KAZI IMEANZA
IV
Ndege ya
Chama Cha Msalaba Mwekundu ilitua kwenye uwanja wa ndege wa Kayibanda mjini
Kigali yapata saa nne kamili. Willy Gamba alichukua mkoba wake na kutelemka.
"Asante",
Willy alimshukuru rubani na kumpa dola mia za kimarekani.
"Asante sana mzee", yule rubani alishukuru
na kufunga mlango tayari kwa kuruka tena.
Willy alikwenda moja kwa moja kwenye jengo la uwanja
wa ndege na kuelekea Uhamiaji. Ulinzi uwanjani ulikuwa bado mkali lakini kwa
sababu alikuja kwa ndege ya Chama Cha Msalaba Mwekundu na alikuwa amefanyiwa
mpango na rafiki yake Dar es Salaam aje apokelewe na mmoja wa maafisa wa
Msalaba Mwekundu walioko Kigali, yeye akiwa kama Afisa wa habari wa Msalaba
Mwekundu kimataifa na ndivyo Chifu alivyomtayarishia pasipoti aliyoikuta
nyumbani, taratibu zake pale uwanja wa ndege zilikwenda haraka bila kipingamizi
chochote.
Katika
pasipoti yake hii jina lake lilikuwa George Mambo.
Alipojitokeza
tu nje, alimkuta mwenyeji wake aliyekuwa amevaa beji ya Msalaba Mwekundu na kwa
vile na yeye toka alipotua tu aliweka beji aliyokuwa amepewa na Msalaba
Mwekundu wakatambuana mara moja.
"Bwana
George Mambo natumai", yule mwenyeji wake alisema huku akitoa mkono wa
salamu.
"Ndio mimi. Habari zako", Willy alijibu na
kusalimu.
"Nzuri, mimi naitwa Vicent Nyemazi, ni afisa wa
habari hapa, na mimi ni Mhutu ila mimi siyo Mhutu mwenye siasa kali",
Vicent alijibu huku akitabasamu.
"Vizuri sana na pole kwa yote yaliyotokea hapa
nchini kwenu".
"Asante sana, ndio hali ya dunia. Gari nimeegesha
hapo mbele", Vicent alieleza.
"Mkahawa wa hapa umefunguliwa?", Willy
aliuliza.
"Ndio, uko wazi".
"Unajuwa nimeondoka asubuhi sana, sijanywa hata
chai na ndege zetu kama unavyojuwa si kama ndege za abiria, hamna chochote hata
kikombe cha chai", Willy alijibu huku akiangalia saa yake.
"Sawa, twende hapa kuna mkahawa mzuri, na hali
imeanza kurudi kama zamani, hivyo vitu vingi vinaendelea kama kawaida.
Walipanda juu kwenye mkahawa na willy aliagiza kahawa
na kipande cha mkate na Vicent akaagiza kahawa peke yake. Willy aliangalia saa
yake kwa chati kabisa, akajuwa ile ndege ya Tanzanair ilikuwa karibu kutua, na
alitaka tu kuona kama kungeweza kuwa na fununu za kuja kwake. Hii ilikuwa
hadhari tu kwani aliamini hakuna mtu ambaye angeweza kujua kuwa anakuja kwa
jinsi alivyokuwa ameondoka Dar es Salaam kisirisiri.
"Ah, vipi hali ya huko Ngara, nasikia hali ya
wakimbizi ni mbaya sana, yaani chakula, maji na madawa ni taabu", Vicent
aliuliza.
"Ni kweli hali ni mbaya, jumuiya ya kimataifa
inajaribu kusaidia lakini wakimbizi ni wengi mno. Fikiria watu kama wa mji huu
mnamo wiki moja watengeneze mji mwingine ambao haukuwepo kabisa, ambako ni
porini tu hakuna huduma za kijamii za aina...". Kabla Willy hajamaliza
kueleza mlio mkubwa ulitokea na mara ukatokea mlipuko. Willy na Vicent
walikimbilia dirishani kuangalia kwenye uwanja wa ndege ambako ndiko mlipuko ulikotokea.
Kwenye barabara zinakoondokea na kutua ndege wakaona vipande vya ndege
vimesambaa na kuwaka moto.
"Kazi imeanza", Willy alisema na kumvuta
Vicent mkono. Wakakimbilia chini kuangalia kwani vishindo vya kukimbia uwanjani
vilisikika kutoka kila pahala.
Walipofika chini na kuelekea uwanjani walikuta magari
ya jeshi aina ya Landrover yakiwa yamejaa askari yakielekea pale mabaki ya
ndege yalipoangukia na wengine wakija huku kwenye jengo la uwanja ili kuzuia
watu wasiende kule uwanjani.
Vicent na Willy walionyesha beji zao za Msalaba
Mwekundu wakiomba wafike kwenye tukio lakini walikataliwa na askari ambao kwa
sasa walikuwa wamechachamaa. Willy aligundua kuwa kumbe walishajua atafika na
maskini yule rubani na afisa wa Msalaba Mwekundu waliuawa kwa kufikiri ni yeye.
Willy alimshukuru Mungu kwa kumfanya afikiri na kufanya kama alivyofanya.
Kweli kama Msoke alivyosema, kazi hii tayari
ilionyesha kuwa ni ya hatari. Ila kilichomshangaza Willy ni jinsi yule mtu
aliyeshambulia ndege ya Tanzanair alivyojuwa kuwa yeye angekuwemo mle ndani ya
ile ndege. Hii ilionyesha kuwa kati ya wale maafisa wa PAM miongoni mwao
kulikuwa na msaliti, lakini kwa sasa hakukuwa na haja ya kufikiria hicho ila
kufanya kilichomleta Kigali. Huyu msaliti angetafutwa baadaye. Jinsi ile ndege
ilivyokuwa imepigwa na kombora. Willy alijua kabisa kuwa hakuna mabaki ya
binadamu ambayo yangeweza kutambuliwa, kwani kombora lililotumika lilikuwa
kubwa wakati ndege yenyewe ilikuwa ndogo.
"Twende zetu, nipeleke hotelini, acha wanajeshi
wafanye kazi yao", Willy alimvuta Vicent wakaondoka huku wakisesera
kuelekea kwenye gari la Vicent.
"Kwanini wameipiga ile ndege?", Vicent
aliuliza huku akifungua mlango wa gari.
"Huenda ilikuwa na hatari, bado unajuwa mambo
hayajatengamaa hapa", Willy alijibu.
"Unafikia hoteli gani?".
"Nafikiri jaribu Meridian Hotel kama kuna
nafasi", Willy alijibu na kuikacha Hotel Des Mille Collines aliyokuwa
amepangiwa na rafiki za Musoke, kwani sasa hakukuwa tena na kumwamini mtu
yeyote kwa vile hakujuwa nani alikuwa ametoa amri ya kupigwa kombora ndege
aliyopaswa kuwemo na huyo mtu alikuwa anajuwa habari kiasi gani kumhusu yeye
Willy.
"Sawa, pale hotelini wanatua na watu wetu kutoka
mataifa ya nje wako pale. Na vilevile pana usalama maana ofisi zingine za jeshi
ziko pale, na maafisa wengine wa jeshi wanakaa pale", Vicent alimweleza
Willy. Wakati wakielekea Meridian Hotel walikutana na magari madogo ya jeshi,
kama matatu, yakielekea uwanja wa ndege. Willy aliona wengi walikuwa maofisa wa
vyeo vya juu na akahisi walikuwa wanakwenda kutathimini tukio lililotokea.
Walipofika Meridian walikuwa watu wako vikundi vikundi
wakizungumza, bila saka walikuwa wamepata habari za tukio la uwanja wa ndege.
Vicent likwenda mapokezi na kuzungumza na mmoja wa wafanyakazi wa pale ambaye
alionekana kumfahamu sana, na baada ya muda kidogo Willy aliitwa kujaza fomu za
kupatiwa chumba. Baada ya kupewa funguo alichukua mkoba wake na vicent
akamweleza kuwa atamsubiri kwenye mkahawa wa hoteli.
"Si utataka twende ofisini?", Vicent
aliuliza.
"Bila shaka", Willy alijibu.
"Basi utanikuta hapo kwenye mkahawa".
"Asante", Willy alijibu na kuelekea kwenye
ngazi kwani alikuwa ameelezwa lifti zilikuwa hazifanyi kazi. Alikuwa amepewa
chumba namba 412, ghorofa ya nne.
V
Baada ya Col. Gatabazi kuhakikisha kuwa hakuna kitu
kilichobaki ndani ya ndege na ndege yenyewe, alielekea nyumbani kwake ili
akampashe habari Jean. Alipompata Jean alimweleza. "Kazi tayari, mtu wako
hata mfupa haukuonekana, kawa hewa".
"Safi sana, hakika mimi hupenda mtu wa vitendo na
siyo maneno", Jean alijibu.
"Lililobaki ni la kujieleza kwanini tumeipiga
hiyo ndege, lakini tayari mkuu nimemwandikia taarifa safi ambayo hawezi kuwa na
mashaka nayo. Wasiwasi wangu Tanzania tu", Col. Gatabazi alieleza.
"Nilikwambia Tanzania niachie mimi. Tuongee
jioni. Kama kawaida mzigo mwingine unatua leo, na ni shehena kubwa", Jean
alijibu na kabla Col. Gatabazi hajajibu alikata simu.
Baada ya kukata simu ya Col. Gatabazi. Jean alimpigia
simu JKS, Dar es Salaam. JKS, aliyekuwa na wasiwasi mkubwa aliipokea simu
haraka ilipolia. "Nani".
"Jean hapa. Kigali Bingo!!, mambo safi".
ITAENDELEA
0784296253
Comments
Post a Comment