KIKOMO

SEHEMU YA PILI

Niliinua simu kumuita Katibu Wangu.

"Luiza, njoo.

Luiza alikuja mara na kuuliza. 

"Niende sasa? Saa saba unusu sasa ingawa nimechelewa naweza kuwabembeleza wakamtibu."

"Mimi sikukuita kukupa ruhusa ila kukueleza kuwa leo hatutoki kwa saa za kawaida, ipo kazi kubwa sana ambayo inanikabiri. Kuanzia kesho, huenda sitakuwa ofisini kwa muda usiojulikana kwa hivi utakuwa na muda mrefu wa kuweza kumaliza shughuli zako binafsi maana sitaacha kazi nyingi".

"Kumetokea nini?"

"Nitakueleza nitakaporudi, sasa hivi hata nikikueleza hutaelewa. Mtume tarishi akuletee chakula chochote utakacho, mimi aniletee soda moja na sambusa nne".

"Asante".

Luiza aliondoka nilianza kupanga mawazo ya namna ya kulitatua tatizo hili nililokuwa limepewa. Akili yangu ilizunguka huku na huku kutafuta ufumbuzi, na kila wazo nililopata nililiandika mara. Niliandika na kufuta na kusahihisha mara kadhaa wa kadha. Hata hivyo mwishowe nilifikia wazo moja maalumu la kuzingatia.

"Soda yako hii".

Nilistuka.

"Asante binti, siku nikibadilishiwa katibu, mimi nitaacha kazi".

"Ahaa, ama kweli utaacha kwani ulimwengu wote katibu akufaae ni Luiza tu? Nafikiri mimi nitakuwa wa kwanza kuacha. hakuna msichana asiyenichukia hapa ofisini".

"Usijali. Sasa saa ngapi?"

"Saa tisa kasoro robo".

"Nitakuletea kazi baada ya dakika kumi na tano hivi. Kazi utakayopata jitahidi kuimaliza kabla ya saa tisa na nusu maana nina mkutano na Chifu saa kumi".

"Ama kweli leo iko kazi, kuna mkutano mwingine saa kumi?"

Alifungua mlango na kwenda ofisini kwake. Niliendelea kuanika mpango wangu kwa makini. Nilipofika hatua ya mwisho simu yangu ikalia.

"Hallo nani?" Niliuliza kwa ukali.

"Kuna bibi kwenye simu" Luiza alijibu kwa woga, maana alijua nimeudhika.

"Hallo nani?"

"Ndiyo saa nane na dakika thelathini na tano juu ya alama ya kikwenu hii! Una maana gani ya kuniweka mpaka dakika hii huku ukijua huji!" Didi alijidai kufoka katika simu.

"Didi mpenzi samahani sana. Nimepata kazi muhimu sana ya haraka sana hata nimeshindwa kutimiza ahadi yangu."

"Mimi najua hunijali hata kidogo, ungekuwa unanijali ungeweza hata kunipigia simu kunieleza yote hayo ili nisikungoje".

"Si hivyo Didi. Wewe wajua kabisa kuwa nakupenda sana. Ni kazi iliyonitinga hata nisipate wasaa wa kukuona. Hata hivyo nitafika, ningoje mnamo saa moja hivi, tafadhali kwaheri".

Nilikata simu kabla hajaaga. Hii kazi yangu inamfanya mtu kuwa kama mtumwa, hata wakikwambia baba yako kafa yakupasa umalize kazi kwanza ndipo uende kwenye kilio. Niliendelea na kazi na baada ya kumaliza nilimpelekea Luiza.

"Piga nakala tano".

Mnamo saa kumi na dakika tano niliingia ofisini kwa Chifu. Maselina alikuwa anapiga chapa.

"Wamo ndani?" 

"Wamo wanakusubiri".

Nilifungua mlango na kuingia ndani. Niliwakuta Chifu, Mkuu wa Polisi na wageni wengine.

"Habari za mchana?" Niliwaamkia.

"Nzuri", walijibu kwa pamoja.

Niliwagawia nakala za mawazo yangu ya awali. Katika taarifa yangu hiyo kitu kilichosisitizwa ni misaada maalumu niliyohitaji na ushirikiano wao wakati nikifanya upelelezi. Wote waliafiki na nikaachwa niendelee na shughuli hiyo. Ilikuwa sasa yapata saa kumi na mbili nilipowaaga.

Chifu aliita nilipofika mlangoni.

"Gamba".

"Naam".

"Tafadhali ujihadhari sana", alisema kwa huzuni.

"Bila ya shaka".

Chifu alikuwa akinipenda sana na kila nilipokuwa nikienda safari za hatari roho yake huhuzunika mpaka nirudipo. Nilimkuta Maselina akisoma gazeti. Aliponiona akatabasamu.

"Vipi? Safari tena?"

"Ndiyo binti".

"Safari salama urudi na zawadi".

"Kama nikirudi".

"Bila ya shaka utarudi. Tutakuombea kwa mola".

"Kwaheri ya kuonana".

Nilipofika ofisini kwangu, nilimkuta Luiza anapiga simu.

"Vipi unapiga simu?"

"Nampigia rafiki yangu huko Kurasini".

"Sasa binti mimi sintakuweapo nitaondoka saa tano kwenda Mwanza kama ulivyoona kwenye ripoti. Shughuli za hapa shughulikia kama kawaida. Tatizo lolote peleka kwa Chifu".

"Unategemea kurudi lini?" 

"Siwezi kujua, naweza kuchukua muda mrefu sana au mfupi sana. Na huenda nisirudi kabisa".

Akijidai kusikitika. 

Ukisema hivyo basi utatufanya wenzio tukonde bure kwa wasiwasi".

Baada ya kuagana na Luiza nikaondoka kwenda kumuona Didi. Didi ni mpenzi wangu wa muda wa miezi sita akiishi katika ghorofa za huko Ilala. Ni mzuri kwa umbo na pia mawazo na mwenendo wetu unapatana. Amehitimu na kupata shahada ya digrii katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakati huo alikuwa akifanyakazi katika Shirika la Bima la Taifa kama Afisa Maslahi na ulikuwa ndio mwaka wake wa kwanza wa kazi. Nilipofika huko nilisimamisha gari langu la kikazi nje, kisha nikapanda ngazi kwenda kwenye ghorofa yake kumbe Didi alikuwa ameniona nikija na kabla sijabisha alifungua mlango.

"Karibu, wa ubani."

"Asante".

"Ndiyo ukanifanyaje leo?"

"Haya basi yamekwisha!".

"Binti nasikitika kukueleza kuwa nitakwenda safari usiku huu. Na safari yenyewe ni ya kikazi na ya lazima."

"Safari zako haziishi mimi bado sijakaa nawe safari! Utajuaje mapendo yangu? Maneno yangu? Wasiwasi wangu! Mbona hivi Willy?"

"Tuliza roho yako ya Mungu mengi siku moja utapata muda mrefu mpaka utachoka."

"Nilikuwa na mambo ya kukueleza lakini sasa naona huna nafasi hata kidogo, ukirudi nitakueleza. Utarudi lini?"

"Inategemea na kazi itakapokwisha."

"Unaenda wapi?"

"Mwanza".

"Willy, nitapungukiwa na mtu! Sijui itakuwaje wakati huu ambao hutakuwapo. Mazoea kweli ni adhabu."

"Uwe na moyo mgumu, nitarudi karibuni."

"Nasikia wivu pia, huenda ukaonana na wasichana wengine huko." 

"Huniamini, Didi? Unanisikitisha sana!"

"Si hivyo Willy, nakupenda mno ndiyo sababu nakuonea wivu." 

Didi alinishika mkono na kunivuta na kunikumbatia. Damu yangu ilikimbia upesi upesi lakini nikajikaza roho na kumsukuma. Didi alikuwa ameng'ang'ania shingoni mwangu.

"Nenda binti, nitachelewa!"

"Haya baba kwaheri." Alisema na huku machozi yakimtoka.

"Hunitoi hata nje!"

"Hata"

Akilia. 

Kwa uchungu nikatoka. Nikafunga mlango wake kwa nguvu nikaondoka. Nilikwenda kwanza kwa daktari anipe mahitaji yangu muhimu kwa kazi kubwa ya upelelezi wa wizi wa almasi.

ITAENDELEA 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU