HOFU

FUNGA KAZI

VI

"Tunaomba vitambulisho", askari wa ulinzi kwenye jumba la mkutano, AICC waliwaambia akina Willy. Willy alitoa kitambulisho chake. Mmoja wao alikiangalia na kushituka. Aliwaruhusu haraka huku akiwa kama anataka kupiga saluti. Walipoingia kwenye uwanja walikuta yule mtu wao ameshafika.

Alikuwa amekaa juu ya boneti ya gari akizungumza na askari mlinzi. Willy alimfahamisha kwa wenzake.

"Huyu mtoto umempata wapi?", aliuliza.

"Huyu ni kuruta wetu", Willy alijibu kwa mzaha. Wote walicheka, baadaye waliingia kwenye chumba cha mkutano. Mkutano ungeanza masaa machache kutoka wakati huo. Waliongozwa na yule askari mlinzi. Willy aligusa mlango ukafunguka.

"Mliacha mlango wazi?", Willy aliuliza.

"Nadhani", mwandalizi alijibu huku akiwasha taa. Wote waliangaza huku na huko.

"Kuna kitu chochote kigeni ambacho hamkukiacha humu ndani ama kukipanga?", Willy aliuliza.

Walizunguka kote halafu mwandalizi wa mkutano akasema.

"Naona ni kama vitu vyote viko kama tulivyoviacha".

"Kwani Willy unafikiri vipi", Bon aliuliza.

"Ni dhahiri kwamba iwapo F.K. na wenzake waliingia ndani. Halafu askari walinzi wakafikiri alikuwa ni Mzee Hamisi eti baada ya kuona gari lake. Bila shaka watu hao walikuja kufanya hujuma ndani ya chumba hiki. Ni lazima kuna kitendo wamekifanya. Ni kazi yetu sisi kufahamu kitendo gani. Baada ya hapo kazi yetu itakuwa imekwisha. Vinginevyo kazi yetu haijakamilika kamwe". Willy alisema.

"Maneno yako ni kweli tupu", Mike aliitikia.

Mara nyingine ni vigumu kuelewa jinsi gani mambo fulani hutokea. Kwa muda wote huo Nyaso alikuwa amesimama kimya. Alikuwa mbali kidogo na Willy ambaye wote walikuwa wakimsikiliza. Yeye alikuwa amevutiwa na jambo moja ndani ya chumba hicho. Vyombo vya kuzima moto hapo ukutani vilikuwa vimepangwa kisanii.

Vyombo hivyo vilikuwa vimepangwa juu ya ukuta. Kwa pande zote nne vyombo hivyo viliangaliana kimoja na kingine jumla ya vyombo vilikuwa kumi na nne.

"Willy", Nyaso aliita. Willy alimsogelea.

"Unasemaje mtoto?", Willy aliuliza.

"Yeyote yule aliyepanga hivyo vyombo vya kuzimia moto?", Willy aliuliza.

Yule mtu aliangalia ule mpangilio wa vyombo hivyo. Halafu alimwangalia Willy kwa mshangao. Pale pale wote wakawa wamegundua sababu ya mshangao wake. Pale pale walihisi jibu.

"Hapana, vyombo vyote vilikuwa chini. Na jumla yake vilikuwa vinne tu katika chumba kizima", alijibu kwa kufadhaika.

Wanaume walipanda juu. Mike alikuwa wa kwanza kugundua ni nini kilikuwa ndani ya vyombo hivyo".

"Willy,  ujuzi na uzoefu wako umeisaidia Afrika huru. Majasusi walitega mabomu ndai ya vifaa hivi. Mabomu yenyewe yanaendeshwa na mitambo yenye saa", Mike alisema kwa masikitiko. Nyaso aliyasikiliza yote hayo. Lakini hakuamini masikio yake.

"Heri tumekuja na mtoto huyu. Kuja kwake kumetupa faida; kweli naawambia wanawake wazuri wanayo mashetani yao", Bon alisema kiutani. Lakini Nyaso hakuwa katika hali ya utani bali alibaki ameduwaa. Ungedhani kapigwa dafrao. Mambo yaliyokuwa yametendeka, yalikuwa yamemzidi kimo. Vyombo vyote vilitelemshwa. Nane kati ya kumi na nne vilikuwa na maboni ndani yake. Kwa kutumia ujuzi wao waliyategua kwa uanalifu mkubwa. Willy alimwendea Nyaso na kumbusu.

"Ahsante sana Nyaso. Nikumbushe kesho nikununulie pipi", Willy alisema.

"Ahsante, Nitaisubiri hiyo pipi. Lakini hata hivyo sasa hivi ni asubuhi", Nyaso alijibu. Willy aliangalia saa na kugundua ilikuwa ni karibu saa kumi na moja alfajiri.

"La, twende tukapumzike. Sasa ni saa kumi na moja. Kazi yetu tumeimaliza. Imebaki ya wazee", Willy alishauri.

"Sawa kabisa. Sasa tuseme wewe mwenzetu unakwenda na sisi ama ndio mambo yamekunyookea", Mike alimtania Willy.

"Eti unasemaje mtoto. Maana sasa neno lako kwangu ni sheria. Ukisema nife, nakufa. Ukisema fufuka, nitafufuka", Willy alimwambia Nyaso.

"Tuwarudishe hotelini. Halafu wewe utakuwa mgeni wangu. Unakumbuka kwamba uliniahidi kitu, na mpaka sasa hujatimiza ahadi yako", Nyaso alisema.

"Bwana weee, tulepeleke kwanza sisi halafu uende ukatimize ahadi. Ahadi ni deni", Mike alieleza.

"Ningekuwa na bahati kama ya Willy ya kumpata mtoto kama huyu, mimi nisingepoteza hata dakika, kwanza kabisa mtoto mwenyee siyo wa kawaida", Bon aliongeza.

"Eeh, jamani! Mnanifanya nione aibu", Nyaso alinena.

"Achana na hao. Ndivyo walivyo. Tutawapeleka kwanz halafu twende kula vyetu", Willy alisema.

"Ahsante mwenzetu. Tukebehi tu", Mike alijibu wote waliekea kwenye gari.

"Askari hakikisha hamtoki kwenye chumba cha mkutano", Bon aliwaagiza askari wanaolinda chumba cha mkutano AICC. Ambao walikuwa wanatweta kwa jasho kwani ilikuwa vigumu kwao kuamini kuwa chumba walichokuwa wakilinda kilikuwa na mabomu. Pamoja na hayo, kundi la akina Willy hawakuona ajabu wala kuogopa. Wao walikuwa wanafurahi kana kwamba hakuna jambo la hatari lililotokea. Walikuwa wanataniana kwenye hali ya hatari. Hata hivyo walijitahidi na kujibu.

"Ndio afande", walimwaga yule mwandalizi wa mkutano.

"Tutaonana baadaye. Kesho ni kazi kwenu wazee. Sisi kazi yetu tumemaliza. Tunakwenda kutumia matuna ya uhuru wa Afrika", Willy alisema kwa mzaha.

"Sijui niwashukru vipi, kazi yenu ni ukombozi kwa Afrika nzima, Afrika ina deni kubwa kwenu", alisema mwandaaji wa mkutano huku Willy na wenzake wakimuaga na kupanda gari kuondoka.

Waliingia ndani ya gari. Mwanga wa mapambazuko uliwaongoza vijana hawa shujaa wa Afrikal. Walikuwa tayari wamemfungia kazi kaburu. Walikuwa wameipa hamasa Afrika huru ili kusaidia wapigania uhuru wa Afrika Kusini.

Wakati wananchi walipokuwa wanaamka kutoka usingizini, mashujaa hawa ndio kwanza walikuwa wanakwenda kulala. Walikwenda kuota ndoto za kweli za ushindi dhidi ya utawala wa makaburu, ambaye ni adui namba moja wa Afrika. Makaburu...

ITAENDELEA

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU