HOFU

MAMBO BADO

V

Wakati mapambano makali yalipokuwa yanaendelea kati ya Mike na P.G. Bon alikuwa anafanya kazi ya kuingia ndani ya jumba la F.K. Hakupata kipingamizi kikubwa. Alipofika kwenye ile sehemu ya kushoto, aliona maiti ya yule askari aliyeuawa na Willy. Aligundua kuwa Willy alikuwa amepitia njia hiyo. Wakati anaangaza ili kuona Willy alikuwa ameingilia dirisha gani, alimwona yule askari mwingine akija. Bon alibana sawa sawa na ukuta akimwangalia askari anasogea kwa wasiwasi na hofu kubwa. Hofu yake iliweza kumfanya yule askari afike mahali alipokuwa Bon bila kuhisi kitu.

Bon aliyekuwa amebana mithili ya kinyonga afanyavyo kunasa inzi, alisubiri mpaka wote wakawa sambamba. Alimvuta na kumtia kabari kisha akamnyang'anya bastola. Alimpekuwa na kukuta hana kitu. Pale pale akimwamrisha.

"Kama unataka kuishi zaidi, nipeleke alipo Willy Gamba. Najuwa yuko ndani", Bon alibahatisha. Hofu ni kitu kibaya sana. Binadamu anaposhikwa na woga, hupoteza uwezo wa kuamua, hivyo akatenda yale ambayo asingeyafanya katika hali ya kawaida.

"Usiniue, twende nikuonyeshe", Hecke alisema kwa hofu.

Hecke alijua hiyo ndio ilikuwa nafasi yake ya mwisho. Alijuwa angemfikisha Bon kwa George, basi huo ndio ulikuwa mwisho wake hivyo Hecke alimwongoza Bon mpaka kwenye chumba cha mateso.

ITAENDELEA.


Comments

Post a Comment

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU