HOFU

HOFU ni miongoni mwa vitabu vya hadithi za kusisimua za upelelezi kuhusu ukombozi Kusini mwa Afrika kilichoandikwa na Mwandishi Mahili wa vitabu vya Upelelezi nchini, shujaa wa Afrika Hayati A E Musiba. Kitabu hiki ni mojawapo ya vitabu vya Upelelezi vitabu vingine ni KIKOSI CHA KISASI, KUFA NA KUPONA, KIKOMO, UCHU na NJAMA, kisome kupitia NYAKASAGANI.BLOGSPOTI.COM.

SEHEMU YA KWANZA

PORT ELIZABETH

Ilikuwa tarehe 24 Machi, baada ya mauaji ya kikatili ya waafrika 19, katika kitongoji cha Langa, karibu na Vitenhage; mji ulio karibu na ule mji wa viwanda wa Port Elizabeth, katika Jimbo la Cape Mashariki. Mauaji hayo yalikuwa yamefanyika tarehe 21 Machi, siku ya kukumbuka mauaji ya kikatili kwenye mji wa Sherpville mnamo mwaka 1960. Wakati wazalendo 69 walipouawa kikatili. Mnamo tarehe hiyo ya 24 Machi, huko mjini Port Elizabeth kulifanyika mkutano katika ofisi ya Mkuu wa Polisi mnamo saa sita usiku.

Ndani ya chumba cha mkutano huo walijumuika watu ambao wamekuwa chanzo cha vilio na malalamiko mengi kutoka kwa wazalendo wa Afrika Kusini dhidi ya makaburu. Katika mkutano huo alikuwemo waziri wa sheria na usalama wa makaburu, Kamishna wa Polisi, Mkurugenzi wa shirika la Ujasusi la makaburu na Kamanda wa kikosi cha Jeshi kiitwacho 'KULFUT'yaani 'Gongo la Chuma' wote hao walikuwa ni makaburu. Lakini vile vile mkutano huo ulihudhuliwa na watu weusi ambao walikuwa wameitwa haraka haraka.

Hawa walikuwa wamefanyiwa mipango maalumu ya usafiri ili mladi wafike kwenye mkutano huo muhimu. Walikuwa wamesafiri kwa kutumia ndege ya Jeshi la Anga la makaburu. Weusi hawa walikuwa ni Mkuu wa Magaidi wa UNITA, wenye kupinga Serikali ya Angola, Mkuu wa Magaidi wa MNR wenye kupinga Serikali ya Msumbiji na Mkuu wa Magaidi wa LLA wenye kupinga Serikali ya Lesotho, kwa kifupi tu ni kwamba, Magaidi wote hawa ni vibaraka wa Serikali ya Makaburu na ilikuwa ni serikali ya makaburu iliyowagharamia kufanya ujahili dhidi ya nchi zilizo mstari wa mbele katika Ukombozi wa Afrika Kusini, ili kuzizorotesha kisiasa na kiuchumi kwa nia ya kuziangusha hatimaye. Waziri wa sheria, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa mkutano huo, alianza kwa kusema;

"Kwanza lazima nitoe shukrani zangu kwa nyinyi wote kuweza kufika hapa kwa muda uliopangwa, shukrani zangu za dhati ziwaendee nyinyi wageni wetu ambao mmetoka nje ya nchi hii. Pili tumeitana hapa usiku wa manane kuzungumzia suala muhimu sana. Ningependa tufanye na kumaliza mazungumzo yetu usiku huu ili muweze kuondoka kabla hapajapambazuka, kwani shughuli hii ni ya siri sana. Mimi nikiwa mwana siasa nitazungumza tu kwa ujumla kuhusu nia ya mkutano. Halafu nitawaachia wataalamu wa utekelezaji walio hapa kuchambua vipengele vinavyohusika kwa undani zaidi".

"Nafikiri nyote mnaelewa kwamba kumekuwa na wimbi la maasi la waafrika katika nchi nzima ya Afrika Kusini. Wimbo hili, kwa kiasi fulani limetutia wasiwasi. Migomo imeongezeka katika sehemu za kazi kiasi cha kutishia uchumi wa nchi yetu. Maandamano yameongezeka kiasi cha kutishia utulivu na amani ya wananchi. Vitendo vya hujuma vinavyofanywa na magaidi wanaojiita wapigania uhuru'wa Afrika Kusini vimeongezeka kiasi cha kutishia mashirika ya nje yenye raslimali zao humu nchini.

"Sasa Serikali imeamua kukomesha vitendo vyote hivi. Serikali ilikuwa na nia ya kulegeza vipengele fulani fulani katika sheria zetu kwa manuafaa ya weusi. Lakini imegundulika kuwa kufanya hivyo kutawafanya watu hawa kuwa kichwa ngumu zaidi. Na kama alivyosema Rais wetu, hakuna mtu yeyote Ulimwenguni atakaetuzuia kulinda usalama wa nchi yetu na watu wake wapendao amani!'. Na hapa nasisitiza tena hatutaki mchezo.

"Ghasia hizi ambazo zimekuwa zinaendelea zimefanya mashirika na makampuni kutoka nje kuwa na mtazamo mpya. Yanaanza kuwa wasiwasi juu ya uwezo wetu na pia kuelekea kuwa na imani katika vyama vinavyodai vinapigania uhuru. Hali hiyo siyo nzuri na ni tishio kubwa kwetu".

"Uchumi wetu umeanza kuanguka. gharama za maisha zimepanda kwa kadri asilimia kumi na saba!, ukame umeathiri uzalishaji wa chakula. Bei ya dhahabu imeanguka saba mwaka huu na kufanya bei za vitu muhimu, kama vile Petroli, kuongezeka kufuatana na kushuka kwa thamani ya fedha yetu, ukilinganisha na thamani ya dola ya kimarekani. Jumuia ya Kimataifa inapiga kelele na kuyataka makampuni yasiweke raslimali na vitegauchumi vyao nchini mwetu".

"Mambo yote haya yanatokana na mwamko wa Ulimwengu dhidi ya siasa yetu ya ubaguzi. suala la kuzungumzia ni nini kufanyike ili kulekebisha hali hii ndio sababu leo mko hapa kutafuta ufumbuzi. kuanzia sasa tunataka kufanya macho ya Jumuia ya Kimataifa kuelekea sehemu nyingine ili sisi tupate nafasi ya kurekebisha mambo humu nchini. Macho yao yanataka yaelekee kwenye nchi zilizo mstari wa mbele na vile vile Namibia. Tutafanya vitendo katika nchi hizo vitaifanya Jumuia ya Kimataifa kushughulikia sana; ikitafuta njia za kuwasaidia wananchi wa hizo. Wakati Jumuia ya Kimataifa inashughulika kiasi hicho, sisi tutaanza kuwapa fundisho hawa watu weusi wanaoleta ghasia hapa nchini. Jumuia ya Kimataifa ikija kugeuza macho yake kuyaelekeza kwetu. tutakuwa tumeisha wakomesha hawa watu weusi ambao ni wakorofi watakuwa wamenyooka kama mpini".

"Hivyo tumeamua kuanzisha 'UTAWALA WA HOFU' dhidi ya weusi walio humu nchini na pia walio katika nchi zilizo mstari wa mbele kwa ujeuri. Ni imani yangu kuwa mmenielewa na ninawashukru tena kwa kunisikiliza. Wakuu wote wa usalama wako hapa. watawaeleza jinsi utekelezaji wa jukumu hili utakavyokuwa. Ahsanteni sana".

Alipomaliza kusema hayo, Waziri wa sheria na usalama alifunika jalada lake, kisha akasimama na wengine wakasimama pia. Huku akiwapungia mkono wa kwaheri, Waziri alisindikizwa na Kamishina wa Polisi mpaka kwenye mlango. Alifunguliwa mlango huo na kutokomea gizani.

Baada ya Kamishina wa Polisi kurudi kwenye nafasi yake, Mkurugenzi wa shirika la Ujasusi la Makaburu alichukua uwanja kueleza namna ya utekelezaji wa mpango huo.
 
"Nafikiri nyinyi wote mmemsikiliza waziri kwa makini. Mambo ni kama hayo na hatuna budi kutekeleza, nyinyi wenzetu wa UNITA, MNR na LLA tunahitaji msaadawenu kikamilifu. Tumesaidiana mambo mengi sana. Bila sisi kusingekuwepo na UNITA, MNR au LLA", alisema huku akiwakazia macho viongozi wa vyama hivyo vya magaidi.

Wote walimwemwesa huku wakionyesha kwa vichwa vyao ishala ya kukubaliana nae.
 "Kuanzia sasa misaada kwenu inaongezwa mara dufu". Wote walishangilia kwa kupiga makofi.


"Lakini", aliendelea Mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi la Makaburu, "Misaada hii haikuongezwa bure. Kutakuwa na kazi kubwa ya kufanya. Alinyamaza huku akiwaangalia viongozi wa magaidi kujua kama walikuwa wanampata. "Mmesikia kuwa tunaanzisha utawala wa hofu' dhidi ya watu weusi waliomo humu nchini na pia nchi zilizoko mstari wa mbele pamoja na Namibia. Utekelezaji wa mpango huo utakuwa kama ifuatavyo.

"Kwanza sisi tutajitangazia uhuru nchini Namibia. Baada ya kufanya hivyo tutapambana na SWAPO. Kama ikibidi tutauwa watu Namibia kwani nchi ile ni lazima kuitawala. Tumeanzisha Jeshi linaloitwa KULFUT, yaani Gongo la Chuma'. Hili ndilo Jeshi litakalosababisha Hofu huko Namibia na nchi fulani fulani zinazojidai kuwa mstari wa mbele. Jeshi hili limeundwa na Makomandoo watupu na lenye uwezo mkubwa.
Limefundishwa kwa kipindi cha miaka kumi sehemu mbali mbali Ulimwenguni na sasa liko tayari kabisa kutia hofu popote litakapotumwa. Upande wetu umejiweka tayari. Baadhi ya vikosi vya Jeshi hili vitaletwa kwenu".

Wajumbe walipiga makofi.

"UNITA", aliendelea "Kazi yenu itakuwa kutia hofu huko Angola. Hakuna mazunguzo na Serikali ya Angola tena. Mtapewa kila msaada wa hali na mali. Lazima kuhakikisha kuwa uchumi wa nchi hiyo unaanguka kabisa. Kamanda wa KULFUT yupo hapa atapewa kikosi cha Jeshi hilo kusaidia katika dhima hiyo, wapiganaji wenu wasiwe na huruma, bali kuchinja na kuua kiumbe chochote kilicho mbele yenu. Hakikisha mnawaangamiza wale wote wanaojiita wapigania uhuru wa Namibia. Sisi tuko nyuma yenu kwa lolote lile litakalotokea. Nguvu zetu mnazijuwa. Kwa hoyo hakuna atakayechezea".

"Nyinyi MNR", alimgeukia kiongozi wa MNR, "Kazi yenu mnaijuwa. Kama watakavyofanya hawa watu wa UNITA. Fanyeni vurugu ndani ya Msumbiji. Watu wapate hofu kuliko wale walioishi wakati wa NAAzI iliyosababishwa na Wajerumani".

Mara alimuona Kamanda wa MNR amenyoosha kidole akitaka kuzungumza.

"Eh, unasemaje?, aliuliza kwa shauku kubwa.

"Sisi tuko tayari kabisa", alisema Kamanda wa MNR, "Lakini lazima niseme kwamba mkataba wenu wa Nkomati unatutatanisha. Ni mkataba wa amani kati ya Msumbiji na Afrika Kusini. Sasa kwetu sisi kuendeleza mapambano inakuwa vigumu ingawa mnatusaidia. Mkataba huo unatuathiri sana".

Mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi la Makaburu alijibu. "Achana na siasa. Mkataba wa Nkomati ni siasa tu. Sahau kabisa. Tangu uwekwe saini hakuna mtu ambaye ameutekeleza. Ndio sababu misaada kwenu imeendelea. Kazi yenu ni kama nilivyosema: fanya hali ya Msumbiji iwe ya hofu tupu. Lengo la mkataba wa Nkomati ilikuwa kuwachota akili viongozi wa serikali ya Msumbiji. Tumegundua kwamba wanawaogopa sana nyinyi watu wa MNR. Nyinyi ndio mlikuwa chanzo cha mkataba huo. Walitaka amani. Sasa kinachohitajika ni kuwatia hofu zaidi kwa vita na si ajabu mkachukuwa madaraka. La sivyo, angalau waje kusujudu kwetu na kutulamba miguu. Kwa hivyo sahau kitu kama mkataba wa nkomati".

"Nakuapia", alisema Kamanda wa MNR, "Watakiona cha mtemakuni".

Ndipo Mkurugenzi wa shirika la Ujasusi la Makaburu alipoendelea, "Kazi ya LLA haina tofauti na wengine askari kutoka jeshi la KULFUT watawasaidia kuleta vurugu na hofu kubwa huko Lesotho na Botswana. Sisi tuachieni Zimbabwe, Zambia na Tanzania. Vikosi vyetu maalumu vya uhujumu katika Jeshi la KULFUT vitazionyesha cha mtemakuni nchi hizo. Ili kuonyesha nguvu zetu, sisi tutaanzia Tanzania. Tunataka tutie vurugu na kuleta rindi la hofu katika nchi hiyo dunia itashangaa. Tanzania haijawahi kupewa fundisho kwa sababu hiyo nchi ina kiburi na ndio shina la hawa wanaojiita wapigania uhuru".

"Bila Tanzania, hawa watu wasingetupa taabu kiasi hiki. Nchi hiyo inawapa hifadhi watu hao na kuwapatia mafunzo ya kijeshi. Baadae inawapenyeza kwetu na kutupa shida, shambulizi tutakalofanya huko Tanzania. litawatia hofu hao wanaojiita wapigania uhuru na kuwafanya wasambae bila mpango, itawachukua karne nzima kuweza kujikusanya tena. Litakuwa pigo takatifu ambalo litaiacha dunia nzima inagwaya. Mipango ya awali juu ya kipigo hicho iko tayari na hatuna wasiwasi".

Mkuu wa UNITA aliamusha mkono ikiwa ni ishara yake ya kuomba kusema.

"Eh, unasemaje?". Mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi la Makaburu alimuuliza Mkuu wa UNITA.

"Mimi nasikia moyo wangu unakwenda mbio kwa shauku", alisema Mkuu wa UNITA. "Kama kweli mtaipa kipigo Tanzania mpaka ikakoma kutamba, basi sisi kazi yetu itakuwa rahisi kama kunywa maji. Nchi hiyo ina kiburi na ndio inayowapa kichwa ngumu wale wanaodai kupigania uhuru, na nchi nyingine za mstari wa mbele. Iwapo Tanzania itashika adabu, basi vyama vyetu vitapata ushindi wa kutawala. Lakini napenda kukutahadhalisha kuwa nchi hiyo ni imara sana. Mimi nimewahi kuishi huko na ninajua kazi yenu haitakuwa rahisi".

Mara alikatizwa na Mkurugenzi.

"Usiwe na wasiwasi", Mkurugenzi alianza kujitapa. "Hakuna nchi itakayonusurika. Na Tanzania itakuwa ya kwanza. Nyinyi mtasikia. Kusema kweli baada ya kipigo hicho, hao wapigania uhuru; na pia nchi nyingine zilizo mstari wa mbele watabaki wanagwaya".

"Ili yakutoke mashaka", alidakiza Kamanda wa KULFUT, "Matayarisho ya kipigo hicho yalianza siku nyingi. Jeshi la KULFUT likishikiana na Shirika la Ujasusi hakuna wasiwasi kuhusu kipigo hicho, nakuhakikishia kuwa Tanzania na wenzake watakipata cha mtemakuni. Tumetumia miaka kumi kujitayarisha na muda huo siyo mchezo".

"Saa zimekwenda sana. Tumetumia muda mwingi sana kuzungumzia suala hili wakati ambapo nyie mnapaswa kuondoka kwa siri sana kabla ya mapambazuko". Hapa Mkurugenzi alinyamaza kidogo kisha akaendelea kusema. "Kamanda wa KULFUT' atawapatia msaada mnaohitaji katika kutekeleza mpango huo. Hatuwezi kukubali kushindwa kwani hiyo ina maana kuwa huo utakuwa ndio mwisho wetu - kitu ambacho hakiwezekani. Lazima nipate ripoti ya maendeleo ya mpango huu kila siku ili niweze kuipa taarifa serikali. Kamishina wa Polisi anasema hana wasiwasi juu ya weusi wa hapa kwani atawatia vurumai mpaka wajute kuzaliwa".

:Nafikiri mmesikia kuwa mwezi Februali tuliwakamata vingozi wa vyama vya upinzani. Hao tumewaweka kiporo na baada ya kuipa kipigo Tanzania. Nyinyi mtasikia vurumai tutakavyoifanya, au uongo Kamishina?".

Akionyesha majivuno, Kamishina wa Polisi alijibu, "Watajuta kuzaliwa kwani walikuwa wanaleta mchezo. walikuwa wamediliki kusababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe hapa nchini. Kitu kama hicho hakiwezi kutokea wakati bado niko hai".

Mkurugenzi alifunga mkutano huo kwa dharura kwa kusema, "Ahsanteni sana. Ni mategemeo yangu kuwa mmeelewa hali halisi na hivyo mtatekeleza itasavyo. Naamini tutakapokutana tena kwenye mkutano kama huu hali haitakuwa hivi, bali kusherekea ushindi dhidi ya adui. Sura ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara itabadilika kwa kupata tawala mpya".

Mkutano ulifungwa saa kumi na moja alfajiri.


INAENDELEA

Comments

  1. mimi naomba msaada wenu kitabu cha Hofu, Kisasi na Kufa na Kupona naweza kupata sehemu gani ya Tanzania hii.

    ReplyDelete

Post a Comment

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru