NJAMA

SURA YA NNE
FUNUNU III

"Mimi naona tukapate chakula cha mchana kwanza", Sherriff alishauri.

"Sawa", walijibu kwa pamoja. Sherriff alikaa nyuma pamoja na Margret na wakati huo mimi naendesha nikiwa katika mafikara mengi, Sherriff alichukua jukumu la kumtuliza Margret akimweleza mambo mengi juu ya matatizo ya binadamu na kumwambia kuwa asihuzunike sana maana ndiyo binadamu. Kadiri Sherriff alivyozidi kusema ndivyo Margret uso wake ulizidi kutokwa na huzuni kwani mimi nilikuwa nawaangalia katika kioo cha kuendeshea. Hata Sherriff alipofika kusema yeye huwa anaamini kuwa kwa kila linalotendeka linatendeka kwa ajili ya uzuri, nilimwona Margret anamwemwesa kwa mara ya kwanza, na ndipo sura yake ilionyesha uzuri aliokuwa nao. Niliona hata Sherriff aligundua uzuri huo, kwani uso wake ulibadilika kiasi cha kwamba moyo wake uliguswa.

Tulifika New Afrika Hoteli, nikaegesha gari wote tukatoka nje. Basi, moja kwa moja tulifuliza kwenda kwenye lifti ya kutupeleka orofa ya kwanza ambapo ndipo Bandari Grill ilipo. Mbele yangu nilimwona Eddy anavuka sehemu ya mapokezi, halafu akazungusha kichwa akaingia kwenye choo kilichopo hapa chini. Hii ilikuwa ishara kuwa alitaka kuniona.

"Samahani jamani nasikia nimebanwa haja ndogo, tangulieni nakuja sasa hivi. Margret, we ndiye mwenyeji washughulikie wagaeni".

"Bila wasiwasi", alijibu akiwa anaanza kupona kutoka katika mshituko alioupata.

Niliingia maliwatoni nikamkuta Eddy ananisubiri.

"Mpaka dakika hii hakuna chochote", aliniambia bila kuniangalia.

"Sawa, nendeni mkale halafu nenda ofisini nitakukuta huko kiasi cha  saa kumi hivi".

"Oke", alisema huku akielekea kwenye mlango wa kutokea.

Mimi nilimaliZa haja yangu ya uongo na kweli nikaondoka kujiunga na wenzangu. Tulipata muro safi sana hapa Bandari Grill, na kwa sababu kila mtu alikuwa na njaa tulikula kimya kimya.

"Nasikia kichwa kinaniuma", Veronika alilalamika.

"Nafikiri kwa ajili ya hali ya hewa. Joto jingi sana kuliko ulilozoea", nilimjibu.

"Kama ni hivyo afadhali ukameze dawa upumzike, sisi tutakwenda kumwona Kiki halafu tutakuja kukuona", Sherriff alishauri.

"Naona hivyo ni sawa", alijibu.

Basi tulikubaliana Veronika apumzike sisi tuendelee na shughuli. Tuliondoka New Afrika na kumtelemsha Veronika Kilimanajaro.

"Vero mpenzi, kuna gari lile pale unaweza kulitumia wakati wowote. swichi iko chini ya zulia", nilimuonyesha gari ambalo Eddy alikuwa ameliacha hapo. Sisi tuliondoka na kuendelea na safari yetu ya Kinondoni.

"Twende kupitia barabara ya Upanga moja kwa moja, halafu tukivuka Salendar briji mbele kuna barabara ya Kinondoni hivyo tutaingia kushoto. Sehemu iko mbele ya makaburi. Baada ya makaburi kuna barabara la vumbi, linakatisha barabara hii. Tukiacha hilo na kuendelea mbele tukakuta barabara nyingine ya vumbi inaingia kushoto na kuna kibao kimeandikwa Bamboo Baa and Restauranti, basi hapo ndipo tutakapoingia", alieleza Margret kwa ufasaha kabisa.

Mimi hupenda maelezo ya namna hii, siyo mtu amefika mahali pa kukata kona ndipo anasema, kata hapa kushoto. Maelekezo hayo ni ya kihuni na ndiyo anayosababisha ajali nyingi.

Nilifuata maelezo ya Margret vizuri kabisa, nilipotaka kuingia kushoto pale kwenye bao la tangazo la Bamboo Baa and Restauranti, Margret alisema, 'Njia hapa si nzuri twende pole pole, halafu mbele kidogo utakata kushoto tena tuelekee kwenye nyumba hizo pale", alinielekeza na kuonyesha kwa kidole.

Niliendesha pole pole nikaikuta njia na kuifuata kuelekea kwenye nyumba hizi za shirika la nyumba.

"Baada ya nyumba hiyo yenye bendera ya CCM, ambayo ndiyo ya mjumbe, ya pili yake".

"Hapa?".

"Ndio, mlango huu huu".

Nyumba hizi zinakaa familia mbili mbili, lakini zimetengwa katikati kiasi kwamba kila familia ina sehemu yake kamili. Tulitoka ndani ya gari, Margret akatangulia na kibisha hodi. Lakini hatukupata jibu. Nilisikia moyo wangu unapiga haraka haraka, hii ni sirika niliyozaliwa nayo, na ilikuwa ni ishara kuwa kuna hatari.

"Hebu ngoja Margret", nilimwambia nikimrudisha nyuma.

Niliujaribu mlango ukafunguka nikamwita Sherriff na kumwambia hakuna mtu, tulifungua mlango mwingine uliokuwa unaelekea jikoni, bafuni na chumba cha kulala. Tukiwa wote na wasiwasi tukibisha hodi kwenye mlango wa chumba cha kulala. Lakini hatukupata jibu. Nilitoa Bastola yangu, na kusukuma mlango wazi.

Tulimkuta mtu ambaye tuliamini ni Kiki amechomwa kisu kifuani!, nilipomshika nikajua alikuwa amekwisha kufa saa nyingi sana. Kisu kilikuwa kimeachwa pale kifuani. Kilikuwa kisu kikubwa na mpini wake mwekundu. Tulimwita Margret aje atuhakikishie.

Akiwa anatetemeka kwa woga alikuja na kusema, "Ndiye yeye masikini", akaanza kulia tena tulimbembeleza na kumvuta na kuondoka haraka haraka ndani ya nyumba hiyo. Tuliingia katika gari langu na kuelekea mjini. Sasa nilianza kuongeza hesabu kwamba mbili na mbili na kupata nne. Na vile vile majahiri hawa walianza kunitisha kwani mbinu zao zilikuwa kubwa. Lakini hata hivyo mbinu za Willy ni kubwa zaidi.

"Mapambano yameanza Sherriff", nilisema kwa sauti ambayo sikuamini ilikuwa yangu.

"Na kweli yameanza", Sherriff alijibu.

Wakati huo tulikuwa tumesimama kwenye taa za usalama barabarani za salendar briji tukuelekea New Afrika. Saa yangu ilisema ni saa kumi na dakika mbili.

"Naona mimi mnifikishe nyumbani", Margret aliomba.

"Unakaa wapi".

"Ninakaa kwenye orofa pale nyuma ya Rex Hoteli".

"Nazijua orofa hizo, uko orofa ya ngapi, maana tunaweza kukuhitaji ama kikazi ama katika hali ya kustarehe, unasemaje?".

"Karibu mimi niko orofa ya pili chumba namba kumi na nane. Simu yangu ni 22221".

Basi wakati huo tulikuwa tumefika Posta ya Azikiwe, tulipofika kwenye sanamu ya Bisimini, tukaingia Independent Evenue.

"Unajua", Margret alitugutusha.

"Ehee", nilijibu na kumwangalia ndani ya kioo cha kuendeshea, maana yeye alikuwa amekaa nyuma.

"Sijui ni mafikara yangu, ila tu limekuja kama wazo la kunishangaza, maana baada ya kutokea mambo haya kila kitu nakiona si cha kawaida kinanigutusha".

"Nini kimekugutuusha?", Sherriff aliuliza akionesha msisimko.

"Unajua pale kwenye lango la kuingia ndani ya ofisi yetu kumekuwa na mwendawazimu ambaye amekaa pale zaidi ya mwezi mzima. Amekuwa amevaa matambalatambala tu na amebeba makopo mengi, sijui mmemuona?".

"Mimi nilimwona", Sherriff alijibu.

"Mimi sikumwona".

"Polisi walikuja kumchukua siku moja, na kumpeleka kunakohusika lakini hazikupita saa tatu akarudi. Alikuwa hatoki pale hata dakika moja, usiku na mchana kutokana na walinzi wa usiku wanavyosema. Leo mlipokuja alikuwepo maana mimi niliona gari lenu linaingia wakati natoka kunywa chai. Gari lenu lilipoingia na yeye alivuka lango akaingia ndani. Hii ni kawaida yake, kwani huwa anaombaomba kwa kila mgeni anayefika pale ofisini na ndio sababu aliitiwa polisi kwa sababu anawafadhaisha wageni wetu. Gari lenu mliliegesha mbele kabisa ya mlango wa kuingia mapokezi na kutoka ndani ya gari haraka hivyo hakuwahi. Mimi nilipoingia pale mapokezi nilikuta nyinyi mmekwisha kwenda ofisini kwa Mantare ila nilimkuta yule kichaa anamuuliza yule msichana wa mapokezi. Hawa watu wanasema wanatoka katika gazeti la Afrika. Yule msichana wa mapokezi alikasirika na kumfokea, Toka hapa! kama wanatoka gazeti la Afrika watakufaa nini wewe?, wana kazi ya maana kuliko kuonana na mwendawazimu kama wewe. Toka!".

"Kitu cha kushangaza ni kwamba wakati tunaondoka pale ofisini kwetu nakumbuka sikumuona wala makopo yake na kilago chake hakikuwepo, sijui jambo hili lina maana yoyote au mnaonaje nyinyi wenyewe?", alimalizia Margret.

"Unasema alikuja hajawahi kutoka pale hata dakika moja, ila tu siku ile aliyochukuliwa na polisi kwa muda wa masaa matatu?", nilimuuliza.

"Nina uhakika kabisa maana mimi damu yangu ilikuwa haipatani na yule mtu kabisa, na ni mimi niliyefanya kampeni ya kumuitia polisi lakini aliporudi alionekana kuwa maafisa wote walidharau kumchukulia hatua tena".

"Ukimwangalia alikuwa anaonekana kichaa au unafikiri anajifanya tu?", nilimuuliza.

"Kitu kilichonikosanisha naye ni kwa sababu siku moja aliniambia yeye si kichaa ila anajifanya tu ili kujipatia pesa bila jasho. maana ilikuwa ukimwangalia sana wakati yeye hana habari anakuwa kama si mtu kichaa, ila huwa anapoona watu anakuwa kichaa kabisa".

"Asante sana, kumbuka jambo hili linaweza likawa na msingi tutaliangalia".

"Asante".

Niliegesha gari mbele ya Rex Hoteli.

"Wakati wowote tutegemee", nilimweleza huku akitelemka.

"Mnakaribishwa", akiwa zaidi anamwangalia Sherriff. Sherriff alitoa mkono wake wakapeana mikono. Tayari kulikuwa na kitu kinapita kati yao, maana nyuso zilikuwa wakati wanapeana mikono, mimi ndiye najua, maana hata mimi hali hii inanitokea. Walikuwa wameanguka katika penzi.

"Mimi naona turudi pale ofisi ya kamati tukahakikishe kama kweli hayupo pale yule kichaa", nikimwambia Sherriff.

"Sawa".

Tulikwenda kimya kimya kila mtu akichambua mambo, tuliyokuwa tumeyapata na kuyaona, tulipofika pale ofisini tulimkuta mlinzi wa jioni anayeingia kazini saa tisa wanapofunga kazi mpaka saa kumi na mbili asubuhi, ilionekana alikuwa anafanyakazi masaa mengi sana, lakini yeye alipenda kazi yake na kuridhika na kipato alichokuwa anakipata, baada ya kutusalimia na kutueleza hizo saa zake za kazi, nilimuuliza.

"Unajua kulikuwa na mzee mmoja kichaa hapa sijui amehamia wapi?'.

"Hata mimi nashangaa, kichaa huyu alikuwa hatoki hapa hata dakika moja. Hata haja zake alikuwa akiifanya hapa hapa karibu. Polisi walimchukua hapa akawachenga akarudi mwishowe wakamwachia akae tu. sasa leo nafika nakuta kiisha ondoka na wala harufu yake hakuna. Nimeshangaa sana. Amekaa karibu mwezi mzima".

"Ulikuwa unapata fursa ya kuzungumza nae?".

"Si mara nyingi, ila tu siku moja nilikuja na ..........akasita kusema.

"Sema tu usiogope, hata kama ni siri, sisi tutakufichia".

"Lakini nyinyi ni akina nani?".

"Sisi tunashughulikia wagonjwa wa akili, tumepata habari toka polisi kuwa kuna mwendawazimu hapa, hivyo unaweza kutueleza tabia yake ili tuweze kumtafuta. Kwa hiyo usisite kutueleza", nilidanganya.

Baada ya kutafakari mambo haya aliendelea, "Siku moja kulikuwa na tafrija hapa ofisini jioni. Mimi niliweza kwa mbinu zangu kujipatia mzinga mzima wa whiski aina ya 'Dimple' nikauficha wagaeni wote walipoondoka, nilitoka nje ya lango na kuanza kunywa huu mzinga wa whiski. yeye alipoona ninakunywa hii whiski alikuja na kopo lake akaniomba kwa vile nilikuwa najuwa siwezi kumaliza chupa nzima nilimgawia nusu basi alikunywa ile pombe kama maji. Basi ilipomkolea akaanza kuzungumza Kiingereza ila mara kwa mara alisema neno sijui 'Sazafrika' neno hili alilirudia mara nyingi. Na nyinyi mnajua vichaa mimi niliachana nae nikaendelea na shughuli zangu. Sasa sielewi kama kilikuwa Kiingereza sawa sawa. Lakini kitu kilichonivutia ni kule kutamka hicho Kiingereza chake kama mzungu. Lakini husema kichaa ana mashetani saba, anaweza kuzungumza lugha saba tofauti."

"Asante sana, na samahani sana kwa kukubugudhi", Sherriff alitoa mfukoni shilingi arobaini akampa. Yule Mzee alifurahi sana.

"Mungu awaongezee wanangu".

Tuliingia ndani ya gari tukaondoka zetu.

"Unaona mambo yalivyo Sherriff?, hii inaonyesha wazi kuwa George Kiki alikuwa ni jasusi aliyepachikwa hapa na mabeberu na wakafanikiwa. Mimi simulaumu mtu yeyote, hata mimi huenda ningemsaidia kupata kazi. Baada ya mabeberu kujua mkataba wa silaha kati ya PLF na Urusi miezi sita iliyopita walichukua hatua ya kuhakikisha hizo silaha haziwafikii wapigania uhuru wa PLF maana inasemekana ni silaha za kisasa kabisa. Tutakapoonana na kiongozi wa PLF atatueleza zaidi, kuajiliwa kwa kiki miezi sita iliyopita kunaoana kabisa na nyakati za mkataba huo. Inaonekana kazi ya jasusi huyo ni kujua mambo yote yanayotendeka juu ya huo ili mwishowe aweze kuiba hizo karatasi za kuchukulia silaha, jambo hili amefanikiwa", nilinyamazi kidogo.

"Kwanini wamwue?", Sherriff aliuliza.

"Kwa sababu hawakuwa na haja nae tena, asije akashikwa na kutoa siri. Hii inanionyesha jinsi watu hawa walivyo wajuzi katika kazi yao, hawataki kufanya makosa".

Wakati huu tukizungumza tulikuwa tukielekea mjini.

"Juu ya huyu kichaa unasemaje?".

"Huyu kichaa nae ni jasusi. Ninavyoona mimi huyu aliwekwa pale ofisini kusudi aweze kuona nini kitatokea hapo ofisini baada ya silaha kuibwa. Aliwekwa mwezi mmoja ili kuondoa mashaka. Hivyo alikuwa anangoja kuona baada ya polisi na maofisa wa usalama ni nani mwingine aliyekuwa na dukuduku juu ya jambo hili. Aliposikia waandishi wa habari wa gazeti la Afrika nao wamejiingiza akawa amemaliza kazi, akaondoka kwenda kupeleka ujumbe, ni wazi kabisa wao walijuwa polisi na maofisa wa usalama watalishughulikia jambo hili na ninafikiri walishapima uzito na kuona wanaweza kukabiliana nao. Hivyo walingoja wajue kama kuna kundi jingine litakalojiingiza katika katika upelelezi wa tukio hili. Sasa wamejua; kwa hivyo waandishi wa gazeti lazima muwe macho. Tokea sasa kaeni katika tahadhari; lolote linaweza kutokea. Unaonaje maoni yangu?'.

"Lo Willy, ndio maana wewe ni mpelelezi maarufu katika Afrika. Maelezo yako yanaeleza hali halisi kabisa. Na swali ulilomuuliza Margret kama kuna mtu mwingine aliyeweza kuona akiweka karatasi ndani ya mkoba, mimi nilikuwa silifikilii kabisa na ndilo swali lililotupa mwanga. Kweli kila mtu na kazi yake", alisifu Sherriff.

"Lakini maswali mliyouliza ninyi vile vile ni ya maana sana, nafikiri kuliko waliyoulizwa na Polisi. Sidhani Polisi wameishafikia hii tuliyofikia kwa muda huu mfupi".

Mara wazo likanijia.

"Lile jambo lililokuwa linakutatanisha nimepata jibu lake. Swali la nani aliyepiga simu kwa Mlingi akiiga sauti ya Mantare na maneno ya Mantare aliyozoea kuzungumza na Mlingi".

"George kiki", alijibu Sharriff.

"Kabisa, unajuwa Kiki alikuwa anaingia ndani ya kila ofisi ya ofisa akiwa kama tarishi. Swali hili nilimuuliza Mantare akakubali. Hivyo Kiki akiwa jasusi aliyefundishwa, ninavyofikilia, haikuwa kazi kumsiliza Mantare katika simu zake nyingi na ninafikiri alifanya kila njia kusikiliza simu kati ya Mantare na Mlingi. Hii inaonekana wazi kabisa".

"Lo tunaanza kuona mwanga sasa", Sherriff alisema.

"Kweli tumeona mwanga, lakini ni mwanga unaotufikisha kwenye giza nene. Maana Kiki ambaye angetupa fununu ya watu hawa amekufa, yule kichaa lazima ameshapotea hewani, gtumerudi pale pale".

"Watu hawa ni akina nani na silaha hizi ziko wapi?", niliuliza swali hili wakati naegesha gari New Afrika.

"Hilo ndio swali gumu lakini afadhali tunajua Afrika Kusini inahusika, maana Kiki katokea huko. Na yule kichaa alipolewa alizungumzia Sozafrika ambayo nasadiki ni South Afrika".

"Sawa kabisa, lazima tujuwe tunapambana na South Afrika na haikosi shirika lao la ujasusi 'BOSS', linasaidiwa na mashirika mengine ya ujasusi ya nchi za kibeberu. Hivyo tutakuwa na kazi ngumu maana watu hawa nimewahi kupambana nao ni watu hatari kabisa".

"Tumwombe Mungu atasaidia".

"Na wewe ukijisaidia", nilijibu.

Wote tukacheka na kutoka ndani ya gari. Ilikuwa saa kumi na moja. Hivyo kabla hatujavuka barabara nilionelea nifike ofisini kidogo halafu niende nyumbani.

"Sherriff mimi nafika nyumbani kidogo, nitakuona saa kumi na mbili kamili".

"Sawa nitakusubiri hapa duka la kahawa".

oke basi saa kumi na mbili".

Niliingia ndani ya gari na kuondoka. Nilipofika ofisini nilimkuta Eddy na vijana wengine. Linda alikuwa ameshaondoka.

"Eddy kuna mtu mmoja anaitwa George Kiki, alikuwa akifanyakazi kwenye ofisi ya Kamati ya ukombozi kama tarishi?, hapa aliingia kama mkimbizi baada ya kutoroka Afrika Kusini. Alifika ofisi za chama cha SANP, ambao walimpeleka kwenye Kamati ya Ukombozi waweze kumsaidia angalau kazi yoyote. Inawezekana hana kisomo cha kutosha. Nataka ukague habari hii kwa kutumia njia zetu za kawaida. Unaweza kuwajulisha makomredi wetu kule Soweto, nadhani watakuwa na maelezo kamili. Habari hizi nazitaka haraka. Kila kitu, aliingiaje hapa alikwendaje kwenye ofisi za SANP alikuwa anaishi namna gani, nani walikuwa rafiki zake nk. wewe unajua".

Eddy aliyekuwa anachuku maelezo haya alijibu.

"Atashughulikiwa bosi, usiwe na wasiwasi".

"Chifu yuko?".

"Kaondoka".

"Haya asante, usitoke mpaka nitakapokujulisha tena".

"Mimi nipo".

Ndio sababu nilimpenda mtoto huyu. Nidhamu yake kwangu ilizidi ya mdogo wangu ambaye tumetoka ndani ya tumbo la Mama Willy. Niliingia ndani ya gari nikaelekea zangu Upanga.

Niliposimamisha gari mbele ya mlango, moja kwa moja macho yangu macho yangu yakaangukia kwenye kitu kilichokuwa kwenye ubao wa juu ya mlango mkubwa wa kutokea nje. Nilitoka nje ya gari haraka haraka nikiwa tayari kwa mapambano.

Nilikuta ni kisu chenye mpini mwekundu kama kile tulichokikuta kwenye kifua cha maiti  Kiki; ncha yake ilitumiwa kama kipini cha kubandika kipande cha karatasi pale mlangoni.
Niliking'oa nikachukua karatasi na kusoma yaliyobandikwa hapo yalisema.

Willy Gamba, kama unathamini maisha yako achana na hao watu wa gazeti la Afrika. na kama ni rafiki zako waambie waondoke hapa mjini tunawapa mpaka saa kumi na mbili jioni wawe uwanja wa ndege. Vinginevyo yaliyompata Kamara Frank yatawapata na nyinyi. Hili ni onyo kali na si mchezo. Shughulika na mambo yako usishughulike na mambo ya watu wengine. Wapo wenyewe wanaohusika waachie. Nasema tena saa kumi na mbili jioni leo wawe uwanja wa ndege na wewe baada ya kuwafikishia habari hizi tusikuone unashughulika zaidi ya kazi yako ya kawaida ya AIA Subiani.

Kwanza nilicheka maana niliona kazi sasa inaanza. Hii inaonyesha upelelezi wetu ulikuwa  umewashitua kuliko wa Polisi. Nilijua yule kichaa alifanya kazi yake vizuri sana, maana ni yeye tu aliyetufahamisha kwa majahiri wenzake. Hiki kisu chenye mpini mwekundu ilimaanisha damu. Nami niljua damu imeanza kunuka.

Nilifungua mlango nikaingia ndani, nikakoga haraka haraka kisha nikabadilisha nguo nilifungua sanduku langu la silaha na kuchukua bastola zingine mbili kwa madhumuni ya kuwapa Sharriff na Verokika kwani hakukuwa na mchezo tena, maana upatapo onyo toka kwa watu kama hawa huwa hawatanii. Kisha niliinua simu na kupiga kituo cha Polisi cha Salendar Bridge.

"Hallo kituo cha Polisi hapa".

"Sikiliza, nenda Kinondoni Hananasifu, Estate kwenye nyumba ndogo ndogo za shirika la Nyumba nambari IIC utakuta kuna maiti ambayo ina zaidi ya masaa ishirini na nne", kabla hajatamka neno nilikata simu. Niliangalia saa yangu muda ulikuwa umekimbia na ilikuwa saa kumi na mbili kamili. Niliingia ndani ya gari nikakimbilia New Afrika.

Nilipoingia duka la kahawa sikumwona Sherriff nikapata wasiwasi. Nikaenda mapokezi kuuliza wakaniambia aliacha habari kuwa amekwenda dukani mara moja nimsubiri. Nilirudi nikasimama nje pale magari yanapoleta watu New Afrika yanapozungukia. Niliangaza huku na huku na mara nikamwona Sharriff anakuja akiwa anavuka tawi la Benki ya nyumba. ghafla alipokuwa anataka kuvuka barabara ilitokea gari sijui wapi ikapiga breki, wakatoka watu wawili haraka kama umeme, wakamvuta Sharriff ndani ya kiti cha nyuma cha gari, na gari hilo likaondoka tena kama umeme. Kitendo hiki hakikuchukua hata nukta tano.

Watu wote waliduwaa wasijue cha kufanya, lakini mimi Willy nilijua la kufanya. Nilikimbia kwenye gari Eddy alilokuwa amekodi na kuliacha New Afrika. Kwa vile alikuwa ameliegesha vizuri niliingia na kuondoka kama umeme. Nilikuwa nimeona lile gari linakata kulia kutoka barabara ya Azikiwe kuingia Azania Front. Nilipoingia Azania Front niliona gari lao linafika kwenye ofisi za NASACO nikacheka.

ITAENDELEA

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru