KIKOSI CHA KISASI

SURA YA TISA 

USIKU WA KAZI 

V

Magari ya akina Papa yalipopishana na gari la akina Willy, nara moja akina Willy waliyatambua.

"Hao wanakwenda plani yangu imefanya kazi," Willy aliwaeleza wenzake.

"Lo, tuna bahati sana usiku huu", alinena Ozu.

"Hii gereji Papadimitriou iko vipi?" Aliuliza Willy.

"Imejengwa sawa sawa na gereji G.A.D. haina tofauti hata kidogo. Jinsi ulivyoona ndani ya G.A.D ndivyo ilivyo hivyo na Papadimitriou", alieleza Kofi.

"Inabidi tutumie uzi ule ule wa kuyalipua makambi haya. Je kuna petroli stesheni mle ndani?" Aliuliza Willy tena.

"Kama nilivyokwambia petroli stesheni ya Papadimitriou iko ndani kama ile ya G.A.D. na imekaa vile vile. Nafikiri hata mahali tanki lilipochimbiwa litakuwa katika sehemu kama ya kule G.A.D.," Kofi alisisitiza.

"Bila shaka", alizidi kusisitiza Ozu.

"Kama ni hivyo operesheni yetu ni kama kawaida. Hapa napo lazima tufanye haraka kama tulivyofanya kule Baninga, maana watu hawa wakikuta wamedanganywa watarudi kama risasi," alieleza Willy wakati anasimamisha gari lake kwenye kona ya barabara ya Assossa na Kabambare. Kila mtu akiwa amechukua silaha yake kamili kamili walikimbia huku wakiwa wanajificha ndani ya vivuli vya nyumba za jirani.

Wote waliamua kushambulia kutoka kwa nyuma, na kwa vile walikuwa wamepandwa na mori sasa walikuwa wakifurahia shughuli yote hii. Walipandishana ukutani haraka haraka na kutumbukia ndani. Walinzi wote wanne waliokuwa wamebaki hapa walikuwa wako mbele ya ofisi wakielezana walivyokuwa na bahati ya kuachwa kwenda kwenye mapambano na watu hawa watatu. 

"Nasikia watu hawa wana ujuzi kweli, kuonana nao ni kutafuta kifo tu, ni watu wasiowezekana," mmoja wao alieleza.

"Mimi leo ndiyo mwisho wangu kwa kazi hii, kesho natoroka moja kwa moja sitarudi," wa pili alieleza. Wote wakacheka bila kujua kuwa wameingiliwa.


"Utaacha pesa zote hizi! mimi niko tayari nipambane na hao watu ili nipate hizi pesa ikiwa nitamaliza mkataba huu hai", mwingine alisema.

Willy na wenzake waligawanyika. Willy alipita upane wa kulia na Kofi na Ozu wakapita upande wa kushoto na kunyatia wakielekea mbele. Walipofika karibu na mbele wote walisikia maneno waliyokuwa hawa walinzi wanazungumza.

Walipokuwa wamefika kabisa kwenye pembe ya kutokea mbele. Willy alijitokeza na kusambaza risasi na Kofi na Ozu wakafanya hivyo vile vile. Walinzi wote wanne waliuawa pale pale.

Bila kupoteza muda walitafuta mahali tanki lilipokuwa limechimbiwa wakapata bila taabu. Ozu alifanya shughuli yake kama kawaida baada ya kufungua mdomo wa tanki, akachovyo kitambaa alichopewa na Kofi ndani ya petroli wakaondoka hatua chache . Ozu akawasha kitambaa akakitupa pale kwenye mdomo wa tanki, na wote wakakimbia na kuondoka pale. Walienda moja kwa moja mpaka kwenye gari lao wakaingia wakawasha moto huku wakingojea mlipuko.

"Haya matanki ya petroli yameturahisishia kazi. Usiku wa leo sintakaa niusahau", alisema Ozu. Mara wakasikia magari yanakuja. 

"Hao wanarudi", Willy aliwatahadharisha wenzake. na wakati huo huo mlipuko ukatokea uliotetemesha sehemu nzima ya Lingwala. "Kwa leo kazi hii imetosha twendeni tukapumzike", Willy alishauri.

ITAENDELEA 0784296253

Comments

Post a Comment

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru