NJAMA

SURA YA SITA
CHIMALAMO

II

"Amka", Vero alinishitua, "ni saa mbili sasa.

Nilimwangalia Vero ambae alionekana kuwa alikuwa ameamka kitambo kwani alikuwa na sahani ya mayai ya kukaanga na vikombe viwili vya kahawa. Alikuwa amevaa pajama zangu; alitoa sura ya kuchekesha, hivyo nilimcheka, maana zilimpwaya sana.

"Unapendeza katika pajama hizo", nilimtania.

"Kwenda huko".

Mimi nikaangua kicheko, nikatoka kitandani na kukaa.

"Mwenzangu umelala fofofo leo. Mimi nimeamka nikafanya mazoezi kisha nimekwenda jikoni nikatayarisha chochote. Haya tunywe kahawa utoe usingizi", alisema huku akikaa karibu nami.

"Mimi naona nikaoge kwanza".

"Hapana. Tunywe kahawa kwanza halafu tutafanya mazoezi ya judo na karate ili niwe katika hali nzuri, halafu ndipo tutakwenda kuoga".

Basi tulikunywa kahawa na mayai ya kukaanga, halafu tukatoka nje uani kufanya mazoezi. Nyumbaq yangu ilikuwa imezungukwa na ua mzuri wa michongoma iliyokatwa vizuri na yenye urefu wa futi saba. Hivi ukiwa uwani kwangu mtu anayepita nje ya ua hawezi kuona kitu chochote kinachofanyika ndani. Basi tulifanya mazoezi ya karate na judo ya hali ya juu sana. Hii ilinihakikishia kuwa Veronika alikuwan na ujuzi wa kutosha. Ilibidi tu kumwonyesha kuwa mimi najua zaidi nilipomwingizia staili nyingine za pekee ambazo hutumiwa na wajuzi wa hali nya juu katika karate na kung-fu kama mimi, ambazo zilimshinda kuzifuata.

"Ujuzi wako unatosha kabisa Veronika. Naamini unaweza kupambana na mtu yeyote, na nina imani ni watu wachache sana wanaweza kukushinda katika karate na judo".

"Asante kwa pongezi laki. Lo, lakini wewe mwenzangu ni zaidi. Mitindo mingine unayotumia sikuwahi kuiona hata kwa walimu wetu huko Japan. Ndio sababu wanasema ulipambana na Inoki na kutoka nae sare. Nilivyani walikuwa wanaongeza chumvi lakini sasa ninaamini ni kweli. Kokote nitakapotembea na wewe hata pakiwa ni pa hatari namna gani sitaogopa kabisa maana nina imani kubwa katika uwezo wako kwa jambo lolote sasa".

"Asante".

Baada ya mazoezi tuliingia pamoja maliwatoni tukakoga.

"Mimi itabidi unipeleke hotelini nikabadili nguo. Angalia hizi zilivgyochafuka kwa ajili ya matatizo ya jana usiku!".

"Usiwe na taabu, lolote utakalosema".

Mimi nilibadilisha nguo, nikavaa vizuri kabisa kama mfanyabiashara. Nilichukua silaha tulizokuwa tumeziteka nikaziweka sehemu yangu ya siri ambako huweka silaha zangu na ni mimi peke yangu ninayepajua mahali hapo. Na hata ukiwa mtu wa namna gani huwezi kupagundua. Nilichukua silaha nyepesi kwa ajili ya siku hiyo kama litatokea jambo lolote. Nilimpatia Veronika bastola yenya sailensa. Nilipoona mipango yote nimekamilisha tuliondoka kuelekea Kilimanjaro hoteli. Ilikuwa saa tatu na robo tulipofika Kilimanjaro.

"Nenda kajitayarishe, kabla ya saa nne mimi nitakuwa hapa".

"Utanikuta tayari", Veronika alijibu.

Niliondoka na kuelekea ofisini. Nilimkuta Eddy nae anaingia. Alipoona gari langu akasimama mlangoni kunisubiri.

"Habari za leo bosi?".

"Nzuri Eddy, umelala salama kijana?".

"Ndio, bila taabu".

"Twende ofisini kwangu". Tulielekea ofisini kwangu. Tulimkuta Linda anazungumza kwenye simu. Alipotuona akasema, "Huyu ameingia", Akanipa simu huku akisema "Maselina huyo.

"Halo mrembo, habari za asubuhi?".

"Nzuri tu, wasiwasi kwako ambaye unalala mpaka saa tatu na waandishi wa habari ".

"Mwongo, nani kakuambia huyo mwandishi kalala kwangu ?".

"Nani hakujui, danganya wengine lakini miye baba unajua kabisa kuwa nakujua kama nyuma ya kiganja changu".

"Haya umeshinda wewe".

"Njoo Chifu anakuhitaji, anataka kujua umefikia wapi mpaka sasa".

"Haya nakuja, nitamweleza mpaka yeye atachoka".

"Haraka basi", alisema Maselina na kukata simu.

"Eddy jambo lolote juu ya Kiki?".

"Si nilikwambia nitakuwa na habari zote saa nne, na saa nne bado". Eddy alijibu.

"Oke, je juu ya bohari la Mamlaka ya Pamba umepata nini?".

"Walinzi wote wa bohari hilo wamekutwa leo asubuhi wameuawa huko Temeke. Inaonekana walilichukua bohari hilo kwa nguvu ili wafanyie kazi zao kwa muda tu. Kila kitu kingine ni salama. Polisi wanashughulikia hayo ya jana na kujaribu kutambua maiti walizozikuta hapo. Wao wanafikilia ni wezi. Gari walilotumia nalo lilikuwa limeibiwa".

Kisha nikamweleza yaliyokuwa yametupata na Veronika, baada ya kuachana nae jioni ile.

"Sasa fanya uchunguzi ujuwe watu hawa wamejiingizaje huko uwanja ya maonyesho ya Saba Saba, maana uwanja huo unalindwa na polisi masaa ishirini na nne!.

"Nafikiri mtindo wao ni ule ule. Wanaua walinzi na kufanya makao ya muda. Wakimaliza shughuli zao wanakwenda kuteka mahali pengine lakini hata hivyo vijana watachunguza".

"Oke, ngoja mimi nikamwone Chifu halafu tutaanza upelelezi wetu, kama kawaida utatufuata toka New Afrika kama jana, sawa>".

"Bila wasiwasi bosi, kiijana ninayefuatana nae ni mzuri sana nafikiri hata nyinyi mlitupoteza".

"Ndio, kazi yenu ya jana ilikuwa nzuri sana, nilimpongeza.

"Bossi unapendeza sana leo".

"Asante sana kwa pongezi lako. Ngoja nikamwone Chifu".

Nilimwacha akiwa anataka kuzungumza mengi na mimi. Nilipanda ngazi na kuingia ofisini kwa chifu.

"Anatusubiri, amesema nichukue ripoti yako", Maselina alisema.

Basi tulifungua mlango na kuingia ofisini kwa Chifu. Chifu alikuwa amekaa kitini mwake akivuta mtemba kama kawaida yake.

"Shikamoo Chifu".

"Marahaba, ketini chini".

"Asante...

Maselina alichukua kitabu chake cha hatimkato na kukaa tayari kuandika mazungumzo yetu".

"Ehee, nieleze kwa kirefu mambo ambayo umeishafanya. Maana huko makamo makuu ya Polisi kuna kelele, mauaji ya ajabu yanatokea mjini hapa kwa mara ya kwanza mpaka wameshindwa mahali pa kuanzia upelelezi. Nilipopata ripoti yao juu ya mauaji haya, nilihisi hii ni kazi ya Namba Moja. Kwa hiyo naomba maelezo kamili ili nami niweze kuieleza serikali maendeleo yoyote juu ya jambo hili maana kuna wasiwasi mkubwa. Jumuia ya Ulimwengu inaikera serikali kwa kutaka kujua ukweli wa jambo hili, na wakati huo huo maadui zetu wanaendelea kutupaka matope bila kupata ukweli wa jambo hili".

Nilichukua muda huu kumweleza yote tangu nilipotoka ofisini mwake; kwenda kwetu bandarini na ofisi ya Kamati ya Ukombozi, barua niliyoikuta mlangoni kwangu; mapambano dhidi ya waliomteka nyara Sherriff na mwisho walioniteka nyara. Nilimweleza kila kitu kwa ufasaha bila kuacha tukio hata moja. Huenda jambo nililoacha ni juu ya tuliyofanya nyumbani kwangu na Veronika ambayo ni siri yetu hata nyinyi sitaki mjue.


"Kwa kutokana na maelezo ya mtu wa kikundi hiki kinachojiita 'Wanamapinnduzi wapinga mapinduzi' mimi naamini hawa watu ni VIBARAKA wa serikali ya makaburu ambao wanataka kupiga vita harakati za ukombozi dhidi ya serikali hizi dhalimu. Na mtu huyu niliyezungumza nae nina imani ni mtanzania kutokana na sura yake na sauti yake ingawaje alijitahidi sana kunidanganya kwa sauti.

Mimi ninavyofikiri kuna chama kimojawapo katika vyama vinavyopigania uhuru, ambacho makaburu wamekidanganya kuwa kikiweza kupiga vita harakati za mapambano ya silaha dhidi ya serikali ya Afrika Kusini itakipa mwanya chama hicho katika serikali ya makubaliano.

"Kwa hiyo chama hiki kimekubali kuwa kibaraka wa Afrika Kusini na kuanza vita dhidi ya vyama vingine vinavyoendeleza mapambano ya silaha. Kwa vile isingekuwa rahisi chama hiki kufanya mapambano bila msaada. Serikali ya makaburu lazima inakipa misaada ya kila hali, yaani wagtu, silaha na fedha. Kwa hiyo Chifu, ni imani yangu kuwa silaha hizi hazikibwa na watu wengine ila majasusi wa makaburu ili kutimiza lengo lao hilo'.

Chifu alikuwa ananiangalia kwa makini sana kisha akatingisha kichwa.

"Nimekuelewa vizuri sana Namba Moja. Hata unavyofikiri mimi naona ni sawa. Lakini tatizo letu liko pale pale; watu hawa wamejipenyezaje nchini humu na sasa silaha hizo ziko wapi?. Maana silaha hizo ni za kisasa kabisa. Hatua uliyofikia kwa siku moja inaridhisha, tafadhali kazana zaidi katika masaa ishirini na manne yajayo tuwe na fununu zaidi.

"Hapa tuna vyama viwili, PLF na SANP na vyama hivi ndivyo vinaendesha mapambano ya silaha huko Afrika Kusini. Kwa hiyo tuna chama kimoja ambacho kiko nje ya nchi hii; ama kiko Afrika ya Kusini ama katika nchi jirani na ndicho kimejipenyeza kuvipiga vita hivi vyama viwili".

"Hata mimi nafiri hivyo. Kwani kuna vyama vingapi vinavyopigana na serikali ya Afrika Kusini?".

"Viko vingi, kati ya hivyo vitatu viko Afrika Kusini na vitano viko nchi ya nje, kwa hiyo jumla ni vinane".

"Hili ndilo tatizo la vyama vingi. kingekuwa chama kimoja yote haya yasingetokea", nilisema kwa huzuni.

"Siasa kijana, wanasiasa ndio wanaleta taabu ulimwenguni; ndio wanayumbisha vichwa vyetu. Kila mtu na siasa yake na imani yake, na kuna wengine hawana cha siasa wala cha nini; nia yao kutaka ukubwa ili wale", alijibu Chifu kwa uchungu mkubwa.

"Sawa, sisi tunaendelea na upelelezi wetu na ushauri wako nitauweka manani".

"Asante sana Namba Moja".

"Polisi wamefikia wapi?".

"Polisi hawajafika popote. Sasa ndio wamechanganyikiwa zaidi baada ya mauaji haya ya usiku. Hivyo mimi nakutegemea wewe, maana umefanya maendeleo mazuri".

Nilisimama nikampigia kope Maselina nae akaminya midomo kuzuia tabasamu alilotaka kunipa. Chifu alinifungulia mlango na kuniambia. "Nakutakia mafanikio katika kazi hii kijana".

"Asante Chifu", nilijibu kisha akafungua mlango.

"Kavae upesi twende zetu Komredi", nilimwambia Sherriff aliyetaka kubadilisha nguo.

"Dakika tano tu", alijibu kisha akaenda haraka haraka.

ITAENDELEA

Comments

Post a Comment

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU