UCHU

WAPENDWA WASOMAJI WETU, BAADA YA KUSOMA KITABU CHA HOFU, SAFARI HII BLOG YA MPIGANAJI INAKUJA NA KITABU KINGINE CHA HADITHI ZA KUSISIMUA ZA UPELELEZI KILICHOANDIKWA NA MWANDISHI MKONGWE WA RIWAYA ZA HAYATI MWANAMAPINDUZI WA AFRIKA A.E MUSIBA KIITWACHO UCHU. KARIBU USOME...


KUMBUKUMBU

Kitabu hiki kimeandikwa kwa heshima ya marehemu Abdool Karrim Essack. Mwanamapinduzi wa Afrika. Karrim Essack ndiye aliyenichochea kufanya utafiti na kukiandika kitabu hiki. Siku chache kabla ya kifo chake alipita ofisini kwangu na kumuuliza Katibu shakasia wangu kama nimemaliza kukiandika kitabu hiki. Alipojibiwa bado aliniandikia maneno yafuatayo, ambayo namnukuu kwa kutafsiri.

"Bwana Musiba. Afrika inaingia katika kipindi kipya, kipindi cha ukombozi wa pili. Ukombozi huu ni ukombozi wa fikra na upiganaji wake utakuwa wa kuwaelimisha waafrika watambue kuwa wao ni taifa lililo kamili na ambalo litakuwa na nguvu kubwa ya kuiongoza dunia katika karne ijayo. Hivyo kuanzia sasa lazima Afrika iwe na uwezo wa kujiamulia mambo yake yenyewe, ijenge uchumi wake imara ili iondokane na dhana ya misaada. Mwandishi kama wewe una wajibu mkubwa wa kupigana vita hivi kwa kalamu. Bwana Musiba andika, na sasa andika zaidi. Punguza kazi zingine. Afrika inakuhitaji kwani kalamu sasa itakuwa na nguvu kuliko mtutu wa bunduki".

Mwanampinduzi huyu alizaliwa India mwaka 1925, akiwa bado kijana mdogo familia yake ilisafiri mpaka Afrika Kusini na kuamua kuhamia Jimbo la Kwazulu Natal. Zama hizo jimbo hilo lilijulikana kama Natal. Baba yake aliamini katika kuwasomesha watoto wa kiume. Hivyo, kaka yake Karrim alihitimu Diploma ya Ualimu katika chuo Kikuu cha Fort Hare na baadaye akaendelea na masomo katika Chuo Kikuu cha Johannesburg Witwatersrand ambako alihitimu na kupata shahada ya BA.

Karrim alianza kujiingiza katika maswala ya kisiasa alipokuwa katika Chuo Kikuu cha Witwatersrand Johannesburg ambako alijuinga na kikundi chenye mwamko wa kisiasa ambacho kilikuwa kikishirikiana na chama cha kisiasa cha umoja (Unity Movement).

Alipoanza kazi ya ualimu mara moja Karrim aliwahamasisha walimu kuupiga vita ubaguzi ndani ya taaluma yao. Vilevile, alikuwa mmoja wa watu waliowahamasisha wakulima wadogo wadogo kupinga serikali kuwahasi ng'ombe wao kwa nia ya kuwalazimisha kutoka vijijini kwenda kufanya kazi mijini.

Chama cha Natinalist kilipoingia madarakani na kuleta sheria nyingi za unyanyasaji dhidi ya walio wengi. Karrim na wenzake, chini ya chao cha Unity Movement, waliwahamasisha wananchi na kuanza kuzipinga vikali sheria hizo.

Baadaye Karrim aliamua kusomea sheria ili awe na uwezo mkubwa wa kuwatetea walio wengi. Alihitimu na kupata shahada ya sheria na kazi yake ya uhamasishaji wananchi kuzipinga sheria za kibaguzi ikashamiri.

Mara uongozi ukamshitukia kwani wananchi walianza kuamka na kuanza kupambana na serikali. Hivyo, mwaka 1959 alipigwa marufuku na kufungiwa kuendesha kazi ya uwakili kwa miaka mitano. Aliwekwa chini ya ulinzi asiondoke mji wa Durban alikokuwa akiishi. Mwaka 1963 viongozi wa ANC walipokamatwa Karrim naye alikamatwa. Mwaka 1964 aliachiwa kwa dhamana na akatoroka na kukimbilia Botswana. 1967 alipokelewa Zambia kama mkimbizi wa kisiasa. Ndipo alipoanza uandishi wa habari katika mtazamo wa kisiasa kuhusu hali halisi ya utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini.

Mwaka 1969, Karrim alialikwa na Mheshimiwa Benjamin Mkapa. Ambaye wakati huo alikuwa Mhariri gazeti la Nationalist Tanzania. Alifanya kazi gazeti la Nationalist kama mwandishi wa makala kuhusu masuala mbalimbali ya kisiasa. Vilevile, alijiunga na Radio Tanzania Idhaa ya nje, na kila wiki alitoa maoni yake kuhusu masuala ya kisiasa na kiuchumi.

Karri alikuwa mstari wa mbele kueleza habari za mapambano ya ukombozi kusini mwa Afrika. Aliandika sana makala kuhusu harakati za ukombozi nchini Zimbabwe, Namibia na Afrika Kusini. Alitumia pesa zake binafsi kuchapisha vitabu, majarida na magazeti na mara nyingi kutoa bure kwa wasomaji.

Wakati Rais Yoweri Kaguta Museveni alipoingia madarakani Uganda mwaka 1986, Karrim Essack alitoa kila aina ya msaada akiandika makala kuhusu chama cha National Resistance Movement katika Uganda. Aliandika kuhusu hotuba za Rais Museveni akizifafanua ili watu wazielewe.

Vilevile Karrim alifanya kazi kama wakili mjini Dar es Salaam na aliandika vitabu vingi. Kwa mfano mwaka 1976 aliandika kitabu cha Armed Struggle Vol I na halafu Armed Struggle Vol II na vingine. Akiwa wakili. Karrim aliwasaidia watu ambao hawakuwa na uwezo wa kumlipa wakili kwa kuwatetea bure. Alitoa huduma hiyo bure.

Mwanaharakati mwanamapinduzi huyu aliishi kariakoo kwenye ghorofa iliyotazamana na Soko la Kariakoo. wafanyabiashara ndogondogo ndio walikuwa rafiki zake wakubwa. Gari lake aina ya Volkswageni ya zamani liliegeshwa pale sokoni bila kufungwa milangwa na hakuna mtu aliyediriki kuiba kitu chochote ndani ya gari, maana mtu yeyote ambaye angediriki kufanya hivyo angekuwa anajitafutia kifo kwa rafiki zake Karrim.

Huyo ndiye alikuwa Abdool Karrim Essack mtu ambaye alikuwa na urafiki na marais akienda kwao bila hata ahadi na asirudishwe na mtu, na wakati huohuo alikuwa kipenzi cha wamachinga.

Karrim Essack alikufa tarehe 29 April 1997 mjini Dar es Salaam baada ya kuuguwa kwa muda mfupi. Hali yake ya kiafya ilianza kutetereka baada ya kurudi kutoka Congo ambako alikwenda kuonana na Rais Laurent Kabila Novemba 1996, alipokuwa ameanza harakati za kumwondoa dikteta Mobutu Sese Seko.

Katika historia ya Afrika Karrim atakumbukwa kama mwanamapinduzi shupavu, aliyeishi maisha yake yote akiutetea uhuru wa Mwafrika. Ikumbukwe kuwa Karrim alikuwa mwanachama mkereketwa wa chama cha Pan African na aliamini katika Afrika moja na yenye nguvu.

Mwenyezi Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi. AMIN.

ITANZA KUTOKA RASMI KESHO

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU