KIKOMO

SEHEMU YA NNE

Nilitaka kuwahi kabla ya saa sita. Niliingia ndani ya gari nikafunga mkanda tayari kwa kuendesha mwendo wa kasi sana. Mnamo saa tano na dakika ishirini nilikuwa nimefika kwenye njia panda ya kwenda Mwadui na Songwa, lakini sababu nilifikiria kwamba sitaweza kurudi na kulala Mwanza nilikata shauri kwenda Maganzo nikalipie mapema chumba cha kulala katika nyumba ya wageni.  

Nilipoingia Maganzo nikazungukazunguka kidogo halafu nikakata shauri kupanga chumba katika nyumba na baa iliyokuwa ikiitwa MASWA. Nilipoingia hapo baa ilikuwa imejaa hivi hata nafasi ya kukaa haikupatikana ingawa nilikuwa na kiu sana ya bia nilijikaza nisitamani.

"Halo," nilimwita mwanamke mmoja wa baa.

"Unasemaje?".

"Nataka chumba cha kulala".

"Subiri".

Baada ya muda mfupi akarudi.

"Kipo chumba kimoja tu, kina vitanda viwili kwa shilingi sitini tu". 

"Sawa tu".

"Haya kalipe pale kaunta kwa yule mama mnene. Una mzigo?"

"Ndiyo, ni mfuko mdogo tu".

"Lipa halafu nitakuonyesha mahali pa kulala".

Nililipa na huyo mama akanionyesha chumba.

"Vyumba vyetu vizuri sana. Vitanda havipigi kelele", alieleza kwa tabasamu.

"Safi sana".

"Wewe unatoka wapi?"

"Mwanza".

"Unashughuli hapa?"

"Bila ya shaka, mtu haendi mahali bila ya shughuli. Lakini nataka kwanza kwenda kumuona rafiki yangu katika Baa ya Bantu".

"Tutaonana ukirudi".

"Asante".

Baada ya kupata chumba nilikifunga nikaondoka na kuingia ndani ya gari. Nilipoingia Songwa Clab ilikuwa saa sita kasoro robo. Kulikuwa na watu wengi, lakini kulikuwa na nafasi. Sikutaka kukaa chini kwenye meza maana ningeonekana mgeni na ningeweza kufahamika upesi.

"Halo, nipe bia baridi", niliagiza.

Bia yangu ilikuja nikaendelea kunywa. Niliangaza macho kwa chati baa nzima ili niweze kumuona mtu ambaye ana hali ya kumsubiri mtu lakini sikuweza kufanikiwa. Ilikuwa inafika saa sita na bado sikuwa nimeona kitu.

"Wewe ni mgeni hapa siyo?" Mtu aliyekuwa karibu yangu aliniuliza.

"Si sana, kwanini unauliza?"

"Nyuso za hapa tunazijua, au umeletwa Mwanza kwa uhamisho?"

"Hapana, kwani wewe unafanya kazi Mwadui?"

"Hapana, mimi nafanya hapo Songwe Stesheni ya Reli."

"Mbona maelezo yako ni kama karibu kila mtu wa Mwadui unamfahamu?"

"Si hivyo, maafisa wengi wa Mwadui huja kunywa na kutembea huku, tuseme maafisa wote wa Kiafrika wenye magari. Kule Mwadui hakuna wanawake, lakini hapa na Maganzo ndiko kwenye soko la watoto wa kike.

"Umekaa hapa Songwa kwa muda gani?"

"Lo, miaka kumi na miwili sasa. Toka nimemaliza darasa la nane nikajiunga na Reli ya Afrika Mashariki. Baada ya kutoka kwenye shule yao huko Nairobi nikaletwa hapa kama karani wa stesheni na leo niko hapa naitwa kama Stesheni Masta. Kwa hiyo Songwa, Mwadui na Maganzo nazijua kama kiganja changu".

"Miaka kumi na miwili, kweli umekaa."

Niliagiza bia zingine mbili, moja kwa huyu mtu. Bia zilipokuja huyu mtu akanishukuru sana.

"Asante sana, hapa watu hawanunuliani bia. Asante sana".

"Usijali".

"Ulisema unaitwa nani?".

"Mimi naitwa Mark, na wewe?"

"Abdul".

"Umetokea wapi?"

"Mimi nakaa Mwanza".

"Aisee". 

"Ilikuwa sasa saa sita na robo na kulikuwa hakuna mabadiliko ya hali.

"Wanafunga saa ngapi siku hizi?"

"Kwa kawaida ni saa sita lakini wakati mwingine mpaka lyamba 

Mara simu ikaanza kulia hapo kaunta. Akaipokea mfanyakazi wa kaunta. Baada ya kuzungumza kidogo akaita.

"We Mwenentumba kamwite Mzee Reuben kule ndani simu yake toka Mwanza.

Nilijisikia moyo wangu unapiga haraka haraka. Muda si mrefu kabisa. Alizungumza kwa muda mfupi akaweka simu chini huku amekunja uso akarudi huko ndani. 

Huyu sehemu yote hii huitwa Pweke. Ni mtu hatari sana kuna tetesi kuwa anafanya magendo ya almasi ya hali ya juu. Polisi inasemekana wanamtafuta wameshindwa. Na ukitaka kumjua sana maisha yako hayawi marefu sana. Ni tajiri sana ana malori sana huko Shinyanga, Maganzo, Dar es Salaam na Mwanza. Vile vile watu humwita Pweke kwa sababu ni mara chache unamwona katika kikundi cha watu wengine", alinieleza taratibu.

"Yeye hukaa wapi?"

"Anakaa Maganzo, Shinyanga, Mwanza na Dar es Salaam, huko kote anakaa ana majumba lakini mara nyingi yuko Maganzo.

"Huenda basi nimemwona Mwanza".

"Bila shaka," Abdul alijibu. Hali yake ilionekana ni ya kulewa. "Tena nasikia yeye huwa anatumia dawa kuingia na kutoka Mwadui kuchukua almasi", aliendelea kueleza.

"Watu toka Afrika Mashariki nzima wanaoshughulika na magendo ya almasi nasikia wanamfahamu sana. Lo, ngoja ninyamaze nisije nikasikika nasema juu yake, maana nasikia ana masikio zaidi ya serikali. Polisi wenyewe tu hawathubutu kumgusa".

Niliagiza pombe zingine.

"Lete pombe".

"Loo, hakika nimefurahi sana, kaka wewe ni mtu mkarimu sana. Bahati mbaya mwezi umeniendea vibaya, miye ningekualika uje tunywe tena kesho, lakini nilikuwa na shilingi ishirini tu na nimeshamaliza. Hawa watu wa hapa hawathubutu kukopesha hata sisi wanywaji wa kila siku".

"Usijali, siku nyingine utajaaliwa."

Maelezo ya Abdul yalikuwa yamenisaidia sana. 

"Mtu huyu ni wa ajabu sana. Ana dawa zinazoweza kusababisha kifo ana kujua mtu yeyote anavyomuwaza", alinieleza. Polisi akimfuatafuata anaweza kupata ajali akafa, au akafukuzwa kazi. Huenda hivi ninavyosema anasikia."

"Hawezi. Mbona una woga hivi".

"Wewe siyo mwoga? Sema baya lolote juu yake hapa Maganzo kama hatutakusikia umekufa kesho asubuhi. Wanawake wote Maganzo anawajua. Inasemekana anawaajiri wampe habari za wageni wote wanaoingia. Yeye huwalipa ujira wa kuwaridhisha hivi kwamba wasieleze habari hizi kwa mtu yeyote, ila Reuben. Askari kanzu wote wanaokuja kupeleleza habari za hapa hufa. Nimekaa hapa miaka kumi na nimeshuhudia wakifa. Wanawake wote sehemu hii ni wapelelezi wake. Lolote utakalosema litafika kwake. Sisi tunamwogopa mno," alimalizia na kisha akanywa matone ya mwisho ya bia yake katika glasi.

"Kunywa nyingine".

"Hapana, nimelewa anaenda".

"Unakaa wapi?. Nitakupeleka."

"Usijali, nakaa hapo mbele kama kilomita mbili tu kuelekea njia panda, lakini kwanza napita kwa rafiki yangu hapo karibu.

"Haya kwaheri nikipata muda nitakuja nikuone hapo stesheni kesho.

"Bila ya shaka karibu. Mara kwa mara urafiki huanzia kwenye tungi".

"Na kweli, basi tutaonana kesho".

Tulipeana mikono Abdul akaondoka. Ilikuwa saa saba kasoro robo hivi nikaagiza bia nyingine ya haraka haraka nielekee zangu Maganzo. Niliyokuwa nimeyapata yalinitosha kabisa ilinibidi kuzicheuacheua habari hizi kulingana na kazi niliyopewa kuwafichua na kuwakamata maharamia wa magendo ya almasi.

Wakati namalizia bia yangu ya mwisho. Mzee Reuben kama anavyoitwa alitoka ndani akamuaga mfanyakazi wa kaunta. Akaondoka kwenda zake. Nilipogeuka nikaona watu wamebaki wachache sana na kwenye kaunta tulikuwa tumebaki wawili tu.

Nilimaliza bia yangu nikamuaga mfanyakazi wa kaunta. Nikaenda zangu. Reuben alikuwa keshakwenda, maana hakukuwa na gari hapo nje. 

Mawazo yangu yalikuwa mengi sana juu ya Reuben, Busy na kundi lao, nilitia gari moto kuelekea Maganzo. Nilipokaribia njia panda kwa mbele niliona kitu kimelala barabarani. Kwanza nilifikiri kwamba ni mbwa amekanyagwa lakini niliposogea karibu nikaona ni mtu. Niliposegea karibu zaidi nywele zangu zikasimama. Ni Abdul! Nikafunga breki bastola yangu ndogo nikaibana kwenye kiganja nikiwa tayari kwa lolote. Nilitelemka kwenye gari. Nilipomfikia nilikuta bado hajakata roho. Moyo wake ulikuwa unagonga kasi. Alionekana kama mtu aliyepigwapigwa sana au kugogwa na gari. Sikuweza kuona damu mahali alipolala.

"Hapo hapo! Nyama we!" sauti ilisikika mara tu nilipoinama ili nimwinue.

"Huyu mtu anakufa, niacheni nimpeleke hospitali", niliwajibu kwa ghadhabu.

"Wewe je? Hujihurumii mwenyewe kwanza?"

"Mniue basi mnangoja nini?" niliwajibu kwa hasira.

Niliamini kwamba saa yangu nami ilikuwa imefika, kwa hiyo kuomboleza kusingenifaa. Ilikuwa kufa na kupona. Bila ya kukawia nilifyatua bastola yangu na risasi zikawapata wawili barabara. Mwenzao wa watatu akakimbia na hamsini zake. Ndipo nikapata nafasi ya kumnyanyua Abdul na kumweka garini.

Maharamia hao wawili walikuwa wakitweta chini - mmoja wao alikuwa na bastola nayo ilidondoka kando. Niliiokona sikuwa na haja ya kuwachunguza bali niliwaburura hadi kando ya barabara na kuwaacha wafe huko. Kama kuna mtu atakayewaona bahati yao kwani palikuwa na majani marefu sana.

Abdul alikuwa hajakata roho. Niling'oa gari kutoka hapo kuelekea Shinyanga umbali wa kilomita thelathini hivi. Nilienda kasi sana hadi hospitali.

"Ndugu, nimemleta mgonjwa mmoja mahututi ndani ya gari", nilimweleza muuguzi.

Yeye haraka haraka akisaidiwa na mfanyakazi mwenzake walichukua machela na kumbeba Abdul. Machela ilisukumwa mpaka kwenye chumba ambacho kilikuwa na daktari ambaye alionekana kama alikuwa akisinziasinzia. 

"Vipi? Ajali ya gari?" Daktari aliuliza huku akisogea kwenye machela.

"Hapana nimemkuta amelala kwenye njia panda ya Mwadui na Shinyanga. Nikatoka garini nikakuta amepigwa na bado anapumua kwa hiyo nikakata shauri kumkimbiza hapa hospitalini haraka iwezekanavyo".

"Lydia tafadhali mpeleke chumba cha uchunguzi, tayarisha vifaa vyote haraka mimi najaza cheti chake".

Lydia na John walisukuma machela kuelekea kwenye hicho chumba.

"Unafikiri atapona?" Nilimuuliza daktari kama mtoto mdogo.

"Sijui, inategemea amepigwa kiasi gani. Ukifika asubuhi tutafahamu, kwani unamfahamu?"

"Hapana. Nimemwokota tu. Hata hivyo ni mgonjwa wangu sasa".

"Sawa, umepiga ripoti polisi?"

"Bado. Nilikuwa sina budi kwanza kumleta huku maana mtu mwenyewe taabani sana"

"Sawa, jina lako nani?"

"Mark Buhulula".

"Unakaa wapi?"

"Mwanza".

"Kabila".

"Msukuma".

"Wa wapi?"

"Ntuzu".

"Haya asante sana. Utakuwa hapa Shinyanga muda?"

"Hapana, niko Maganzo".

Daktari akamtupia jicho na kurudisha mara. 

"Haya asante. Ukiweza kufika asubuhi tafadhali njoo unione nitakueleza hali ya mgonjwa wako. Mimi ninamaliza kazi saa tatu asubuhi".

"Nitajaribu kuwahi daktari".

"Haya kwaheri, asante sana".

"Kwaheri na nyinyi, asanteni sana".

Niliondoka moja kwa moja hadi Maganzo. Nilitaka kumpigia simu Chifu usiku huo, lakini nikata shauri nimpigie asubuhi. Mawazo ya visa vya usiku yalinisumbua sana. Nilifikiri kuu ya majambazi hawa pamoja na vifo vyote. Kule Abdul kunong'onezana nami tu tayari ilikuwa imeshafahamika kuwa amesema mambo mengi, na wakawa tayari kumwadhibu kiasi kile cha kumuua.

Ilionekana kweli kuwapo kwangu Maganzo kulifahamika na nilikwisha kuwa mashakani. Na lile jambazi lililokimbia huenda limepeleka habari za kufa wenzi wao kwa Pweke.

Nilipokuwa nakaribia Maganzo nikakumbuka maneno ya Abdul kwamba hilo jambazi Pweke limenunua wanawake wote wa mji kwa kuwafanya macho na masikio yake katika kupata habari zozote zile.

Maganzo ilikuwa tayari kimya. Mji mzima ulikuwa tayari umeshatulia sana. Mabaa yote yalikuwa yamefungwa kwa hiyo niliendesha moja kwa moja kuelekea Bantu. Nilipofika Bantu Bar nikaegesha gari langu vizuri nikaanza kufunga milango kama kawaida. Baada ya hapo nikatembea kuelekea mlango ambao nilikuwa nimeonyeshwa nipite nikikuta baa imefungwa. Huu mlango niliukuta wazi, nikaingia ndani.

Nilienda moja kwa moja mpaka kwenye mlango wa chumbani kwangu. Niliangalia vizuri kuona kama umewahi kufunguliwa, lakini haukuonyesha wasiwasi. Nilifungua mlango bastola mkononi na kuingia ndani. Nilipoingia tu nikasikia sauti. 
"Karibu ndani ndugu. Funga mlango na uwashe taa. Usilelte matata, kama hutaki kiadhirika".

Kwa kuwa kulikuwa na giza sikujua huyo mtu alikuwa peke yake au wengi. Nilikata shauri nifanye kama nilivyoagizwa. Nilirudisha bastola yangu mfukoni. Nikarudisha mlango na kuusingika. Nikawasha taa.

Ndani mlikuwa na watu watano. Mmoja wao alikuwa ameshika bastola imara na imeelekezwa usoni kwangu. Nilipowaangalia vizuri hao wengine kumbe nao walikuwa na bastola, wameelekeza kwangu.

"Kaa chini ndugu, usiwe na wasiwasi. Tungetaka kukuua usingefanya lolote, ungekufa tu".

Kulikuwa na meza ndogo na kiti. Nikakivuta nikaketi.

"Abdul ana hali gani?"

"Sijui, nilimwacha bado amezirai".

Nikamwangalia vizuri huyu mtu aliyeniuliza. Alikuwa kijana mwenye umri wa miaka ishirini na mitano hivi. Alionekana jasiri sana.

"Mimi nakuona wewe ni mtu jasiri sana, na ingawa nimeamriwa kukuua, nimeonelea kwanza nikupe onyo kama kawaida yangu niwaonyavyo kwanza wote waingiliao mipango yetu. Wengi nimewaonya, hawakusikia na wote wamefifia duniani. Ningependa na wewe uwe kwenye kundi hilo, kwa hiyo nakuomba uondoke sasa hivi baada ya sisi kuondoka, urudi zako Dar es Salaam. Mambo yaliyokuleta tunayajua. Mark Buhulula, na una bahati sana. Sasa hivi ungekuwa ulimwengu wa marehemu. Usipoondoka sidhani hiyo bahati itaendelea. Tatizo unalotaka kulitatua ni gumu mno. Linataka jeshi zima na si mtu mmoja. Saa tisa na nusu uwe umeshaondoka hapa mjini la sivyo usilalamike yakikupata".

"Nikikataa kuondoka je?"

"Kama wewe una akili naamini utaondoka, lakini kama umechoka na maisha baki. Tuone kama jua ya kesho litakukuta hai. Yaliyompata Mathayo umesahau, kwaheri ya kuonana kama umesahau. Twendeni zetu".

"Kwaheri, nitafikiria".

Bila kunijibu huyo kijana aliondoka huku akifuatwa na watu wake. Alinishangaza sana kwa utulivu wake na akaniogopesha vile vile. Nilibana mlango nikazima taa. Nilikaa kwenye kitanda nikifikiri. Nilifikiri kutimka niende zangu Mwanza halafu Dar es Salaam, lakini nikakumbuka kwamba nimetumwa kuja kufanya kazi. Nilikuwa nimekuja kuinua uchumi wa wananchi. Kwa hiyo nilikuwa sina budi kujitoa mhanga kama wenzangu walivyokuwa wamejitoa mhanga waliotangulia kabla yangu.

Baada ya mafikira haya nilikata shauri nisiondoke na nikae nione kutatokea nini. Kuja kunitisha nilijua lazima na wao 
wana wasiwasi. Hivyo nilichukua mfuko wangu nikavua nguo nikatengeneza kitanda kama vile mtu amelala. Nikavuta kiti nikaa karibu na mlango. Nilitoa bastola yangu tayari kwa matatizo yoyote. Nikasinzia kidogo kwa sababu ya uchovu.

ITAENDELEA 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU