BUNGE LAMSHANGILIA MWANARIADHA ALPHONCE SIMBUBunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lilizizima kwa nderemo na shangwe pale alipotambulishwa rasmi mwanariadha Alphonce Simbu (pichani juu wa pili kulia), ambaye ni Mshindi wa medali ya dhahabu wa Mumbai Marathon, na mmoja ya washindi wa London Marathon 2017 alipokutana na Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa.

Mwanariadha huyo ambaye pia ni balozi maalum wa DStv, alilitembelea Bunge kama mgeni maalum wa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Dkt. Harison Mwakyembe (pichani juzi kulia) akiambatana na muwakilishi wa DStv Johnson Mshana (kushoto) na maafisa kadhaa waandamizi wa Jeshi la kujenga Taifa akiwemo Kanali K.J Mziray – Mkuu wa Utawala na Mafunzo wa wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT)

Mara baada ya Naibu spika wa Bunge Dkt. Tulia Akson kumtaja Simbu, bunge lilizizima kwa shangwe kwa muda  hali iliyoashiria kuraha kubwa kwa wabunge kuweza kumshuhudia mwanariadha huyo ambaye ni tegemeo kubwa la Tanzania katika mashindano ya riadha ya Dunia yatakayofanyika Agosti mwaka huu jijini London.

Baada ya ziara hiyo, Simbu alipata fursa ya kusalimiana na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa na kisha kuwa na mazungumzo mafupi na Waziri Mwakyembe.

Akiongea wakati wa kupiga picha ya pamoja na Simbu, Waziri Mkuu Majaliwa alimpongeza mwanariadha huyo na kusema kuwa Serikali inatambua na kuthamini sana jitihada zilizofanywa na wadau wote katika kufanikisha ushindi wa Simbu. Pia alimtakia kila la heri katika maandalizi na kisha ushiriki wake katika mashindano ya Dunia yanayomkabili mwishoni mwa mwaka huu.

Naye Waziri mwenye dhamana ya Michezo Dkt. Mwakyembe ambaye ndiye aliyemwalika Simbu Bungeni, alisema Wizara imekuwa ikishirikiana na wadau kwa karibu ambapo hata wakati wa Safari ya Simbu kwenda London, wizara ilihakikisha safari hiyo inafanikiwa. Ameonyesha kufurahishwa kwake na vipaji vilivyopo na kusema nguvu za ziada zitawekwa ili kuhakikisha kuwa vipaji hivyo vinaibuliwa na kukuzwa kwa manufaa ya taifa zima.

Kwa upande wake, Simbu alisema kitendo cha yeye kualikwa bungeni kimempa faraja kubwa na pia alifurahi sana kuona jinsi wabunge walivyomshangilia na kumpongeza. “Kwakweli ujio wangu bungeni umenipa faraja kubwa kuona ni jinsi gani wabunge wote walivyofurahishwa na mafanikio niliyopata na sifa niliyoiletea nchi. Hii imenipa sana moyo na uzalendo kwani ni dhahiri kuwa taifa zima liko nyuma yangu na linanunga mkono kikamilifu” alisema Simbu

Alitoa shukrani za pekee kwa wadhamini wake DStv, pamoja na Waziri Mwakyembe kwa jitihada kubwa anazofanya. Amesema anaamini kwa mwenendo huu yeye, wanariadha wengine na wanamichezo wote wa Tanzania watafika mbali na hatimaye Tanzania itakuwa kinara katika ulingo wa michezo duniani. Pia alilishukuru Jeshi la Kujenga Taifa JKT kwa kumruhusu kufanya mazoezi na kushiriki katika mashindano mbalimbali.

Simbu ambaye ni miongoni mwa wanariadha bora wa Tanzania alivunja rekodi yake aliyoiweka mwaka jana nchini Japan ya muda wa 2:09:19 na hatimaye katika mashindano ya London Marathon mwaka huu alitumia muda wa 2:09:10 ambao ndio muda wake bora zaidi.

Simbu ni miongoni wa wachezaji wa timu ya taifa ya riadha watakaoshiriki mbio za Dunia mwezi Agosti mwaka huu jijini London.


Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru