NJAMA
VERONIKA NA SHERRIFF II
ILIKUWA saa tatu kamili niliposimama mbele ya chumba namba 208 katika ghorofa ya pili ya hoteli ya Kilimanjaro, niligonga mlango mara mbili haraka haraka, halafu nikatulia kidogo kisha nikagonga tena. Hivi ndivyo nilivyokuwa nimeelekezwa.
"Karibu", nilisikia sauti kali ya juu ikitokea ndani ya nyufa za mlango. Nilifungua nikajikuta katika sebule ya chumba hiki ambamo Veronika alikuwa amevaa kaputula na sidiria tu akifanya mazoezi ya viungo. Alikuwa ameelekea upande mwingine na kunionesha mgongo na kuendelea na mazoezi yake kama kwamba hakuna mtu aliyeingia. Nilirudisha mlango, nikauegemea na kutazama jinsi binti huyu alivyokuwa akichukua mazoezi.
"Karibu Willy Gamba, kaa kwenye kiti upumzike", alinielekeza bila kugeuka na huku akiendelea na mazoezi yake. Kisha akaanza kusema kana kwamba anajizungumzia yeye peke yake.
"Willy Gamba anayejiita mfanyabiashara huku ni mpelelezi mashuhuri wa Afrika. Afadhali ningejua mapema naamini ingekuwa furaha kubwa kuonana na mtu huyu mashuhuri nyumbani kwetu. Lakini nimekuja kujua mjini London katika ofisi za gazeti la 'Afrika', hasa ni hii teknolojia iliyoingia ulimwenguni maana tumeelekezwa na komputa ya pale ofisini. Sherriff aikuwa na mashaka kuwa amewahi kusikia jina la Willy Gamba mahali. Hivyo kufika tu London akailisha komputa hiyo jina la Willy Gamba. Maana komputa hiyo imeweka kwenye ubongo wake waandishi wote maarufu wa habari, wapelelezi wote maarufu ulimwenguni, wakubwa wote wa serikali mbali mbali na watu wote maarufu katika nyanja mbali mbali.
"Lo! alipoilisha jina hili ndipo ikatutolea maajabu. Ilionyesha kuwa Willy Gamba mwenye umri wa miaka ishirini na tisa, mwenye urefu wa futi tano na inchi kumi na mwenye umbo la kupendeza sana ni mpelelezi maarufu ulimwengu mzima. Iliendelea kusema kuwa Willy Gamba amehitimu katika chuo kikuu cha Dar es Salaam na kupata shahada katika sheria. Baada ya kutoka chuo kikuu moja kwa moja aliteuliwa kwenda kujifunza mambo ya upelelezi kwa kutokana na sifa zake alizoandikiwa na wakubwa wa Jeshi la Kujenga Taifa, wakati akiwa katika Jeshi hilo".
"Komputa ilieleza kuwa Willy Gamba anasemekana amepata mafunzo katika nchi mbali mbali kama vile Uingereza, Cuba, Urusi, Marekani, China na Japan. Kutokana na mafunzo haya amejulikana kama mtu hatari katika kutumia aina yoyote ya silaha. Vile vile anajua karate na Kung-fu ya hali ya juu kwani wakati akiwa Japan aliwahi kushindana na Inoki na kutoka sare naye. Watu wanashangaa kwanini hakuendelea maana bila shaka sasa angekuwa bingwa wa dunia. Zaidi ya yote anaaminika kuwa amehitimu mafunzo ya kikomandoo. Komputa ilizidi kuonesha kuwa Willy Gamba ana I.Q ya hali ya juu sana, hivi sasa ni mtu anayeweza kusokoroa matatizo yaliyojisokota sana. Na iliendelea kuonyesha kuwa ameifanyia 'OAU' kazi nzuri sana hasa kuhusiana na Ukombozi wa Afrika Kusini".
Alipofika hapa alinyamaza, kisha kama umeme alikatisha mazoezi yake na kunigeukia na kurukia kifuani pangu kwani bado nilikuwa nimesimama mlangoni nikisikiliza kwa makini.
"Kwanini usinieleze toka mwanzo Willy mpenzi, kwanini?".
Nilimkumbatia kifuani kwangu na badaa ya kujibu swali lake nilisema. "Veronika Amadu".
Aliinua macho akaniangalia usoni, mimi bila kusita niliendelea. "Mwandishi maarufu wa gazeti la "Afrika", Veronika Amadu mwenye umri wa miaka ishirini na sita, mwenye urefu wa futi tano na inchi tano, mwenye macho na umbo la kupendeza la vipimo 38'-22'-36'. Alihitimu katika Chuo Kikuu cha Ibadani nchini Nigeria na kupata shahada katika uandishi, baada ya kuhitimu aiajiriwa na gazeti la 'Newsweek' la Marekani, akiwa mwandishi wao katika Afrika Magharibi. Kwa vile gazeti lilitaka kumtumia mwandishi huyu kupata habari zingine ambazo kuzipata kwake itabidi uhatarishe maisha yake, lililazimika kumpeleka Japan kujifunza namna ya kujikinga kwa mikono, hatari yoyote itokeapo, hivyo mwandishi huyu amehitimu katika Judo na Karate na kupata mkanda mweusi. Baada ya kuwa na gazeti hili kwa muda mrefu aliacha na kujiunga na gazeti a Afrika. Anajuikana kuwa msichana mwandishi jasiri sana, amewahi kusafiri na majeshi ya Chama cha wapigania uhuru wa Sahara Magharibi kiitwacho "The Popular Front for the Liberation of Saguiet el-Hamara na Rio de Oro" yaani "POLISARIO", katika mapambano yao dhidi ya majeshi ya Morocco ambayo yameshika sehemu hiyo, inasemekana mwandishi huyu alikaa na majeshi haya na kuandamana nayo katika uwanja wa mapambano kwa muda wa miezi sita na kuwa mwandishi wa kwanza kuandika habari kamili za mapambano haya akiwa shahidi wa macho. Je unasemaje Veronika Amadu".
"Sasa naamini kabisa wewe ndiye Willy Gamba, maana mimi nilifikiri tumekutangulia kumbe wewe ndiye umetutangulia zaidi. Naamini hata Sherriff sasa umamfahamu kama nyuma ya kiganja chako hebu nieleze".
Nilimweleza. "Ahmed Sherriff mwandishi mashuhuri wa gazeri la Afrika hasa juu ya mapambano ya Kusini mwa Afrika. Ahmed Sherriff mwenye umri wa miaka thelathini na mbili, mwenye urefu wa futi tano na inchi kumi na moja na mwenye masharafa mengi, alihitimu katika Chuo kikuu cha Patrick Lumumba mjini Moscow, Urusi. Baada ya kuhitimu kwake alipotea isijulikane aliko kwa muda wa mwaka mmoja. Lakini habari za kuaminika zinasema kwamba alikuwa akichukua mafunzo ya kijeshi katika kambi za kijeshi za Wapalestina huko Mashariki ya Kati. Baada ya kuonekana alipatiwa kazi moja kwa moja na gazeti la Afrika ambalo linaaminika lilipata fununu juu ya mafunzo ya kijeshi ya Sherriff huko Mashariki ya Kati. Kwani baada ya kumwajiri tu alipelekwa moja kwa moja Kusini mwa Afrika ambako aliandamana na majeshi ya wapigania uhuru wa Frelimo, MPLA na siku hizi anaandamana na majeshi ya SWAPO katika uwanja wa mapambano huko Namibia.
"Vile vile kuna habari zinazosema kuwa alikuwepo katika mkasa uliotokea Soweto na ndiye aliyeandika habari za kuaminika juu ya tukio hilo. Hivyo ujasiri wake huu umemfanya kuwa mwandishi maarufu sana anayechukiwa sana nan tawala dhalimu za Afrika Kusini na Rhodesia na nchi zote zinazopinga mapinduzi ya Afrika na harakati zake za kujikomboa kutokana na ubeberu. Umeridhika sasa."
"Sasa naamini ukiambiwa mtu ana I.Q ya hali ya juu, lazima utambue kuwa kwa kila jambo unalotaka kufanya yeye yuko hatua nyingi mbele yako", Veronika alijibu na kuanza kunibusu huku midomo yake ikiwa ya chumvi chumvi sababu ya mazoezi.
"Ngoja nioge mara moja ili tukaonane na Sherriff tukaanze mazungumzo yetu ya kwanza."
"Sawa". Aliniacha na kwenda maliwatoni. Mimi nikabaki katika mawazo makali jinsi ya kuanza kulishambulia tatizo hili.
INAENDELEA
Comments
Post a Comment