KIKOSI CHA KISASI

SURA YA TISA 
  
USIKU WA KAZI

Wakati wanaelekea gereji G.A.D. Willy aliwaeleza wenziwe mpango aliokuwa nao juu ya mashambulizi ya usiku huu. Baada ya mabishano kwenye mambo fulani fulani walikubaliana mpango huo. "Kwa hiyo jamani usiku huu utakuwa ni usiku wa kazi kubwa," Willy alimalizia.

"Tumwombe Mungu." OZu alisema.

"Mungu atatusaidia, maana sisi tunachopigania ni haki za ndugu zetu huko Kusini mwa Afrika na wala hatumuonei mtu," Kofi aliongezea.

Gereji G.A.D. ilikuwa sehemu za Gombe barabara ya T.S.F karibu na stesheni ya Televisheni lakini kwa upande mwingine. Willy alikuwa ameitafuta gereji hii wakati wa mchana na alikuwa ameiangalia kwa uangalifu sana. Basi akiwa anaendesha kwenye hi barabara ya 30 Juin alikata kona na kuingia barabara ya T.S.F. Akiwa anaendesha kwa mwendo wa kawaida alipita mbele ya gereji.

Ozu aliangalia saa yake ilikuwa ni saa nne kasoro. "Bado mapema sana, tungoje mpaka watakapofunga stesheni hapo saa tano," Ozu alishauri.

"Hata mimi naona hivyo maana hata mitaa ya huku bado ina watu, waweza kutuletea kisanga," Willy alisema, Kofi ambaye macho yake na mawazo yake yalikuwa kwenye hilo jengo la G.A.D. aliangalia ingawaje kwa upesi na kuona kuwa kulikuwa na walinzi upande ule wa mbele wa jengo hili.

"Kutakuwa na ulinzi mkali kwenye jengo hilo baada ya tukio la jana," aliwaeleza wenziwe.

"Lazima tutegemee hivyo," alijibu Ozu. Willy alienda mbele kidogo akageuza gari na kurudi huku wakipita kwa kasi sana mbele ya jengo hilo.

"Naona twende Cafe de la Paix tukapoteze muda pale, nadhani ni mahali penye usalama wa kutosha", Willy alishauri.

"Pale ni pazuri sana, tunaweza tukauwa hii saa moja pale bila shida," alijibu Kofi. Cafe de la Pix iko barabara ya 30 Juin. Willy aliendesha gari hadi pale, akaliegesha wakatelemka.

"Tukae kwenye viti vye nje", alisema Willy. Walikaa hapo nje na wakaagiza vinywaji. Kila mmoja wao aliagiza Whiski. Wakati wakiendelea na kinywaji chao Willy alimwita mfanyakazi mmoja aliyepita pale karibu.

"Samahani ndugu naomba kukuuliza", Willy alimwambia.

"Bila samahani", alijibu. 

"Unaijua gereji Baninga?"

"Ndiyo".

"Iko wapi?"

"Iko huko sehemu za Kintambo, barabara ya Bangala iko karibu na shule."

"Asante sana nimeelewa", Willy alijibu na yule mtu aliondoka.

Mahali penyewe nimepafahamu sasa nimeishafika pale. Mbele ya ile shule kuna kiwanja cha mpira na gereji hii inatazamana na goli la mwisho kama ukiwa unatokea Kasavubu", alieleza Kofi.

"Basi hamna taabu," alijibu Ozu. Ilipotimia saa tano, waliondoka na kuingia ndani ya gari lao na kuelekea gereji G.A.D. Walipoingia barabara ya T.S.F. waliegesha gari lao karibu na majengo ya stesheni ya Televisheni na wote wakatelemka. Wakati wafanyakazi wa stesheni ya Televisheni walikuwa wamemaliza zamu yao ya saa tano walikuwa wanaishiaishia kuondoka. Kwa hivi kuegesha gari lao wakati ule ilikuwa vigumu kutambulika.

"Mimi na Kofi tutatangulia kuingia ndani. Ozu atatufuata mara tu ukisikia mlio wa bunduki", Willy alieleza.

"Vizuri," alijibu Ozu.

"G.A.D. Gaereji" ilikuwa imejengwa kwa mtindo sawa na 'Garage Papadimtriuo' Willy na Kofi waliamua kuingilia gereji hii kwa kupitia nyuma. Waliingia kwenye uchochoro uliokuwa kati ya nyumba ya pili na ya tatu toka kwenye gereji na kuelekea nyuma ya nyumba hizi na nyumba ya barabara ya pili.

Walitembea kwa tahadhari kubwa, lakini walipofika nyuma ya ngome ya gereji hawakukuta ulinzi wowote.

"Nitatangulia mimi", Kofi alimnong'oneza Willy. Kofi alipanda juu ya mabega ya Willy akashika juu kabisa ya ngome. Aliangaza chini akakuta yuko nyuma ya ofisi kama vile alivyoona kule 'Gereji Papadimitriuos'. Hakukuwa na mlinzi yeyote kitu kilichomshangaza sana. kwani baada ya tukio la jana alitegemea kukuta ulinzi mkali kwenye magereji ya hawa watu. Alipanda juu akajitandaza juu ya ukuta wa ngome kisha akampa Willy mkono wake na kumvuta ili kumsaidia kupanda. Walipokuwa wamepanda wote ukuta walitelemka taratibu na kuangukia ndani ya ngome.

"Kama nyumba hii imejengwa kama ile ya Papadimitriuo, kuna dirisha kubwa kuzidi hili la nyuma kwa upande wa kushoto. Dirisha hili liko kwenye chumba cha mkutano, Tukiweza kupita humo tutakuwa tumeingia ndani ya chumba cha mkutano," Kofi alimnong'oneza Willy.

"Tutajaribu kupitia huko", Willy alijibu.

Walipoenda kwenye pembe ya upande wa kushoto Willy aliona kuna mlango upande ule, na wakati akichungulia mlango huo ulifunguliwa. Alimfanyia ishara Kofi na kumtahadharisha. Watu wapatao sita wakiwa na bunduki kubwa kubwa, walitokea kwenye mlango huu. Willy alishukuru bahati yao nzuri kwani alitambua kuwa walikuwa wamewawahi wakati watu hawa aidha akijitayarisha au wakihutubiwa. Ilionekana watu hawa hawakutegemea shambulio lolote kabla ya saa sita, watu wanne kati ya hawa sita walielekea upande wa mbele wa nyumba na wawili walielekea upande huu wa nyuma ambako Willy na Kofi walikuwa.

"Watu wawili wanakuja huku", Willy alimnong'oneza Kofi. Walijibanza sawa na ukuta kusubiri. Watu hawa bila kujua kuna nini walikuja wanazungumza pole pole. Walipofika kwenye pembe hii ya kwenda nyuma wakasimama wakaweka silaha zao tayari. Kwa sababu hapakuwa na mwanga wa kutosha hawakuweza kuwaona upesi akina Willy kwa namna walivyokuwa wamejibanza kwenye ukuta. Willy alimwacha yule wa mbele akampita kidogo, yule wa pili aliyekuwa anafuata wenzake karibu karibu huku wanaangalia kwenye ngome alimgusa Willy maana alipita karibu sana na ukuta. Kugutuka tu Kofi na Willy waliwashambulia kabla akili zao hazijajua ni nini kinatokea. Kofi alimshambulia yule wa mbele na Willy yule wa nyuma. Watu hawa walipigwa na kuwaua kwa mikoni bila hata kupiga kelele. Pala karibu kulikuwa na gari bovu wakalifungua wakarundika maiti za watu hawa humo ndani zikafichika. Walipoangalia zile bunduki wakakuta ni 'machine gun' ambazo zilikuwa zimeishapakiwa risasi tayari kwa kutumika. 

"Loo tumepata silaha, sheria yake", alisema Kofi huku anaipima pima bunduki aliyochukua kutoka kwa yule mtu aliyemuua. Willy naye alichukua ile ya mtu mwingine. 

"Nia yangu ni kutaka kuingia ndani, hivyo tutaingilia kwenye mlango huo waliotokea hawa watu", Willy alimnong'oneza Kofi.

"Sawa". KOfi alijibu. Wakiwa sasa wamebeba hizi 'machine gun' tayari tayari walielekea kwenye mlango. Walipofika kwenye ule mlango Wili aliweka sikio kwenye tundu la kuwekea ufunguo wa kufungulia, lakini hakusikia kitu. Alijaribu mlango akakuta umefungwa. Alitoa funguo zake malaya, akafungua kufuli taratibu bila kelele. Wakati huo Kofi alikuwa tayari tayari kwa lolote ambalo lingeweza kutokea. Walifungua mlango, na kuingia ndani na kufunga tena na funguo. Walijikuta wamo kwenye chumba kikubwa ambacho hakikukwa na kitu chochote ndani.

"Nafikiri wanachukulia mazoezi humu." Kofi alisema. 

"Nafikiri", Willy alijibu kwa mkato. Walienda na kujaribu mlango mwingine wa kutokea ndani, wakakuta haukufungwa. Willy aliufungua taratibu akachungulia, hakukuwa na mtu ukumbini, akamfanyia Kofi ishara, wakajitokea ukumbini. Chumba kilikuwa kinatazamana na chumba walichokuwa wametoka kilikuwa kimewekwa kibao kilichoandikwa 'MKURUGENZI' Willy alimuonyesha Kofi ishara kuwa alikuwa anataka waingie mle. Willy alijaribu ule mlango akakuta umefungwa, alitoa funguo zake malaya akajaribu tena zikafungua, wakaingia ndani na kujifungia. Kofi alitoa kurunzi ndogo mfukoni akaangaza kwenye meza kubwa iliyokuwemo, mbele ya meza kulikuwa na kibao kilichoandikwa "Jean Vergence" Hiki kibao kiliwafahamisha kuwa hii ofisi ilikuwa ni ya mwenye gereji. Willy alichukua kurunzi kutoka kwa Kofi akaanza kuangaza kwenye ukuta. Nyuma ya kiti kwenye meza hii kulikuwa na kabati la chuma. Willy alifikiria kuwa humo ndani ya hili kabati ndimo kungekuwa na makaratasi ya maana ambayo yangeweza kuwasaidia katika shughuli zao. Alisogelea kabati akaanza kulichunguza kama angeweza kulifungua. Kofi naye alisogea na kuliangalia. Willy alitoa fungu la funguo malaya zikiwemo funguo kadhaa malaya za kufungulia makabati kama haya. Funguo hizi alikuwa amezichukua kwani alitegemea matatizo kama haya. Alijaribu ufunguo wa kwanza lakini haukufungua, alijaribu wa pili nao ulikataa, alipojaribu wa tatu ukafungua. Ndani ya kabati hili la chuma mlikuwa na sanduku dogo la fedha. Willy hakuwa anatafuta hicho hivyo alimulika mle ndani vizuri akaona mlikuwa na saraka ndani. Alivuta akakuta imefungwa alitoa funguo zake malaya tena akaanza kujaribu kufuli la saraka hii, kwa bahati alipojaribu tu mara moja ikafunguka. Alipovuta akakuta mna bahasha moja kubwa akaitoa na kuifungua. Mara akasimama na bahasha yake mkononi. 

"Hawa watu wamekwenda wapi?" walisikia mtu anauliza ukumbini.

"Hatujui maana sisi tulikuwa wanne tulioelekea mbele na wenyewe wakaelekea nyuma ya ofisi kama walivyotupanga, sasa hatuelewi imekuwaje..." sauti nyingine ilijibu. Walisikia mlango wa kile chumba walichoingilia unafunguliwa na sauti ikapotea.

"Wanawatafuta, watawaona sasa hivi." Kofi alinong'ona.

"Tuondoke humu", Willy alijibu.

Willy aliweka bahasha aliyokuwa ameichukua vizuri ndani ya shati, akafunga mkanda wake wa suruali sawa sawa, akafungua mlango akiwa 'machine gun' yake ameiweka begani na bastola mkononi tayari kukabiri hatari yoyote. Kofi naye alitoka nyuma ya Willy na kurudisha mlango. Ghafla mlango wa mbele wa nyumba ulifunguliwa na mlango wa kile chumba kikubwa nao ukafunguliwa. Kwa sababu taa ilikuwa inawaka ukumbini wale watu waliofungua milango hii walionana ana kwa ana na Kofi na Willy. Wale watu walizubaa kidogo maana wao hawakutegemea kukutana na mtu yeyote ukumbini. Yule wa mbele alitaka kurudisha mlango lakini Willy aliwahi kumpiga risasi kabla yeye hajaweza kufanya hivyo. Alipoanguka chini bastola yake ilifyatuka na kufanya kelele nyingi. Bastola za akina Willy zilikuwa hazikufanya kelele kwani walikuwa wakitumia sailensa.

Baada ya mlio huu wa bastola, walisikia watu wanakimbia kwa nje. Kusikia hivi wakajua mambo yameiva. Waliweka bastola mifukoni, na kushikilia 'machine gun' vizuri. Kisha wakaruka ndani ya chumba kikubwa, wakasubiri kwani walisikia nyayo zikija, kwa upande wa mlango wa kutokea nje wa chumba hiki. Mara mlango ukafunguliwa kwa teke na risasi zikamiminika ndani ya chumba hiki, wao wakabana kabisa kwenye ukuta. Yule mtu aliyekuwa anamimina risasi alipohakikisha kwamba hakuna mtu, aliingia ndani na hapo ndipo alishambuliwa na Kofi aliyemwauza kwa risasi. Walipokwisha kufanya hivi walitoka nje kwa kutokea mlango walioingilia pembeni mwa nyumba hii. Kofi aliekea nyuma na Willy akaelekea mbele ya nyumba hii. Wakaanza mashambulizi thabiti.

Ozu aliyekuwa amejificha kwenye uchochoro mmoja karibu na gereji hii, aliposikia mlio tu wa bunduki alijua kuwa kazi imeanza. Alikimbia mpaka kwenye lango la mbele, na kama alivyofikiria alikuta walinzi waliokuwa pale mlangoni wanakimbilia ndani kufuata mlio wa bunduki ulikotokea. Hivi hakupata upinzani wa aina yoyote pale langoni, kwa bahati alikuta lango limerudishwa tu bila kufungwa. Alisukuma lile lango na kuingia ndani, huku akiwa amejikinga mwenye magari mabovu akielekea kule kwenye ofisi ambako ndiko kulikuwa kunatokea milio ya bunduki.

Masamba ambaye ndiye alikuwa ameachiwa jukumu la kulinda gereji hii wakati Jean ameondoka alijikuta katika wakati mgumu sana. Alikuwa ameachiwa walinzi sita wakiwemo wapiganaji bunduki sita hodari sana. Yeye mwenyewe alikuwa muuaji hodari wa 'WP'. Na kazi hii alikuwa ameitekeleza vizuri kabisa kila alipokuwa ameamriwa kufanya. Akiwa katika ofisi yake, na huku akisikia mapigano yanaendelea huko nje, aliinua 'machine gun' yake na akachukua bastola mbili akaondoka tayari kwa kusaidia walinzi wake kwenye uwanja wa mapambano. Willy na Kofi walikuwa wamewazingira walinzi wa gereji hii. Ilikuwa rahisi kwao kuwazingira kwani walinzi hawa walikuwa wamekimbilia kule mlio wa bunduki ulikuwa bila kwunza kuangalia mambo yanakwendaje. Walitupiana risasi na Kofi kwa upande ule wa nyuma ya ofisi. Willy ambaye aliwaingilia kwa kutokea mbele hawakumuona, wao walifikiria wako kule risasi zilikokuwa zinatokea tu.

Willy alitambaa juu huku akiwa amezuiwa na magari haya mavovu. Kofi aliendelea kijibishana risasi na hawa watu ili kumpta nafasi Willy kuwashambulia kwa nyuma bila wao kutambua. Willy alipofika karibu kabisa nao, aliweza kuona jinsi walivyokuwa wamejipanga. Alitoa bastola yake na kuwapiga walinzi wawili risasi waliokuwa karibu naye. Kwa sababu bastola yake ilikuwa na sailensa wale walinzi wengine hawakutambua maana kulikuwa na giza. Akasogea tena mpaka akawakaribia wengine wawili nao akawapiga risasi, mmoja wao haikumpata vizuri hivi akageunza na kuanza kupiga risasi upande ule wa Willy alikokuwa lakini Willy alimuwahi na kummaliza. Tukio hili ndilo liliwafahamisha walinzi waliokuwa wamebaki kuwa walikuwa wameishaingiliwa kwa nyuma. Kwa hofu walianza kupiga risasi hovyo hii ikampa nafasi Kofi kutoka kwenye kona aliyokuwa amejibanza na kushambulia watu hawa kwa 'machine gun'. Wawili kati ya walinzi hawa waliuawa, na mmoja alitupa silaha yake akakimbilia mwenyewe magari kuelekea mlangoni.

Willy walikutana na Kofi na kujibanza kwenye gari moja.

"Naona tumewamaliza", alidai Kofi.

"Sina uhakika", alijibu Willy.

Ozu aiyekuwa anatafuta mlio wa bunduki taratibu na kwa tahadhari kubwa alijigonga kwenye kitu. Alipoangalia amejigonga kwenye nini, akakuta ni mdomo wa tanki la petroli, linalopeleka petrol ndani ya gereji. Mara mawazo yake yakashituliwa kwani aliona mlango wa mbele unafunguliwa. Aliona mtu anachungulia kwa uangalifu sana halafu akatokeza akiwa ameshikilia bunduki yake tayari. Ozu aliona huyo si Kofi wala Willy, hivi akamwendea. Alichukua jiwe akalitupa nyuma ya huyu mtu. Mtu huyu aligeuka kama umeme huku akimimina risasi. Ozu alichukua nafasi hii akampiga risasi ambayo ilimpata huyu mtu kwenye bega, akatupa bunduki yake na kuruka wakati huo huo nyuma ya gari mojawapo, Masamba alijua huu ndiyo mwisho wa maisha yake. Hakujua mtu aliyekuwa amempiga risasi alikuwa amepiga kutokea sehemu gani. Alifikiria kukimbia lakini akaona hakuna njia ya kutoka sehemu hii, hivi aliamua apigane na watu hawa mpaka mwisho wake.

"Lazima Ozu ameingia unasikia mlio huo," Kofi alimnong'oneza Willy.

"Kumbe bado kuna walinzi, wewe zunguka ulikotokea, mimi nitarudi nilikotokea. Ukifika kwenye pembe ya nyuma na ya upande wa kushoto piga risasi, hii itanipa mimi nafasi ya kuwaingia watu hawa kumsaidia Ozu," Willy alieleza. Ozu alijua amempiga yule mtu risasi, lakini haikuwa imemuingia sana kwa kutokana na yule mtu alivyoruka baada ya kupigwa risasi. Ilimdhihirishia Ozu kuwa mtu huyu alikuwa ni hodari, hivi alikata shauri amwendee kwa pupa. Mara alisikia risasi zinalia upande aliokuwa ameangukia huyu mtu. Hii ikampa nafasi Ozu na Willy kujua mtu huyu alikuwa wapi. Ozu alipiga risasi mahali pale ambako Masamba alikuwa . Masamba alijiviringisha kutoka mahali pale lakini Willy akamuona na kumwachia risasi chungu nzima, na kumuua pale pale. Baada ya hapo kila mmoja wao alijibanza kukawa kimya. Ozu alipiga mluzi ambao ulikuwa ni wa kujijulisha. Willy alijibu halafu Ozu akabibu walisubiri tena kidogo kuhakikisha kuwa hakuna mtu mwingine ndipo wakapigiana mluzi wa kuondoka. Wakati wanakutanika mbele ya ofisi hii ndipo waliona yule mlinzi mmoja aliyekuwa ametupa bunduki yake na kukimbia akipitia kwenye lango na kukimbia nje.

"Huyo mmoja amewahi kutoroka", Ozu aliwaonyesha.

"Tuondoke hapa, maana polisi au kundi la watu hawa linaweza kufika wakati wowote", Willy alishauri.

"Pale mbele nimeona mahali ambapo tanki ya petrol lilipochimbuliwa, mnaonaje tukilipua gereji isionekane tena kabisa?" Alieleza Ozu.

"Wazo zuri sana, hakika tukilipua gereji hii tutakuwa tumebomoa kambi moja ya hawa wadhalimu na kubakiwa na makambi mawili ambayo vile vile itabidi tuyalipue,"alijibu Willy. Ozu alichukua machine gun iliyokuwa imetupwa na Masamba, na haraka haraka wakakimbilia pale kwenye mdomo wa tanki. Mfuniko wa mdomo wa tanki ulikuwa umefungwa na kufuli. Ozu alipiga kufuli kwa risasi likasambaa na akafungua mfuniko wa tanki hili. Tanki lilikuwa limejaa petroli.

"Tangulieni," Ozu aliwashauri. Willy na Kofi walikimbia kwenye uficho na kumwacha Ozu akishughulika. Ozu alichukua kitambaa chake, akakilowanisha ndani ya petroli akachukua kiberiti toka mfukoni kwake, akaenda mbele hatua chache halafu, akakiweka kile kitambaa moto, akakitupa pale kwenye mdomo wa tanki akaondoka mbio. Kufika mlangoni akakuta akina Willy wameshafika ndani ya gari, akarukia na wakaondoka kasi. Walipofika kwenye kona ya T.S.F. na 30 Juin walisimama kidogo kungojea kama mlipuko utatokea au vipi! Lakini waliona gari la polisi linakuja ikabidi waondoke.

"Tunaelekea 'Garage Baninga'... kabla hata Willy hajamaliza kusema, kulitokea mlipuko mkubwa ambao uliitingisha sehemu nzima ya Gombe.

ITAENDELEA 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru