KIKOSI CHA KISASI

SURA YA KUMI 

MAPAMBABO BADO YANAENDELEA 

IV

Ilikuwa saa nne unusu juu ya alama Willy aliposimamisha gari lake mbele ya ofisi za O.A.U. Robert naye alikuwa tayari ameishatelemka pale chini, alipomuona Willy anaegesha gari alimfuata.

"Ingia twende", Willy alimwambia.

"Gari langu niliache?" Robert aliuliza.

"Liache", Willy alimjibu. Robert aliingia ndani ya gari wakaondoka.

"Vipi umeweza kufaulu kumuona Kadima?" Willy aliuliza. 

"Ndiyo nimefanikiwa", Robert alijibu.

"Sasa twende tubane mahali pale Wizarani kwao tumsubiri, akitelemka tu, tumteke nyara, ili tukamuulize vizuri," Willy alishauri.

"Lakini pale Wizarani pana watu wengi, kumteka nyara patakuwa na kazi," Robert alieleza.

"Si kitu tutafanya kila mbinu hata ikibidi tufanye ghasia ili tumchukue tutafanya," Willy alijibu.

"Vipi mambo yako, yameenda namna gani?" Robert alimuuliza.

Willy alimweleza mambo yote yaliyotokea tangu alipofika Hoteli Memling na vile vile akamweleza juu ya mazungumzo yake na Tete. Alieleza yote haya wakiwa wameegesha gari lao kwenye nafasi ambayo walikuwa wanauona mlango wa mbele wa Wizara ya mambo ya nchi za nje, na kuhakikisha kuwa kila mtu aliyetoka ndani wanamuona.

"Msichana huyu ameenda ofisini kwake lakini atakuja huko nyumbani kwako baada tu ya kutoka kazini," Willy alimalizia kueleza.

"Hii sasa imeleta picha yote ya mambo ilivyo. Ninaweza kusema bila kusita kuwa huyu Maximillian ni jasusi wa Shirika la Ujasusi la Ufaransa 'SCEPE' maana SCEPE, BOSS na CIA zinafanya kazi zao kwa pamoja katika Afrika. Mimi kila siku nasema ningekuwa rais wa nchi yoyote huru ya Afrika lazima ningepiga kelele nchi za Afrika zisiwe na uhusiano wowote na Ufaransa." Alisisitiza Robert.

"Siasa ni kitu kingine, utakuta Mkuu wa nchi hii ana sababu zake za kuhusiana na nchi fulani na Mkuu wa nchi nyingine ana sababu zake za kuhusiana na nchi nyingine ili mradi kila mtu apate maslahi yake. Umasikini wa nchi za kiafrika ndio tatizo kubwa linalozifanya zisiwe na msimamo thabiti wa kisiasa." Willy alieleza. Ilikuwa imeishatimia saa tisa na nusu lakini Kadima alikuwa bado hajatokea. Watu walikuwa wanatoka lakini Kadima alikuwa hajatokea.

"Vipi huyu mtu hakuja nini?" Willy aliuliza.

"Habari nilizopata na ni za uhakika ni kwamba yupo ndani ya mkutano. Huenda mkutano haujaisha", Robert alijibu.

Mara watu wawili walitokea wakiwa wamebeba mikoba yao. "Huyo wa upande wa kushoto ndiye Kadima," Robert alimweleza Willy.

"Twende," Willy alimweleza Robert. Walitelemka kama watu wa kawaida tu, wakaelekea kwenye maegesho ya magari hapo Wizarani huku wanajifanya kama kwamba wana mazungumzo kati yao. Kadima alisimama akizungumza na yule mwenzie.  Willy na Robert nao walisimama.

"Nenda ukalete gari sehemu hii. Atakapomaliza mazungumzo yake mimi nitamfuata." Willy alimweleza Robert.

Kadima aliagana na yule mwenzake na kila mtu akaelekea kwenye gari lake. Willy alimkatisha na kuonana naye kabla hajafika kwenye gari lake.

"Bwana Kadima nafikiri," Willy alimsemesha.

"Ndiyo kijana nikusaidie nini?" Kadima alijibu baada ya kumwangalia Willy na kumuona kijana muungawana kabisa.

"Ningependa kuzungumza nawe kidogo", alisema Willy na wakati ule ule Robert akasimamisha gari pembeni mwao. Willy alitoa bastola yake alikokuwa ameificha na akamwamrisha Kadima. "Ingia ndani ya gari na usipige kelele kwa usalama wako."

Kadima ambaye tokea azaliwe alikuwa hajawahi kuonyeshwa bastola au silaha ya aina yoyote alikuwa karibia azimie. Bila kusema neno aliingia ndani ya gari na Willy akaingia pembeni mwake Robert akaondoa gari. Waliondoka naye moja kwa moja mpaka nyumbani kwa Robert. Njiani kila mtu alikuwa kimya. Kadima ambaye mawazo yake yalikuwa yakizunguka huku na kule ili kujua kwa nini ametekwa alikaa amezubaa kabisa. Walipofika nyumbani kwa Robert walimteremsha na kumuingiza ndani ambako walimkaribisha kitini. Robert alienda akachukua glasi tatu akaweka barafu halafu akaweka kinywaji na kuwakaribisha. Kadima alishangaa sana kujikuta ameletwa ndani ya nyumba nzuri na vile vile alijua nyumba za mtaa huu zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya maafisa wa vyeo vya juu nchini na mabalozi. Alizidi pia kushangazwa na vijana hawa walioonekana waungwana sana. Woga wake kwa ujumla ulipungua.

"Bwana Kadima samahani sana kwa jinsi tulivyokuchukua kwa sababu hakukuwa na njia nyingine. Mimi naitwa Willy na mwenzangu anaitwa Robert. Ndugu Robert ni Katibu Mwenezi katika ofisi ya OAU iliyoko mjini hapa huenda utakuwa umewahi kumsikia kwani kazi zako na zake zinakaribiana", Willy alimfahamisha.

"Sijawahi kumwona", Kadima alijibu kwa mkato.

"Tuna maswali machache ambayo tungependa kukuuliza na tungeomba usitudanganye maana sisi tayari tunaelewa mambo mengi. Usishangae ukikuta tunabadilika na kuwa watu wabaya", Willy alimwekea mikwala.

"Wewe ni nani? Maana umesema jina lako tu hukujieleza wewe ni nani?" Kadima aliuliza.

"Mimi utanijua muda si mrefu", Willy alijibu.

"Haya kama ni maswali ninayoyajua nitayajibu kama siyajui sitaweza." Kadima alieleza.

"Vizuri. Wewe ndiye unashughulika na mambo ya Ukombozi wa Kusini mwa Afrika Wizarani kwenu", Willy aliuliza.

"Ndiyo", alijibu Kadima.

"Siku chache zilizopita Mkuu mmoja wa vyama vya wapigania Uhuru Kusini mwa Afrika aliuawa mjini hapa sijui kama una habari hizi?" Willy aliuliza.

Jasho jembamba na baridi lilimtoka Kadima. Sasa ndipo alikuwa amegundua kwa nini amekamatwa na kuletwa hapa kwani asubuhi ile alikuwa amepata habari kutoka kwa Fernand wa Agence Sozidime kuwa kulikuwa na wasiwasi wa mambo, lakini alikuwa amemweleza ya kuwa wangezungumza baadaye.

"Siku za mwizi ni thelathini na tisa ya arobaini unakamatwa", Kadima alifikiria.

Willy alihisi kuwa Kadima alikuwa amegutuka kutokana na swali hili kwa vile aliliona jasho lililomtoka na jnisi mikono yake ilivyotetemeka kiasi cha kutoweza kushika glasi.

"Habari hizo ninazo, na hivi leo nimetoka mjini Lusaka kupeleka mizigo ya marehemu." Kadima alijibu taratibu.

"Kifo cha marehemu ni miongoni kati ya vifo vingi ambavyo vimetokea kwa wapigania uhuru katika nchi kadhaa za Afrika. Na kifo hiki ni cha pili katika Kinshasa kwa muda huu wewe ukishughulikia idara hiyo katika Wizara ya mambo ya nchi za nje. Sijui unaweza kutueleza ni nini chanzo cha mauaji haya?" Willy alimuuliza huku amemkazia macho.

"Siwezi kujua, polisi na idara ya upelelezi ndio wanajua," Kadima alijibu.

"Bwana Kadima sina haja ya kupoteza muda wako mwingi, hivi sina haja ya kuzunguka, au kusumbuana na huku mambo yanaeleweka waziwazi. Hivi nataka utueleze uhusiano ulionao kati yako na Mkurugenzi wa Kampuni ya Sozidime Agence au wenye magereji ya G.A.D. Papadimitriou, Baninga na Du Peuple", Willy alimuuliza.

Kadima alitetemeka kabisa, alitambua kuwa huu ndio ulikuwa mwisho wake na kwa sababu hakuwa mtu aliyezoea matatizo hivi hakuwa mtu mwenye moyo mgumu. Siku moja aliwahi kujifikiria kuwa kupenda pesa kulikuwa kunampeleka mbali. Alianza kukumbuka miaka mitatu iliyopita simu ya Pierre Simonard ambaye alikuwa ameunda urafiki kutokana na kupeleka gari lake kwenye gereji yake. Pierre alimuomba waonane Hoteli Intercintinental jioni hiyo kama yeye akikubali. Jioni ile walipoonana, Pierre alikuja na mtu mwingine aliyemjulisha kwake kuwa alikuwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Agence Sozidime.

Ni jioni hiyo ambapo uhusiano kati yake na Fernand ulipoanza. Na tokea hapo ndipo walipomshawishi na kumfanya kibaraka wao wa kuweza kuwapasha habari zote juu ya wapigania uhuru. Alikuwa amelipwa pesa nyingi sana na sasa hivi alikuwa kati ya maafisa tajiri sana katika Zaire. Alikuwa na pesa chungu nzima huko Geneva, na alikuwa na majumba na hoteli kubwa huko Paris. Sasa leo maji yalikuwa yamemfika shingoni, kwa sababu alikuwa hajui watu hawa wanajua kiasi gani, na kwa sababu alikuwa anaogopa kufa, na kwa vile alitambua vijana hawa lazima ni wapelelezi aliamua kuwaeleza ukweli. Lakini kabla ya hapo alitaka kujua ki ukweli huyu kijana ni nani.

"Kijana umeniuliza swali la maana kabisa. Lakini kabla sijakujibu naomba kitu kimoja unieleze wewe ni nani na unawakilisha nini. Halafu mimi nitakueleza kila kitu bila kuficha. Nimechoka kukaa na mzigo huu, moyoni mwangu, na kama wewe ndiye mtu mwenyewe unayefaa nikueleze nitakueleza. Lakini kwanza nieleze wewe ni nani?" Kadima alieleza. Willy alijua mtu huyu alikuwa anazungumza ukweli na alijua ataeleza ukweli akijibiwa swali lake. Maana Willy alikua ameishaona watu wengi wa namna hii kutambua kama mtu huyu atasema ukweli au vipi. Hivyo Willy aliamua kumweleza yeye ni nani, na alikuwa amekuja hapa kufanya nini. Vile vile alimweleza mambo juu juu ya kuonyesha kuwa tayari walikuwa wamepata habari za kutosha juu ya 'WP' kwa hivi Kadima kuficha kusema ukweli kusingemsaidia neno.

"Lo poleni sana, sasa nisikilizeni kwa makini, nikimaliza kueleza mnaweza kunifanya lolote", Alianza Kadima. Kadima alieleza tokea siku ile Pierre alipomfahamisha kwa Fernand mpaka tukio hili la Mongo. "Mimi nimewasaliti ndugu zangu shauri ya pesa. Na katika nchi hii tuko wengi. Hiki kikundi cha 'WP' kimeotesha mizizi mirefu katika nchi hii na ina vibaraka wengi sana. Jambo hili limewezekana katika nchi kwa kufuatana na siasa ya nchi hii. Viongozi wote wa nchi hii wako tayari kufanya lolote ili kujaza tumbo lao. Mimi nimekuwa hivyo ingawaje jambo hili limekuwa linanikera moyoni. Sasa mnaweza kunifanya mnavyotaka mimi nimetubu yote niliyoyafanya nayajutia", Kadima alimalizia machozi yanamtoka.

"Lo masikini Afrika", Robert alilalamika.

"Tamaa ya viongozi ndiyo inaiangamiza Afrika. Mpaka hapo tutakapopata viongozi wenye kuipenda Afrika kwa dhati na siyo matumbo yao ndipo Afrika itakapoendelea", Willy alisikitika.

"Ni viongozi wachache wanaoipenda Afrika kwa dhati" Kadima alithibitisha.

"Kwa sasa hivi bwana Kadima utakaa hapa mbapa hapo tutakapokuruhusu. Tutakupa mwanya upige simu nyumbani kwako uwaeleze umepata safari ya ghafla. Tutakata shauri juu yako baadaye", Willy alimweleza Kadima.

Kadima ambaye roho yake ilikuwa imechoka kabisa alijibu, "Lolote mtakaloniambia, nitafanya ili mradi tu mtakapomaliza kazi zenu mnisikilize mambo yangu, Fernand na Pierre ni watu wabaya sana ndio wamenifanya mimi nikatumbukia katika maovu haya, mkiwakamata wapeni salamu zangu", Willy alimuongoza katika chumba kimojawapo baada ya kupiga simu na kumfungia ndani. Chumba hiki kilikuwa kidogo na dirisha dogo ambalo Kadima asingeweza kupita.

Robert alimwita Willy akamweleza, "Unajua nilitaka kusahau, Nilipata habari kutoka kwa Chifu anaeleza kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ukombozi ya OAU anaingia mjini hapa leo jioni. Ameeleza sisi tuendelee kama kawaida yeye anakuja na mipango kamili."

"Ahaa vizuri, kama akitutaka atatujulisha, nafikiri Chifu atakuwa amemweleza jinsi ya kutupata. Sasa hivi tuwangojee akina Ozu, tupange mipango ya leo jioni". Willy alieleza.

ITAENDELEA 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU