kofi alimuunga mkono.

"Haya wengi wape", alijibu Robert kwa masikitiko.

"Wewe ni balozi bwana tuachie sisi huu unyama", Ozu alimtania.

"Nimeishiwa risasi, Robert nisaidie," Willy aliomba.

Robert aliingia chumbani na kurudi na pakiti mbili za risasi. Willy alijaza bastola yake halafu akawauliza kama wenziwe walikuwa wanahitaji nao.

"Sisi tuko tayari kabisa", Ozu alijibu. Kofi alionyesha bastola zake mbili alizokuwa ameisha zijaza risasi tayari. Willy aliwagawia wenzake risasi za akiba. Roberti alimletea Willy shati la kubadilisha. baada ya hapo wakaondoka kuelekea 'GARAGE GAD'  
ITAENDELEA 0784296253

Comments

  1. safi sana bwana mkubwa, tutupie kama vipande vitatu hivi kwa sababu (...)

    ReplyDelete
  2. pongezi kwako mkuu haina jinsi tutaendelea kusubiri tu hadi mwisho

    ReplyDelete

Post a Comment

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU