HOFU

SEHEMU YA KUMI NA MOJA

FUNGA KAZI

"Hapa", sema sasa nakupa sekunde moja", F.K. alimwambia Willy. Willy ambaye alikuwa amejitahidi kupitisha muda akitafuta njia ya kujiokoa alijuwa kuwa sasa amepatikana. Mara wazo lilimjia ghafla ... F.K. alikuwa ameshika chombo mkononi. Kazi ya chombo hicho ilikuwa ni kuendesha (kwa mbali), mashine ya umeme ambayo ilikuwa kwenye mti ambao Willy alikuwa amefungwa..... Kama angeweza kukata umeme huo kwa njia yoyote ile, basi mfumo mzima wa chumba kile ungeathirika.

Huku akijifanya kana kwamba alikuwa hajapata fahamu sawa sawa, alichunguza kwa chati ile nguzo alikokuwa amefungiwa. Aligundua kuwa ilikuwa na magurudumu chini. F.K. na George walikuwa hatua moja mbele yake. Hivyo Willy aliamua kutenda jambo ambalo wasingeweza hata kufikiria maisha yao yote. Lakini kwa bahati Willy hakupata nafasi ya kutenda kitendo hicho kwani vitu viwili vilitokea ghafla.

Mlango wa nyuma ulifunguka ghafla na kwa nguvu Bon alimsukumiza ndani Hecke. Hecke alimkumba George na F.K. kutoka kwa nyuma na wote wakaingukia ile nguzo alikofungiwa Willy. Kukatokea kishindo kikubwa.

"Kisanduku hicho hapo juu", Willy alipiga kelele.

Kana kwamba walikuwa wamepanga shambulizi hilo kutoka kushoto. Mike alivunja dirisha kubwa la kioo. Huku akiwa na rungu na upanga mikononi, alitumbukia ndani kupitia dirishani. Alikuwa amekatwa na vipande vya kioo lakini alionekana kutotambua. Vitendo hivyo vilitokea ghafla mno kiasi kwamba George na F.K. walipoteza sekunde mbili ama tatu kabla ya kujua nini kilikuwa kimetokea.

Hapo hapo Bon na Mike walichukua nafasi hiyo kufanya kitendo kimoja kwa haraka. Mike alikata kamba alizokuwa amefungiwa Willy kwa kutumia upanga mkali. Bon alikipiga risasi kile kisanduku kama alivyoelezwa na Willy. Mara chumba kikawa giza. Kisanduku kile ndicho kilikuwa kikitumika kuendesha vyombo vya chumba kizima cha mateso.

Kitu cha kwanza ambacho George na F.K. walifanya ilikuwa kujihami. Kama njiwa, George aliruka na kupitia kwenye diridha ambalo Mike alikuwa ameingilia. Lakini pamoja na vurugu hilo Willy alikuwa amemwona. Alitenda vitendo karibu kwa wakati mmoja. Alifungua kamba na kuruka dirishani akimfuata George.

F.K. alijiviringisha na kumkumba Bon mpaka chini. Halafu alipitiliza mpaka kwenye mlango na kukimbilia ukumbini. Bon aliinuka na kumfuata. Hecke aliliwahi lile rungu aliloingia nalo Mike. Alihamaki na kumpiga Mike akaenda chini. Upanga ulimtoka Mike mkononi.

Hecke aliukimbilia ule upanga, lakini kabla hajaushika Mike alimpiga teke la farasi ambalo lilimpeperusha mpaka akaenda chini. Wakiwa wanaonana vyema kutokana na mwanga uliokuwa unatoka kwenye chumba cha pili. Mike alimrukia tena Hecke na kumtia dhoruba ya kichwa wakati Hecke alipokuwa anajaribu kusimama. Hata hivyo, wote wawili walianguka chini. Dhoruba ya Mike ilimfanya Hecke aone nyota na barabara iendayo ahera. Mike alisimama haraka na kuchukua upanga wake. Kama alivyofanya P.G. aliikata shingo ya Hecke na kichwa chake kikaanguka chini.

"Makaburu wenzako watakaposikia juu ya staili ambayo umechinjwa, bila shaka watagwaya, kamwe hawatathubutu kuichezea Afrika huru", Mike alijisemea kimoyomoyo. Akiwa na upanga wake mkononi. Mike alitoka mbio na kuwafuata wenzake ili afahamu ni kitu gani kilikuwa kikifanyika.

ITAENDELEA

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru