KIKOSI CHA KISASI

SURA YA KUMI NA MOJA

USHINDI NI DHAHIRI

I

Ilikuwa saa nne za usiku na hapo gereji Du Peuple huko Limete kulikuwa na pilika pilika nyingi sana. Kundi zima la 'WP' lilikuwa limewasili isipokuwa Muteba. Pierre alizunguka kila sehemu kukagua ulinzi ulivyokuwa umepangwa. Alikuta kila mtu ameshika nafasi yake. Baada ya kuridhika na ulinzi uliopangwa alirudi ofisini mwake ambamo Jean na Papa walikuwa wanamsubiri.

"Muteba amepatwa na maafa ama vipi?" Pierre aliuliza.

"Sijui, Patron, alikuwa ameniambia kuwa atakuwa hapa kabla ya saa tatu lakini ninashangaa mpaka sasa bado hajafika," Alijibu Papa. Alipomaliza kusema hivyo tu walisikia mlango unagongwa halafu ukafunguliwa na Muteba akaingia. Wote wakapumua walipomuona. Muteba alikuwa amechelewa kwa sababu alipokuwa ameachana na wenzake baada ya shambulio lile la Hoteli Intercontinental, alienda moja kwa moja nyumbani kwake na kubadili nguo. Baada ya kubadilisha nguo aliondoka kwenda nyumbani kwa Tete ambako alitarajia kumweleza mipango ya kuondoka naye kama BOSS ilivyokuwa imewaletea habari. Alipofika nyumbani kwa Tete hakumkuta. Akaanza kumtafuta kila mahali alipofikiria kuwepo asiweze kumuona. Jambo hili lilikuwa karibu limtia Muteba wazimu. Alitumia zaidi ya masaa manne akimtafuta Tete bila kumuona kabisa mwishowe akajikuta ameishachelewa kufika gereji Du Peuple kama alivyokuwa anatakiwa ndipo akaondoka na kuja moja kwa moja gereji Du Peuple. 

Wenzake walipomwangalia walijua kulikuwa na kitu kinamsumbua rohoni. "Vipi, mbona hivi?" Pierre alimuuliza bila kuficha jinsi alivyokuwa amemtafuta Tete. "Sahau hayo mambo ya mwanamke tukimaliza shughuli hii salama, mambo haya yatanyooka tu. Bila shaka anashughuli zake" Pierre alimshauri. 

"Huenda huyu Willy amemkamata baada ya kujua kwa kikamilifu juu ya uhusiano wangu na wake", Muteba alilalamika.

"Achana na mawazo hayo, sasa hivi tuna kazi muhimu kuliko kufikiria matatizo ya mwanamke." Pierre alisema kwa ukali. Muteba alijigundua kuwa alikuwa kweli amefanya kosa la kikazi kuwa na mawazo mengine wakati mbele yao kuna kazi muhimu kabisa. Hivi alijisahihisha akasema. "Samahani Patroni, tuendelee".

Pierre alieleza tena ulinzi ulivyokuwa umepangwa na wote wakaridhika nao kabisa. "Vijana tayari, wameishashika sehemu zao," alisema akimwangalia Muteba.

"Nimewaona wakati naingia, hakika ulinzi umepangwa vizuri kabisa". Muteba alikubaliana. Papa ataongoza ulinzi wa mbele, Jean utaongoza wa nyuma na Muteba utaongoza sehemu zilizobaki," Pierre aliwaeleza. "Sasa twendeni wote tukakague sehemu zenu, na ikiwa kuna marekebisho turekebishe halafu tuwangojee washenzi hawa kama watathubutu kuja," Pierre alieleza.

ITAENDELEA 0784296253

Comments

Post a Comment

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU