HOFU

SEHEMU YA TANO

Dar es Salaam

II

Willy Gamba alikuwa ni mpelelezi maarufu aliyekuwa akifanya kazi katika idara ya upelele ya Tanzania. Sifa zake zilitapakaa katika Bara zima la Afrika. Kutokana na ujasiri wake, watu wengi walifikiri mtu huyu alikuwa wa kubuniwa tu maanaa watu walifikiri kuwa vitendo vya Willy Gamba vilikuwa kama mchezo wa sinema.

Lakini ukweli ni kwamba huyu mtu yupo na vitendo vyake ni vya kweli tupu. Kijana huyu alikuwa amefanyakazi kubwa sana katika kusaidia harakati zinazoendeshwa na umoja wa nchi huru za Afrika. Kwa sababu hiyo yeye alijulikana katika Afrika nzima. Watu wengi waliohusika na kazi yake na wale waliobaki waliishia kusoma na kusikia habari zake bila kuamini.

Wakati akiendesha gari lake kuelekea mjini, Willy alikuwa na mawazo mengi. Maswali mengi yalimjia kichwani. Kwanini, kwa mfano, Chifu alikuwa anamhitaji wakati wa sikukuu kama hii?, lakini alihisi kulikuwako na kazi muhimu, kwani haikuwa kawaida ya Chifu kumbugudhi wakati wa mapumziko kama hayo. Chifu, kama alivyoitwa, ndiye alikuwa mkubwa wake wa kazi. Alikuwa Mkurugenzi wa upelelezi nchini Tanzania. Alikuwa Mzee wa miaka mingi katika kazi hiyo na sifa zake zilitapakaa mahali pengi, hasa kwa kumtoa kijana shupavu kama Willy.

Willy alipofika njia panda kati ya New na Old Bagamoyo ndipo mawazo yake yaliporudi kwa huyu msichana ambaye alikuwa pamoja nae kwenye gari. Msichana huyu alikuwa ameanza kusinzia. Mwana alikuwa anaishi sehemu za Mwenge, sehemu iliyo nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

"Mwana", Willy alisema. "Nitakupeleka nyumbani kwako halafu mimi nitaendelea na safari".

"Aka, babu, twende wote", Mwana alilalamika.

"Kwani huyo Mzee wako mimi siwezi kumpeleka Hospitali?".

"Wewe unajuwa Mzee anayeumwa ngili anakuwaje?, unataka kukosa radhi kwa kuangalia vitu vya wazee, nini?", Willy alimwasa huku akipinda kona kuingia barabara ya New Bagamoyo.

"Hukosi sababu wewe. si ajabu ni mwanamke mwingine unayemfuata huku ukinidanganya, maana wewe umezidi", Mwana alijibu huku machozi yanamlengalenga.

"Wacha wivu usiokuwa na msingi mama, haukusaidii kitu. Kama ningekuwa na bibi mwingine kwanini nikuchukue wewe tangu asubuhi?, na huyo bibi ana nini mpaka nikurudishe na kumfuata yeye wakati wewe kwangu ndio mipango inanyooka?", Willy aliuliza huku akicheka.

"Eh, huenda mipango yake ni zaidi. Nitajuaje mie?", MWana alisema kwa kejeli.

"Afadhali ningekuwa na bibi kama huyo. Lakini hawajaanza kuzaliwa. Nasikia wataanza kuzaliwa mwaka Elfu mbili", Willy alijibu.

"Wacha maneno mengi, utarudi?".

"Usiwe na wasiwasi. Nikimaliza shughuri na mzee nitarudi".

"Au ukaniache nyumbani kwako", Mwana aliomba kwa sauti nyororo.

"Mimi nitakuja kwako, si mzee yuko nyumbani au hunielewi?".

"Si mimi nitampikia?".

"Asante, lakini bado sijakutambulisha rasmi. Subiri mpaka nifanye hivyo kwani wazee hawa wana nyadhifa zao", Willy alisema huku akikata kona kuelekea nyumbani kwa Mwana. Walipofika Mwana alimvuta Willy na kumpa busu kali kisha kumwachia huku akisema, "Usiporudi usishangae kusikia kuwa nimekula kulolokwini kumi, wala usinilaumu".

"Nitarudi", Willy aliahidi.

Baada ya Mwana kutelemka, Willy aliondoa gari, moyoni alikuwa anashangaa jinsi wasichana walivyo. Hii ilikuwa miadi ya pili tu kati yake na Mwana. Hata hivyo msichana huyu alikuwa amekufa hasa kwa Willy. Willy aliendesha moja kwa moja hadi ofisini kwake katika mtaa wa Samora, katikati ya Jijini. Baada ta kuegesha gari alipanda ngazi. Aliongoza moja kwa moja mpaka kwenye ofisi ya Chifu. Alipofungua mlango kuingia kwa Katibu Muhtasi wa Chifu, alimkuta Maselina ameng'ang'ana na simu.

"Pole mwenzangu, nakwambia kazi hii itakuja kutuua siku moja", Maselina alimkebehi Willy.

"Inatufaa lakini. Yupo?", Willy aliuliza.

"Aende wapi!, leo kawa mzee ile mbaya, sijui nini kinamtia homa mzee wako", Maselina alimwalifu.

"Basi ukiona hivyo ujuwe mambo ni yale yale. Asipostaafu huyu mzee atakuja kutufia humo ofisini kutokana na ugonjwa wa moyo".

"Afe kwa ugonjwa wa moyo?, kwa ugonjwa huo utakufa wewe kabla yake. Mzima kweli huyo", Maselina alisema.

"Umeshajaribu kutingisha kiberiti na kujua ziko njiti ngapi nini?", Willy alitania.

Maselina alichukua rula na kutaka kumpga nayo. Willy aliepa huku akikimbilia mlango wa ofisi ya Chifu.

"Muhuni mkubwa, we!", hayo ndio maneno aliyoyasikia Willy yakitoka kinywani mwa Maselina.

Watu hawa wawili walikuwa wamefanyakazi pamoja kwa muda mrefu. walikuwa wakielewana kiasi kwamba walikuwa kama kaka na dada mtu au hata mpenzi.

Willy alipofungua mlango wa kuingia ndani alimkuta Chifu anasoma gazeti la Daily News.

"Shikamoo mzee", Willy alisalimia.

Chifu aliinua kichwa na kumtazama usoni.

"Marahaba. Imebidi nikuite maana nimepata habari ambazo zinahitaji sisi kuzishughulikia mara moja", Chifu alieleza.

"Nimepata habari kutoka Lusaka kuwa kumefanyika mkutano kati ya wakurugenzi wa upelelezi wa Zambia, Zimbabwe, Angola, Msumbiji na Botswana, pamoja na wakuu wa upelelezi wa wapigania uhuru. Sisi hatukuweza kuwakilishwa kutokana na sababu ambazo hazikuweza kuzuilika. Mazungumzo yao yalihusu mkutano wa wapigania uhuru ambao utafanyika kesho kutwa huko Arusha. Nafikiri unazo habari".

"Ndio ninazo".

"Kuna habari za kuaminika kwamba makaburu wana nia ya kuleta maafa makubwa na kuvuruga mkutano huo. Habari hizi ni za kipelelezi. Sasa sisi tunaombwa tuwe macho. Ingawa idara ya Polisi ilishajidhatiti kwa ulinzi huko Arusha, ni lazima na sisi tushughulikie suala hili kikamilifu. Hii ni kwamba kama kweli makaburu wamenuia kutenda kitendo hicho, bila shaka watatumia majasusi wa hali ya juu ambao wana uwezo mkubwa. Tayari wapigania uhuru wameshatuma mpelelezi wao maarufu Bon Sipele. Serikali ya Zimbabwe nayo imetuma mpelelezi wake mashuhuri Rocky Malele. Hao watawasili hapa leo jioni wakiwa njiani kuelekea Arusha...".

"Kwa hiyo hatuna budi kuungana nao leo hii ili kuimalisha usalama wa mkutano huu. Wakuu wa nchi wamekwisha julishwa. Vile vile Kamati ya ukombozi wa nchi huru za Afrika pamoja na wapigania uhuru wameaziimia mkutano huo lazima ufanyike. La sivyo, litakuwa pigo kubwa kwa wapigania uhuru na Afrika nzima na ushindi kwa makaburu. Kwa hiyo Willy hatuna uhakika makaburu watatumia mbinu gani. Ni dhahiri kuwa makaburu hawatatumia Jeshi ingawa Jeshi letu tayari limewekwa katika hali ya tahadhari tunahisi makaburu watatumia majasusi ili kuhujumu mkutano na ikibidi kuua wajumbe wengi kadiri inavyowezekana...".

"Kazi yako wewe na wenzako ni kuhakikisha kwamba jambo hili halitokei na mkutano utafanyika kama ulivyopangwa. Huo ndio utakuwa ushindi kwa Bara la Afrika na vile vile kuwatia hamasa wapigania uhuru. Baada ya mkutano huo wapigania uhuru watakuwa na nguvu mpya. Hivyo makaburu watakiona cha mtema kuni. Nafikiri umenielewa", alimalizia Chifu.

"Hatua gani za tahadhari zimechukuliwa awali, kwani inawezekana majasusi na makaburu wameshaingia nchini tayari", Willy aliasa.

"Walinzi wote kwenye mipata wameshatahadhalishwa na jeshi la polisi linafanya kazi yao. Viwanja vya Ndege vya Dar es Salaam na Kilimanjaro viko kwenye hali ya tahadhari. Wana usalama wanapekuwa vikali kila mtu anayeingia na kutoka. Wote wako macho. Kama ni kuingia nchini Majasusi hawawezi kuingia nchini mapema kwa kuogopa kugutukiwa", alijibu Chifu.

"Je wajumbe wameshawasili?", Willy aliuliza.

"Kufuatana na ripoti ya Polisi baadhi ya wajumbe wameshaanza kuingia. Wengine wako Arusha tayari. Ndio sababu lazima nyinyi muondoke leo. Tuketi yako iko tayari kwani Maselina kaishaandaa kila kitu kwa ajili ya safari yako", Chifu alimwambia Willy.

"Ni nani tutashughulika nae huko Arusha?".

"Hatutaki Polisi huko Arusha wajuwe kuwa nyinyi mnakwenda huko. Wakijuwa hivyo wanaweza kuridhika kuwa usalama upo halafu wasifanye kazi yao barabara. Hata hivyo Afisa Usalama wa mkoa anayo habari. Hivyo huyo ndiye mtu wa kumuona. Ndiye mtu wa kumwamini".

"Ni sawa kabisa, Hamisi ni mtu wa kuaminika. Lakini mbali na Hamisi, nisingependa mtu mwingine ajuwe kwani mimi nafahamu majasusi wa makaburu wanavyofanya kazi yao", Willy aliongezea.

"Sasa nenda ukajitayarishe. Vile vile nataka ripoti kutoka kwako kila wakati unapogundua kuna kitu kipya. Kama utahitaji msaada wa vijana wako uko huru kufanya hivyo, kwani watakaa hapa ofisini katika hali ya tahadhali", alisema Chifu.

"Ahsante, tuombe Mungu", Willy alijibu.

Alipofika karibu na mlango Chifu alimwita tena.

"Willy, chunga sana kwani makaburu siyo watu wa kawaida", Chifu alionya.

"Nitajihidi na Mungu atatusaidia". Willy alijibu na kutokea kwenye ofisi ya Katibu Muhtasi.

"Kwanini ukunibonyeza kwamba ninasafiri na wewe ndiye uliyekata tiketi, una visa wewe", Willy alimwambia Maselina.

"Nikwambie nini, mimi ndiye niliyekuajiri?. Mimi siyo mmbeya, bwana wewe", Maselina alisema.

"Najua unafurahi rohoni kwa kuwa mimi nasafiri. Wacha roho mbaya".

"Wewe Willy, wacha kuniumiza roho. Unajuwa jinsi gani ninavyojisikia ovyo unaposafiri. Mimi siyo kama hao wahuni wako, leo ukienda usirudi kesho wanao wengine. mimi kwangu wewe ni rafiki ambaye hana kifani na siwezi hata kufikiri ninaweza kuishi vipi bila wewe", Maselina alieleza kwa masikitiko makubwa.

"Niombee na Mola atanisaidia", Willy alijibu.

"Nakuombea kila siku", alimwambia Willy huku akimpa tiketi yake, "Chunga sana".

"Ahsante Maselina, nitajitahidi", Willy alijibu akainama akambusu kwenye shavu halafu akaondoka.

ITAENDELEA

 

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru