KIKOSI CHA KISASI

SURA YA KUMI 

MAPAMBANO BADO YANAENDELEA 


VII

Ilikuwa saa kumi na nusu Ozu alipowasiri nyumbani kwa Robert. Alipoingia aliwakuta Willy, Robert pamoja na msichana mmoja mzuri sana ambaye alitambua kuwa msichana huyu atakuwa ndiye Tete. Alimwangalia Willy na Robert machozi yalianza kumtoka tena, mara Willy na Robert wakatambua kuwa Kofi ameuawa. Robert alikimbia akaweka Whiski ndani ya glasi akampa Ozu ambaye alikuwa bado machozi yanammiminika.

"Tueleze imetokea vipi?" Willy alimwambia.

Ozu alikunywa glasi yote ya Whiski kwa mara moja halafu akawaeleza ilivyotokea, "Kofi amekufa mbele ya macho yangu mimi ninaona hivi hivi, Watu hawa ni wanyama watakufa kwa mkono wangu, Mungu anisaidie," Ozu alimalizia machozi yalianza kumtoka tena.

Willy alitambua uchungu Ozu aliokuwa nao akamwambia, "Ozu, hata sisi jambo hili limetushitua sana, sasa lililopo ni kutulia na kupanga jinsi ya kupambana na watu hawa," Willy alieleza taratibu.

Tete aliyekuwa amekaa pembeni kidogo alimwambia Ozu na ghafla naye akaanza kulia. Jambo hili lilimshitua Ozu na kumfanya atulie na kuelekea maliwatoni.

Mimi sasa namchukia Muteba na wenzake kiasi ambacho sijawahi kumchukia mtu maishani mwangu. Tokea sasa mimi nitachukua nafasi ya Kofi," Tete alisema bila kutania.

"Kazi hiyo haikufai mama, kazi uliyokwishafanya inatosha kabisa "Willy alimjibu.

"Mimi najua kitu nitakachowasaidieni. Mimi ni dereva stadi sijui kama kati yenu kuna dereva kama mimi. tafadhali sana msiniache mtakapokwenda kwenye mapambano ya leo. Tafadhali naomba mniridhishe nafsi yangu. Kule kuwaendesha tu nitajiona nimelipa deni kubwa kwa Mwadi, maana ni mimi niliyefanya akina Muteba wamfahamu. Hivyo Willy mpenzi usiniache," Tete aliomba akaanza kulia tena.

Ozu aliporudi kutoka maliwatoni alikuwa na hali nzuri kidogo. Alipofika alianza kuwaeleza plani yote ya gereji Du Peuple na jinsi alivyokuwa amefikiria wanaweza kuiingilia.

"Hata wakiwa watu hamsini, tukiwashambulia hivi tunaweza tukawapenya, ili mradi tu, tuwe na silaha za kutosha. Mimi naona 'machine gun' na bastola tulizonazo zinatosha kabisa," alimalizia Ozu. Willy naye alimwelezea Ozu juu ya Kadima. "Na jambo jingine ni kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ukombozi ataingia hapa usiku", Willy alimweleza.

"Nafikiri atafika wakati unaofaa kabisa, maana leo mimi nataka kuona mwisho wa watu hawa," Ozu alisisitiza. Waliendelea na mipango ya siku ile na mwishowe hata ombi la Tete lilikubaliwa.

"Yeye anazifahamu ofisi za Sozidime vizuri sana hivi anaweza kuwa wa msaada sana kwetu ingawaje ni jambo la hatari", Ozu alisema.

"Mimi siogopi hata kidogo hiyo hatari nataka niipate. Mimi naomba mnihesabu kama mmoja wenu," Tete alizidi kuomba. Baada ya kukubaliwa. Willy na Tete waliondoka kwenda chumbani ambako Willy alikuwa analala. Huko alitoa silaha zake huku akiwa anaongea na Tete, alizitia mafuta. Robert na Ozu nao walishughulikia silaha zao kuziweka tayari.


 ITAENDELEA 0784296253

Comments

Post a Comment

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU