UCHU
     
KAZI IMEANZA  

III

Ilikuwa saa tatu na dakika kama tano hivi, Mulamba alipompigia simu JKS. JKS alikuwa tayari amefika ofisini.

Simu ya moja kwa moja kwa JKS ililia na haraka akainua. "Nani", aliuliza kwa shauku.

"Mulamba, mzee".

"Haya vipi mmempata?".

"Mzee huyu mtu tumeweza kupata nyendo zake zote, ila hatukuweza kumpata yeye kabisa maana alikuwa hatua moja mbele kila tulipokuwa karibu kumpata".

"Una maana gani, hebu sema mambo ya kueleweka", JKS aliuliza kwa ukali.

"Ndio nilitaka nikupe ripoti kamili mzee. Kutokana na taarifa za uchunguzi wetu, aliondoka Arusha jana kwa ndege ya kukodi ya Tanzanair, hivyo hakulala Arusha ila alilala hapa Dar es Salaam. Leo asubuhi ameondoka Dar es Salaam kwa ndege hiyo hiyo ya kukodi ya Tanzaniair na anaelekea Kigali. Habari za watu wangu nilizozipata hivi punde ni kwamba ameondoka Mwanza mnamo saa tatu kamili kuelekea Kigali. Hali ndivyo ilivyo mzee. Sijui tukusaidie nini tena?", Mulamba aliuliza.

"Ndege hiyo ya Tanzaniar ni namba ngapi?", JKS aliuliza.

"Namba zake ni MHZT 12".

"Sawa basi asante, nikikuhitaji nitakutafuta".

"Haya, asante mzee", Mulamba alijibu huku akipumua kwani alikuwa amejawa na wasiwasi angetakiwa kufanya nini tena kwani hakutaka kazi yoyote ya kuhusiana na Willy Gamba, maana mtu huyu alikuwa ni moto wa kuotea mbali. Alibaki anashangaa tu hasa ni nini kilikuwa kinatokea kati ya serikali na Willy Gamba.

JKS alijishika kichwa na kujua kazi imekuwa ngumu na yeye peke yake asingeiweza. Huyu Willy Gamba alikuwa kweli kabisa mtu wa hatari na hakika kuwapo kwake Rwanda kungezua balaa, lazima kila njia ifanyike kabla hajaleta madhara. Hakukuwa na njia nyingine ila kurudi kwa Jean maana yeye alikuwa na uwezo mkubwa kufanya mambo Rwanda kuliko yeye. Uwezo wa JKS uliishia ndani ya mipaka ya Tanzania, isipokuwa tu propagada ya kisiasa ndio angeweza kusaidia kokote ulimwenguni kwani alikubalika sana duniani kote kisiasa. Ingawaje Jean alikuwa amemwamru ampigie simu ikiwa Willy ameshauawa, lakini JKS alionelea afadhali atukanwe kuliko kunyamaza. Aliinua simu akampigia Jean kwenye simu yake ya kutembea nayo (Mobile).

"Hallo", Jean alijibu baada ya kupokea.

"JKS hapa".

"Ehe, mambo mazuri?", Jean aliuliza kwa shauku.

"Hapana, mambo yanazidi kuwa magumu", JKS alijibu na akamweleza jinsi sasa Willy Gamba alivyokuwa anaelekea Kigali.

"Mbona mtu huyu nitampenda", Jean alijibu kwa kejeli.

JKS alinyamaza. Hakuwa na la kusema.

"Hapa kweli tunashughulika na mtu mjuzi, huyo anatakiwa apambane na watu wenye ujuzi kama yeye. Basi niachie huyo mtu kwa sasa. Nitarudi kwako baadae, nipe hiyo namba ya ndege na maelezo mengine yote kuhusu hiyo ndege na huyo mtu wako", Jean alimalizia.

JKS alimpa maelezo yote huku akifurahi kuwa Jean ameelewa na hakuweza kumkasirikia. Baada ya kumpa maelezo JKS alikata simu na kuinuka kitini na kwenda kusimama dirishani mwa ofisi yake na kuwaangalia ndege aina ya tausi waliokuwa wakicheza nje tu ya dirisha lake.

Mara mawazo yake yakarudi kwa Willy Gamba. Kuuawa kwa Willy ndio kupata kwake Urais, maana huyu mtu asipouawa anaweza kuchokonoa ukweli wa mambo na kuleta kashifa ambayo ingeweza kumgusa hata yeye kwani JKS alikuwa mmoja wa watu waliokuwa wanahusika na swala zima la Rwanda, tokea maswala ya kisiasa mpaka kufikia mauaji. Na serikali ya Tanzania ilikuwa imeweka mambo yote yahusuyo Rwanda chini yake na ofisi yake kwa vile aliaminika kuwa ni kiongozi mwadilifu. 

Baada ya kukata simu ya JKS, Jean alipiga simu Rwanda kwa rafiki yake alikuwa ndani ya Jeshi la RPF. Baada ya RPF kushika madaraka Rwanda, Col. Gatabazi alikuwa wa kwanza kupata simu iliyofanya kazi. Hii yote ilikuwa kwa hisani ya Jean ambaye alikuwa na uhusiano wa karibu na mkuu wa jeshi la Ufaransa lililokuwa Rwanda pamoja na mkuu wa Idara ya Usalama wa Nje wa Ufaransa (DGSE). Inasemekana kuwa Jean ndiye aliyewasaidia hata kupata vyeo hivi kutokana na kuwa kwake karibu na uongozi wa juu wa serikali ya Ufaransa.

Jean alikuwa kama ndiye mshauri mkuu wa serikali ya Ufaransa kuhusu maswala ya Rwanda. Kutokana na kuwa kwake karibu na Rais pamoja na watu wote muhimu ndani na nje ya serikali ya Rwanda. Kwa hiyo baada ya Kigali kuangukia mikononi mwa RPF tu na maofisa wa jeshi hilo kujinyakulia nyumba za kukaa zilizokimbiwa na maofisa wa serikali ya MNRD. Col. Gatabazi ambaye siku zote alijulikana kama mkereketwa mkubwa wa RPF, hakuwa mkereketwa ila msaliti na ndiye aliyekuwa akitoa siri zote za RPF kwa Jean, na Jean akazitoa kwa rafiki zake wa serikali ya MNRD. Kwa hiyo, baada ya kupata nyumba tu Jean alihakikisha kuwa Col. Gatabazi anapata simu ili kila kilichokuwa kinaendelea ndani ya RPF kimfikie.

Kutokana na huo uhaini wake Col. Gatabazi alijipenyeza na kujiweka karibu kabisa na kiongozi wa RPF na akaaminika sana. Inasemekana alikuwa Mhutu, lakini mama yake alikuwa Mtutsi. Baba yake alifariki akiwa na umri wa miaka miwili na akakulia kwa mjomba wake na kwa vile alikuwa amechukuwa umbo la mama yake alitambuliwa kama Mtutsi tu. Ila yeye alijuwa ni Mhutu na inasemekana aliwahi kuambiwa kuwa baba yake aliuawa na wajomba zake kwa vile hawakutaka dada yao aolewe na Mhutu. Hivi kinyongo alikuwa nacho moyoni na ndio sababu alipopata nafasi ya kuwasaliti Watutsi alifanya hivyo kwa moyo mmoja. 

Baada ya serikali ya MNRD kuanguka na RPF kuingia, Jean alimhakikishia Col. Gatabazi kuwa serikali hiyo isingeweza kukaa madarakani kwa muda mrefu kwani ingepinduliwa na yeye angeiongoza serikali inayofuata. Jean alimhakikishia kuwa serikali ya Ufaransa isingeiruhusu serikali ya RPF ikae madarakani kwani viongozi wake walikuwa na mwelekeo wa Kiingereza kwa kukaa kwao Uganda na hivyo wangeathiri nguvu (influence) ya Ufaransa ndani ya Rwanda kitu ambacho Ufaransa isingekiruhusu kabisa. Kwa hiyo kwa kushirikiana na viongozi wa serikali ya MNRD waliokimbia na watu wengine walio ndani kama Col. Gatabazi kwa msaada wa serikali ya Ufaransa. Jean alikuwa anatayarisha jeshi la kuivamia tena Rwanda na kuchukua madaraka toka kwa RPF. Kwa hiyo, Col. Gatabazi alikuwa anajitayarisha kuwaggeuka wenzake mara wakati wa kufanya hivyo utakapofika.

Col. Gatabazi alikuwa anataka kutoka nyumbani kwenda ofisini kwake, Merridian Hotel, ambako ndiko ofisi zake zilikuwa kwani ndiye aliyekuwa anashughulikia uratibu wa shughuli zote za vikosi mbalimbali vya jeshi la RPF na kuripoti kwa mkuu wa majeshi.

Simu ililia. Hallo Col. Gatabazi?".

"Jean".

"Mbona leo unanipigia simu saa hizi? Saa zetu unazijuwa", Col. Gatabazi aliuliza.

"Kuna dharura", Jean alijibu na kumweleza juu ya Willy Gamba na athari za kuwa kwake Kigali.

"Hivyo ni vizuri hiyo ndege yake ingetunguliwa ikiwa hewani iwe mwisho wa tatizo la huyu mtu maana toka jana anatusumbua, nafikiri hiyo ndio njia rahisi", Jean alimalizia.

"Si Tanzania italalamika sana na kwa sasa hivi serikali ya RPF inataka sana kueleweka vizuri, hasa kwa serikali kama ya Tanzania", Col. Gatabazi alijibu kwa njia ya kuuliza swali.

"Usijali, Tanzania inaunga mkono kwa kusema hiyo ndege iliruka anga zetu bila ruhusa hata haikutoa habari huko Tanzania kama ilikuwa inakuja Kigali. Hilo niachie mimi na wewe utasikia itakavyokuwa maana utacheka", Jean alijibu.

"Basi ngoja niwahi kwani watatua kwenye dakika thelathini zijazo kutokana na maelezo yako ya saa walizoondoka mjini Mwanza".

"Asante, kwa heri, ila nipigie simu baada ya tukio".

"Sawa", Col. Gatabazi alijibu. 

ITAENDELEA 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru