HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

MAJESHI YA UGANDA YALIVYOINGIA KAGERA

MWAKA 1978, Majeshi dhalimu ya Nduli Idi Amin Dadaa wa Uganga, yalivamia Ardhi ya Tanzania, eneo la Mto Kagera, katika mkoa wa Ziwa Magharibi na kufanya uharibifu mkubwa wa mali na kuua wananchi wa mkoa huo, NYAKASAGANI MASENZA anasimulia kupitia vyanzo mbali mbali vya habari jinsi majeshi hayo yalivyoingia Tanzania na Amin kutangaza rasmi kuwa eneo hilo la Mto Kagera ni sehemu ya Uganda.

DAIMA Tanzania imekuwa mstari wa mbele kwa ukombozi wa Bara la Afrika, ikiwa miongoni mwa mataifa masikini zaidi duniani, lakini iliyojariwa viongozi wenye hekima, kuanzia muasisi wake Hayati Mwalimu Julius Nyerere, Rais wa pili Mzee Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete.

Busara za viongozi wa Tanzania zilianza kuonekana mwaka 1961, baada ya Mwalimu Nyerere kuwanasua watanzania kutoka mikononi mwa utawala kandamizi wa wakoloni, wakati huo pia akiwa tayari kuchelewesha Uhuru wa Tanganyika ili nchi zingine zilizokuwa kwenye mchakato wa uhuru zipate Uhuru siku moja na Tanganyika.

Msimamo dhabiti Mwalimu Nyerere, uliweza kujenga Tanzania imara na kuifanya kuwa Taifa kimbilio la vikundi na vyama vya wapigania uhuru Kusini mwa Afrika, ambao walipewa hifadhi ya kudumu na kutumia ardhi ya Tanzania kuwa sehemu ya mapambano ya kudai uhuru wao, ambao waliupata kupitia mgongo wa Tanzania.

Viongozi kama Hayati Edward Mondolane, Samora Macheli wa Msumbiji, Nelson Mandela wa Afrika Kusini, Yoweri Mseveni wa Uganda, ni sehemu ya viongozi waliopitia mikononi mwa Mwalimu Nyerere wakati wakipigana nchi zao zikombolewe.

Watanzania walianza kuingiwa na wasiwasi mwaka 1971, wakati Nduli Idi Amin Dada alivyoasi na kuchukuwa madaraka ya Uganda kwa nguvu baada kuungusha utawala halali wa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Hayati Milton Obote na kutangaza kuitawala nchi hiyo kijeshi.

Mwanzo wa utawala wake waganda pamoja na mataifa mengine walidanganyika, wakawa na matumaini makubwa juu ya kiongozi huyo wa kijeshi, kutokana na ahadi zake nyingi kwamba yeye ataitala uganda na kuhakikisha eneo lililoko Tanzania, sehemu ya mto kagera, katika mkoa wa Ziwa Magharibi litakuwa sehemu ya Uganda.

Mwaka huo huo, Idi Amin alijaribu kutimiza madai yake kwa kuishambulia sehemu hiyo ya Mto Kagera, lakini watanzania walikuwa imara katika kulinda ardhi yao sehemu hiyo akashindwa, baada ya majeshi yake kurudishwa nyuma na majeshi hodari ya Tanzania.

Pamoja na majeshi yake kurudishwa nyuma, Fashiti huyo aliyejitangaza kuwa Rais wa maisha wa Uganda, akiwapongeza wapiganaji wake kwa kurudishwa nyuma huku akiwasifia kupata jeraha kidogo kutoka kwa majeshi ya Tanzania.

Baada ya wapiganaji wake kurudishwa nyuma Idi Amin alisema huo ni mwanzo tu, awamu nyingine atatumia silaha nzito zaidi ikiwa pamoja na makombola ya kurushwa kwa ndege na kuwaongezea nguvu askari wa miguu, jambo ambalo liliwafanya waganda kuingiwa na hofu kutokana na utawala huo wa mabavu, baada ya Amin kuanza kuwatilia shaka wananchi na kuwaua hovyo.

Mauaji ya kinyama yakawa kitu cha kawaida katika Uganda, wananchi wengi wasiokuwa na hatia walipoteza maisha, watu mashuhuri kama Jaji Mkuu Benedicti Kiwanuka na Askofu Mkuu Jamal Luwumu, waliteswa na kuuawa chini ya utawala wake.

Aitoa amri kuwa watu wote wanaopinga utawala wake, wapigwe risasi hadhalani, katika kutekeleza moja ya ndoto zake alizodai kuwa ni mazungumzo baina yake na Mwenyezi Mungu, aliwafukuza kutoka Uganda, Waasia wote waliokuwa na pasi za kusafiria za Uingereza na kuwanyanganya mali zao zote.

Baada ya shutuma nyingi za uongo dhidi ya Tanzania, mnamo tarehe 30 )ktoba 1978 Idi Amin aliyaamuru majeshi yake kuvuka mpaka na kulivamia eneo la Tanzania, ambapo watanzania zaidi ya 10,000 wasiokuwa na hatia yaliangamizwa na eneo la kilomita za mraba 1850 zilichukuliwa na majeshi ya Uganda.

Majeshi hayo ya Amin yalilikalia eneo la mto Kagera sehemu ya kyaka na kufanya vitendo vya kinyama kwa kuua wananchi wa mkoa wa Ziwa Magharibi hovyo, kuchoma nyumba, viwanda, kupora mali nyingi na kuzipeleka Uganda.

INAENDELEA

Comments

  1. Tatizo vijana tunasomaga magazeti ya udaku tu..Ahsanteni kwa taarifa....

    ReplyDelete
  2. Najisikia furaha kuwa mmoja ya wakazi wa mkoa huu wa kagera

    ReplyDelete
  3. nothing new..unatoa maneno yote kutoka katika ile video ya vita ya kagera

    ReplyDelete

Post a Comment

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru