RAIS MAGUFULI KUTEUZA WAPINZANI ZAIDI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli (pichani kulia) amesisitiza kuwa ataendelea kuteua viongozi ‘wenye akili’ kutoka vyama vya upinzani kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya Taifa na kwamba uteuzi wake hautaangalia kabila wala dini. Rais Magufuli ameyasema hayo wakati wa ziara yake mkoani Tabora wakati akihutubia wananchi siku ya mwisho ya ziara yake ya siku tatu mkoani humo, ambapo alizindua mradi mkuwa wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda miji ya Tabora, Igunga na Nzega, barabara za lami za Tabora - Nyaua na Tabora Nzega. 

Kauli hiyo ya Rais Magufuli inaweza kutafsiriwa kuwa ni majibu kwa baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani kuhoji kuhusu uteuzi wa viongozi, wakieleza kuwa wanaoteuliwa si wapinzani halisi. Tayari Rais, alimteua aliyekuwa mshauri wa ACT- Wazalendo, Profesa Kitila Mkumbo kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji huku pia akimteua Mwenyekiti wa Chama hicho, Anna Mghwira kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro. 

Mara kadhaa Rais huyo wa Awamu ya Tano amekuwa akiwasifia viongozi na makada wa vyama vya upinzani, akiwamo aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila. Juzi akiwa Nguruka, mkoani Kigoma, Rais Magufuli alimsifia Kafulila kwa ujasiri wake wa kuibua sakata la uchotwaji wa mabilioni ya fedha kwenye akaunti ya Tegeta Escrow, huku Kafulila mara kadhaa akinukuliwa na vyombo vya habari akieleza kuwa akiwa mbunge huku Magufuli akiwa Waziri alimtaka asichoke kuzungumzia sakata hilo kwa maelezo kuwa ni dili. 

Kitendo cha Kafulila kufananishwa na tumbili na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema alipoibua sakata hilo bungeni, kilionekana kumuudhi Rais ambaye juzi alibainisha kuwa waliomwita Kafulila tumbili, wao ndio tumbili zaidi. Lakini jana huku akionekana kukubali baadhi ya uwezo na utendaji wa makada wa vyama vya upinzani, alisema: 

“Nitaendelea kuchagua wapinzani wenye akili kwa kuwachomoa, wale nitawaacha kwenye vyama vyao, Watanzania wanahitaji maendeleo, wanahitaji barabara, maji na dawa,” alisema Magufuli. Rais Magufuli alisema hakuna ukabila nchini na kusisitiza kuwa kila mwenye uwezo ana haki ya kupewa nafasi ya kuongoza, kufuatana na misingi iliyowekwa na Rais wa Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere. 

Alifafanua kuwa hadi sasa kuna makabila 123 yanayoishi bila ubaguzi huku akibainisha kuwa kupandikiza dhana ni kutaka kupinga juhudi za kujenga maendeleo. Kuhusu amani Katika hotuba yake, Rais Magufuli alisema kuna anayevuruga amani na kuonya kwamba mtu huyo siku si nyingi atakiona cha moto. Kuhusu kero za wananchi aliwataka viongozi wa ngazi zote kutatua kero hizo, badala ya kutatua matatizo yao binafsi, akiwataka kupanga wakati wa kusikiliza na kutatua kero hizo, huku akimwagiza Mkuu wa Mkoa huo, Aggrey Mwanry kushughulia kero zilizoandikwa na wananchi kwenye mabango waliyobeba kwenye mkutano huo, akiahidi kufuatilia kama zimeshughulikiwa. 

Aliwataka wananchi wa mkoa huo kuacha kuendekeza uchama bali washirikiane kuiletea nchi maendeleo bila kujali wanatoka chama gani, cha siasa kwani maendeleo hayana chama. Pia aliwataka wananchi waliojenga kwenye hifadhi ya Reli ya Kati wajiandae kuondoa kabla ubomoaji haujaanza akiwahadharisha kuwa endapo watafungua kesi ya kupinga kuhama na Serikali ikishinda watatakiwa walipie gharama za ujenzi.

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU