NJAMA


SURA YA SITA
CHIMALAMO

"Baada ya kuzungumza na wewe kwenye simu, niliondoka kwenda New Afrika kama tulivyoagana. Niliona hakuna sababu ya kuchukua gari, hivyo niliondoka kwa miguu kwani nilijua dakika kumi ningenitosha. Nilikuja moja kwa moja na barabara ya Azania Front nikakatisha pale kwenye kanisa la Kilutheri na kutokea barabara ya City Drive. Kama unavyojua New Afrika inajengwa kwa mbele kwa hivyo nilijipenyeza kwenye mwanya wa jengo la Benki ya Taifa ya Biashara tawi la City Drive na Azikiwe, nikawa nimetokea karibu kabisa na pale ulipoegesha gari lako".

Ghafla nikaona watu wawili, mmoja wao akifungua mlango wa gari lako. Mimi nikasimama na kujibanza kwenye moja ya nguzo za jengo hili la Benki huku giza likinisaidia. Yule wa mbele aliingia na nyuma akaangalia huku na huko hakuona kitu nafikiri, maana alitoa bastola mwenye joho lake nae akaingia. Kama unavyojua gari hili lina milango miwili tu, hivi waliinamisha kiti na kuingia nyuma ya gari.

Mara moja nikajua nia yao; nilijua wanakusubiri wewe ama kukuua ama kukuteka nyara. Nilipofikiri sana niliona nia yao kukuteka nyara kwani kama ni kukuua wasingeingia ndani ya gari, hasa nyuma, na mahali penyewe pakiwa karibu sana na New Afrika. Huwa naamini sana akili zangu zinavyonituma hivyo nikaona kuwa nia yao ni kukuteka nyara. nilifikiri nikufuate lakini sikuwa najua ofisi yako ilipo. Hivyo nikaamua kitu kimoja, kuingia ndani ya buti la gari kama iwazi. Kwa kuwa gari yako ina nyavu kioo cha nyuma, nilijua watu hawa hawataniona wala kunisikia, kwani nilijua na wao watakuwa wamelala chini ili usije ukawaona wakati unaingia".

Alinyamza kidogo ili kulegeza koo kwa mate, akaniangalia akanikuta mimi naendesha taratibu huku nikimsiliza kwa makini sana. Kisha akaendelea, "Nikisaidia na giza la ukuta wa mabati uliozungushiwa jengo hili la mbele la New Afrika huku nikinyata nimeinama kimo cha buti la gari. Kama bahati ilivyokuwa na mimi nilikuta buti lako halikufungwa na funguo. Jihadhari sana siku nyingine utabeba adui ndani ya gari lako".

"Nimekuwa sina aduin Tanzania, hivyo nimekuwa nikiamini kuwa hakuna mtu wa kunifanyia ubaya, maana hata sijawahi kugombana na mtu hapa Dar es Salaam".

"Haya sasa lazima utambue kuwa umepata maadui; lazima ujihadhari".

"Sawa nitajihadhari lakini vile vile kama ningekuwa nimefunga usingeweza kuniokoa, hivyo kujiachia mambo mara nyingine ni vizuri".

"Haya nimekubari kushindwa, lakini hata hivyo ningepata njia nyingine. Basi taratibu nilifungua buti la gari na kuingia ndani, kimya kimya kabisa bila kelele yoyote. Niliwahi kusafiri ndani ya buti wakati ninakaa na majeshi ya POLISALIO, hivyo najua sana hali ilivyo ndani ya buti la gari kiasi kuwa kwangu hewa ya mle ninaweza kuistahamili ingawa ni kidogo. Unajua gari linapoanza kutembea hewa inajaa kabisa. Basi baada ya kuingia na kulifunga kinamna, kiasi ambacho lisingeweza kunishinda kufungua, baada ya kuliangalia kufuli lenyewe.

"Muda si mrefu nilisikia mlango unafunguliwa; unajua hili gari lako lilivyoundwa ukiwa ndani ya buti unasikia maneno yanayozungumzwa ndani ya gari. Basi niliwasikia wakikuamrisha kuendesha gari ndipo nikajua nilivyohisi ni sawa. Ulipopiga honi na kusimama kama ulivyoamrishwa, nilijua tunaingia mahali na nikajua kuna mtu anayefungua na kufunga mlango ni wa kundi lao hivyo atakuwa ni mlinzi mwenye silaha.

"Tulipoanza kuondoka niliinua mlango wa buti kidogo sana na nikamuona mtu huyu nusu amebeba bunduki. Niliendelea kuchungulia hivi hivi nikaona njia tuliyotokea kutoka kwenye lango mpaka gari liliposimama nikabana tena mlango. Nikasikia wanakuamru toka kisha nikasikia sauti zingine hapo nje halafu pakawa kimya, ndipo nikafungua taratibu mlango na kutoka nje. nikakata shauri lazima nipate silaha ili niweze kukuokoa. 

"Hapo ndipo nilipoanza kurudi mbio kwenye lango ili nikamnyanganye silaha yule mlinzi. Nilipokaribia lango nilimuona yule mlinzi amesimama anavuta sigara huku anaangalia upande wangu. Nililala chini na kusubiri. Alipogeuka na kuangalia upande mwingine nilianza kutambaa chini kimya kimya. Nilikuwa nimefundishwa na wanajeshi wa Polisalio namna ya kumnyemelea mtu kwenye giza bila yeye kushituka. Nilipokuwa karibu nae kabisa, nilisimama na kupiga kelele, "Yeeeeee".

"Alishituka na kuingiwa na hofu na kabla hajatokwa na hofu nilipiga teke mikono yake bunduki ikaanguka chini. Alipoona hivi akaanza kukimbia. Niliruka na kumpiga teke mgongoni akaanguka chini. Bila kuchelewa nilimrukia shingoni, ndivyo ikawa kwaheri. Nilimvua joho nikalivaa halafu nikatafuta kofia. Nilipoipata nikaivaa halafu nikachukua bunduki nikakuta ni aina ambayo wanaitumia wana mapinduzi wa Polisalio, yaani SMG ya kichina, hii bunduki niliitumia sana wakati nimekaa na hawa mashujaa wa Polisalio.

"Nilipoipata silaha hii, nilikimbia kurudi kwenye kibanda mlichoingia nipokaribia nikaona watu wawili wenye bunduki nikononi wakizunguza. Mimi nilizunguka nyuma ya kibanda cha karibu, halafu nikakohoa kisha nikazunguka haraka kutoka pale nilipokoholea. Nilisikia mmoja wao akisema; "Umesikia hicho".

"Ndio", alijibu mwenzake.

"Wewe zunguka huku na mimi nitapita huku".

"Hii ilinipa nafasi kujitayarisha, sikuwa nahitaji kutumia bunduki maana mrio ungewashitua watu waliokuwa ndani ya kibanda. Kwa vile nilikuwa nimevaa nguo kama wao na kofia, nilizunguka na kukutana na mmoja wao, yeye alinichukulia ni mwenzake shauri ya mavazi na giza. Tulikaribiana sana akabweteka; "Umeona nini?". Mimi niliinua mkono kumuonyesha nyuma yake na alipogeuka tu nikamkata karate ya shingo iitwayo ua na bila shaka alikufa pale pale. Nilimdaka haraka haraka na kumlaza chini bila kishindo. Kisha nikageuka upesi upesi ili nikutane na yule aliyepita upande mwingie sikuchukua hata hatua tatu tukawa tumekumbana hata yeye mavazi yalimdanganya na kufikiri mimi ni mwenzake.

"Huku hakuna kitu", aliniambia kwa sauti ya chini chini. Nilimdanganya kwa kumuonyesha kwa ishara aangalie nyuma yake na yeye akadanganyika. Hapo ndipo nilipomrukia nikamtia kabali ya hali ya juu mpaka niliposikia shingo linakatika nikamwachia. Sina mkanda mweusi wa judo na karate bure Willy, najua jinsi ya kuutumia".

"Zaidi ya ambavyo ningetegemea mrembo kama wewe kuutumia", nilimjibu huku nikitoa tabasamu.

"Asante. Baada ya hapo ndipo nilikimbia na kupiga teke mlango kwani nilisikia mlio wa bastola kabla sijapiga teke mlango. nilipoingia nilikuona chini hivyo nikafanya kama ulivyoona. Lo! Willy mpenzi niliogopa niliposikia mlio wa bastola nikafikiri wamekuua!".

"Si lahisi kuniua".

Nia yao ilikuwa nini?".

Nilimweleza yote waliyoniuliza.

Wakati namaliza kumweleza nilikuwa nataka kutoka barabara ya Upanga na kuingia nyumbani kwangu na kupeleka gari moja kwa moja gereji. Tukashuka nikafunga mlango wa gereji.

Karibu ndani vero.Hapa ndipo nyumbani kwangu".

Nilifungua mlango na kuwasha taa ya sebuleni halafu nikamkaribisha ndani akaketi kwenye
kochi.

"Asante lakini sitakaa sana, maana nasikia uchovu, nataka kurudi hotelini nikalale".

"Hakuna haja Vero nina mengi sana ya kukusimulia, maana hata sijakueleza yaliyotupata na Sherriff. Halafu....... nikasita kidogo".

"Halafu nini?", aliuliza kwa shauku.

"Halafu uliniahidi tulipokuwa Siera Leone kuwa tutafahamiana vizuri zaidi Dar es Saalaam, lazima ujuwe kwamba ahadi ni deni".

"Haya baba umeshinda".

"Asante".

Nilichukua vinywaji ndani ya barafu, halafu nikamkaribisha katika chumba cha kulala. Nilizima taa sebuleni nikafunga mlango wa mbele, nikakagua vyumba vyote vya nyumba pamoja na madirisha na milango. Nilipoona kila kitu ni salama nilirudi chumbani nikafungua mlango wa maliwatoni, nikajaza maji kwenye karai la kuogea. Nilimwita Veronika aje tuoge. Tulioga pamoja na mtoto huyu mara moja nikasahau matatizo yangu yote na uchovu wote wa jioni ile. Baada ya kutoka maliwatoni tulikuwa tayari kulala.

"Haya nieleze sasa wakati tukipumzika", Veronika alisema huku amelala karibu yangu.

Nilizima taa yenye mwanga mweupe, nikawasha yenye mwanga wa bluu. Nikaleta chupa yenye whiski kwenye meza ya kitanda nikammiminia Vero ndani ya glasi nikaweka mawe ya barafu na mimi nikatengeneza yangu.

"Na tunywe kwa usalama wa maisha yetu wote".

Tulianza kunywa huku nikimweleza yote yaliyotupata. Baadae tukaelezana mambo yetu binafisi ambayo yalitufanya tujishitukie tumekumbatiana na kubusiana.

ITAENDE:LEA

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru