TAFUTA
UKWELI
II
Baada ya
Musoke na Willy Gamba kuondoka nyumbani kwa Temu, kila mtu alitawanyika
kuelekea kwenye hoteli yake.
Malisa
aliyekuja kwenye mkutano huo akitokea Dar es Salaam, alikuwa amefikia Hoteli ya
Sabasaba. Alijulikana sana katika kundi la wasomi na kiserikali alikuwa mmoja
wa watu waliokuwa mstari wa mbele katika kupigania kuwepo Umoja wa Afrika. Hata
maafisa wa ngazi za juu serikalini mara nyingi walitafuta ushauri kwake kila
walipotaka kuzungumzia swala la Umoja wa Afrika.
Malisa
alikuwa msomi na Mhadhili wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika kitivo cha
Sayansi ya Jamii. Mara hii alipokuwa anakuja kwenye mkutano huu Arusha, Afisa
mmoja wa ngazi za juu kabisa serikalini alimwomba amweleze mazungumzo na
makubaliano ya mkutano wao, kwani serikali ilipenda kujuwa mambo gani PAM
inafikiria kuhusu tatizo la Rwanda ili serikali nayo iweze kusaidia. Huyu Afisa
wa serikali alimpa namba zake za simu za nyumbani na kumwomba ampigie baada tu
ya mkutano.
Malisa
alipofika Hotelini tu, ikawa yapata saa kumi na mbili na robo, alichukua
ufunguo wa chumba chake mapokezi na kueleka chumbani. Alipofika chumbani
alimwomba opereta wa simu pale hotelini ampatie simu ya Dar es Salaam na kumpa
namba.
"Subiri
kidogo nitakuita", opereta alimwambia.
"Haya
asante, lakini nifanyie haraka maana nataka kutoka nina miadi", Malisa
alimwomba opereta.
"Sasa
hivi", aliambiwa.
Baada ya
muda si mrefu simu iliita chumbani kwa Malisa.
"Hallo".
"Namba
yako ya Dar es Salaam inaita", opereta alijibu.
"Haya
asante", na akaunganishwa na namba hiyo ya Dar es Salaam ambayo iliendelea
kuita.
"Hallo",
mtu aliitikia baada ya muda kidogo.
"Hapa
ni Arusha, mzee yupo?", Malisa aliuliza.
"Yupo,
subiri".
Na baada ya
muda kidogo akasikia, "Hallo, nani mwenzangu?".
"Malisa
hapa, shikamoo".
"Marahaba,
habari ya huko?".
"Salama".
"Vipi
mkutano".
"Tumemaliza".
"Ehee,
hebu nipe maazimio yenu kwani wazee huku wana shauku ya kusikia".
"Haya
tega sikio nikueleze, mambo ni mazuri sana", Malisa alijibu na kumweleza
mambo yote tokea mwanzo mpaka mwisho.
"Hizo
ni habari njema", yule afisa alijibu na kuendelea. "Willy Gamba ni
kijana wetu na ni mtu shupavu. Kwa hakika ataifanikisha hiyo kazi. Na mimi
nitawaeleza wazee naamini wataridhika na hatua mliyochukuwa. Mnajua sisi kama
serikali ni vigumu kuchukua hatua yoyote dhidi ya nchi nyingine, lakini nyinyi
mkiwa umoja usio wa kiserikali mnaweza kutusaidia sana kwa mambo kama haya.
Willy amefikia wapi?".
"Yuko
hoteli ya Impala chumba namba 212. Huenda mzee si vizuri kumpigia simu sasa
hivi tu atashituka", Malisa alijibu.
"Na
kweli, ingawa ni kijana wetu basi tuache nyinyi muendelee nae. Asante sana kwa
kazi nzuri, na mwanzo mzuri, watu wenye uchungu na Afrika kama nyinyi ndio
mtakaoisogeza Afrika mbele katika kuleta maendeleo wakati tukielekea katika
karne ya sayansi na teknolojia. Asante sana", yule afisa wa serikali alijibu
na kukata simu.
Bila kujua
alichokuwa amefanya, Malisa alifurahi sana kusikia sifa alizozitoa mtu huyu
mashuhuri katika serikali ya Tanzania, kwa umoja wao. Minongono mingi jijini
Dar es Salaam ilikuwa ni kwamba afisa huyu, ambaye watu wengi walipenda kumwita
kwa kifupi tu kama 'JKS' alitegemewa kugombea Urais baada ya muda wa Rais wa
sasa kumalizika.
Baada ya
kukata simu ya Malisa tu, JKS alipiga simu nyingine. Mara hii ilikuwa simu ya
masafa marefu, alipga Paris, Ufaransa. Na mara moja ikaitikiwa.
"Hallo,
naomba kuzungumza na Jean Yves Francois".
"Subiri
kidogo", alijibiwa.
"Hallo
Francois, nani anaita?".
"Yaani
huwezi kutambua sauti".
"Ah
JKS. Ehe, nipe habari".
"Habari
nzuri, sijui wewe huko?".
"Huku
salama, tunasubiri tu kwa hamu kusikia Umoja wa Mataifa mahakama ya mauaji ya
Rwanda ianze lini".
"Nasikia
itaanza miezi minne ijayo huko Arusha".
"Aha,
majina?", Jean aliuliza.
"Majina
ni yaleyale mpaka sasa".
"Kwa
hiyo upande wa watu wetu hakuna aliyeguswa?".
"Bado
kabisa, ila kumetokea hali ambayo inaweza kutuletea madhara".
"Hali
gani?", Jean alihoji kwa shauku.
"Unakumbuka
niliwahi kukueleza juu ya chama kiitwacho kwa kifupi PAM?", alimwuliza.
"Nakikumbuka
na nimekitafiti vilevile kujua msimamo wake. Wanachama wake wanapigania umoja
wa waafrika ili kuleta haraka uhuru wa watu weusi dhidi ya ukoloni mambo leo,
ili watu weusi waweze kujiamulia mambo yao wenyewe. Na vilevile walikuwa
mojawapo ya makundi yaliyotoa shinikizo katika mkutano wa Arusha ili mgogoro wa
Rwanda umalizike kwa njia ya amani. Hata mkutano wa Algers, walikuwepo
wawakilishi wao, niliwaona maana nilikuwepo. Haya sema watu kama hawa wanaweza
kuleta madhara gani?", Jean aliuliza.
"Wanaweza
kuleta madhara makubwa sana", JKS alimjibu na kisha akaanza kueleza kwa
kirefu jinsi Malisa alivyomweleza, na hatua ambazo tayari zilikuwa
zimechukuliwa.
"Huyu
Willy Gamba ni hatari, anaweza kuchambua kila kitu mpaka akafikia ukweli
unaweza kukugusa hata wewe", JKS aliasa.
"Lililopo
ni kuzuia asiende", Jean alijibu.
"Tutamzuia
vipi na hayuko chini yetu?", JKS aliuliza.
"Mbona
huelewi, kwani maiti inasafiri?".
"Aha,
sasa nimekuelewa, lakini hiyo ni kazi kubwa", JKS alijibu.
"Hiyo
ni kazi ndogo kabisa, si umeeleza kuwa mtu wako ameeleza kuwa leo huyo Willy
Gamba analala Arusha. Hotel ya Impala na chumba amekupa namba zake, au
sikukuelewa vizuri?", Jean aliuliza.
"Ni
sawa kabisa, alinipa kila habari bila kuelewa maana yake, na mimi aliponieleza
sikuelewa habari hiyo itakuwa muhimu", JKS alijibu.
"Hiyo
ilikuwa muhimu sana. Unakumbuka kuwa tuna watu wetu kule Arusha, ambao walikuwa
wasafiri na Rais aliyeuawa, lakini kwa ajili ya ujumbe wa Rais wa Burundi
hawakwenda na wapo kule Arusha kama wageni wa serikali yako?", Jean
aliuliza katika hali ya kukumbusha.
"Hao!
hata juzi nilizungumza na kiongozi wao maana alikuwa ametokea Ngala kwenda
makambi ya wakimbizi wa Rwanda kwa ajili ya kuwachukuwa vijana kumi muhimu
ambao waliingia Tanzania baada ya kufunga kazi kule Rwanda. Alikuwa anataka
msaada wangu kwa ajili ya makazi, nami nimewafanyia mpango katika nyumba za
mashirika ya serikali pale Arusha na sasa wako salama salimini", JKS
alijibu.
"Hiyo
ni kazi nzuri sana. Kwa kazi hiyo na kwa habari ulizonipa leo, nitapeleka dola
za kimarekani elfu ishirini kwenye akaunti yako kule Uswisi, kufika kesho jioni
pesa zitakuwa zimeingia. Na kama kazi hii ya usiku ikifanikiwa dola zingine
elfu ishirini zitapelekwa", Jean alimweleza JKS.
"Asante
sana, nami nitafanya kazi kwa upande wangu. Nitampigia simu kiongozi wao hapo
Arusha, Bwana Phillipe Habimana, atume vijana wawili waimalize hiyo kazi.
Umeshatoa agizo, na agizo lako litatimizwa", JKS alijigamba.
"Oke,
vizuri; unajuwa vijana wetu wana ujuzi wa hali ya juu, na swala la kuua kwako
si swala tena la maana wameishaua sana kiasi kwamba kuua kwao sasa ni sawa na
kunywa chai", Jean alijibu huku akiangua kicheko cha kejeli.
"Tena
sana, juzi tu kwenye kambi huko Ngala wamemaliza kuua vikaragosi
vinavyojipendekeza kwenye serikali mpya, kwa kuwashawishi wakimbizi waanze
kurudi ili ionekane serikali ya sasa imeshaleta amani na usalama Rwanda ili
iweze kuungwa mkono na jumuia za kimataifa. Ni baada tu ya kumaliza hiyo kazi
ndipo Phillipe alipokwenda kuwachukuwa kwa msaada wangu. Hivyo, nikiwaagiza
leo, hakika huyu Willy ajihesabu ni marehemu maana bado wana mori kabisa",
JKS alijibu.
"Haya
basi, nipigie simu kesho, baada ya kumaliza hiyo kazi. Na kama ukisikia habari
zingine zozote, fanya kama kawaida na mimi nitafanya kama kawaida yangu",
Jean alijibu na kukata simu.
Jean na JKS
walikuwa wanafahamiana yapata miaka mitano sasa. Uhusiano wao ulianza wakati
JKS alipokuwa na wadhifa wa kuamua juu ya ununuzi wa silaha mbalimbali
zilizokuwa zinahitajiwa na serikali ya Tanzania. Jean Yvers Francois alikuwa
kijana bado yapata miaka therathini na minane, na alikuwa tayari mfanyabiashara
maarufu sana duniani. Alikuwa akifanya biashara ya kuuza silaha katika nchi
zinazoendelea, na alimudu sana kupata biashara hiyo kwa urahisi kwa vile watu
wengi walisema kuwa alikuwa mtoto wa kiongozi wa ngazi za juu kabisa katika
serikali ya Ufaransa.
Kwa kutumia
wadhifa wa baba yake na umaarufu aliokuwa nao baba yake katika nchi
zinazoendelea, kijana huyu hakukosa biashara hii ya silaha na biashara
nyinginezo zilizokuwa zikipita mbele yake. Lakini vilevile alinong'onwa kuwa,
kijana huyu alijua kuwazawadia waliompa biashara, hasa viongozi wa ngazi za juu
katika nchi za Kiafrika. Kutokana na sifa hii ya kutoa asilimia kumi na zawadi
zingine, kijana huyu alikuwa akitafutwa na biashara badala ya yeye kuzitafuta
hata ikasemekana kwamba viongozi fulanifulani wa nchi za Kiafrika iliwabidi
wazungumze naye kwanza kabla hawajatoa maamuzi yoyote muhimu ya kibiashara.
Kwa hiyo,
wakati JKS alipoagizwa na serikali ya Tanzania kutoa zabuni ya kisiri kwa
makampuni yanayotengeneza silaha, mara moja alimtafuta Jean, maana viongozi
wenzake walishawahi kumweleza kama angetaka kunufaika na wenzake pia wanufaike
basi Jean ndiye alikuwa mtu wa
kuwasiliana naye. Ingawa wakati huo walikuwa hawafahamiani, lakini JKS alikuwa
tayari ana anuani ya Jean kutoka kwa rafiki zake. Hivyo hakusita, akawasiliana
naye. Ni baada ya kuwasiliana naye na kufanya biashara ya kwanza ndipo urafiki
wa karibu sana ulipoanza kati yao.
Kwa vile
Ufaransa ilikuwa na uhusiano wa karibu sana wa kiserikali na serikali ya
Rwanda, Jean alijikuta ana uhusiano wa karibu sana na uongozi wa serikali ya
nchi hiyo kuliko ilivyokuwa serikali za nchi nyingine za Kiafrika alizokuwa
akifanya nazo biashara. Inasemekana kuwa, kwa njia moja ama nyingine, Jean
ndiye aliyekuwa mshauri mkuu wa uongozi huo na hakuna uamuzi wowote uliofanyika
bila yeye kuhusishwa. Kiuchumi, Jean alimiliki njia zote muhimu za uchumi wa
Rwanda kwani uongozi wa serikali ya Rwanda ulimpa uwezo wa kufanya biashara
yoyote aliyoitaka nchini humo, na uongozi huo ulinufaika kwa kujilimbikizia
mali, na kumwachia anyonye jasho la wananchi wa Rwanda kwa kununua mazao yao
yote kwa bei rahisi na kuwauzia bidhaa kwa bei ghali.
Kwa jinsi
hii Rwanda ilimtajirisha Jean na viongozi wa serikali isivyo kifani. Na ndio
sababu wakati wa mkutano wa kusuruhisha pande zote za mgogoro wa Rwanda mjini
Arusha, Jean alikuwepo. Inasemekana alimtumia sana JKS kujaribu kuipotosha
serikali ya Tanzania ili isione ukweli wa mambo ulivyokuwa Rwanda kutokana na
urafiki wao wa karibu uliotokana na kupeana bakshishi.
Baada ya
Jean kukata simu, JKS alitafuta kitabu chake cha simu na kutafuta simu ya
Phillipe Habimana kule Arusha. Baada ya kuipata alimpigia simu.
"Hallo
Habimana".
"Habari
za leo", JKS alijibu na mara moja Phillipe akaitambua sauti.
"Nzuri
mzee, shikamoo".
"Marahaba,
sikiliza kwa makini, nina kazi nataka vijana wako wakaifanye usiku huu,
tafadhali sitaki makosa ya namna yoyote yafanyike kwani yanaweza kuleta madhara
kwa suala lenu zima. Nimeshazungumza na Jean.
JKS alitoa
maagizo yake kwa kirefu na akamalizia.
"Narudia
tena, mtu huyu ni hatari sana; vijana wako wasifanye mzaha wakafikiria ni mtu
wa kawaida, si wa kawaida, hadhari yote ichukuliwe".
"Hamna
matatizo mzee, hesabu kazi imekwisha, tuonane kwenye msiba wa Willy
Gamba", Phillipe alijigamba.
ITAENDELEA…
0784296253
Comments
Post a Comment