KIKOMO

SEHEMU YA NANE

Nilipozinduka nikajikuta kwenye chumba kidogo, nikiwa nimelazwa kitandani na huku nimefungwa bandeji kila mahali nilipokuwa nimeumia na nilipoinua macho karibu yangu alikuwa ameketi msichana mrembo sana huku akitabasamu nikashangaa.

"Unajisikiaje sasa?" Aliniuliza.

Nikatabasamu.

"Mbele ya mtoto mzuri kama wewe nitashindwaje kujisikia vizuri".

"Watu wa hali yenu ni watu wa ajabu sana".

"Kwanini?".

"Hata hushangai umekujaje hapa?".

"Ili mradi nimetibiwa na msichana mrembo kama wewe, na unaniganga na hakuna watu wenye sura zilizokunjana wakiwa wameshikiria bastola, najua niko kwenye mikono mizuri".

"Ni kweli".

Nilijaribu kuinuka.

"Daktari amesema upumzike kwa muda mpaka upate nguvu".

"Tayari nina nguvu, sasa ni saa ngapi?"

"Saa saba unusu usiku".

Nikatambua kuwa nilikuwa nimezirai kwa muda wa masaa matano hivi na nikataka kujua nini kilikuwa kimenitokea muda wote huo ili niweze kujua nini cha kufanya maana hata hapa nilipokuwa sikujua ni wapi na huyu msichana sikujua ni nani.

"Wewe ni nani na hapa ni wapi?"

"Mimi naitwa Amanda Mwakasege, na hapa ni nyumbani kwa rafiki yangu, Songwe Madukani.

"Nani alinileta hapa?"

"Mimi na Patrick".

Moyo wangu ulishtuka kwa jina hilo.

"Yuko wapi?"

"Amerudi Maganzo na atarudi wakati wowote".

"Kwa hiyo nyinyi ndiyo mlioniokoa kutoka mikononi mwa Pweke?"

Bila shaka".

Hii ilinishangaza sana.

"Nafikiri uko tayari kunieleza juu yako mwenyewe na jinsi gani unahusika katika kesi hii, maana wewe hukuajiriwa pamoja na sisi. Vile vile jinsi gani mlijua nilipokuwa na vile mlivyoniokoa".

"Nitakueleza kwa ufupi ili uweze kujua mpaka sasa pilikapilika yako hii imefikia wapi".

"Asante, endelea".

"Mimi naitwa Amanda Mwakasege, kama nilivyokwisha kukueleza. Ni Mwandishi mahsusi wa Meneja wa Kampuni ya Mwadui. Utashangaa nimejiingizaje katika jambo hili au sivyo?".

"Nina mshangao mkubwa sana, maana ukiwa mwandisi halafu ujiingize kwenye jambo la hatari namna hii haieleweki."

"Kweli haieleweki. Mimi nilikuwa na mchumba wangu akiitwa Inspekta Joel Zonga, nafikiri uliwahi kumsikia?|

"Nilikuwa nimesikia habari zake ambazo zilitokana na kifo chake. Alipata ajali ya ndege iliyokuwa mali ya Kampuni Mwadui alipokuwa akisafiri kwenda Mwanza kikazi. Mpaka leo chanzo cha ajali hiyo hakikujulikana maana ndege ilipasuka vibaya mno. Polisi walikisia kuwa mlikuwa na bomu lililotegwa lakini hawakuweza kuendeleza upelelezi wao mbali".

"Ndivyo ilivyokuwa."

"Pole sana".

"Siku moja Joel alikuja nyumbani kwangu akiwa na mawazo mengi sana. Nilitengeneza chakula lakini hakuweza kula vizuri. nikajua alikuwa na kitu kilichokuwa kinamsumbua nilimdadisi sana mwishowe akanieleza. Alinieleza ya kwamba alikuwa hapendezewi na jinsi mambo yalivyokuwa yakienda hapo Mwadui na kwamba alikuwa ameamua kufanya uchunguzi madhubuti.

"Alinieleza kuwa alikuwa amefanya uchunguzi kiasi na kuona ya kwamba kulikuwa na mpango wa hali ya juu sana wa kuiba almasi toka Mwadui! Ila alisema kilichokuwa kinamkera ni kwamba angeweza kuwa hatarini.

"Alieleza ni nini kilichomfanya afikiri hivyo?"

"Alikuja kunieleza baadaye. Aliendelea na uchunguzi wake na hatukulizungumzia jambo hili tena. Baada ya miezi miwili hivi siku moja alikuja akiwa na hali isiyo yake ya kawaida. Nilipomuuliza alinieleza ya kwamba mambo aliyokuwa anafikiria ni kweli na sasa alikuwa hatarini.

Alinieleza kwamba alikuwa amekata shauri kunieleza jinsi mambo yalivyokuwa kusudi ikiwa jambo lolote likimpata siku moja anaweza akaja mtu mwenye kuweza kuendeleza upelelezi huu na habari hizi zingemsaidia sana. Nilimwambia asiseme hivyo, na siku hiyo alilia sana.

"Alieleza nini?"

Alinieleza kuwa maafisa wengi wa polisi wa chini wa hapo Mwadui walikuwa wamehongwa na kundi la majambazi ambalo lilikuwa linaendelea na kuendesha wizi wa hali ya juu wa almasi toka Mwadui na ndiyo sababu hali ya uchumi utokanao na machimbo hayo ya almasi ulizidi kwenda chini siku hata siku.

"Alisema kuwa hili kundi lilikuwa limepachika watu wake kila idara na kila sehemu zinazohusika na almasi. Na hawa watu ndio walikuwa wakitorosha almasi kidogo kidogo na kwa sababu polisi waliokuwa wanahusika wote wamehongwa na walikuwa wanawajua basi ilikuwa rahisi sana kwao kutorosha almasi.

"Alinieleza kuwa katika miezi hii miwili aliweza kukamata watu kama kumi ana kwa ana na almasi mkononi lakini alipoenda kupiga ripoti kwa maofisa wa juu waliweza kutaka hata kumgeuzia yeye kuwa ndiye mwizi. Hata akanieleza kuwa siku moja wamewahi kuficha almasi nyumbani kwake halafu kukafanywa uchunguzi zikutwe kwake lakini yeye alinong'onezwa kabla na rafiki yake mmoja na walipofika hawakukuta kitu.

"Kutokana na uchunguzi wake alikuwa amegundua kuwa kwa nje kulikuwa na mtu aitwaye Pweke, ndiye alikuwa mkubwa wa kundi na alikuwa mfanyabiashara wa hapo Maganzo. Kwa ndani mtu aliyekuwa akiongoza kundi Inspekta Mwandamizi Khamis Omari. Huyu Khamis ndiye aliyekuwa anapokea habari na ndiye aliyekuwa kiungo kati ya kundi la nje na la ndani. Vile vile kwa wafanyakazi wa idara zingine".

"Kwanini hakupeleka habari hizi kwa Mkuu wa Polisi wa Mwadui au Mkuu wa usalama?"

"Alisema alijaribu kupeleka kwa Mkuu wa Polisi, lakini alipuuzwa na kuelezwa kwamba alikuwa anaanzisha majungu jambo ambalo serikali haipendi hasa jeshini na kwa hivi angeweza kuchukuliwa hatua. Alipoona hivi akaonelea aendelee kufanya uchunguzi wake yeye mwenyewe sasa. Siku aliyokuwa amekuja kwangu na huzuni kunieleza mambo haya ndiyo siku aliyokuwa amekuja kwangu kunieleza kuwa amepata kitisho kutoka kwa mtu aliyekuwa akiitwa Elungata akisema asiingilie mipango yake la sivyo maisha yake yangekuwa mafupi sana".

Jina la Elungata mara moja nilikumbuka kwani marehamu Matayo Buluba alikuwa ameniletea barua kutoka kwa marehemu Jack Mbwile na hiyo barua ilikuwa na neno moja tu 'Elungata' Sasa nilianza kuona mwanga zaidi.

"Aliweza kuchunguza na kujua huyu Elungata alikuwa nani?".

"La hasha. Baada tena siku moja kwenye Mkahawa wa polisi hapo Mwadui alinieleza kuwa alikuwa amegundua tu ya kwamba Pweke siyo mkubwa kabisa wa kundi ila mkubwa alikuwa Elungata, lakini ajabu huyu Elungata hata hakuweza kupata fununu yake".

Wiki tatu zilizopita akaja siku moja kuniaga kuwa alikuwa anaenda Mwanza kuonana na Mkuu wa Polisi wa Mwanza ampe habari hizi kwa maana sisi tulikuwa tumekata shauri ya kuoana baada ya mwezi mmoja toka siku hiyo kwa hiyo asingekuwa na nafasi ya kuendelea na uchunguzi. Na siku hiyo alipoondoka ndiyo waliyomtega bomu katika ndege. Akafariki".

Alianza kulia. Nilimvuta na kuanza kumbembeleza.

"Basi, basi kifo ni mapenzi ya Mungu. Ni jambo la kusikitisha sana lakini kulizuia hatuwezi. Yeye alipangiwa na Mungu mwisho wake uwe huo. Ulikuwa mwisho wa fahari maana alikufa kwa sababu ya kupenda nchi yake na kwa kuitumikia vizuri. Maadui wa maendeleo yetu wamemuua. Kwa hilo linalotupasa mimi na wewe ni kuwafutilia mbali hawa maadui wa nchi yetu".

"Asante Willy lakini ni vigumu kusahau na vile vile ndiyo sababu nimejitoa mhanga wa kufa na kupona kusudi watu waliomuua mpenzi wangu Joel na wao watiwe nguvuni".

"Joel alikueleza haya yote kwa sababu alijua atakuwa hatarini na alifanya vizuri. Je umetimiza wajibu wako kwa mzigo aliyekuachia?".

"Nafikiri leo hii na dakika hii nimetimiza wajibu. Hata hivyo baada ya mazishi na matanga sikukaa bure. Uchungu niliokuwa nao ulifanya nami nianze uchunguzi wangu. Inspekta Mwandamizi Khasimu Omari ambaye ndiye bila shaka aliyepanga kuuawa kwa mpenzi wangu Joel alikuwa akitaka mapenzi nami siku nyingi. Niliporudi tu kazini baada ya matanga alianza kunifuatafuata".

..."Alinieleza kuwa ili niweze kusau mapema kifo cha ghafla cha mpenzi wangu ilinibidi nipate mtu wa kunifariji kwa sababu nilikuwa najua habari zake, wazo lilinijia kuwa ningeweza kupata habari za kunisaidia kuchunguza kifo cha mpenzi wangu joel".

"Kwa hiyo ukamkubali!"

"Nilimkubalia kwenye mdomo tu si rohoni".

"Sawa".

"Siku moja nilianza kwa kumsifu juu ya vile alivyo tajiri kuliko polisi wengine, jinsi alivyokuwa na akili kuliko polisi wengine na kadhalika. Nilimweleza kuwa ningejua kwamba yeye ana pesa hivyo hata nisingejisumbua kupoteza muda wangu na Joel. Nikamweleza kuwa ni bahati nzuri upande mwingine kwamba Joel amekufa. Hii ilimfurahisha sana akaanza kujitapa akanieleza kuwa yeye alikuwa tajiri sana na utajiri wake usingeweza kupungua kwani alikuwa ameishashika Mwadui nzima mkononi mwake."

"Siku hiyo nilimfanyia mapenzi ya kila aina mpaka akanieleza juu ya siri zake. Akanieleza baada ya muda si mrefu angeacha kazi na kunioa halafu tungeenda kuishi nchi za nje. Aliniambia ana almasi chungu nzima. Nikamkebehi ya kwamba mbona nasikia kwamba Pweke ana hela kuliko yeye. Akacheka na kusema bila ya yeye Pweke si kitu".

"Hakugutuka kuwa unamfahamuje Pweke?".

"Asingeweza, maana Maganzo nzima wanamfahamu Pweke. Ana pesa chungu mbovu. Wakati wote huu nikawa natafuta njia ya kujua mengi lakini sikuweza kuwa na bahati. Waswahili husema mvumilivu hula mbivu, kwa hiyo mimi nikaendelea kumganda nikisubiri bahati yangu huku nikimlaghai kwa mapenzi kwa kweli ya Mungu mengi jana ndiyo siku yenyewe.

"Jana alikuja nyumbani kwangu huku jasho likimtoka. Nikatengeneza chakula kama kawaida, lakini hakuweza kula na alionekana na wazo linalomsumbua au tuseme mawazo yalikuwa mengi sana. Nilimuuliza nini kilikuwa kinamsumbua. Hakutaka kunieleza. Nikazidi kumbembeleza. Nikambusu, nikamweleza kuwa matatizo yake ni yangu na mimi kwa vile nilikuwa nimekata shauri la kuolewa sikuona kwa nini anifiche jambo lolote hata kama ni kuua mtu.

"Mwisho akanieleza kuwa mpelelezi mmoja maarufu wa serikali kwa jina la Willy Gamba alikuwa ameanza kuleta matatizo. Nikamwambia mtu mmoja tu si kitu, hatamudu kufanya lolote, kwa hiyo asijali hata kidogo. Basi akafurahi akanishika akanibusu.

"Akanieleza kwamba ameonelea lazima achukue livu kesho yake maana tungeweza kuondoka ghafla kwa muda. Nilimwambia kwamba isingekuwa taabu. Moyoni nikajua nafsi yangu imefika ya kumtafuta huyu Willy Gamba ili nimweleze yote niyajuayo ili kwamba nitakuwa nimemlipizia kisasi mpenzi wangu Joel."

"Ama kweli umekuwa kiumbe wa ajabu! Umeweza kufanya yote haya kwa ajili ya mpenzi wako Joel basi".

"Nakwambia, watu hawajui. mwanamke akipenda kitu huvumilia sana usituone hivi!"

"Kweli nami nimeona kitu kiitwacho mapenzi ya kweli maana mtu kafa na bado anapendwa tu".

"Basi leo asubuhi nikaenda ofisini. Nikachukua livu, nikampigia simu sikumpata kwa simu ofisini wala nyumbani. Nikakata shauri kwenda nyumbani kwake sikumkuta lakini mimi nina ufunguo mwingine wa nyumba yake nikaingia ndani, nikaenda chumba cha kulala nikachukua bia, nikajilaza kitandani nikinywa huku mawazo yakinitembeatembea.

"Mnamo saa sita hivi nikasikia watu wanacheka ukumbini nikasikia mwingine akisema Willy kafa kifo cha kijinga sana cha kugongwa na gari moshi. Khasimu akajibu, ndiyo, sawa hiyo, hakuna hata cha kuuliza. Basi roho yangu ikafa kabisa niliposikia hivyo. Nikajua matumaini yangu yamekwisha".

"Naona nina maisha marefu," nilisema kwa furaha.

"kweli una maisha marefu. Khasimu aliponikuta chumbani akaja akanibusu. Nikamuonyesha karatasi zangu za livu. Akaniambia kwamba sasa hamna wasiwasi, tungepanga mambo yetu taratibu. Wakati bado tumekaa, simu ikalia. Alienda kuzungumza na nikasikia akisema, George, basi wamalizie mbali mbali na yeye halafu hana wasiwasi Ole yuko Mwanza, atamaliza tatizo hilo halafu akarudi".

"Na katika watu wanaovumilia wewe nambari moja!" Nilimpongeza, "Wanawake kwa kawaida wangekuwa wameisha ropoka".

"Kila nikimfikiria Joel, roho yangu inakuwa jasiri sana. Mnamo saa kumi na moja na nusu hivi simu ikalia. Khassimu alikuwa amelala akaamka na kwenda kuijibu. Nikasikia akisema kwa hasira, nini? Willy yuko hai? Willy au jina lake? Nani, Ole? Ole kafa! lo, mambo yameharibika. Washenzi hao Pweke hakikisha Willy akiingia Maganzo Bar, ndiyo hoteli yake, lazima auawe mara moja. Nani kakupa habari? Basi lazima atafikia Maswa Bar, ndiyo hoteli yake kama atakuwa kaondoka kule saa kumi na moja, saa moja hivi atakuwa Maganzo. Mtume Tausi saa moja pamoja na kundi, yeye ni mbovu sana kwa wanawake. Lazima akimuona tu Tausi hawezi kumwachia. Mpeleke kwenye banda mkiweza kumkamata, mwuweni huko huko. Mimi nitazungumza na mzee najua atakasilika sana. Tuonane kwenye chumba chetu Bantu. Wengine wote watafika saa nne usiku kwaherini!"

"Kisha akaja akaniambia, mpenzi fungasha nguo zako chache na zangu mimi nitarudi kwenye saa tano au sita hivi nina shughuli.

"Nikamwambia, hamna taabu. Alipoondoka tu na mimi nikaanza kutafuta njia gani ya kuwahi kufika Maganzo kabla ya saa moja niweze kukupa tahadhari. Nilitafuta gari mpaka kwenye saa moja ndipo nilipopata. Kufika Maganzo na kuingia Maswa Bar saa moja na nusu, na nilipoangaza angaza nikaona hakuna dalili ya mtu kama wewe. Nikajua tayari wamekuwahi. Nikajua wamekupeleka kwenye banda. Na banda mimi nililijua, nilishapelekwa na Khasimu, lakini kukufuata peke yangu ilikuwa haiwezekani. Nikatoka nje ya baa, nikaanza kulia. Bado machozi yananitoka nikaona taksi inasimama na anatoka mtu na mfuko. Moyo ukanieleza ndiye wewe, nikamkimbilia huyu mtu. Bila ya hata kuogopa nikamuuliza kama yeye ni Willy Gamba? Akashituka na kuniuliza, 'kwanini?' Nikamwambia wanakutafuta watakuua. Wanajua utakuja hapa bila ya shaka.

Alinivuta kando, kisha akanieleza kuwa yeye anaitwa Patrick na ni rafiki yake na Willy Gamba. amekuja kukutana na Willy hapo. Ndipo nikamweleza mipango yao yote. Akafungua mfuko wake, akatoa bastola mbili. Akazijaza risasi akaniambia nimuonyeshe hilo 'banda' lilipo. Basi nikampeleka mpaka kwenye banda. Hii nyumba inayoitwa 'banda' imejengwa mbali kidogo na nyumba zingine. Khasimu alisema hutumika kama kuna sherehe fulani ya vinywaji. Basi nikamleta na kumuonyesha nyumba akanipa mfuko na tukaanza kuinyemelea nyumba akiwa na bastola mbili tayari.

"Upande wa mlango wa kuingilia, tukamuona mtu na bunduki, Patrick akamnyemelea akampiga konde la shingoni, akazirai bila ya kutoa sauti. Mwingine alikuwa akiangaza upande mwingine, Patrick akamwahi na risasi lakini bunduki haikupiga kelele. Ndipo katika kusikiliza akasikia sauti inatokea kwenye chumba walichokuwa wanakutesa. Alipoangaza akaona dirisha juu kabisa. Akapanda juu kama nyani. Alipofika juu alipiga waya wa umeme na wakati huo huo alikuwa ameishawaona walivyokaa na wewe uliko kwa hiyo ilikuwa rahisi kuwawahi hao wenye silaha. Anasema usingejitupa na kiti wangeweza kukupata na risasi. Wale watatu wenye bastola wote amewaua. Pweke na Tausi wamekimbia. Basi Patrick akaniita, akakufungua, tukakubeba na kukuweka kwenye gari la Tausi. Patric akafungua boneti akaliwashia huko hadi tukafika hapa.

"Hiki ni chumba cha rafiki yangu, anafanya kazi stesheni ya reli hapa Songwa lakini yuko likizo. Tulienda kumtafuta daktari akaja akakutibu na akasema hukuvunjika chochote ila tu umepoteza damu nyingi. Akaomba upumzike mpaka kesho asubuhi utapata nafuu. Hivi ndivyo ambavyo tumeweza kuonana. Ni hadithi ndefu au sivyo?"

"lO, ama kweli ni ajabu na kweli. Sina budi kukushukuru sana"

"La hasha! usinishukuru. Nifanyalo ni wajibu wangu ili kulipiza kisasi cha Mpenzi wangu Joel!"

"Hakukueleza Patric yuko wapi?"

"Amewafuata Bantu ambako walisema wataonana"

"Ameenda pekee yake? Watamuua ni watu wabaya sana"

"Hapana, ameenda na mdogo wa yule daktari maana wao pia wanakisasi na Pweke maana alikataa kufanya mapenzi nao na huyu kijana ni Polisi wa relwe"

"Bado haitoshi lazima niwafuate"

"Una silaha? Silaha huna tena bado una maumivu. Wily usiende Patric na huyo kijana Mungu atawasaidia na watamudu"

"Silaha nitapata usijali lazima niwafuate.

Nikasikia sauti nje ya mlango wa chumba.

"Huna haja ya kuwafuata"

Jasho likatutoka wote.


ITAENDELEA 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU