Analog Clock

NSSF

NSSF
NSSF TANGAZO

Tone Radio Tz

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

Tuesday, September 19, 2017

KIKOMO

SEHEMU YA KUMI

Kabla hajamaliza hiyo tatu taa zikazimika. Kufumba na kufumbua nikamrukia huyo aliyekuwa tayari kumchoma Patrick, Pweke alikuwa amenikosa, maana baada ya kuruka tu nikasikia Pweke akiguna.

"Aaa nakufa!"

"Washenzi" Sauti ya Elungata ilisikika.

Huyu mtu niliyekuwa nimemrukia kwa woga aliangukia Upanga huku akitoa kelele.

"Mama wee"

Taa ziliwaka, nikamuona Wilfred Mbogo aliyekuwa sasa ameshaingia chumbani akanitupia bastola, yeye akabaki na bunduki.

"Nilinde nimfungue Patrick," nilimwamrisha.

"Hamna tabu" nilichukua upanga wa Pweke nikakatakata kamba alizokuwa amefungwa Patrick.

"Asante sana Wilfred."

Patrick alishukuru huku bado hana maumivu mengi.

"Amanda yupo nje tumuwahi" Wilfred alinong'oneza kila mtu bastola mkononi, tukatoka nje kwa mapambano na kundi la Elungata.

"Nyumba hii ina milango mitano ya kutokea nje sasa sijui Elungata na wenziwe watatokea mlango gani." alieleza Patric huku akituonyesha mahali ilipo.

"Wewe Wilfred tokea mlango wa uani. Patrick mlango wa pembeni na mimi nitatokea mlango wa mbele" 

Wilfred alipiga risasi mbili. na hapo hapo tukaona taa zinazimika kwa upande niliotokea niliruka chini na kujivingilisha, risasi zilipigwa lakini zilinikosa. Nilisikia mlio wa bunduki ya Wilfred tena.

Taa zikawaka. Nikawaona watu wawili kabla hawajafyatua risasi zao, mimi nikawawahi. Upande wa Patrick nikasikia bastola inalia. Baada ya muda kidogo gari likatoka mbio.

"Wanakimbia hao" nilisikia sauti ya Amanda.

niliachia risasi lakini gari likawa linaenda tu.

"Elungata na wenziwe wawili wamekimbia" PatricK alieleza.

"Kwa hiyo watatu wamekufa yule msichana yuko wapi?" niliuliza.

"Hata mimi sijui"

"Mtazame ndani" 

"Ok" 

Nilisikia mlio wa bunduki upande wa Wilfred na nikasikia msichana akilia.

"Niache. Niache haa haa usiniue" 

"Usimuue" nilipiga kelele nikijua ni tausi.

Wilfred. Amanda na Tausi walijitokeza na kisha Patrick.

"Elungata na wenziwe wamekimbia na almasi zote" Tausi alipiga kelele.

"Huna haja nazo sasa.Uhalifu wako leo umefika kikomo"

"Mimi ndiye niliyekuwa opareta wa umeme. Unaonaje?" Amanda alijidai.

"Alaa mimi nilikuwa nashangaa sana, hizi taa zilikuwa zinazimishwa na kuwashwa na nani. Binti umefanya kazi nzuri sana na kweli una nidhamu."

"Mara tukasikia mlio wa gari za polisi 999"

"Tumeegesha gari mbele ya pale barabarani" Amanda alisema.

Haya twendeni tusije tukakutwa na Polisi. Muda wa kuonana na polisi bado.

Tuliingia ndani ya gari, Amanda akanipa ufunguo wote watano tukaingia ndani. Safari kituo cha polisi.

"Mmejuaje huku?" nilimuuliza Wilfred.

"Mlipotoka tu walikuwa wamemwacha mmoja wao basi nikamvizia nikamtwanga halafu tukamlazimisha atulete huku nikamtuma Amanda akachukue hilo gari ambalo ni la kaka yangu tukawafuata. Tulijua tu kuwa mtakuwa katika taabu maana yule mtu alitueleza jinsi hapo mahali panavyolindwa. Basi tukaja pamoja na msaada na robo ya ushujaa wa Amanda ambaye aliweza kupenya mpaka kwenye swichi kuu ya mtambo mkubwa wa kuwasha na kuzimisha umeme".

"Mungu si Athuman", Patrick alisema. Tukawa tumeingia kituo cha polisi. Tulimnyanyua Tausi na kumpeleka kaunta.

"Ofisa wa zamu yuko wapi?"

"Yuko ndani", alijibu Koplo mmoja wa kaunta.

Tulipofika ndani nikamkuta Inspekta wa zamu. Nikatoa kitambulisho changu.

"Mweke huyu mama ndani mpaka utakapopata amri nyingine, Nkuu wa mkoa wa Polisi yuko hapa Shinyanga?"

"Ndiyo yupo."

"Mpigie nyumbani kwake". 

Ilikuwa sasa yapata saa kumi na moja asubuhi.

"Hallo", aliita Inspekta.

"Kuna ndugu wa Idara ya Upelelezi, Ndugu Willy Gamba anataka kuzungumza nawe".

"Hallo, Willy Gamba hapa".

"Habari gani?" aliamkia huku sauti ikitetemeka.

"Jambo la kwanza funga barabara zote gari lolote lisiweze kuingia wala kutoka Shinyanga sasa hivi, usichelewe hata dakika moja, na uwaeleze Mwanza na Geita washike kila gari linaloingia toka Shinyanga sasa hivi na wangoje amri nyingine".

"Sawa, asante sana".

"Pili kuna nyumba moja huko Ushirika, Polisi wa 999 wameenda huko, tafadhali wakae hapo hapo mpaka amri nyingine itakapotoka. Wewe tuonane saa moja hapa Kituo cha Polisi".

"Sawa ndugu".

Kisha nilichukua simu nikapiga kwa Chifu. Wakati nangojea simu nikashauri Amanda akapumzike.

"Hata mimi naona hivyo", Patrick alisema.

"Kazi uliyoifanya inatosha, Amanda", niliongezea.

Aliniangalia kwa jicho la mahaba sana.

"Nitakuona tena Willy?".

"Bila ya shaka. Si uko likizo? Basi nenda kashike chumba Shinyanga Hoteli, pumzika mimi nitakukuta hapo".

"Sema sisi", Patrick alitania.

Wote tukacheka.

"Haya, nitasubiri kwa hamu kubwa. Mungu awasaidieni mumkamate Elungata".

"Siku za mwizi ni arobani, nafikiri karibu siku zake zitatimia", Wilfred alisema.

"Nafikiri Wilfred ampeleke halafu aturudie sisi hapa", Patrick alishauri.

"Sawa, Wilfred mpeleke".

Wilfred na Amanda wakaondoka. Inspekta akamshika Tausi mkono ili kumpeleka rumande.

"Mimi mtanifanya nini?" Tausi aliuliza.

"Sisi hatutakufanya lolote, ila wananchi ambao umekuwa unawadhulumu watajua la kukufanya. Sisi tutakupeleka mikononi mwao. Lazima ujuwe kuwa uhalifu haulipi", nilimjibu.

Niliinua simu. Inspekta akamvuta Tausi na kumpeleka rumande.

"Halo Willy hapa".

"Unasemaje?" Chifu aliuliza.

Nilimweleza maendeleo yote mpaka dakika hiyo.

"Kazi nzuri sana", alijibu.

"Tunakuomba uchukue ndege na ufikie haraka hapa Shinyanga bila kuchelewa".

"Kwanini?".

"Njoo kuna mambo mengine ambayo sitaweza kukueleza. Nataka uje uyaone mwenyewe kwa macho".

"Sasa ni saa kumi na mbili kasoro robo. Saa tatu nitakuwa hapo. Tuonane Tanganyika Hoteli."

"Asante sana".

Nikaweka simu.

"Anakuja?" Patrick aliuliza.

"Ndiyo, anakuja".

"Kwanini umemwita?" Patrick aliuliza zaidi kwa kushangaa.

"Na yeye aje apambane na Elungata, tumechoka na sisi".

Wote tukacheka lakini nikajua jibu langu halikumridhisha Patrick.

"Sasa tufanye nini?"

"Tumungoje Wilfred. Yeye ana rafiki hapa na tunaweza, sasa tunaweza kwenda kuoga, tukapumzika kidogo, saa moja tuwe hapa kuonana na Mkuu wa Polisi wa Mkoa".

Mara Wilfred akatokea huku jasho likimtoka.

"Mbona jasho linakutoka hivi?" nilimuuliza.

"Hee bwana, kuna makubwa tena, watu watatu wamekutwa wamekufa ndani ya lile gari alilotoroka nalo Elungata!".

"Upande gani?"

"Karibu na kituo cha mabasi. Ina maana watu wamekufa?"

"Si waliotoroka na Elungata walikuwa wawili na yeye wa tatu?" Patrick alihoji.

"Si kitu cha kushangaza. Polisi wametambua moja wapo za maiti kuwa ni maiti ya Mkuu wa Polisi wa Mwadui."
Hii haikunishangaza sana ingawaje Patrick alionekana na mshangao.

"Tena wameuawa kwa kupigwa risasi kifuani", alimalizia.

"Hii ina maana Elungata amekata shauri kuwarusha wenziwe. Sasa kabaki peke yake na mali yote", nilisema.

Niliingia ndani mpaka ofisini kwa Inspekta.

"Tafuta kama kuna gari lolote lililoibiwa mjini hapa yaani kama kuna mtu amepotelewa na gari lake".

"Sawa ndugu".

"Sisi tunatoka tutarudi hapa saa moja."

Tuliondoka kuelekea kwa rafiki yake Wilfred. Tulioga na kupata chai. Ilipofika saa moja tukaanza safari ya kurudi Polisi. Tulipofika huko nikaenda moja kwa moja mpaka ofisini kwa Inspekta.

"Umepata habari yoyote?" Nilimuuliza.

"Ulipoondoka tu nilituma magari ya polisi 999 matatu lakini sikupata taarifa yoyote ya kuibiwa gari".

"Vizuri".

Nilitoka na kuwafuata akina Patrick ambao walikuwa ndani ya gari.

"Inspekta anasema hakuna gari lolote lililoibiwa".

"Ina maana kuwa Elungata bado yuko Shinyanga kama hakuondoka kwa miguu, jambo ambalo haliwezekani", alisema Patrick.

"Sawa kabisa, hata mimi nafikiri Elungata yuko hapa hapa mjini.

Mara likanijia wazo, moyo wangu ukapiga upesi upesi. Nikaona nifanye kama mawazo yangu yanavyonituma.

"Vipi mbona umeduwaa?", Wilfred aliniuliza.

"Nilikuwa nafikiri Wilfred, asante sana kwa shughuli yote uliyofanya".

Nilitoa kibeti changu, nikatoa fedha.

"Chukua hizi shilingi elfu tatu, iwe nauli yako ya kwenda Dar es Salaam".

"Niende Dar es Salaam kufanya nini?" alidakia kwa kushangaa.

"Fika Dar es salaam. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Umwone Mkuu wa Polisi wa Tanzania, tarehe kumi na tano mwezi huu. Utakuta habari zako zote huko".

"Habari gani?".

"Utazijua wakati huo. Ni lazima ujivune, maana jina lako litakuwa kwenye vitabu vya mashujaa wa Tanzania kwa sababu umepigana kiume, kuyaangusha haya majambazi".

"Lakini mbona bado hatujamkamata Elungata?".

"Hiyo tuachie sisi. Kazi iliyobaki ni ndogo sana, kwa kusema ukweli imekwisha. Soma gazeti la keshokutwa na utashangaa".

"Haya kwaheri. Mungu akipenda tutaonana".

Tuliagana huku machozi yakitulengalenga. Wilfred aliondoka na gari.

"Ulishafanya mipango au vipi?" Patrick aliuliza.

"Nikirudi tu Dar es salaam sina budi kufanya mpango, kazi aliyofanya lazima impatie maslahi fulani.

"Sawa, hakika huyu kijana kafanya kazi kama mmoja wetu. Kusema kweli anastahili sifa na tuzo. Twende zetu tukatafute hoteli ya kulala". 

"Itabidi tukae hoteli mbali mbali".

"Tupite Shinya Hoteli tuone kana kuna nafasi, halafu twende Butiama. Tukipata nafasi Shinyanga wewe utalala hapo", Patrick alisema huku akitabasamu.

"Kwanini?"

"Amanda yuko huko".

Wote tukacheka.

"Si lazima".

Tukacheka tena.

"Hapana iko sababu, kama nafasi ipo Shinyanga Hoteli wewe utakaa hapo. Utajua baadaye kwa nini".

"Sawa, wewe ndiye bosi".

Wakati tunataka kuondoka tu Mkuu wa Polisi wa Mkoa akafika na gari.

"Umechelewa sana, sasa karibu saa mbili kasorobo", nilimwambia.

"Nilikuwa nachunguza mambo yalivyokwenda. Toka saa zile hakuna gari lililotoka Shinyanga. Magari yote yaliyoingia yamekaguliwa vizuri kabisa. Jambo la kusikitisha tu ni kwamba nimepata habari za mauaji ya Mkuu wa Polisi wa Mwadui".

"Hata sisi tumesikitishwa sana".

"Tunajaribu hivi sasa kutambua maiti zingine zilizokuwemo ndani ya gari".

"Fanyeni hivyo".

"Nimepata simu toka Dar es Salaam kuwa Mkuu wa Polisi atafika hapa mnamo saa tatu".

"Vizuri, lakini sasa tunaomba gari moja", nilimwambia.

"Bila ya wasiwasi chukueni".

"Ukipata habari zozote tuwekee, tutakuja kuulizia".

"Mimi sitatoka, niko hapa hapa namsubiri Mkuu wa Polisi".

Tukaondoka mpaka Shinyanga Hoteli.

"Vyumba vipo?" niliuliza.

"Vipo".

"Hebu nipe kitabu cha wageni niandike".

Nilipewa kitabu. Nikaangalia majina yote yaliyokuwemo. Jina la Amanda lilikuwa chini kabisa, chumba nambari tisa. "Patrick njoo uchague chumba".

Akaangalia majina yote.

"Nachagua chumba nambari kumi, lakini usilie wivu, wewe mwenyewe unayataka".

Tukacheka. Baada ya hapo tukaelekea Butiama Hoteli.

"Kuna vyumba vya kulala?| 

"Kimebaki kimoja tu chenye vitanda viwili".

"Sawa, nipe kitabu".

Alinipa kitabu, nikaanza kuangalia. Mara moyo wangu ukaruka kidogo. Jasho likanitoka, nikajikaza mshangao wangu usionekane. Kisha nikajaza kitabu kama ilivyohitajika.

"Mna mizigo?" aliuliza mpokezi wageni.

"Tutaleta".

"Haya, vizuri".

Ilikuwa yapata saa mbili na nusu sasa.

"Twende tukapate chakula cha asubuhi Tanganyika Hoteli wakati tunangoja Chifu afike," nilimwambia Patrick.

"Sawa, hata mimi nasikia njaa sana. umesema jambo la maana sana.

Tulienda zetu Tanganyika Hoteli tukaagiza chakula. Chakula kikaja, tukala kimya kimya, maana kila mtu alikuwa na njaa.

"Lo, mnakula kama kwamba mnangombana na chakula", Chifu alitushtua.

Chifu na Mkuu wa Polisi walikuwa wameingia bila ya kuwaona kwa jinsi tulivyokuwa tunakishughulikia chakula kikamilifu.

"Lo, nyuso zenu vipi, mbona kama mmeraruriwa na chui", Chifu alitania kama kawaida yake.

"Kuna binti mmoja ana kucha huyo, afadhali ya Chui," nilitania.

Tuliinuka na kuwavutia viti.

"Shikamoo", tulisalimu kwa pamoja.

"Marahaba", wote wakajibu kwa pamoja.

Nilimwita mhudumu wa hoteli awahudumie. 

"Nasikia mliweka ulinzi gari lisiingie wala kutoka, mbona kiwanja cha ndege mlisahau? Hamfikirii kuwa mtu angeweza kutoroka kwa kupitia njia hiyo?". aliuliza Mkuu wa Polisi.

"Sijui", Mkuu wa Polisi wa Mkoa", nilimjibu.

"willy, huwezi kumjibu Inspekta Mkuu hivyo!" Chifu alinikanya.

"Samahani mzee, nafikiri akili yangu imevurugika sana.

"Kuna zaidi mpaka sasa, kuliko kifo cha Mkuu wa Polisi wa Mwadui?" Mkuu wa Polisi aliuliza.

"Hapana zaidi", nilijibu.

"Sasa mmetuitia nini? Elungata mmeshamshika?" Chifu alifoka kwa sauti ya chini chini.

"Kukujibu maswali yako mawili kwa pamoja bado hatujamshika, tumekuita uje kutusaidia.

"Willy, tusitaniane. Unadhani".

"Basi Chifu, sidhani kama kawaitia hilo. Hata mimi hajaniambia. Nafikiri tungoje, atatueleza anavyofikiri yeye", Patrick aliingilia.

Chifu alisonya kwa hasira, lakini hakunishtusha, maana ndivyo alivyo. Hujiwa na hasira mara moja na kupoa hasa afikiriapo kwamba unajaribu kutaniana na huku yeye akiwa na maana kazi. Tulimalizia kula chakula tukiwa kimya. Tulipomaliza kula na kulipa, nikasimama.

"Sasa twende kwanza hotelini tukazungumze vizuri, hapa si mahali pa kuzungumzia kazi ila mahali pa kula".

"Ndiyo sababu ukawa matata?" Chifu alisema akitabasamu.

Tulipofika Mkuu wa Polisi akasema. "Mimi nafikiria twende tukaelezane kwenye Kituo cha Polisi". 

"Sisi siyo Polisi, kama unataka kuchukua maelezo kwenye karatasi za polisi ni..."

"Willy, nilikwambia nini? Mbona unakosa nidhamu!" Chifu alionya tena.

"Kweli, samahani nasikitika sana. Nafikiri sijalala vizuri siku nyingi. Kichwa changu bado hakifanyi kazi sawaswa".

"Basi twende zetu huko hotelini kwake anakokusema." Mkuu wa Polisi alisema.

"Mna gari?" niliwauliza.

"Tulikuja na taksi kutoka kiwanja cha ndege, tukairuhusu iondoke baada ya kufika hapa".

Patrick aliwafungulia milango ya gari. Niliendesha mpaka Butiama Hoteli. Tulitelemka tukaingia hotelini. Kufika tu mapokezi akanidakia.

"Mizigo iko wapo, kama huna mizigo hupandi juu!".

Nikatoa kitambulisho changu. 

Akanipa funguo huku akitetemeka.

"Orofa ya kwanza kiko mkono wa kulia".

Tulipoanza kupanda ngazi tu nikatoa bastola yangu na Patrick naye bila ya kuchelewa akatoa bastola yake, Chifu na Inspekta Mkuu wakatazamana bila ya kusema lolote na kumeza mate.

Tulipofika orofa ya kwanza nikaangalia vyumba. Chumba nilichokuwa nakitafuta kilikuwa upande wa kushoto. Nilielekea upande huo nao wakanifuata. Nilipofika karibu na chumba nilichokuwa nakitafuta, nikamuonyesha Patrick ishara ya kuwakinga Chifu na Inspekta Mkuu iwapo kutatokea taabu yoyote. Nilipowaangalia Inspekta Mkuu akatoa kitambaa na kuanza kufuta jasho. Nilipokuwa sawasawa na mlango nikarudi nyuma kwenye ukuta bastola mkononi. Nikaruka na kuupiga mlango kwa magoti yote mawili. Mlango ukafunguka nikaangukia ndani.

"Usisogee popote, kaa kama ulivyo," nilimwamrisha na huku nimemlenga bastola, "Patrick walete wazee ndani".

Patrick akiwa na bastola mkononi aliwangiza Chifu na Inspekta Mkuu ndani. Wote walipoingia wakashtuka, wakashikwa na bumbuwazi.

"Oswald Mengi umefika huku lini?" Inspekta Mkuu aliuliza kwa mshangao. 

Kabla hajajibu nikasema, "Onaneni na Oswald Mengi Elius Elungata Kamishna Mkuu wa Polisi na mkuu wa Majambazi wa wizi wa almasi".

"Mwongo, mwongo ananisingizia ," alipiga kelele huku akitetemeka kwa woga.

Chifu, Patrick na Inspekta Mkuu walikuwa bado katika mshangao.

"Chifu, nilikuita kusudi uje ujionee mwenyewe jinsi baadhi ya viongozi wetu walivyo waovu. Ni jambo la kusikitisha sana kufahamu kuwa Kamishna Mkuu wa Polisi ambaye anapaswa kuupiga vita ujambazi ndiye Mkuu wa majambazi".

"Mimi sielewi hata kidogo", Patrick alidai.

Chifu na Inspekta Mkuu wote walionyesha mshangao!

"Ni mwongo ni mwongo mkubwa. Anataka kunisingizia tu. Kashindwa kumtafuta Mkuu wa majambazi. Ananisingizia mimi. Nimekuja kwa ajili ya kazi hii hii huku nikiwa nimemwacha mke wangu mahututi. halafu unakuja kunisingizia kiasi hiki. Mimi niwe Mkuu wa majambazi. Wewe Willy una kichaa? Kichaa", Oswald Mengi alisema kwa ukali.

"Kama tungechelewa kidogo, Elungata angepotea kabisa na tungeonana na Oswald Mengi peke yake, akidai kuwa baada ya kupata habari kuwa Inspekta Mkuu na Chifu wako hapa na yeye akaja. Wote tungeamini na Elungata asingepatikana kamwe kwa sababu Elungata ndiye Oswald Mengi!" 

"Kweli kabisa nimekuja kupigana nanyi bega kwa bega dhidi ya majambazi," alipiga tena kelele.

Wote walikuwa wapo na mshangao.

"Chifu kaeni kwenye viti"

Mlikuwa na viti viwili Patrick akaegemea kwenye mlango huku bastola yake ikimlenga Mengi. Mimi nikakaa juu ya meza, bastola yangu ikimlenga vile vile.

"Nitawaeleza mambo yote toka mwanzo mpaka mwisho"

Wote wakaa chini wakiwa bado wameshangaa la kusema hawana!

"Katika mashimo ya almasi ya Mwadui kumekuwa na wizi mdogo mdogo wa almasi, ambao ulianza miaka mingi toka hata wakati wa ukoloni na nyote mnajua. Wizi ambao ulianza kushtusha serikali umetokea miaka miwili tu hivi iliyopita. Na kama mnakumbuka, Mengi alikuwa mkuu wa Polisi wa Mwadui kwa miaka mitano na wakati wote huu wizi ulikuwa ni mdogo mdogo tu.

Miaka miwili na nusu iliyopita, Mengi alipandishwa cheo na kuwa kamishna Mwandamizi wa Polisi na kuhamishiwa Dar es Salaam, Miaka yote hii alipokuwa Mwadui alikuwa anapanga jinsi gani anaweza kuanzisha wizi wa almasi, lakini akaona kuna hatari ya kuweza kugunduliwa. Wakati amepanda cheo na kuhamishwa ndipo akapata nafasi. Na kama mnakumbuka yapata miaka miwili na nusu sasa toka atoke Mwadui na ni baada ya miezi sita tu ndipo wizi kabambe ulipoanza.

"Mkuu wa Polisi wa Mwadui, ambaye sasa hivi ni marehemu alihamishiwa Mwadui miaka miwili iliyopita na kama sitakosea Mengi ndiye aliyependekeza jina lake na akapendekeza kuhamishwa kwa Mkuu wa Polisi aliyekuwa amekaa hapo muda mfupi tu Mengi alimpa huyu marehemu mipango yake na jinsi ya kuitekeleza.

"Na huko Mwadui alikuwa na kijana wake Khasimu Omari ambaye alikuwa Inspekta Mwandamizi na alimwelekeza akafanya naye kazi bega kwa bega chini ya mwongozo wake. Kwa hiyo hii iliwapa nafasi nzuri sana ya kuweza kuendesha wizi bila wasiwasi. Na kwa upande wa Mengi ingekuwa vigumu sana mtu yeyote kumfikiria. Vile vile ingekuwa vigumu kuwashika, maana mara utokeapo uchunguzi ilibidi yeye Mengi ahusike katika kuutekeleza na hivyo aliweza kujua mbinu za kuangamiza uchunguzi wa hali yoyote kabla haujafika mbali.

Khasimu Omari alikuwa anajuana na Pweke ambaye kwa mara nyingi alikuwa anaendesha wizi mdogo mdogo na kwa jinsi ile yeye ndiye aliyekuwa akijua masoko ya wizi wa almasi za wizi. Kwa hiyo upande wa soko ilikuwa kazi ya Pweke ambaye alijuana na wale watu niliowapa majina muwakamate ma kuwaweka chini ya ulinzi, maana hao ndio waliokuwa wakala wa almasi kwa wafanya magendo kwa nchi za nje. Kwa jinsi ile mambo yalienda vizuri bila ya wasiwasi maana kila upande ulikuwa na mpango thabiti.

"Kwa hivi, Chifu kila alipokuwa akituma wapelelezi, walikuwa hawawezi kufua dafu, maana habari zilijulikana tu baada ya kuondoka hapa. Wote akina Jack Mwile, Makungu Majula na wengineo waliweza kuuawa kwa urahisi kwa sababu hiyo hiyo. Mbile katika uchunguzi wake alifika mbali kiasi cha kujua kuwa mtu aitwae Elungata ndiye aliyekuwa Mkuu wa majambazi, lakini aliuawa kabla hajaweza kuleta ripoti kamili. Kwa bahati aliweza kunifikishia ujumbe juu ya hili jina.

"Kila uhalifu una kikomo chake, maana itajatokea siku moja atafanya kosa kidogo na ndipo atajisaliti.

"Wakati mimi naondoka, watu waliojua juu ya kuondoka kwangu, ni wewe Chifu, Inspekta Mkuu, Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi, na bila ya shaka, Mengi ambaye Inspekta Mkuu alienda kumweleza akiwa kama msaidizi wake mkuu.

"Kosa la kwanza alilofanya Mengi ni kuwa mimi nilipofika tu Mwanza, habari zangu zilikuwa tayari zimefika, maana sikukaa hata masaa mawili kabla ya chumba changu hakijakaguliwa na hali nilikuwa nimebadilisha sura na jina. Ingekuwa vigumu mtu yeyote nje ya hao niliowataja kunitambua. Kwa hivi mara moja nikaanza kuhisi kuwa kuna mtu miongoni mwetu aliyekuwa na uhusiano na haya majambazi. Kwa hiyo nikaanza kujihadhari sana huku nikijaribu kumtafuta huyu mtu kati yatu.

"Jambo lilonidhihirishia kabisa kuwa huyu mtu yu miongoni mwetu ni wakati George alipokuja, kwani na yeye kabla hajafika habari zake zilikuwa zimefika. Na wakati huu watu walikuwa wanajua habari za safari ya George ya Mwanza, Ni wewe Chifu na Mengi, maana Waziri pamoja na Inspekta Mkuu walikuwa wamekwenda Lusaka. Kwa hivi ikabidi nichunguze zaidi kati yenu ni nani.

"Mambo yalipozidi kwenda vibaya kwa upande wake Mengi akatoa amri ufanyike wizi wa hali ya juu kabisa na kumweleza Khasimu na Mkuu wa Polisi wa Mwadui kuwa anawasili Maganzo kitu kilichonifanya sasa nimtuhumu Mengi peke yake ni wakati Patrick alipokuja, Habari zake hazikuwa zimefika kwa kuwa Mengi hakujua kuwa Patrick alikuwa akija maana yeye alikuwa wakati huo ameisha omba ruhusa ya kwenda kumuona mkewe aliyepatwa na ajali. Kwa hivi Patrick alipofika hakuna aliyejua.

"Habari kuwa mkewe alikuwa amepatwa na ajali ilikuwa ni uongo. Hii ilikuwa njia ya kutafuta namna ya kuja Maganzo. Kwa hiyo badala ya kwenda Arusha, ambako kweli ndiko mke wake aliko, amekodi ndege ya Tim Air na kuja Shinyanga. Ukitaka kuthibitisha utakuta mtu kwa jina la Ochald Mengi amekodi ndege kuja Shinyanga jana jioni kwani walimtegemea kufika Maganzo mnamo saa nne.

"Alipofika Maganzo na kukuta mambo yameharibika zaidi, akawachukua wenzie mpaka Shinyanga, ambako wangegawana almasi zilizoibiwa jana, halafu kila mtu aende zake. Kwa bahati sisi tukaweza kuwagundua. Kitu kingine kilichofanya nijue kwamba lazima huyu mtu tunamfahamu ni wakati tumeshikwa mimi na Patrick Elungata alikuwa akizungumzia kwenye chumba akiwa amejificha na sauti aliyokuwa anaitoa ungejua kuwa ni ya kuiga. Hii ilizidi kunidhihirishia kuwa huenda hisia zangu ni sahihi.

"Watu waliokuwa wakifahamu kuwa Elungata ndiye Oswald Mengi, walikuwa watu wawili tu, Khasimu Omari na Mkuu wa Polisi wa Mwadui kwa hiyo kuuawa kwa Khasimu Omari kwenye hiyo nyumba huko Ushirika ilimpa Mengi wazo la kutoroka na hao wengine, sisi tubaki tuwamalize wale waliobaki ndani ya ile nyumba. Lakini yeye akawamaliza hao alioondoka nao akiwemo Mkuu wa Polisi wa Mwadui, ambaye ndiye peke yake aliyebaki akimjua yeye ni nani.

"Alijua kwamba kaisha waua hao atakuwa amebaki na almasi zote na angeweza kujitokeza kama vile anavyosema sasa kuwa naye amekuja kuona mambo yanakwendaje. Lakini kwa vile nilikuwa nimeisha muhisi, nilipata habari za kuuawa kwa hawa watu ndani ya gari akiwemo huyo Afisa wa Polisi. Nikajua karibu tunapata mzizi wa tatizo letu ndipo nikaomba ufike ujionee mwenyewe.

"Kwanza nilifikiria kwamba atatoroka. Lakini nilipoambiwa kwamba hakuna gari lililotoka, nikajua dhahiri kuwa bado Elungata yumo Shinyanga. Kusudi niweze kuthihirisha mambo yote niliyokuwa nimekisia, nilienda kila hoteli nitafuta jina linalofanana kidogo na Oswald Mengi. Kwa bahati nilipofika hapa Butiama Hoteli kuangalia katika rejista. Nikakuta jina la Ochard Mengi. Hii ikanidhihirishia kuwa makisio yangu yalikuwa sawa. Maana jina la Ochard Mengi ni kidogo sawa na Oswald Mengi.

"Chifu, hivyo ndivyo mambo yalivyokuwa. Sasa kutaka kukudhihirishia asilimia mia moja kuwa yote niliyosema ni kweli bila ya kumsingizia mtu unayemtafuta ni yeye, subiri. Patrick mwangalie, akileta ujanja wowote piga risasi".

Nilifungua kabati la nguo la humo chumbani. Nikakuta hicho nilichokitaka, kisanduki kidogo cheusi.

"Wewe mshinzi sana. Willy, umenimaliza", Mengi alisema.

Nilifungua hicho kisanduku, ambacho ni cha gharama sana, kikiwa na mifuko ya siri mingi ndani. Katika mfuko mmoja wa siri nikakuta nilichokuwa nikitafuta. Nilitoa mkoba uliojaa almassi tele, zilizokwishapigwa muhuri tayari kwa kusafirishwa ng'ambo.

"Kweli kikulacho ki nguoni mwako". Chifu alisema kwa masikitiko makubwa.

"Piga simu hapo chini ita polisi 999," Inspekta Mkuu alimweleza Patrick.

Patrick akaondoka kwenda kuita 999.

"Kikulacho ki nguoni mwako ni kweli Chifu. Mtu kama huyu anayestahili kulinda uchumi wa wananchi, yeye mwenyewe anakata shauri kuwanyonya na kuwatesa. Ningekuwa na madaraka mtu kama huyu ningemweka hadharani wananchi wenyewe watoe hukumu", alimalizia. 

"Mimi nafikiri kuna haja ya kufanya marekebisho katika ngazi zote za uongozi. Kila kiongozi amulikwe maana ni afadhali kuwa na watu wa kawaida elfu moja waovu kuliko viongozi au hata kiongozi mmoja mwovu", alisema Inspekta Mkuu.

"Lililopo sasa ni kuishauri serikali ifanye uchunguzi na iwapo kuna kiongozi anayeonekana msimamo wake ni wasiwasi basi aachishwe uongozi. Wale wanaobaki wapigwe msasa, waweze kuelewa wajibu wao kwa wananchi ni nini, wajibu kwa kazi waliyokabidhiwa na wananchi ni nini. Watoe tamaa ya kujinufaisha wenyewe bali wajitoe mhanga kwa faida ya taifa zima. Jambo la huyu Mengi litasikitisha wengi lakini imekuwa fundisho kwa serikali na wananchi kwa ujumla, kuwa kati ya viongozi wenyewe wa nchi hii, yamo majambazi nambari moja. Mara kwa mara watu hufikiria watu wadogo. Lakini tokea sasa tutakaza macho kwa watu wakubwa, maana hawa ndiyo rahisi sana kuangusha taifa hili kiuchumi. Ni aibu kwa mtu kama huyu", Chifu alisisitiza huku machozi yakimlengalenga.

"Nitahakikisha kuimarishwa kwa Jeshi la Polisi kikamilifu, na naomba iwe hivyo katika sehemu zingine kwa manufaa ya wananchi. Ni jambo la kusikitisha sana, maana nilimwamini sana Mengi, ni sikitiko lililoje!".

Wakati huo huo polisi wakafika pamoja na Patrick.

"Mnaweza kuchukua wiki moja na kupumzika", Chifu alituambia.

"Asante sana", tulishukuru.


MWISHO

MANJI AKUTANA NA WCHEZAJI NJE YA MAHAKAMA


WACHEZAJI na baadhi ya viongozi wa Klabu Bingwa ya Soka Tanzania Bara, Yanga na benchi lote la Ufundi, leo wamekutana Mwenyekiti wao wa zamani, Yussuf Manji ili kumjulia hali ambaye awali aliachiwa huru na kutoka katika gereza la Keko Jijini Dar es Salaam wiki iliyopita baada ya kufutiwa mashitaka ya Uhujumu Uchumi yaliyokuwa yanamkabiri. 

Wakati Manji anaachiwa huru, Wachezaji na benchi la ufundi la Yanga walikuwa katika mikoa ya Njombe na Ruvuma kwa ajili ya kushiriki michezo miwili ya ligi kati ya Njombe Mji na Njombe na Majimaji ya Sonea, ambapo Yanga imeambulia pointi nne na magoli mawili baada ya kushinda mchezo dhidi ya Njombe na kutoka sare na Majimaji.

Wachezaji hao wakiongozwa na Kocha Mkuu, Mzambia, George Lwandamina walimfuata Manji katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kusutu, Dar es Salaam ambako alikwenda kusikiliza kesi yake nyingine inayomkabiri ya tuhuma za kutumiwa dawa za kulevya.

Pamoja na kusalimiana na kupeana mikono na wachezaji wote, lakini Manji alizungumza na kirefu na Nahodha, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kana inavyoonekana katika picha ya juu. Manji alizungumza na Cannavaro akitoka mahakamani kusikiliza kesi yake, ambayo imeahirishwa tena hadi Septemba 25, mwaka huu.
Mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu, Cyprian Mkeha, Wakili wa utetezi, Hajra Mungula alisema  kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kusikilizwa na wako tayari. Alisema mteja wake anahitaji kutoka kwa ajili ya matibabu kwa sababu yuko nje kwa dhamana, hivyo akaiomba Mahakama hiyo iisikilize kesi hiyo kwa siku tatu mfululizo.

Kwa upande wake, Wakili wa Serikali Timon Vitalis alidai kwamba anataka kusafiri mchana na hatoweza kusikiliza kesi hiyo. Hakimu Mkeha alisema kwamba anakwenda kwenye kikao na kuahirisha shauri hilo hadi Septemba 25 litakaposikilizwa kwa siku tatu mfululizo hadi Septemba 27.

Ikumbukwe, Manji anadaiwa kutumia dawa za kulevya aina ya Heroin kati ya Februari 6 na 9, 2017 katika eneo la Upanga Sea View Ilala alitumia dawa za kulevya aina ya Heroin. Kesi hiyo ipo katika hatua za usikilizwaji wa mashahidi upande wa utetezi ambapo shahidi wa kwanza katika kesi hiyo,

Hata hivyo Mkugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Prof.Mohamed Janabi aliieleza mahakama kuwa Manji ana Vyuma kwenye moyo. Alhamisi iliyopita Septemba 14, mwaka huu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilimuachia huru Manji baada ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka (DPP) kumfutia mashtaka baada ya kusota jela kwa miezi miwili.

Mbali na Manji, wengine walioachiwa huru ni Meneja Rasilimali watu wa Kampuni ya Quality Group Ltd, Deogratius Kisinda, Mtunza Stoo, Abdallah Sangey na Thobias Fwere. Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi amemueleza Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kuwa wameomba 'remove order' na kwamba Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka (DPP) kwa niaba ya Jamhuri wanaiarifu Mahakama kwamba hakusudii kuendelea kuwashtaki Manji na wenzake katika kesi hiyo.

Hivyo wanaomba kuiondoa kesi hiyo chini ya kifungu cha 91(1) cha sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Baada ya kueleza hayo Wakili wa Manji, Hajra Mungula ameeleza kuwa sheria inaruhusu DPP kufanya hivyo na kutokana na hatua hiyo, Hakimu Shaidi amesema kesi hiyo imefutwa na kuanzia sasa washtakiwa wapo huru.

Monday, September 18, 2017

KIKOMO

SEHEMU YA TISA

Mlango ulifunguliwa wakati mimi nikiwa tayari kwa lolote litakalotokea na kwa mshangao wangu Patrick aliingia ndani. Niliruka hapo nilipokuwa. 

"Patrick!".

"Willy". 

Tukakumbatiana. 

"Na nyinyi nanyi! Mnapendana hivyo?" Amanda alisema.

"Usijali," nilimjibu. 

"Yule mdogo wa daktari yuko wapi?" Amanda aliuliza kwa woga.

"Yupo atakuja," Patrick alijibu.

"Patrick nipe habari kwa ufupi maana nimekuwa nje ya hii shughuli kwa masaa kwa hiyo niko nyuma sana na habari." 

"Nafikiri Amanda kishakueleza jinsi tulivyokupata."

"Ndiyo, kanieleza." 

"Huko Dar es Salaam nilipata habari kama saa kumi na moja unusu hivi Chifu alinieleza kwa ufupi juu ya habari zote na maendeleo ya shughuli hii. Mambo mengine yote alimweleza Kamishna Mkuu wa Polisi ashughulikie kama vile kuwatia nguvuni hao majambazi uliokuwa unawakisia. Mimi aliniambia niwe kiwanja cha ndege saa kumi na mbili kamili tayari kwa kuondoka.

"Wakati nikiwa kiwanja cha ndege nikapata habari toka kwa Chifu kuwa Kamishna Mkuu wa Polisi ndugu Oswald Mengi kapata safari ya ghafla. Maana baada ya kuongea na Chifu alipata habari kuwa mkewe aliyekuwa anasafiri toka Arusha alikuwa amepata ajali kati ya Arusha na Moshi na inasemekana kuwa huenda amekufa kwa jinsi hii ameruhusiwa kwenda kumuona mkewe kwa hiyo sasa mambo yote yako mikononi mwa Chifu na Mkurugenzi wa Upelelezi, Mkuu wa Polisi ameitwa arudi haraka maana jambo hili limefikia hatua ya juu haliwezi kushughulikiwa na maafisa wa chini wa polisi.

"Baada ya kupata habari hizi nilipanda ndege ya jeshi na mnamo saa moja unusu nilikuwa Maganzo na ndipo nikaonana na Amanda. Mambo mengine yote nafikiri kesha kueleza."

"Nipe habari za Bantu Bar".

"Baada ya kukuleta hapa nilionelea niwafuate kwa kufuatana na habari nilizopewa na Amanda. Huyo mdogo wake daktari akasema twende naye nami nikaona bora. Tulipofika hapo tulipeleleza uwezekano wa kuwepo huo mkutano lakini hakukuwa na dalili. Tulingoja sana lakini hatukuonana dalili yoyote. Tukajua kwamba lazima kulikuwa na mabadiliko ya mipango."

"Mlingoja mpaka saa ngapi?". 

"Mpaka saa tano unusu hivi. Mimi nilionelea nirudi nikamuacha Wilfed Mbogo ambaye ndiye huyo mdogo wake daktari aendelee na uchunguzi na apatapo habari yoyote aje kutueleza kabla sijaja nikaonelea nimpigie simu Chifu, nimweleze tumefikia wapi na mambo yalivyo. Nilipiga nyumbani kwake nikapata habari kuwa amerudi ofisini. Hii ilinishangaza. Nikampigia ofisini. 

"Nilipompata nikamweleza mambo yalivyo mpaka dakika hii. Kisha nikamuuliza kwanini alikuwa ofisini mpaka dakika hiyo. Akanieleza kuwa alikuwa amepata habari zingine za kusikitisha toka Mwadui leo jioni. Habari hizi ni kuwa umetokea wizi wa ajabu, maana almasi zote zilizokuwa tayari kusafirishwa kwenda kwenye masoko yake zimeibiwa!"

"Zimeibiwa? Saa ngapi?"

"Anasema ni kati ya saa kumi na saa mbili usiku huu!"

"Kwa hiyo inaonekana majambazi hawa wameamua kuchukua kwa mara ya mwisho na kukimbia."

"Hata mimi nafikiri hivyo hivyo."

"Nafikiri ndiyo sababu Khasimu alinieleza kwamba nifungashe vitu." Amanda alinieleza.

"Nadhani walikuwa wamefanya mpango wa kuziiba hizo almas halafu watoroke nchi za nje."

"Hiyo ni kweli kabisa na vile vile Chifu kanieleza kuwa wale watu uliompigia ripoti watiwe ndani chini ya usalama anashangaa kupata habari kuwa wote hawaonekani na wala haijulikani wako wapi. Mbinu za kila aina zimetumiwa na idara ya upelelezi, Polisi lakini hawaonekani kabisa".

"Ahaa. Sasa naanza kupata mwanga mkubwa. Hii ina maana kuwa wote wameondoka kuja Maganzo kugawana hizi almasi halafu kila mtu aangalie usalama wake, baada ya kuona karibu watashikwa. Hii ikiwa ni kweli lazima wataonana mahali fulani hapa mjini au wameshaonana au wanaonana saa hizi".

"Vile vile kumbukeni kuwa Khasimu alisema kwenye simu anamtegemea Mzee leo saa nne." Amanda alitukumbusha.

"Kwa hiyo hii inazidi kudhihirisha kubuni kwetu. Na kama hata Mzee wao yuko hapa hapa bila ya shaka inabidi tujitoe mhanga na tulikamate hili kundi kabla halijasambaa. Au unasemaje Patrick?"

"Itabidi tuwe tayari kupambana na Elungata. Maana nahisi huyu Elungata ambaye ni Joel tu aliyewahi kusikia sauti yake, huenda ndiye wanamwita Mzee. Kwa hiyo ndiye kichwa". 

"Bila shaka, lazima tupambane naye. Lililopo sasa ni kufanya mpango wa namna ya kuwasaka watu hawa",

"Mimi ninavyofikiria, lazima tumkamate Khasimu na Pweke kwanza. Hawa watu wawili ndio watakaotupeleka hata kwenye kichwa".

"Sawa Patrick, Khasimu alikuwa amemchukua Amanda kati ya saa sita sasa ni saa ngapi?"

"Saa saba na nusu." Amanda alijibu.

"Kwa hiyo atakuwa amesharudi nyumbani halafu atakuwa amemkuta Amanda. Hii itamfanya acheleweshe mipango yake kwani hatajua Amanda yuko wapi. Na kwa vile anampenda sana, atajaribu kumtafuta na hii itatupa sisi nafasi ya kuweza kumpata", 

"Milimweleza ndugu Mbogo awe hapa kabla ya saa nane unusu, ikiwa hatakuwa amefika ina maana kuwa jambo fulani limemtokea na itabidi kumfuata kwa hiyo mimi naonelea tujilaze kwa muda huu mchache wa saa moja unaweza kutusaidia kupoteza usingizi mpaka hiyo saa nane unusu"

"Sawa Patrick nafikiri nyinyi watu wawili mnahitaji sana huo usingizi hasa Amanda ambaye hakuzoea kukaa macho hadi saa hizi".

"Na wewe pia lazima ukumbuke bado unaumwa kwa hiyo wote hatuna budi kupata usingizi kabla ya mapambano dhidi ya hawa majambazi hayajaanza" Amanda alisema.

Tulizima taa tukajilaza mimi kichwa kilikuwa bado kinanigonga sana lakini ilinibidi kujitahidi niweze kufanya mapambano ya mwisho kwa hawa majambazo, Mambo haya yalinikera sana kuwa sikuweza kupata usingizi mnamo saa nane na dakika ishirini mlango wa chumba uligongwa, bastola mkononi, Patrick alienda kuufungua.

"Uko salama", aliuliza huku akiwasha taa.

"Salama".

Sisi wote tukaamka na kukaa.

"Itabidi tuondoke hapa mara moja wanatutafuta", alisema Wilfred Mbogo.

"Wamejuaje?" Niliuliza.

"Nitawaeleza njiani watafika hapa wakati wowote". 

Tulichukua vitu vyetu na mara moja tukawa tunaondoka. Patrick alinipa bastola mbili zenye kiwambo cha kunyamazisha sauti.

"Mimi nafikiri tubane tuwasubiri. Tukiwa na bahati ya kushika mmoja wao anaweza kutupeleka mpaka kwa huyo wanaemuita mzee", nilishauri.

"Sawa, lakini kama ni hivyo itabidi Amanda atusubiri mahali fulani kwani panaweza kutokea mapigano makubwa sana", Patrick alishauri.

"Hata kidogo na mimi lazima niwe katika hayo mapambano mpaka nione mwisho wake. Nikifa kwa ajili ya Joel nitakuwa nimekufa kifo cha fahari, Niko nanyi mpaka mwisho mtake msitake".

"Haya mama ni mapenzi yako", nilimjibu.

Kabla hata Wilfred hajaanza kutueleza gari likatokea kwa kasi lakini lilikuwa bado mbali kidogo. Nafikiri ni hao, Wilfred alipiga kelele.

"Wote kwenye majani", niliamrisha.

Karibu na nyumba kando ya barabara kulikuwa na majani marefu basi tulijificha humo gari lilikuja kasi lilipofika karibu na hiyo nyumba likafunga breki na watu wote watano wakatoka na bastola zikiwa mikononi. 

"Ila Willy na Amanda wanahitajiwa kwanza". Mmoja wao aliwaeleza wenzie.

Kila mmoja akachukua sehemu yake tayari kwa mashambulizi, watatu walibaki nje wawili wakaingia ndani. Wote tulikuwa tumelala karibu karibu. "Patrick unaweza kufungua buti ya hiyo gari?" Nilimuuliza kwa sauti ya kunong'ona.

"Naweza bila ya wasiwasi".

"Mimi nataka niingie kwenye buti ndani nikiwa na bahati wanaweza kunifikisha kwenye watu wenyewe ninaowatafuta".

"Wazo zuri," alijibu mwenzangu. "Hata tukisema tuwaue hawa tutakuwa hatujafanya lolote. Naona twende wote ndani ya buti la hilo gari,  Amanda na Wilfred watatusubiri kwa Wilfred".

"Najua mkifanya hivyo safari yenu ni mpaka Shinyanga sasa hivi hakuna muda wa kuelezana niliyosikia. Tuonane Shinyanga Relwe nyumba nambari 13. Mimi na Amanda tutasubiri hapo", Wilfred alitoa rai.

"Oke vizuri," nilikubali.

Gari lilikuwa karibu sana na tulipokuwa, "Nendeni mimi nitawalinda ikiwa watawaona," Wilfred alisema. 

Tulinyata na kwa sababu mawazo yao yote yalikuwa ni ndani ya nyumba, tuliweza kuingia ndani ya buti ya kuwashitua. Buti la gari kama alivyosema Patrick lilikuwa kubwa sana, mlikuwa na taili moja na supana. Hewa iliyokuwamo ilikuwa kidogo lakini ingeweza kututosha.

"Wameisha ondoka ndani ya chumba hamna mtu wala kitu," tulisikia mmoja wao akisema, "Twendeni zetu tukatoe habari mara moja, huenda ana wazo au habari za mahali walipo."

Waliingia ndani ya gari na safari ikaanza. Walielekea barabara ya Maganzo. Mara kwa mara tulifungua mlango wa buti kuingiza hewa na kuangalia wapi tulipokuwa. Walipofika Maganzo hawakusimama bali waliendelea moja kwa moja kwenye barabara inayoelekea Shinyanga. Kwa vile walikuwa wakienda kasi sana. Patrick na mimi niliweza kunong'onezana juu ya mpango wetu na tulimuomba Mungu atusaidie.

Kama tulivyokuwa tumebuni gari liliingia Shinyanga mjinina kuelekea barabara iendayo nyumba za watu wa hali ya juu. Kisha gari likasimama na kuzima injini. Mlango wa geti ulifungwa na dereva aliamurishwa kulisogeza mpaka mbele kidogo. Punde milango ikafungunguliwa wakatoka nje.

""Twendeni ndani, wanawasubiri kwa hamu sana", kiongozi wao alisema.

Tuliwangoja waende kwanza. Hatmaye tukainua buti ili kuona kama hakukuwa na mtu. Tulipohakikisha kuwa ni salama, nikashika kifuniko cha buti ili Patrick atoke kwanza kisha nami nikafuata. Bahati mbaya nikagusa debe, likapiga kelele. Mtu wao mmoja aliyekuwa kwenye mlango wa mbele ya hiyo nyumba akaja kuangalia. Sisi tukabana kwenye sehemu ya seng'enge ya ua. Alipokaribia Patrick alikuwa ameshamzunguka. Akamnyemelea, akamkata 'karate' ya shingo na kufa hapo hapo. Hatmaye akanigeukia na kuniamrisha.

"Nenda sasa, lakini jihadhari sana".

"Hakuna taabu", nilimpa imani. 

Nilipitia mlango wa mbele, nikaingia ndani. Nilisikia sauti zinatoka kwa mbali kwenye chumba cha ndani. Nilipotaka kuingia mlango ukafunguliwa, nikabana. Akatoka mtu mmoja na bastola mkononi. Kwa vile hamkuwa na taa kwenye ukumbi, hakuniona.Nikamlisha risasi na alipoanguka nikamvuta. Nikamtupa kwenye magunia yaliyokuwa karibu na hapo.

Nilifungua mlango wa nyumba taratibu.Taa zilikuwa zinawaka lakini hakukuwemo mtu. Nilisikia sauti zikitokea kwenye chumba cha pili yake. Nikazima taa za chumba hiki cha kwanza nikaenda mpaka kwenye mlango wa chumba cha pili. Nikasikia sauti ya kiaskali ikifoka.

"Kwa nini mlirudi. Nendeni mkawatafute mpaka muwapate. La asivyo msirudi watu kumi na wawili hamuwezi kushindwa na watu wawili"

"Tutajaribu" Mwingine alijibu.

"Hakuna kujaribu" 

Nilihisi hiyo sauti ya Khasimu maana ilikuwa ya kiaskari hasa.

"Khasimu lazima uende nao mumtafute Willy na Umuue pamoja na mwenziwe" sauti hii moja iliamuru.

"Ndiyo Mzee" Khasimu alijibu kwa sauti ya woga.

"Twendeni" walijihimiza.

Mlango wa chumba nilichokuwemo ukafunguliwa 

"Nani alizima taa ?" Khasimu aliuliza.

"Sijui, huenda Saidi" alijibu mmoja wao.

"Washa" 

Taa haikuwaka. Nilikuwa nimetoa globu yake. Wakati huo nilikuwa nimebana nyumba ya mlango.

"Hamna globu" 

"Nini?"

"Hamna globu" 

"Angalieni huenda Willy tayarai yupo hapa" Khasimu alitahadharisha.

Kundi lote lilikuwa humo chumbani na wote walikuwa bado hawajaniona. Vilele hawakuwa wanategemea, hivi hawakuwa tayari. Kwa hiyo nikachukua nafasi ya kumjibu.

"Ndiyo tayari niko hapa Elungata." 

"Nikaachia risasi toka kwenye bastola zangu mbili na kuwaua wote, maana wote walishikwa na bumbuwazi.

"Njooni,njooni ndani tumeingiliwa. Willy ndani, tumeingiliwa Willy yuko ndani, mkamateni." Sauti ya kutisha ilisikika.

Nilirukia chumba cha pili. mlikuwa hamna mtu tena kulikuwa na mlango unaoeleka chumba kingine. Nilirudi nyuma bastola ikiwa mkononi. Nikaruka nikaupiga teke na kuingia ndani huku nikiviringika sakafuni. Hamna mtu! Niliposimama tu. Pweke alikuwa tayari amesimama mlangoni na bastola mkononi. Kwa vyovyote vile angeniwahi.

"Weka bastola chini" alihamru.

"Mpelee sebule ile. Mikono juu" Nikaweka mikono juu

"huna ujanja tena!" 

Nilipofika sebuleni nikashangaa kumuona Patrick naye amekamatwa amefungwa kwenye kiti na huku damu zikimtoka hovyo. nikajua kwamba tumekwisha.

"He, He unashangaa kumuona mwenzio Patrick? Mtanikoma" hiyo sauti ya kutisha ilisema, "Willy Gamba, huu ndiyo mwisho wako. Wengi wamejaribu wameshindwa. Wewe umejaribu sana, na kwa hiyo ninakupongeza."

"Sina haja ya kupongezwa na wewe". 

"Wewe ulijaribu kuingilia himaya ya Elungata, aliyoijenga kwa miaka mingi. Je, Ungeweza?" 

Nikasikia sauti zinajibu "Asingeweza!" nikajua ya kwamba majambazi wenziwe walikuwa tayari wamewasili na wote walikuwa hapa Khasimu tu ndiye alikuwa amekufa.

"Leo, Gamba, ni siku ya furaha sana kwangu na vijana wangu. Siku ambayo nimeweza kuichukulia Serikali kiasi cha Almasi inayotoka kwa mwaka mzima. Ni utajiri ulioje! na wakati huo huo Gamba unauawa mbele ya macho yangu nilifikiri kwamba baada ya leo nitaacha shughuli hii. Lakini sasa nitaendelea, maana baada ya kusikia umekufa hakuna hatakayethubutu tena."

"Una kichaa, hujui kuwa wananchi wa nchi hii hawatakata tamaa bali wataendelea kupambana nawe na kundi lako kwa ujasiri na ari zaidi, ili mradi kulinda uchumi wa nchi yao. Hawatakata tamaa kupambana na mtu juha kama wewe. Wengi wataendelea kujitoa mhanga mpaka siku watakayoweza kukuweka mbaroni. Wamenyonywa na wakoloni na sasa wamekataa kuonewa tena. Wakoloni wenyewe wanawaogopa wananchi wa nchi hii. Hawataki kuonewa wala kunyonywa tena sembuse wewe kibaraka chao. La hasha wananchi watakumaliza, na siku hiyo watakugawanya vipande."

"Ha, ha, ha! wewe ndiye mwenye kichaa nini kizuri kuliko pesa? utajiri. Ha ha ha, pesa inanunua kila kitu. hawa wananchi unaowasema hii pesa itawanunua na himaya yangu itakaa milele."

"Wananchi wa nchi hii wanajali utu na kulinda uhuru wao, hawajali fedha. Hao wanaojali fedha ndiyo majuha kama wewe na hao tutawapiga vita na kuwamaliza kama tulivyommaliza mkoloni"

Mpaka dakika hii nilikuwa nasikia sauti tu yeye alikuwa haonekani.

"Kabla hamjaniua nawahakikishia kwamba Elungata na wenzio akina Johnstone MWita, Mashaka Athumani, Samweli Gichuki na Tom Omondili, Pweke na bibi yako Tausi, hujuma za wananchi zinawasubiri".

"Piga magoti mbwa wee!" Pweke aliamuru.

"Kwa kheri Willy Gamba pamoja na rafikiyo Patric. Tangulieni ahera. Elungata anawatakieni maisha mema huko. Mnalipia matendo yenu ya kuniingilia!" Pweke alitoa upanga mkali. Mara akatokea mtu mwingine naye na upanga mkali. akasimama nyuma ya Patrick.

"Nikisema moja mbili tatu mnawachoma moyoni kwa pamoja mmesikia?" Elungata alisema kwa sauti ya ghadhabu.

"Ndiyo Mzee" walijibu kwa pamoja.

Haya moja mbili ta...

ITAENDELEA 0784296253

ACACIA YAWAAGA WAFANYAKAZI 1,200

 Wafanyakazi katika mgodi wa Bulyanhulu, ulioko mkoani Geita wakakiendelea na maandalizi ya sherehe ya kuwaaga wafanyakazi 1,200 waliopunguzwa kazi. Muonekano wa viti watakavyokaa wafanyakazi wa Acasia. Magari yakiwa yamepaki. Baada ya Acacia kukamilisha usitishaji wa uchimbaji madini katika mgodi wa Bulyanhulu. Mgodi huo umepunguza wafanyakazi 1,200, wakandarasi 800 na kubaki wafanyakazi 200. Ikielezwa kuwa mwenendo wa soko la madini kutikisika.
 Sehemu iliyoandaliwa kwa sherehe ya kuwaaga wafanyakazi 1,200 waliopunguzwa kazi katika mgodi wa Bulyanhulu.
Magari rasmi yaliyokuwa yakifanyakazi ya kuhamisha mchanga mgodini yakiwa yameegeshwa na Kampuni ya Acacia

Friday, September 15, 2017

KIKOMO

SEHEMU YA NANE

Nilipozinduka nikajikuta kwenye chumba kidogo, nikiwa nimelazwa kitandani na huku nimefungwa bandeji kila mahali nilipokuwa nimeumia na nilipoinua macho karibu yangu alikuwa ameketi msichana mrembo sana huku akitabasamu nikashangaa.

"Unajisikiaje sasa?" Aliniuliza.

Nikatabasamu.

"Mbele ya mtoto mzuri kama wewe nitashindwaje kujisikia vizuri".

"Watu wa hali yenu ni watu wa ajabu sana".

"Kwanini?".

"Hata hushangai umekujaje hapa?".

"Ili mradi nimetibiwa na msichana mrembo kama wewe, na unaniganga na hakuna watu wenye sura zilizokunjana wakiwa wameshikiria bastola, najua niko kwenye mikono mizuri".

"Ni kweli".

Nilijaribu kuinuka.

"Daktari amesema upumzike kwa muda mpaka upate nguvu".

"Tayari nina nguvu, sasa ni saa ngapi?"

"Saa saba unusu usiku".

Nikatambua kuwa nilikuwa nimezirai kwa muda wa masaa matano hivi na nikataka kujua nini kilikuwa kimenitokea muda wote huo ili niweze kujua nini cha kufanya maana hata hapa nilipokuwa sikujua ni wapi na huyu msichana sikujua ni nani.

"Wewe ni nani na hapa ni wapi?"

"Mimi naitwa Amanda Mwakasege, na hapa ni nyumbani kwa rafiki yangu, Songwe Madukani.

"Nani alinileta hapa?"

"Mimi na Patrick".

Moyo wangu ulishtuka kwa jina hilo.

"Yuko wapi?"

"Amerudi Maganzo na atarudi wakati wowote".

"Kwa hiyo nyinyi ndiyo mlioniokoa kutoka mikononi mwa Pweke?"

Bila shaka".

Hii ilinishangaza sana.

"Nafikiri uko tayari kunieleza juu yako mwenyewe na jinsi gani unahusika katika kesi hii, maana wewe hukuajiriwa pamoja na sisi. Vile vile jinsi gani mlijua nilipokuwa na vile mlivyoniokoa".

"Nitakueleza kwa ufupi ili uweze kujua mpaka sasa pilikapilika yako hii imefikia wapi".

"Asante, endelea".

"Mimi naitwa Amanda Mwakasege, kama nilivyokwisha kukueleza. Ni Mwandishi mahsusi wa Meneja wa Kampuni ya Mwadui. Utashangaa nimejiingizaje katika jambo hili au sivyo?".

"Nina mshangao mkubwa sana, maana ukiwa mwandisi halafu ujiingize kwenye jambo la hatari namna hii haieleweki."

"Kweli haieleweki. Mimi nilikuwa na mchumba wangu akiitwa Inspekta Joel Zonga, nafikiri uliwahi kumsikia?|

"Nilikuwa nimesikia habari zake ambazo zilitokana na kifo chake. Alipata ajali ya ndege iliyokuwa mali ya Kampuni Mwadui alipokuwa akisafiri kwenda Mwanza kikazi. Mpaka leo chanzo cha ajali hiyo hakikujulikana maana ndege ilipasuka vibaya mno. Polisi walikisia kuwa mlikuwa na bomu lililotegwa lakini hawakuweza kuendeleza upelelezi wao mbali".

"Ndivyo ilivyokuwa."

"Pole sana".

"Siku moja Joel alikuja nyumbani kwangu akiwa na mawazo mengi sana. Nilitengeneza chakula lakini hakuweza kula vizuri. nikajua alikuwa na kitu kilichokuwa kinamsumbua nilimdadisi sana mwishowe akanieleza. Alinieleza ya kwamba alikuwa hapendezewi na jinsi mambo yalivyokuwa yakienda hapo Mwadui na kwamba alikuwa ameamua kufanya uchunguzi madhubuti.

"Alinieleza kuwa alikuwa amefanya uchunguzi kiasi na kuona ya kwamba kulikuwa na mpango wa hali ya juu sana wa kuiba almasi toka Mwadui! Ila alisema kilichokuwa kinamkera ni kwamba angeweza kuwa hatarini.

"Alieleza ni nini kilichomfanya afikiri hivyo?"

"Alikuja kunieleza baadaye. Aliendelea na uchunguzi wake na hatukulizungumzia jambo hili tena. Baada ya miezi miwili hivi siku moja alikuja akiwa na hali isiyo yake ya kawaida. Nilipomuuliza alinieleza ya kwamba mambo aliyokuwa anafikiria ni kweli na sasa alikuwa hatarini.

Alinieleza kwamba alikuwa amekata shauri kunieleza jinsi mambo yalivyokuwa kusudi ikiwa jambo lolote likimpata siku moja anaweza akaja mtu mwenye kuweza kuendeleza upelelezi huu na habari hizi zingemsaidia sana. Nilimwambia asiseme hivyo, na siku hiyo alilia sana.

"Alieleza nini?"

Alinieleza kuwa maafisa wengi wa polisi wa chini wa hapo Mwadui walikuwa wamehongwa na kundi la majambazi ambalo lilikuwa linaendelea na kuendesha wizi wa hali ya juu wa almasi toka Mwadui na ndiyo sababu hali ya uchumi utokanao na machimbo hayo ya almasi ulizidi kwenda chini siku hata siku.

"Alisema kuwa hili kundi lilikuwa limepachika watu wake kila idara na kila sehemu zinazohusika na almasi. Na hawa watu ndio walikuwa wakitorosha almasi kidogo kidogo na kwa sababu polisi waliokuwa wanahusika wote wamehongwa na walikuwa wanawajua basi ilikuwa rahisi sana kwao kutorosha almasi.

"Alinieleza kuwa katika miezi hii miwili aliweza kukamata watu kama kumi ana kwa ana na almasi mkononi lakini alipoenda kupiga ripoti kwa maofisa wa juu waliweza kutaka hata kumgeuzia yeye kuwa ndiye mwizi. Hata akanieleza kuwa siku moja wamewahi kuficha almasi nyumbani kwake halafu kukafanywa uchunguzi zikutwe kwake lakini yeye alinong'onezwa kabla na rafiki yake mmoja na walipofika hawakukuta kitu.

"Kutokana na uchunguzi wake alikuwa amegundua kuwa kwa nje kulikuwa na mtu aitwaye Pweke, ndiye alikuwa mkubwa wa kundi na alikuwa mfanyabiashara wa hapo Maganzo. Kwa ndani mtu aliyekuwa akiongoza kundi Inspekta Mwandamizi Khamis Omari. Huyu Khamis ndiye aliyekuwa anapokea habari na ndiye aliyekuwa kiungo kati ya kundi la nje na la ndani. Vile vile kwa wafanyakazi wa idara zingine".

"Kwanini hakupeleka habari hizi kwa Mkuu wa Polisi wa Mwadui au Mkuu wa usalama?"

"Alisema alijaribu kupeleka kwa Mkuu wa Polisi, lakini alipuuzwa na kuelezwa kwamba alikuwa anaanzisha majungu jambo ambalo serikali haipendi hasa jeshini na kwa hivi angeweza kuchukuliwa hatua. Alipoona hivi akaonelea aendelee kufanya uchunguzi wake yeye mwenyewe sasa. Siku aliyokuwa amekuja kwangu na huzuni kunieleza mambo haya ndiyo siku aliyokuwa amekuja kwangu kunieleza kuwa amepata kitisho kutoka kwa mtu aliyekuwa akiitwa Elungata akisema asiingilie mipango yake la sivyo maisha yake yangekuwa mafupi sana".

Jina la Elungata mara moja nilikumbuka kwani marehamu Matayo Buluba alikuwa ameniletea barua kutoka kwa marehemu Jack Mbwile na hiyo barua ilikuwa na neno moja tu 'Elungata' Sasa nilianza kuona mwanga zaidi.

"Aliweza kuchunguza na kujua huyu Elungata alikuwa nani?".

"La hasha. Baada tena siku moja kwenye Mkahawa wa polisi hapo Mwadui alinieleza kuwa alikuwa amegundua tu ya kwamba Pweke siyo mkubwa kabisa wa kundi ila mkubwa alikuwa Elungata, lakini ajabu huyu Elungata hata hakuweza kupata fununu yake".

Wiki tatu zilizopita akaja siku moja kuniaga kuwa alikuwa anaenda Mwanza kuonana na Mkuu wa Polisi wa Mwanza ampe habari hizi kwa maana sisi tulikuwa tumekata shauri ya kuoana baada ya mwezi mmoja toka siku hiyo kwa hiyo asingekuwa na nafasi ya kuendelea na uchunguzi. Na siku hiyo alipoondoka ndiyo waliyomtega bomu katika ndege. Akafariki".

Alianza kulia. Nilimvuta na kuanza kumbembeleza.

"Basi, basi kifo ni mapenzi ya Mungu. Ni jambo la kusikitisha sana lakini kulizuia hatuwezi. Yeye alipangiwa na Mungu mwisho wake uwe huo. Ulikuwa mwisho wa fahari maana alikufa kwa sababu ya kupenda nchi yake na kwa kuitumikia vizuri. Maadui wa maendeleo yetu wamemuua. Kwa hilo linalotupasa mimi na wewe ni kuwafutilia mbali hawa maadui wa nchi yetu".

"Asante Willy lakini ni vigumu kusahau na vile vile ndiyo sababu nimejitoa mhanga wa kufa na kupona kusudi watu waliomuua mpenzi wangu Joel na wao watiwe nguvuni".

"Joel alikueleza haya yote kwa sababu alijua atakuwa hatarini na alifanya vizuri. Je umetimiza wajibu wako kwa mzigo aliyekuachia?".

"Nafikiri leo hii na dakika hii nimetimiza wajibu. Hata hivyo baada ya mazishi na matanga sikukaa bure. Uchungu niliokuwa nao ulifanya nami nianze uchunguzi wangu. Inspekta Mwandamizi Khasimu Omari ambaye ndiye bila shaka aliyepanga kuuawa kwa mpenzi wangu Joel alikuwa akitaka mapenzi nami siku nyingi. Niliporudi tu kazini baada ya matanga alianza kunifuatafuata".

..."Alinieleza kuwa ili niweze kusau mapema kifo cha ghafla cha mpenzi wangu ilinibidi nipate mtu wa kunifariji kwa sababu nilikuwa najua habari zake, wazo lilinijia kuwa ningeweza kupata habari za kunisaidia kuchunguza kifo cha mpenzi wangu joel".

"Kwa hiyo ukamkubali!"

"Nilimkubalia kwenye mdomo tu si rohoni".

"Sawa".

"Siku moja nilianza kwa kumsifu juu ya vile alivyo tajiri kuliko polisi wengine, jinsi alivyokuwa na akili kuliko polisi wengine na kadhalika. Nilimweleza kuwa ningejua kwamba yeye ana pesa hivyo hata nisingejisumbua kupoteza muda wangu na Joel. Nikamweleza kuwa ni bahati nzuri upande mwingine kwamba Joel amekufa. Hii ilimfurahisha sana akaanza kujitapa akanieleza kuwa yeye alikuwa tajiri sana na utajiri wake usingeweza kupungua kwani alikuwa ameishashika Mwadui nzima mkononi mwake."

"Siku hiyo nilimfanyia mapenzi ya kila aina mpaka akanieleza juu ya siri zake. Akanieleza baada ya muda si mrefu angeacha kazi na kunioa halafu tungeenda kuishi nchi za nje. Aliniambia ana almasi chungu nzima. Nikamkebehi ya kwamba mbona nasikia kwamba Pweke ana hela kuliko yeye. Akacheka na kusema bila ya yeye Pweke si kitu".

"Hakugutuka kuwa unamfahamuje Pweke?".

"Asingeweza, maana Maganzo nzima wanamfahamu Pweke. Ana pesa chungu mbovu. Wakati wote huu nikawa natafuta njia ya kujua mengi lakini sikuweza kuwa na bahati. Waswahili husema mvumilivu hula mbivu, kwa hiyo mimi nikaendelea kumganda nikisubiri bahati yangu huku nikimlaghai kwa mapenzi kwa kweli ya Mungu mengi jana ndiyo siku yenyewe.

"Jana alikuja nyumbani kwangu huku jasho likimtoka. Nikatengeneza chakula kama kawaida, lakini hakuweza kula na alionekana na wazo linalomsumbua au tuseme mawazo yalikuwa mengi sana. Nilimuuliza nini kilikuwa kinamsumbua. Hakutaka kunieleza. Nikazidi kumbembeleza. Nikambusu, nikamweleza kuwa matatizo yake ni yangu na mimi kwa vile nilikuwa nimekata shauri la kuolewa sikuona kwa nini anifiche jambo lolote hata kama ni kuua mtu.

"Mwisho akanieleza kuwa mpelelezi mmoja maarufu wa serikali kwa jina la Willy Gamba alikuwa ameanza kuleta matatizo. Nikamwambia mtu mmoja tu si kitu, hatamudu kufanya lolote, kwa hiyo asijali hata kidogo. Basi akafurahi akanishika akanibusu.

"Akanieleza kwamba ameonelea lazima achukue livu kesho yake maana tungeweza kuondoka ghafla kwa muda. Nilimwambia kwamba isingekuwa taabu. Moyoni nikajua nafsi yangu imefika ya kumtafuta huyu Willy Gamba ili nimweleze yote niyajuayo ili kwamba nitakuwa nimemlipizia kisasi mpenzi wangu Joel."

"Ama kweli umekuwa kiumbe wa ajabu! Umeweza kufanya yote haya kwa ajili ya mpenzi wako Joel basi".

"Nakwambia, watu hawajui. mwanamke akipenda kitu huvumilia sana usituone hivi!"

"Kweli nami nimeona kitu kiitwacho mapenzi ya kweli maana mtu kafa na bado anapendwa tu".

"Basi leo asubuhi nikaenda ofisini. Nikachukua livu, nikampigia simu sikumpata kwa simu ofisini wala nyumbani. Nikakata shauri kwenda nyumbani kwake sikumkuta lakini mimi nina ufunguo mwingine wa nyumba yake nikaingia ndani, nikaenda chumba cha kulala nikachukua bia, nikajilaza kitandani nikinywa huku mawazo yakinitembeatembea.

"Mnamo saa sita hivi nikasikia watu wanacheka ukumbini nikasikia mwingine akisema Willy kafa kifo cha kijinga sana cha kugongwa na gari moshi. Khasimu akajibu, ndiyo, sawa hiyo, hakuna hata cha kuuliza. Basi roho yangu ikafa kabisa niliposikia hivyo. Nikajua matumaini yangu yamekwisha".

"Naona nina maisha marefu," nilisema kwa furaha.

"kweli una maisha marefu. Khasimu aliponikuta chumbani akaja akanibusu. Nikamuonyesha karatasi zangu za livu. Akaniambia kwamba sasa hamna wasiwasi, tungepanga mambo yetu taratibu. Wakati bado tumekaa, simu ikalia. Alienda kuzungumza na nikasikia akisema, George, basi wamalizie mbali mbali na yeye halafu hana wasiwasi Ole yuko Mwanza, atamaliza tatizo hilo halafu akarudi".

"Na katika watu wanaovumilia wewe nambari moja!" Nilimpongeza, "Wanawake kwa kawaida wangekuwa wameisha ropoka".

"Kila nikimfikiria Joel, roho yangu inakuwa jasiri sana. Mnamo saa kumi na moja na nusu hivi simu ikalia. Khassimu alikuwa amelala akaamka na kwenda kuijibu. Nikasikia akisema kwa hasira, nini? Willy yuko hai? Willy au jina lake? Nani, Ole? Ole kafa! lo, mambo yameharibika. Washenzi hao Pweke hakikisha Willy akiingia Maganzo Bar, ndiyo hoteli yake, lazima auawe mara moja. Nani kakupa habari? Basi lazima atafikia Maswa Bar, ndiyo hoteli yake kama atakuwa kaondoka kule saa kumi na moja, saa moja hivi atakuwa Maganzo. Mtume Tausi saa moja pamoja na kundi, yeye ni mbovu sana kwa wanawake. Lazima akimuona tu Tausi hawezi kumwachia. Mpeleke kwenye banda mkiweza kumkamata, mwuweni huko huko. Mimi nitazungumza na mzee najua atakasilika sana. Tuonane kwenye chumba chetu Bantu. Wengine wote watafika saa nne usiku kwaherini!"

"Kisha akaja akaniambia, mpenzi fungasha nguo zako chache na zangu mimi nitarudi kwenye saa tano au sita hivi nina shughuli.

"Nikamwambia, hamna taabu. Alipoondoka tu na mimi nikaanza kutafuta njia gani ya kuwahi kufika Maganzo kabla ya saa moja niweze kukupa tahadhari. Nilitafuta gari mpaka kwenye saa moja ndipo nilipopata. Kufika Maganzo na kuingia Maswa Bar saa moja na nusu, na nilipoangaza angaza nikaona hakuna dalili ya mtu kama wewe. Nikajua tayari wamekuwahi. Nikajua wamekupeleka kwenye banda. Na banda mimi nililijua, nilishapelekwa na Khasimu, lakini kukufuata peke yangu ilikuwa haiwezekani. Nikatoka nje ya baa, nikaanza kulia. Bado machozi yananitoka nikaona taksi inasimama na anatoka mtu na mfuko. Moyo ukanieleza ndiye wewe, nikamkimbilia huyu mtu. Bila ya hata kuogopa nikamuuliza kama yeye ni Willy Gamba? Akashituka na kuniuliza, 'kwanini?' Nikamwambia wanakutafuta watakuua. Wanajua utakuja hapa bila ya shaka.

Alinivuta kando, kisha akanieleza kuwa yeye anaitwa Patrick na ni rafiki yake na Willy Gamba. amekuja kukutana na Willy hapo. Ndipo nikamweleza mipango yao yote. Akafungua mfuko wake, akatoa bastola mbili. Akazijaza risasi akaniambia nimuonyeshe hilo 'banda' lilipo. Basi nikampeleka mpaka kwenye banda. Hii nyumba inayoitwa 'banda' imejengwa mbali kidogo na nyumba zingine. Khasimu alisema hutumika kama kuna sherehe fulani ya vinywaji. Basi nikamleta na kumuonyesha nyumba akanipa mfuko na tukaanza kuinyemelea nyumba akiwa na bastola mbili tayari.

"Upande wa mlango wa kuingilia, tukamuona mtu na bunduki, Patrick akamnyemelea akampiga konde la shingoni, akazirai bila ya kutoa sauti. Mwingine alikuwa akiangaza upande mwingine, Patrick akamwahi na risasi lakini bunduki haikupiga kelele. Ndipo katika kusikiliza akasikia sauti inatokea kwenye chumba walichokuwa wanakutesa. Alipoangaza akaona dirisha juu kabisa. Akapanda juu kama nyani. Alipofika juu alipiga waya wa umeme na wakati huo huo alikuwa ameishawaona walivyokaa na wewe uliko kwa hiyo ilikuwa rahisi kuwawahi hao wenye silaha. Anasema usingejitupa na kiti wangeweza kukupata na risasi. Wale watatu wenye bastola wote amewaua. Pweke na Tausi wamekimbia. Basi Patrick akaniita, akakufungua, tukakubeba na kukuweka kwenye gari la Tausi. Patric akafungua boneti akaliwashia huko hadi tukafika hapa.

"Hiki ni chumba cha rafiki yangu, anafanya kazi stesheni ya reli hapa Songwa lakini yuko likizo. Tulienda kumtafuta daktari akaja akakutibu na akasema hukuvunjika chochote ila tu umepoteza damu nyingi. Akaomba upumzike mpaka kesho asubuhi utapata nafuu. Hivi ndivyo ambavyo tumeweza kuonana. Ni hadithi ndefu au sivyo?"

"lO, ama kweli ni ajabu na kweli. Sina budi kukushukuru sana"

"La hasha! usinishukuru. Nifanyalo ni wajibu wangu ili kulipiza kisasi cha Mpenzi wangu Joel!"

"Hakukueleza Patric yuko wapi?"

"Amewafuata Bantu ambako walisema wataonana"

"Ameenda pekee yake? Watamuua ni watu wabaya sana"

"Hapana, ameenda na mdogo wa yule daktari maana wao pia wanakisasi na Pweke maana alikataa kufanya mapenzi nao na huyu kijana ni Polisi wa relwe"

"Bado haitoshi lazima niwafuate"

"Una silaha? Silaha huna tena bado una maumivu. Wily usiende Patric na huyo kijana Mungu atawasaidia na watamudu"

"Silaha nitapata usijali lazima niwafuate.

Nikasikia sauti nje ya mlango wa chumba.

"Huna haja ya kuwafuata"

Jasho likatutoka wote.


ITAENDELEA 0784296253

NABII WA KIMATAIIFA KUOMBEA NCHI NA VIONGOZI

Mhubiri wa Kimataifa Prophet Nicolaus Suguye (pichani), wa Kanisa la Huduma ya The Word of  Reconciliation Ministries (WRM), lenye Makao Makuu yake Kivule Matembele ya pili Jijini Dar es Salaam,  akishirikiana na vingozi mbalimbali wa kiroho watafanya maombi maalum ya kuliombea Taifa Tanzania na viongozi wake, ili Mungu awaepushe na mabaya yote, ili kuwe na upendo amani na utulivu uzidi kudumu kwa ustawi wa jamii na taifa kwa ujumla.

Tukio hilo maalumu linatalajiwa kutafanyika katika mkutano mkubwa wa injili, utakaohudhuriwa na watu wa dini zote na madhehebu yote kutoka ndani na nje ya nchi, utafanyika katika viwanja vya Hali ya hewa, vilivyoko Banana, Ukonga Dar es Salaam,  kuanzia Septemba 27 hadi Octoba Mosi mwaka huu.


Kwa mjibu wa Nabii Saguye, watu wenye shida mbalimbali wataombewa. Mtumishi huyo wa  Mungu, aliyabainisha hayo katika mahojiano maalum na Mwandishi Maalumu, alipotaka kujua kwa jinsi gani viongozi wa dini wanaunga mkono juu za serikali katika kuwaletea maendeleo ya wananchi. Nabii Saguye alisema kuwa huduma yake imekuwa mstari wa mbelee katika kusaidiana serikali katika suala zima la kuwaletea wananchi maandeleo na kuongeza ajira kupitia Nyanja tofauti ikiwemo vyombo vya habari vinavyomilikiwa na  Huduma hiyo.

‘’Tumekuwa tukifanya mambo mengi ya kimaendeleo lakini pia tumekuwa tukifunga  na kuwambea viongozi wetu ili Mungu azidi kuwatia nguvu katika kuwatumikia wananchi.Ttunathamini sana  kazi wanayoifanya katika kuwaletea wananchi maendeleo bila ubaguzi wowote.

Nabii Saguye amesema viongozi wa kiroho wana jukumu la kuombea nchi na serikali ili Mungu azidi kushusha neema na nguvu, kuwaepusha na hila mabaya katika kufanya kazi ya nchi ambayo ni kuwatumikia wananchi. Amesema wameandaa mkutano mkubwa  wa njili  hapa Dar es Salaam, kwa ajili ya kuombea viongozi wa nchi na kumuomba Mungu, amani na utulivu tuliyonao uendelee kudumu.


Amesema wanaunga mkono kazi Nzuri sana na iliyotukuka inayofanywa na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli. "Rais Magufuli amedhamilia kuwaletea watanzania maendeleo ya kweli’’  amesema Nabii Prophet Suguye

Aidha alisisitiza kuwa mbali na kuliombea taifa kutakuwa na maambezi maalum kwa ajili ya watu wote watakaohudhuria  Mkutano huo na wenye shida mbalimbali na wanasumbuliwa na majini na nguvu za giza watafunguliwa na kuwekwa huru baada ya  maombezi hayo.

Taarifa zinasema Mkutano huo  wa Injili wa siku tano  unategemewa kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kiroho na serikali kutoka ndani na nje ya nchi ya Tanzania na utakuwa wa madhehebu yote na dini zote bila ubaguzi wowote wa kiimani wala kidini.

 Nabii Prophet Nicolaus Suguye akipiga goti wakati wa maombi
 Nabii Prophet Nicolaus Suguye akiwaombea wananchi
Naboii Prophet Nicolaus Suguye akisoma Biblia.
Nabii Prophet Nicolaus Suguye akihubiri neno la uzima