Kondoa wagundua Dhahabu

 Mbunge wa viti maalum mkoa wa Dodoma, Bi. Moza Said (katikati), akiangalia maji yaliyochanganywa na udongo wenye dhahabu kwenye machimbo mapya ya Tumbelo wilayani Kondoa leo. wengine ni wachimbaji wadogo wa madini.........

Dhahabu imegunduliwa katika kijiji cha  Tumbelo nje kidogo ya mji wa Kondoa, mkoani Dodoma, ambako mgodi huo umeanza kutema madini kwa wingi na kuwafanya wachimbaji wadogo wadogo kutoka mikoa ya Tanzania Bara kupiga kambi eneo hilo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tumbelo Gold Mine, Bw. Moshi Changai amesema mgodi huo umegunduliwa mwezi uliopita, baada ya mchimbaji mdogo wa kijiji cha Tumbelo, Bw. Hamisi Gori kugundua dhahabu hiyo.

Amesema taarifa ya kuvumbuliwa dhahabu hiyo iliwafikia wachimbaji kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania na nje ya nchi ambako wanaendelea kufurika kuchimba dhahabu hiyo.

Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Dodoma, Bi. Moza Said akizungumza na wachimbaji dhahabu hao aliwataka watume nafasi hiyo kujipatia ajira na mapato ya madini hayo yaboreshea maisha yao na familia zao kuondokana na umasikini.

Alisema mgodi wa Tumbelo utawafanya wanananchi wa vijiji vya jirani vya Changaa, Mnenia na Bolisa, kupata ajira ya kuchimba, kupika chakula na kusafirisha abiria kwa Bodaboda.

Mvumbuzi wa mgodi huo Bw. Gori amebainisha kuwa ilikuwa bahati kubwa kwake baada ya kuchimba mwamba na kusaga ambako alipata gramu 47 za dhahabu yenye thamani mil.2 hivyo ilimlazimu kutoa taarifa kwa uongozi wa kijiji cha Tumbelo kuhusu ugunduzi huo.

“Nimefarijika kugundua dhahabu ambayo inawasaidia watanzaia wenzangu, naendelea kuchimba nategemea kupata dhahabu nyingi kwa sababu wachimbaji wameanza kupata dhahabu kwa wingi” alisema Bw. Gori.

Mwenyekiti wa kijiji cha Tumbelo Bw. Omari Ngarima alisema kutoka mgodi huo uvumbuliwe mwezi mmoja uliopita, wachimbaji kutoka sehemu mbalimbali wamefika kuchimba madini hayo na kuiomba Serikali iwakingie kifua kwa wachimbaji wakubwa wasiwanyan’ganye mgodi kwa kisingizio cha uwekezaji.

Mnunuzi wa dhahabu hiyo, Bw. Japhet Jeremiah alisema dhahabu inayopatikana katika mgodi wa Tumbelo ni nyingi ambayo itawaletea utajiri wakazi wa wilaya ya Kondoa.

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU