Mbunge wa Jimbo la Kahama Bw. James Lembeli ambaye pia nina mwenyekiti wa
kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, amesema alifanyakazi ya ziada na
wakati ngumu katika kumng’oa aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii,
Bw.Ezekiel Maige (pichani kulia na Waziri mpya Hamisi Kagasheki).
Ameyasema hayo jana wakati akijibu maswali ya wananchi wa Kata ya Majengo,
Kahama mjini baada ya kuulizwa kwanini hakuonekana wakati wabunge wengine
wakiweka saini ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu Bw.Mizengo Pinda
ajiuzulu.
Bw.Lembeli amesema, kupambana na mafisadi ni kazi ngumu ambayo uliianza baada
Spika wa Bunge, Bi. Anne Makinda, kumtaka atoe taarifa ya Kamati yake pamoja
na mapendekezo yake.
"Katika mambo ya msingi kwa maslahi ya taifa na maendeleo, nitakuwa mbele kuwa
mkweli daima na kupiga vita ufisadi na matendo maovu katika kazi zangu za ubunge
ambao sasa ni miaka saba mnanichagua kuwawakilisha" alisema Lembeli.
Anasema baada ya kubaini mizengwe iliyokuwa inafanywa ili asisome maazimio ya
kamati yake, alimfuata Spika wa Bunge na kumuambia kama taarifa yake haitosomwa
atajiuzulu Uenyekiti wa Kamati ya ardhi , Maliasili na Mazingira.
"Nilimwambia Spika Anna Makinda, kama taarifa yangu haitasomwa nitajiuzulu
nafasi yangu, kwani tumetumia zaidi ya shilingi milioni 200 kuchunguza ufisadi
ndani ya wizara ya maliasili na utalii" alisema Bw.Lembeli .
Anasema, ulizuka uvumi bungeni kuwa kamati yake ilihongwa fedha nyingi ili
isisome taarifa hiyo, ndipo alipopatwa na wakati ngumu na kuamua kuchukua
maamuzi mazito ya kupigana kuhakikisha taarifa hiyo inasomwa.
Mbunge huyo amesema isingekuwa haki kuona kamati yake haitoi taarifa ya mambo
ambayo tayari yamefanyiwa uchunguzi na kujua yaliyokuwa yakifanyika kutokana
na mizengwe ya kutaka kutukwamisha ukweli wa taarifa.
"Ningependa pesa, ningechukuwa maana zilikuwa nje nje na kunifanya niziache
kutokana na ukweli wangu, Kahama mlichagua Mbunge makini, asiyependa rushwa.
Mapendekezo ya taarifa ya kamati ya bunge ya Ardhi maliasili na mazingira
yaliyomwondoa waziri wa maliasili na utalii ambae ni mbunge wa jimbo la
msalala katika wilaya ya Kahama Bw. Ezekiel Maige yamepokelewa kwa hisia
tofauti na wananchi na kuleta mgawanyiko mkubwa wa kisiasa na kuwepo
malumbano ndani ya Chama Cha Mapinduzi CCM.
Comments
Post a Comment