HOFU

ARUSHA
III

Ilikuwa saa mbili na nusu asubuhi. Peter Gerrit alikuwa anazungumza na maafisa wa Uhamiaji na Ushuru wa Forodha wa upande wa Tanzania. Alidai alikuwa anakwenda Arusha kuhudhuria mkutano wa wapigania uhuru. Paspoti yake ilimtambulisha kama Askofu Peter Jackson kutoka Zimbabwe. Alipitishwa haraka haraka bila kushukiwa. Wakati ule ule Mike Maina alikuwa na mazungumzo ofisini kwa Mkurugenzi wake ofisini.

"Kama Willy yuko Arusha, basi wasiwasi wangu umekwisha", Mike alisema.

"Kwa vipi?".

"Kwa sababu hawa wageni wa Peter ni majasusi wa makaburu na tayari wako Arusha. Aidha Peter yuko Arusha ambako ndiko alikokimbilia ili kuungana na wenziwe".

"Sawa kabisa. Sasa?", Mkurugenzi aliuliza.

"Sasa naomba umwalifu mwenzako huko Dar es Salaam kuwa mimi niko njiani kwenda kuungana na Willy na wenzake. Hii ni lazima kwani nilimwahidi marehemu Mwaura kwamba nitalipiza kisasi dhidi ya Peter Gerrit", Maina alisema.

"Unayo ruhusa", Mkurugenzi alisema. "Heri uende kuongeza nguvu dhidi ya majahili haya yenye nia ya kuhujumu mkutano wa ukombozi kusini mwa Afrika".

"Ahsante, mzee", Maina alishukuru.

"Nakutakia kila la heri".

"Nashukuru".

"Ukifika Arusha utamkuta Willy New Arusha Hoteli. Atakuwa na habari zako. Matayarisho mengine yako tayari kama kawaida", Mkurugenzi alimalizia.

Mike aliondoka. Wakati anatelemka ngazi alianza kumfikiria Will Gamba.

Walikuwa wamefanyakazi pamoja huko Angala kwa mara ya mwisho.

"Mbona itakuwa hatari", alijisemea huku akimwemwesa. Aliangalia saa yake ilionyesha kuwa ni saa tatu asubuhi.

"Chakula cha mchana leo nitakula mjini Arusha". Maina alijisemea tena.

ITAENDELEA

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU