HOFU


MAMBO

VII

Ilikuwa saa saba za usiku. Mjini Nairobi Maina na Mwaura walipanda ua na kuingia ndani ya uwanja wa jumba hili la kifahari la Peter Gerrit. Waliangaza na kumwona mlinzi aliyekuwa bado amekaa kwenye kijumba chake huku akisinzia sinzia. Walizunguka nyumba kwa uangalifu mkubwa ili waweze kupata mahali pazuri pa kuingilia.

"Wewe zungukia kulia na mimi nizungukie kushoto, kisha tukutane mbele", Maina alimweleza Mwaura. "Jaribu kuangalia mahali pazuri pa kuingilia".

"Sawa, Mzee".

Walipokutana, Mwaura alimwambia Maina. "Kuna mlango pembeni. Nafikiri unatokea jikoni. Unaonaje tukiingilia huko?".

"Funguo zako unazo?".

"Ndio".

"Na! kufuli ni la aina gani?".

"Ni la kawaida. Nitafungua, hamna taabu", alijibu Mwaura.

Huku kila mtu akiwa ameweka bastola yake tayari, walifungua mlango huo. Mara walijikuta wako jikoni. Wafungua na kujikuta kwenye chumba kikubwa. Walihisi hicho kilikuwa chumba cha chakula. Kwani humo ndani kulikuwemo meza kubwa iliyozungukwa na viti visivyopungua kumi na nane. Wakifanya tahadhali kubwa, walisonga mbele . Walikwenda wakiangalia chumba hadi chumba. Jumba lenyewe lilikuwa kubwa kiasi cha mtu kuweza kupotea.

"Shiii!", Maina alimtahadhalisha Mwaura.

Alifanya hivyo kwa sababu alikuwa amesikia kitu kama mashine ya teleksi inalia kutoka kwenye chumba alichokuwa amekitazama. Huku akimuonyesha ishara abaki nyuma ili aweze kumsaidia iwapo ingetokea shida yoyote, Maina alifungua mlango ule. Mle chumbani hakukuwa na kitu, lakini bado alisikia mlio wa mashine ukizidi. Aliangaza huku na kule ndipo, kutokana na uzoefu wa kazi yake wa siku nyingi, alipouona mlango aliokuwa akiutafuta. Alibonyeza kifungo hapo ukutani na mlango ule ukafunguka. Mwaura alichungulia huku moyo wake ukipiga haraka haraka. Mara alimwona Maina anamuonyesha ishara ya kumfuata baada ya muda mfupi. Aliingia ndani na kuurudisha mlango.

Alikuta ngazi zinazoelekea chini ambazo alizifuata. Sasa alikuwa na hakika kabisa ndani ya jumba hili kulikuwamo makubwa. Alichunguza bastola yake ya kawaida na ile ya akiba. akajiweka tayari wakati akizidi kutelemka chini.

Aliufikia mlango mwingine. Huku ameweka bastola yake tayari, aliufungua. Hapo alijikuta kwenye ukumbi mkubwa uliomuonyesha kuwa alikuwa kwenye sehemu za maofisi. Alitega tena masikio yake vizuri. Ndipo alipogundua ni chumba gani ambacho mlio wa mashine ulikuwa ukitokea.

Aliangaza huku na kule na kusikia kimya, alianza kufungua ule mlango. Kwanza alifungua kidogo kiasi cha kuweza kuangalia ndani. Aliona Wazungu watatu wakiangalia mashine kubwa ya komputa ikileta habari. Wawili walikuwa wamesimama na yule aliyekaa Maina alimtambua kuwa ni Peter Gerrit. Aliweza kumtambua kwani waliwahi kuonana wakati wa upelelezi kuhusu mauaji yaliyotokea katika Visiwa vya Shelisheli.

Alirudisha mlango kidogo, akafikiri, halafu akaufungua ghafla na kwa nguvu.

"Hapo hapo mlipo!", Maina aliamru kwa sauti kali. "Mtu akileta ushenzi amekufa!. Mikono juu!.

Waligeuka na bila kubisha wakainua mikono juu. Bila kupoteza wakati. Maina alisoma maandishi yaliyokuwa kwenye ile mashine:

"LAZIMA UTUONGEZEE WATU MAANA HATUTAKI KUSHINDWA IKIWA HATA HUYU GAMBA YUKO HAPA HAPA JIBU".

Ghafla maandishi yalifutika.

"Peter, jibu", Maina alimwambia Peter.

"Nijibu nini".

Wakati huo Maina alikuwa tayari amewafikia na kuwapekuwa ili kuhakikisha kama walikuwa na silaha. Alikuta wale Wazungu wengine wanazo bastola ambazo aliwanyang'anya na kuzitupa kando.

"Maina mbona unanifuata fuata. Kazi inaitaka ama huitaki".

"Naitaka Peter, na safari hii huwezi kunipo...".

Ghafla chumba kikawa giza Maina alijirusha kutoka aliposimama na kuanguka kando. Wakati huo huo risasi zikamiminika pale alipokuwa amesimama. Naye alijibu mapigo huku akijiviringisha chini.

"Oh, nakufa", sauti ya mtu ilisikika.

Watu waliobaki walifungua mlango na kukimbia nje. Huko alisikia risasi zinalia na akajua Mwaura alikuwa kazini.

Aliinuka haraka na kufungua mlango wa ukumbini alikuta maiti nyingine mbili. Aliamua kuelekea sehemu aliyosikia mlio wa risasi. Mwaura alikuwa amefanya kazi kubwa. Mara aliona maiti nyingine moja. Mambo yalikuwa yanakwenda haraka. Kumbe sehemu hiyo pia kulikuwa na ngazi nyingine. Maina alizifuata ngazi hizo. Mwisho wa ngazi chini alimkuta Mwaura ameanguka chini baada ya kupigwa risasi ya kifua.

"Bosi, wamebaki wawili tu, wawahi, Mwaura alisema kwa maumivu.

"Mwaura! Mwaura!", Maina aliita kwa uchungu. Mwaura aligeuza macho na kumtazama Maina, kiasi akakata roho.

Machozi yakamtililika Maina.

"Umekufa kishujaa, Mwaura, mimi nitakulipizia kisasi. Natoa ahadi.

Kwa haraka alikimbia kumfuata Peter lakini alikuwa amechelewa. Kwani alisikia gari linawashwa na kuondoka. Kwa kasi.

Alirudi ukumbini ambamo kuliwa na simu. Alimpigia Mkurugenzi wa Upelelezi nyumbani kwake.

"Ni nani...?", Mkurugenzi aliuliza kwa sauti ya kulalamika. Lakini maelezo ya Maina yalifuta mawazo yake.

"Peter amekimbia. Mwaura ameuawa katika mapambano. Majasusi sita wameuawa. Maiti zote ziko hapa nyumbani. Naomba Polisi wafike haraka ili waweze kuchukua ushahidi ambao ni mkubwa na wa uwazi. Vile vile viwekwe vizuizi kwenye barabara zinazotoka mjini hapa. Wasiliana na wenzako huko Tanzania. Nataka kujua Willy Gamba yuko wapi".

"Sawasawa. Tuonane ofisini saa kumu na mbili. Nafikiri hapa kuna kazi kubwa", Mkurugenzi alijibu.

"Kwaheri, mzee", Maina alijibu halafu akaweka simu chini na kuondoka.


ITAENDELEA

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU