Nchi zilizo
msitari wa mbele katika Ukombozi Kusini mwa Afrika zimetendewa mambo mengi maovu na
Utawala dhalimu wa Makaburu... Hata hivyo halikupata kutokea tishio zito la
kutisha kama hili, ambalo linakaribia kutokea. Tukio la kutatanisha ambalo
linawatoa machozi wananchi wa nchi mbalimbali za kiafrika. Wanajitokeza
mashujaa na kwenda Afrika Kusini, ili kulikabiri tishio hilo lakini kila aendaye
huko harudi na roho yake.
Inspekta
Kombora nchini Tanzania jasho linamtoka. Anawatambua na kuwakumbuka mashujaa
wengi lakini anamtambua shujaa mmoja. Joram Kiango. Jambo la kusikitisha ni
kwamba sasa hivi Joram Kiango ni mtumiaji mzuri ambaye sasa anatembea kutoka
jiji moja hadi lingine akiwa na yule msichana wake mzuri Nuru kwa ajili ya
kustarehe. Juhudi za Kombora kumsihi Joram arejee kazini hazifui dafu. Badala
yake Joram anafanya maajabu mengine ambayo yanalichafua jina lake hapa nchini
Tanzania na kote duniani. Wakati huo siku ambayo utawala wa makaburu umeweka
ili kuachia pigo lao la mwisho inazidi kukaribia. Sasa yamebaki masaa...
**********************************************************
HADITHI HII
INAWAJIA KUFUATIA MAOMBI YA WASOMAJI WENGI WA BLOG YA MPIGANAJI, TUMELAZIMIKA
KUWALETEA HADITHI HII KUTOKA KATIKA KITABU CHA 'TUTARUDI NA ROHO ZETU'
KITABU KILICHOANDIKWA NA MTUNZI WA RIWAYA ZA KUSISIMUA ZA UPELEELZI, BEN R. MTOBWA.
BAADA YA KUANDIKA KITABU HII BEN R. MTOBWA ALITOA KIDOKEZO KUWA 'IWE ZAWADI
YAKE KWA KILA MWANAMAPINDUZI WA AFRIKA'. SASA ENDELEA.
*********************************************************
SURA YA
KWANZA
Kama maji ya
Bahari ya Hindi yangekuwa na hisia, basi yangejisikia fahari sana kupata fursa
nyingine ya kuburudisha miili ya viumbe hawa wawili ambao walikuwa wakiogelea
kando ya ufuko huu wakicheza na kucheka. Walifanya picha ya kuvutia sana
hususan sura zao zuri zilipoibuka kutoka majini na kumezwa na tabasamu ambalo
lilisababishwa na mizaha waliyokuwa wakifanyiana chini ya maji. Baada ya
kuogelea kwa muda mrefu walirejea nchi kavu ambako walijitosa juu ya mchanga na
kuruhusu joto likaushe maji miili yao. Ufuko pia ungekuwa na kila sababu ya
kusherehekea fahari ya kulaliwa na viumbe kama hawa. Kwani walioana kimaumbile kama
pacha, ilihali hawakuwa mtu na dada yake.
Walikuwa
kama pea ya kiatu cha kiume kwa cha kike. Mwanamume hakuwa mwingine zaidi ya
yule kijana mwenye umbo refu, mkakamavu, aliyekaa kiriadhariadha na sura nzuri,
yenye dalili zote za hekima, ushujaa na ucheshi. Kwa jina anaitwa Joram Kiango.
Naye
msichana alibahatika kupewa umbo lenye kila kitu ambacho msichana anahitajika
kuwa nacho, wakati huohuo akiwa na kila ambacho mvulana legelege asingekuwa
nacho, ni yule ambaye akutazamapo ungependa aendelee kukutazama, achekapo
utafarijika, atembeapo unaburudika. Yule ambaye kuna madai kwamba alikuja
duniani kwa makosa baada ya kuumbwa ili awe Malaika. Madai ambayo kama si ya
kweli basi yako mbali sana na uongo. Hata jina lake halikutofautiana sana na
sura yake. Wanamwita Nuru.
Baada ya
kuhakikisha kuwa miili yao ilikuwa imekauka, walijifuta vizuri kisha
wakazichukua taulo zao na kuondoka wakaifuata gari yao. Macho ya watu wengi,
waswahili kwa watalii ambao walikuwa katika ufuko huo, hayakukoma kuwafuata.
Kutazamwatazamwa, hasa wanapokuwa pamoja halikuwa jambo geni tena kwao. Mara
kwa mara macho ya kiume yalikuwa ya yakimwandama Nuru huku macho ya kike
yakimfuata Joram kila mahali walipopita. Walijifunza kuzoea hata wakaanza
kusahau kuwa wanatazamwa. Hivyo, walipolifikia gari lao waliingia, Joram
akalitia moto wakaondoka kwa mwendo usio wa haraka.
Hawakuwa na
sababu yoyote ya kufanya haraka. Ratiba yao ya starehe ilikuwa ikielekea kwisha
mapema zaidi ya walivyokusudia. Walikuwa wamekubaliana wakae katika miji yote
mashuhuri hapa nchini kwa muda wa wiki nzima kwa kila mji. Lakini hii ilikuwa
wiki ya pili tu na tayari walikuwa wameishi Zanzibar, Moshi, Arusha, Dodoma,
Mwanza na kujikuta wamerejea Dar es Salaam. Kila mji waliuona unakinaisha baada
ya siku mbili tu. Maisha ya mahotelini waliona yanawafaa watu wavivu, nazo
mbuga za wanyama ziliwasisimua watalii, ilihali miji iliwaridhisha wenyeji, na
safari za hapa na pale zilikinaisha.
Hivyo ingawa
walirejea Dar es Salaam na kuendelea na starehe zao wakiishi katika hoteli ya
Kilimanjaro, ingawa waliendelea kucheza na kucheka, ingawa hakuna aliyetamka
neno lakini bado haikuwa siri tena kuwa maisha ya Kula, kulala...kula, tena,
kulala tena", yalikuwa yameanza kuwachosha. Maisha hayo yalikuwa yameanza
usiku ule ambao Joram Kiango asingeweza kusahau. Usiku hadi leo bado unamtia
maumivu moyoni, kila anapokumbuka alivyozulumiwa haki na wajibu wake wa kuitia
risasi katika kichwa cha Proper, yule katili ambaye pamoja na kuwaangamiza watu
wengi ambao hawakuwa na hatia, alikuwa amemuua Neema Iddi kinyama. Ni siku hiyo
ambayo Joram alitupa bastola yake na kuamua kuishi kivivu kama wanavyoishi watu
wengine. Msichana huyu Nuru alikuwa amehusika sana katika mkasa huo ambao
tayari mtu alikuwa ameuandikia kitabu na kukiita Salamu Toka Kuzimu. Kamwe Nuru
alishindwa kuachana na Joram na asingeweza kusitahimili kumwona Joram akiteseka
na msiba huo peke yake. Alimfuata na kumsihi hata kulipopambazuka wakajikuta
wako pamoja juu ya kitanda kimoja.
Tangu hapo
hawakuachana, Joram hakuwa mtu aliyeweza kuachwa kirahisi. Naye Nuru kadhalika
alitofautiana sana na wale wanawake wazuri ambazo uzuri wao ni pindi wanapokuwa
wamevaa nguo tu. Alikuwa na mengi ambayo alikuwa ameyatenda kwa nia moja tu -
ya kumfariji Joram, naye Joram alijikuta akianza kujisamehe. Lakini asingeweza
kusahau......
**********************************************************
Walipowasili
chumbani katika hoteli ya Kilimanjaro, walijipumzisha vitandani mwao kwa muda
huku wakilainisha koo zao kwa viwanyaji vitamu. Kisha walifuatana bafuni na
kuyaondoa maji ya chumvi miilini mwao kwa kuoga vizuri kwa sabuni. Baada ya
hapo waliekea kwenye chumba cha maakuli ambapo walikula na kujiburudisha kwa
vinywaji vikali na maongezi laini.
Joram akiwa
katika vazi lililomkaa vema, suti ya kijivu iliyooana na viatu vyeusi kama
kawaida, alikuwa tishio kubwa kwa wanaume waliokuja na wasichana wao. Hata
hivyo, walijifariji kwa kujua kuwa asingekuwa mwendawazimu wa kuvutwa na yeyote
kwani aliyeketi nae hakuwa msichana wa kawaida.
"Kwanini
wanaishi hapa bongo watu kama wale", mtu mmoja alimunong'oneza jirani
yake.
"Tazama
wanavyopendeza, wangeweza kwenda zao nje na kutajirika sana endapo wangecheza
mchezo mmoja tu wa sinema", alidakia mwingine.
"Kweli
kabisa", aliungwa mkono. "Hata maumbile yao yanafikiana. Yule dada
anatosha kabisa kumtia mwanaume yeyote wazimu kiasi cha kumfanya auze hata
nyumba yake.
Maongezi
hayo hayakumfikia Joram wala Nuru. Lakini alikwisha zoea kuyasoma katika macho
ya watazamaji wao. Hivyo, alitabasamu kidogo na kuagiza kinywaji kingine. Nuru
alikuwa akiongea neno. Joram aliitika bila kumsikia. Waliendelea kunywa kwa
muda hadi walipoamua kuwa wametosha ndipo walipofuatana katika ukumbi wa muziki
ambapo walisikiliza muziki na kucheza kwa masaa kadhaa. Walipokinai walikiendea
chumba chao ambacho kiliwalaki na kuwapa usiri. Katika usiri huo, kwa mara
nyingine miili yao iliburudika na kusherehekea afya zao.
Kesho yake
baada ya kufungua kinywa walitazamana katika hali ya kuulizana waitumie vipi
siku hiyo. Nuru aliweza kuzisoma dalili za kuzikinai ratiba zao ambazo
zilikuwemo katika macho ya Joram. Ingawa walikuwa wakistarehe na kujiburudisha
furaha ilikuwa dhahiri kuwa burudani hizo zilikuwa zikiuburudisha mwili wa
Joram kamwe hazikuwa zikiburudisha akili yake. Ingawa uso wake ulikuwa
ukitabasamu mara kwa mara, roho yake ilikuwa ikiwaka kwa hasira kali dhidi ya
adui zake. adui wa taifa na maendeleo ya jamii. Adui ambao walikuwa wamefanya
maovu mengi yasiyokadilika na kumtia lile donda la rohoni kwa kumuua kikatili
msiri wake mkuu Neema. Nuru kwa dhamila ya kumsahaurisha Joram na uchungu huo
ndipo akajitoa kwake mwili na roho. Lakini ilikuwa dhahili kuwa jeraha hilo
lilikuwa bichi katika roho ya Joram, na lisingepona kabisa isipokuwa kwa dawa
moja tu kulipiza kisasi. Hayo alikuwa akiyaona wazi katika macho ya Joram
ingawa alijisingizia kufurahia starehe zao. Iko siku Nuru aliwahi kumwambia.
"Sikia Joram. Huonekani kufurahia lolote tunalofanya. Kwani usirudie ofisi
yako na kuendeleza harakati zako, nitakuwa kama alivyokuwa Neema. Nitakusaidia
kwa hali na mali. Joram alicheka na kumjibu Nuru. "Mara ngapi nikwambie
kuwa nimeacha shughuli hizo. Nitaendelea kustarehe hadi nitakapoishiwa senti
yangu ya mwisho. Ndipo nitakapotafuta kazi na kuifanya kwa utulivu kama vijana
wenzangu".
"Kwanini
lakini, kifo cha msichana mmoja tu kinakufanya usahau wajibu wako".
"Sivyo
Nuru. Isieleweke kuwa nimechukia kwa kufiwa na Neema. Yeye ni mmoja tu kati ya
wasichana wanaouawa kwa dhuluma na ukatili aina kwa aina ulioko duniani. Ni
mmoja tu kati ya maelfu ya vijana wanaoteseka kwa shida ambazo wanazipata kwa
makosa ya watu wengine. Ni mmoja tu kati ya mamilioni ya binadamu wanaoumia kwa
umasikini ambao hawakuomba na dhiki ambazo hazina umuhimu wowote".
"Sidhani
kama nimekuelewa Joram, unazungumza kama mshairi".
"Labda.
Ninachotaka kusema ni kwamba bastola yangu haitoshi kukomesha maovu yote
yanayotendeka hapa duniani. Kote Afrika na duniani binadamu hawako sawa
kiuchumi. Wako wanaoshinda njaa na kuna wanaomwaga chakula. Kama kweli
nakusudia kuondoa dhuluma na ukatili kwa nchi dhidi ya nchi nyingine, basi sina
budi kuukomesha pia ukatili dhidi ya mwingine. Maadamu hayo yako nje ya uwezo
wangu naona sina budi kusahau yaliyopita na kuanza kula na kunywa kama vijana
wenzangu".
"Hasira
hizo Joram. Upende usipende ukweli ni huo huo. bastola yako haiwezi kuwaelekea
viongizi wazembe na wenye choyo ambao wanasababisha hali ngumu kwa wananchi.
Lakini inawajibika kuwakomoa maadui ambao dhamila yao ni kuhakikisha hatulifikii
lengo letu la kujenga taifa ambalo rais wake wanafaidi matunda ya uhuru wao.
Unafahamu fika kuwa wanatunyima nafasi ya kufanya hayo"... Maongezi hayo
yalikuwa yamefanyika siku chache zilizopita. Nuru alikuwa ameyakumbuka tena leo
baada ya kuziona dalili za kukinai katika macho ya Joram. Alijua na kuamini
kama wanavyoamini watu wote wanaomfahamu Joram kuwa starehe yake kuu ni pindi
anapopambana na adui na burudani yake ni hapo anapowashinda. Vinginevyo Joram
alikuwa akijisingizia starehe.
"Leo
wapi mpenzi", Nuru aliona amchokoze Joram.
"Leo
najisikia kulala tu".
"Kulala
mchana, tangu lini umeanza tabia hiyo ya kulala mchana".
"Tangu
nilipoacha kuwa Joram Kiango na kuwa kijana mtumiaji anaitwa Joram
Kiango".
"Nilijuwa
utachoka Joram. Kwanini usirudi ofisini na kuanzia leo?".
"Sikia
Nuru. Usianzishe tena ubishi ambao siupendi. Kweli nitakuwa hapa nikiendelea
kutumia tu na si vinginevyo".
"Sidhani
kama unasema ukweli. Huonekani mtu wa kustarehe maishani". Joram
hakumjibu. Alijilaza kitandani na kujisomea gazeti. kisha jirani yao chumba cha
pili aliingia akiwa katokwa na macho. Hakujali kupiga hodi. Wala macho yake
hayakuvutwa kuhusudu uzuri wa Nuru kama ilivyokuwa kawaida yake. badala yake
alimwendea Joram kitandani akasema, "Hujasikia, Samora Machel amefariki,
ndege yake imeanguka huko Afrika Kusini".
"Amekufa",
Nuru alidakia na kuuliza kwa mshangao.
"Amekufa,
na hii siyo bure. Iko namna haiwezi kuwa ajali ya kawaida".
"Afrika
Kusini, alienda kufanya nini huko", Joram aliuliza kwa utulivu. Hata hivyo
macho yake yalikuwa yakiwaka kwa hasira, ingawa hakupenda kujidhihilisha wazi
kwa Nuru.
"Siku
hizi hata taaifa za habari husikilizi Joram?", Nuru alimuuliza.
"Samora
hakwenda Afrika Kusini. Alikuwa akitokea nchini Zambia ambako alikutana na rais
Mobutu Seseseko wa Zaire na Waziri Mkuu wa Zimbabwe, Robert Mugabe kutafuta
suruhisho na mbinu za kuiwekea Afrika Kusini vikwazo zaidi vya uchumi".
"Wanasema
chanzo cha ajali hakijapatikana. Bila shaka watakuwa waliosababisha ajali hiyo
kwa njia moja ama nyingie", alisema kwa masikitiko.
"Nadhani
wamezoea kutuangamiza wapendavyo. Kwao sisi ni sawa na vifaranga wanaofugwa.
Yeyote ambaye hawampendi wanamponda kwa urahisi. Jambo la kusikitisha ni kwamba
sisi hatuwezi kufanya lolote baya dhahiri ni kwamba tutaendelea kuuawa mpaka
lini. Kwanza walimuua Mondalane. Sasa wamemuua mrithi wake Samora na siyo hao
tu. Viongozi wengi wa Afrika wamekuwa kama mifugo yao. Tunaorodha ndefu ya
viongozi wetu wanaouawa ama kupinduliwa kwa matakwa yao. Tutaendelea kuvumilia
mpaka lini", Nuru alikuwa akizungumza kama peke yake. Lakini macho yake
yalikuwa yakimtazama Joram. Alitamani aone kitu katika macho yake. Hakukiona.
Jambo ambalo lilimfanya ainame chini na kuruhusu matone kadhaa ya machozi
yamdondoke. Yalikuwa machozi ya hasira zaidi ya hudhuni.
***********************************************************
Kifo hiki
cha kijana shujaa aliyeheshimiwa kote dunia, aliyependwa na wapenzi wake na
kuogopwa na adui zake, kilifuatiwa na minong'ono mingi kote dunia. Watu
walisema hili na lile, wakipingana na kuafikiana.
"Walimuua
au...".
"Bila
shaka".
..."Njama
za Afrika Kusini".
"Na
vibaraka vyao".
Siku chache
baadae maongezi yalibadilika.
"Umesikia
Makaburu wanadai kuwa wataendelea kuwaadhibu viongozi na wananchi wa nchi zote
za mstari wa mbele ambao wanajifanya vichwa ngumu?".
"kweli?,
washenzi sana wale. Wanaweza kufanya lolote".
Na baada ya
siku chache mambo yakaanza kutokea. Magazeti na vyombo mbalimbali vya habari
duniani viliandika habari za kusikitisha.
Watu mia nne
wamefariki dunia, mia tisa kujeruhiwa vibaya na wengine maelfu kuponea
chupuchupu kufuatia ajali isiyokuwa ya kawaida iliyotokea katika jiji la Lagos
Nigeria. Watu hao walikuwa katika uwanja wa mpira wakati wa mchezo kati ya timu
ya taifa ya nchi hiyo na Zaire. Dakika chache kabla ya mchezo huo kwisha, moto
mkali umelipuka na kubomoa uwanja na kusababisha maafa hayo. Wachunguzi wa
mambo wanahisi kuwa huenda utawala wa Afrika Kusini unahusika.
Kabla watu
hawajasahau habari hiyo, ilifuatia taarifa nyingine ya kutisha vilevile.
Harare,
Zimbabwe
Maghala
manane ya serikali yaliyokuwa yakihifadhi chakula yameungua moto kwa pamoja.
Chanzo cha moto huo hakijajulikana. Jambo la kushangaza ni jinsi maghala hayo
yalivyoungua kwa pamoja wakati yako katika wilaya mbalimbali za nchi hiyo. Kuna
mashaka kuwa tukio hili kwa njia moja ama nyingine linahusiana na maafa ya
Nigeria.
Na baada ya
siku chache
Dar es
Salaam, Tanzania
Katika matukio
ya kutisha na kushangaza yanayoendelea kutokea katika nchi zenye msimamo wa
kimapinduzi za Afrika leo asubuhi, Tanzania imepata pigo kubwa la kusikitisha.
Jengo la Benki kuu ambalo lilikuwa likikamilisha marekebisho baada ya ule moto
wa awali limeungua tena. Safari hii haielekei kuwa kutakuwa na matengenezo
yoyote yanayoweza kulilekebisha zaidi ya kujengwa upya. Chanzo cha mto huo
hakijafahamika.
Habari hizi
zilitisha Afrika na kuishangaza dunia. Kila mtu aliyezisikia radioni na
kuzisoma magazetini alishangazwa na matukio haya ambayo mfano wake haukupata
kutokea katika historia ya Afrika na dunia.
Ajali ni
jambo la kawaida. Kadhalika kuna watu wanaoamini kuwa kuna kitu kinachoitwa
mkosi, na bahati mbaya, lakini mikosi mingi kiasi hiki na bahati mbaya
kuziandama nchi chache za Afrika zenye msimamo mmoja katika suala la ukombozi
ni jambo ambalo lilisababisha nyongeza katika fikra za wasomaji na wasikilizaji
wa vyombo vya habari. Kitu kinachoitwa roho mbaya, kilipenya katika fikra hizo,
ingawa hakukuwa na hakika katika mawazo hayo. Baadhi hata waliwahi kutamka
hadharani kuwa kuna mkono wa mtu katika matukio hayo. Mawazo hayo yalifuatiwa
na hofu katika mioyo ya wananchi na serikali zao walipojiuliza. Kipi
kingefuata, "Joram, tutakaa kimya kusubiri maafa zaidi", Nuru alikuwa
akimuuliza Joram baada ya kusoma habari za tukio la benki kuu katika gazeti.
Alikuwa amejitahidi kustahamili kutosema lolote aliposoma matukio ya Lagos na
Harare. Lakini hili la nyumbani lilimgusa zaidi Nuru. "Aibu iliyoje",
aliendelea Nuru. Tuendelee kustarehe kwa vinywaji na muziki huku tukisubiri
maafa mengine yatatokea, haiwezekani Joram. Lazima tufanye jambo".
Ndio habari
hizo hazikuwa zimempendeza Joram. Hata hivyo alikuwa amezisoma kama raia
wengine bila kudhihilisha dalili yoyote ya nia ya kufanya lolote kama
alivyokuwa awali. Jambo ambalo lilimfanya Nuru atokwe na machozi.
"Serikali
inao polisi na wapelelezi wake, ambao inawalipa pesa nyingi", Joram
alisema. "Mimi ambae nimeacha shughuli hizo nitasaidia nini?".
"Huwezi
kusema hivyo Joram. Siamini kama moyo wako wa uzalendo umedidimia kiasi
hicho".
"Haujadidimia,
uko palepale kama ilivyo mioyo ya wazalendo wengine".
"Lakini
wewe si mzalendo wa kawaida Joram. Taifa linakuthamini na kukutegemea. Huwezi
kulisalti kiasi hicho bila sababu ya kuridhisha. Lazima ufanye jambo.
"Ndio.
Nitafanya jambo. Nitastarehe na kuendelea kustarehe kama wanavyofanya vijana
wenzangu. "Njoo kitandani Nuru. Tafadhali. Njoo tustarehe acha wenye shibe
waendelee kulinda shibe yao. Wewe na mimi tuna nini katika nchi hii".
"Joram...".
"Nuru
njoo tafadhali. Na kama umenichoka sema nimtafute Nuru mwingine ambaye
hachoshwi na starehe. Nuru angependa kukataa. Lakini asingeweza. Akamfuata
Joram kitandani na akajilaza kando yake kitandani huku machozi yakimtoka kama
kondoo anayesubiri kuchunwa.
**********************************************************
ITAENDELEA
0784296253
big up
ReplyDeleteShukrani kubwa
ReplyDelete