HOFU


FUNGA KAZI

II

Willy aliporuka na kupitia dirishani, alimkuta George anamsubiri tayari. Alikuwa amewasha taa ambayo swichi yake ilikuwa karibu na dirisha hilo. George alikuwa amesimama. Alimwonyesha Willy ishara ya vita vya maninja. Pale pale Willy aligundua kuwa George alikuwa ninja. Bila kuchelewa Willy alipiga magoti na kuinamisha kichwa. Hiyo ilikuwa ishara na imani yao. Kwa kutumia viganja vyake, Willy 'alisema' sala ya ninja vidole vya mikono yake vinaingiliana na kuachama kama meno ya mamba. George naye alifanya vile vile kama Willy alivyofanya. Kama kawaida sala yao ilichukua kama muda wa dakika kumi. Ndipo vita kali ilipoanza.

III

F.K. alikimbia na kutoka nje ya nyumba. Alibana karibu na mlango akimsubiri Bon ambaye alikuwa anamfuata. Bon alitokea akikimbia F.K. alimtegea na kumkata ngwara. Bon alianguka chini. F.K. aliruka haraka na kumpiga Bon teke la ubavuni kabla hajasimama na kurudi chini. F.K. alimtupia teke la pili. Alikuwa na nia ya kumpiga kichwani, lakini Bon alikuwa macho. Aliudaka mguu wa F.K. na kumfanya aanguke chini Mara wote waliinuka na kukabiliana.

"Leo ndio mwisho wako F.K", Bon alisema.

"Hee, nyie hamjui nguvu ya Afrika Kusini kijeshi. Hata mkituua sisi haiwezi kuwasaidia. Zaidi ya hayo mtazidisha hasira ya makaburu. Hapo ndipo mtakapokiona cha mtema kuni. Vitendo vyenu vitafuatiwa na mashambulizi ya kutisha. Vitendo hivyo vitazisanya nchi zilizo mstari wa mbele na Afrika huru kwa ujumla kukoma ubishi. Kamwe hamtaichokoza tena serikali imara ya Afrika Kusini", F.K. alijigamba.

"La hasha! Sisi tutawaangamiza nyinyi vibaraka na majasusi wa makaburu. Baada ya hapo. Serikali ya Afrika Kusini itatambua kuwa Afrika sasa ni imara. Zaidi ya hayo, kipigo tutakachotoa kitawatia hamasa wapigania uhuru wa Afrika Kusini. Vile vile vijana mashujaa wa Afrika Kusini watapata moyo wa kuendelea kupambana kwa nguvu zaidi. Na lazima makaburu watasalimu amri.... Na sasa hivi kifo chako kimefika, msaliti wee", Bon alisema.

Mara Bon alimrukia F.K. na kumpa vipigo vinne vya haraka haraka. F.K. alipepesuka huku damu zikimtoka midomoni. Hapo hapo F.K. aligundua kuwa hakuwa na uwezo wa kupambana na Bon Sipele.

F.K. alikuwa anafikiri haraka ni nini cha kufanya. Mara aliona gari lilikuwa njiani kuelekea kwenye nyumba yake. Aliangalia taa zake, akagudua kuwa gari lile lilikuwa aina ya Benzi. Na zaidi ya hayo Benzi hilo lilikuwa la kwake mwenyewe F.K. Katika mawazo yake F.K. alifikiri kwamba Stumke alikuwa ndani ya gari hilo. Alidhani kuwa alikuwa amemtoroka Willy na kuwafuata AICC. Mawazo yake yalimdanganya. Hali hiyo ilitokana na woga mwingi uliokuwa umemwingia F.K. kwa mara yake ya kwanza alifikiria kifo na woga wake ukaongezeka. Kufumba na kufumbua F.K. alitimua mbio kuelekea kwenye gari hilo lililokuwa linakuja kwa mwendo wa kasi. Bon alishangazwa na mbio za F.K. Alianza kumfukuza. Mara alijiwa na mawazo kuwa huenda wale walikuwa adui. Hivyo alisimama na kujiweka tayari kwa mapambano ya ziada.

Wakati ule ule Mike alikuwa ameshika upanga wake mkononi. Alikuwa amemuua Hecke. Baadae alimfuata Bon ili kumuongezea nguvu. Alipotoka nje, alimwona F.K. anatimua mbio huku akifukuzwa na Bon. Hivyo Bon naye aliamua kuwafukuzia. Alipomwona Bon anasimama naye akasimama pembeni. Mike alihisi vile vile wale walikuwa maadui. Gari hilo lilizidi kuja kwa kasi. F.K. alilikimbilia kwa kasi pia. Alikuwa ameinua mikono juu kama ishara ya kutaka lisimame. Bon na Mike walibaki wamesimama kushuhudia tukio hilo. Kitendo kilichofuata, kiliwashangaza. Badala ya gari hilo kupunguza mwendo, lilienda kasi zaidi kuelekea kwa F.K. ambaye alijaribu kulikwepa. Hata hivyo lilimkumba.

"Eeeeh! Nakufa!", F.K. alisema maneno yake ya mwisho. Alipogongwa, alirushwa juu na kuangukia kwenye seng'enge.

Bon na Mike waliona gari hilo likisimama mahali pale lilipokuwa limeegeshwa gari la Mzee Hamisi. Wote wawili walifichama nyuma ya mti. Walishangaa zaidi kuona mtu aliyeshuka kwenye gari hilo alikuwa Nyaso.

"Nyaso", Bon alimwita. Mike akaelekea kule ilipoangukia maiti ya F.K.

"Willy yuko wapi?", Nyaso alihoji huku machozi yakimtoka. Pale pale Bon aliwakumbuka Willy na George. Mambo hayo yalikuwa yemetendeka haraka sana.

"He! He! Hapa... hapa", sauti zilisikika.

"wako huku", Bon alimshika Nyaso mkono wakaenda mbio. Walielekea kule sauti zilikokuwa zimetokea. Hata hivyo Bon alikuwa bado ameshangazwa kitendo cha msichana huyu. Ilikuwa vigumu kwake kuelewa jinsi Nyaso alivyomgonga na kumuua bwana yake halafu asijali. Utafikiri hakuna jambo lililokuwa limetokea; ama kwa Nyaso alikuwa amegonga mbwa!.

"Ni vigumu kuwaelewa wanawake", Bon alijisemea kimoyomoyo.

ITAENDELEA

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU