MWANARIADHA SIMBU KUTUA BUNGENI DODOMA

Mwanariadha wa Kimataifa wa Tanzania, Alphonce Simbu aliyeshika nafasi ya tano katika mashindano ya London Marathon 2017 atakuwa mgeni wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kesho Alhamisi April 27 akiwa ni mgeni maalum wa Waziri wa Habari, Sanaa, Michezo na Utamaduni, Dkt. Harison Mwakyembe. 

Baada ya kutembelea bumge hilo Simbu pia atakuwa na mazungumzo na Waziri Mwakyembe. Simbu ataambatana na mwakilishi wa wadhamini wake DStv pamoja na maafisa waandamizi wa Jeshi la Kujenga Taifa JKT.
 
Akizungumzia mwaliko huo, mwanariadha huyo amesema kuwa amefurahishwa sana kupata mwaliko wa Waziri anayehusika na 
sekta ya michezo kwenda bungeni kama mgeni wake maalum. Amesema hii inaonyesha kuwa serikali inatambua jitihada 
zake anazozifanya katika kuiwakilisha vyema nchi katika mashindano ya kimataifa. 

“Nimefurahi sana kualikwa na mheshimiwa Waziri kumtembelea bungeni, bila shaka hii itakuwa fursa nzuri ya hata wabunge kutambua jitihada tunazofanya vijana wao katika kuliletea taifa sifa. Natumaini pia nitapata fursa ya kuongea ana kwa ana na Waziri” alisema Simbu na kuongeza kuwa atatumia fursa hiyo kumueleza Waziri changamoto nyingi wanazokabiliana nazo wanamichezo hapa nchini.
 
Amesema kuna mengi ya kuongea na Waziri na kwamba anaamini mazungumzo yao yatakuwa na tija na manufaa si kwake tu, bali kwa wanamichezo wote kwa ujumla. Kwa upande wake, Meneja Uhusiano wa Multichoice Tanzania Johnson Mshana, ambaye anaandamana na Simbu, amesema kuwa anaamini ziara hiyo na mkutano na Waziri utakuwa na manufaa makubwa kwani pia itakuwa ni fursa nzuri ya kujadili namna bora zaidi ya Serikali kushirikiana na wadau katika kuimarisha na kuendeleza michezo hapa nchini. 

“Sisi kama wadhamini wa mwanariadha huyu tunaamini kuwa kitendo cha Waziri kutualika ni ishara kuwa kweli anadhamiria kushirikiana na sisi wadau wa michezo ili kuongeza nguvu za pamoja za kuimarisha michezo hapa nchini” alisema Mshana
 
Multichoice Tanzania kupitia DStv imekuwa ikimdhamini Simbu tangu mwaka jana na udhamini huo pia umewanufaisha 
wanariadha wengine ambao wamekuwa kambini kwa muda sasa pamoja na simbu. “Kambi ya mazoezi ya Simbu ambayo 
ilidhaminiwa na DStv pia ilikuwa na wanariadha wengine ambao wote walinufaika moja kwa moja na udhamini huo. 

Tunaamini kuwa pia kati ya hao tutapata wanariadha watakaofanya vizuri siku zijazo”. Alphonce Simbu, ambaye pia ni mshindi wa medali ya dhahabu katika mashindano ya Mumbai Marathon ni miongoni mwa wanariadha wa timu ya Taifa itakayoshiriki katika mashindano ya Dunia yatakayofanika jijini London  mwezi Agosti mwaka huu

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU