TUNAMTAMBUAJE KIONGOZI MCHAPA KAZI

WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA JAMII DKT. SEIF RASHID 

TANZANIA imejaaliwa kuwa na viongozi wachache wenye moyo wa uzalendo na mapenzi makubwa ya kutumikia jamii, lakini michango wao kwa jamii hiyo inaweza isionekana kwa baadhi ya wananchi wasiofahamu uwezo na sifa za kiongozi anayepaswa kuwa mfano wa kuigwa na wengine.

Nimelazimika kuandika makala hii baada ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bw. Abdulhman Kinana, aliye katika ziara mikoani kuwataja baadhi ya mawaziri wa serikali ya awamu ya nne, akidai kuwa ni mizigo kwa wananchi.

Mawaziri waliotajwa na Bw. Kinana alipozungumza na wananchi, mkoani Tabora hivi karibuni ni Dkt. Seif Rashid wa Afya na Ustawi wa Jamii (pichani), na Bw. Christopher Chiza anayeshughulikia Kilimo, Chakula na Ushirika.

Hii ni mara ya pili kwa Bw. Kinana kuwasema mawaziri wa serikali ya awamu ya nne kwa wananchi kuwa wameshindwa kusimamia majukumu waliyopewa na Rais Jakaya Kikwete na hivyo kumshawishi rais awaondoe kwenye baraza la mawaziri kwa madai kuwa ni mizigo.

Alipofanya ziara kama hiyo mikoa ya Kusini, Bw. Kinana aliwataja mawaziri Bi. Hawa Ghasi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Bw. Mathayo David (aliyekuwa Mifugo na Uvuvi), Shukru Kawambwa wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Bw. Adamu Malima (aliyekuwa Naibu Waziri Kilimo, Chakula na UShirika)

Si kusudi langu kumpiga ama kubeza maneno ya Katibu Mkuu wa CCM, Bw. Kinana wala si lengo langu kuandika makala hii ili mpendelea Waziri wa Afya na Ustawi wa jamii, Dkt. Seif Rashid.

Kama nilivyoanza kusema katika makala hii, Tanzania imejaliwa kuwa na baadhi ya watu wachache wanaoweza kutumia muda wao mwingi kwa ajili ya kutumikia jamii, pia wako tayari hata kutoa uhai wao kwa ajili ya kutetea taifa. Mmoja wa watu hao ni Waziri wa Afya Dkt. Rashid.

Hivi karibuni nilifanya ziara isiyo rasmi Wilayani Rufiji, ambako Dkt. Rashid ni Mbunge wa Jimbo hilo, nilifanya hivyo kutokana na wananchi wa eneo hilo kukumbwa na mafuriko makubwa yaliyoharibu mashamba, miundombinu ya barabara na baadhi ya wananchi kupoteza maisha.

Kutokana na janga hilo kubwa kwa taifa, Dkt, Rashid alifanya ziara isiyo rasmi jimbo kwake, ambako aliwatembelea wahanga wa mafuriko hayo na kuangalia njia mbadala za kusaidia wananchi wake kupata msaada wa chakula haraka.

Hata hivyo alilazimika kusafiri kwa shida, pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Rufiji kumwambia kuwa mawasiliano ya barabara kutoka Kibiti kwenda Utete yalikuwa yameharibika vibaya hivyo hataweza kupita kwa urahisi. Hata hivyo Dkt. Rashid alifanya ziara na kuwafikia walengwa.

Akiwa njiani, Dkt. Rashid alilazimika kuvua koti lake la Uwaziri wa Afya na Ustawi wa Jamii na kulazimika kushirikiana na wananchi kusukuma baadhi ya magari ya abiria yaliyokwama njiani kutokana na miundombinu ya barabara kuharibiwa na mvua kubwa zilizonyesha.

Nilivutiwa sana na kitendo cha uzalendo, kilivyofanywa na Dkt. Rashid kushirikiana na wananchi wengine kusukuma magari. Tulizoea kuwaona baadhi ya viongozi wetu wenye nyadhifa ndogo tu za Ukurugenzi, lakini wakajiona wao ni miungu watu, wakashindwa kuwasaidia wananchi wenzao wakati wa matatizo kama nilivyoeleza hapo mwanzo.

Kila alipopita Dkt. Rashid alikutana na wananchi wa rika zote, wapo walioeleza hisia zao kwake, nami nikashawishika kumuuliza maswali machahe kuhusu vifo vya mama na mtoto vinavyotokea nchini, ambayo alinijibu kwa ufasaha bila kung'ata ulimi.

"Wizara ya Afya tumejipanga vizuri kuhakikisha hakuna vifo vya mama na mtoto, nakuhakikishia hatulali usingizi, tunaumiza vichwa kuhakikisha jambo hili tunalitafutia ufumbuzi. Mimi na wenzangu wizarani tunaumia sana kusikia vifo vya mama na watoto", anabainisha Dkt. Rashid.

Dkt. Rashid anasema lengo la Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ni kuhakikisha huduma za Afya kwa jamii zinawafikia watanzania mahali popote waliko, bila kujali mijini ama vijijini.

Anasema changamoto waliyonayo wizarani ni kuboresha vituo vya Afya na zahanati zilizoko kwenye baadhi ya vitongoji, vijiji na Kata viweze kutoa huduma bora za Afya ili kupunguza vifo vya mama na watoto.

"Pia tumejipanga kukabiliana na baadhi ya watoa huduma za Afya wenye tabia mbaya na kauri chafu kwa wagonjwa. Wapo madaktari, wauguzi na watoa huduma za afya wenye tabia zisizofaa kwa jamii,  tukiwabaini hatutawaache waendelee kuharibu sifa nzuri ya Serikali yetu", anasema Dkt. RAshid.

Katika udadisi wangu nabaini kuwa Dkt. Rashid ni mmoja wa Daktari bingwa wenye taaluma ya upasuaji. Nashawishika kumuuliza kabla hajagombea ubunge na hatmaye kuwa Waziri wa Afya amefanya mema gani kwa wagonjwa yanayofaa kukumbukwa na jamii, anacheka kidogo kisha anaeleza.

Anabainisha kuwa jambo la kujivunia katika maisha yake ya udaktari, ni jinsi alivyoweza kumfanyia upasuaji mama mmoja mkoani Morogoro. Anasema baada ya kuchukua vipimo vyake, aligundua kuwa mama huyo ana kiasi kidogo cha damu mwilini, hivyo alianza kutafuta damu ya ziada bila mafanikio.

Anasema kutokana na umuhimu wa upasuaji huo kwa mgonjwa huyo, alilazimika kutoa damu yake ili aweze kuokoa maisha ya mgonjwa huyo, ambaye kiasi fulani alikuwa katika hali mbaya, kwani angechelewa mgonjwa angeweza kupoteza maisha.

"Naikumbuka sana siku hiyo, unajua huwezi kufanya upasuaji bila kuwa na damu ya ziada, na yule mgonjwa alikuwa amepungukiwa damu, nafurahi kwamba nilisaidia kuokoa maisha yake ni fahari kutenda vile, mimi kama daktari na pia mwanadamu, nilitimiza ndoto yangu ya kusaidia kuokoa maisha ya mama huyu aliyekuwa mgonjwa", anasema Dkt. Rashid.

Hata hivyo Dkt. Rashid anasema, baada ya mama huyo kupata nafuu, alielezwa na wauguzi kuwa daktari aliyemfanyia upasuaji alilazimika kutoa damu yangu kwa ajili ya kuokoa uhai wake. Mama huyo alimkatisha tamaa baada ya kutoa kauri isiyofaa kuwa hiyo ndio kazi ya daktarya daktari.

Huyo ndiye Dkt. Seif Rashid. Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii niliyemfahamu, hata nikashawishika kuandaa makala hii, baada ya kuvutiwa na utendaji kazi wake kwa wananchi na jamii. Kiongozi bora huonekana kuanzia nyumbani.

DKT. RASHID AKIZUNGUMZA NA WANANCHI WA JIMBO LA RUFIJI, WALIOKUMBWA NA MAFURIKO YALIYOTOKANA NA MVUA ZILIZONYESHA NCHINI MWAKA HUU

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru