UCHU MIGUU YA NYOTA

II

Willy alipofika kwenye nyumba ya Luteni Biniga taa za ndani zilikuwa zikiwaka. Nyumba hii ilikuwa imezungushiwa ua kama alivyokuwa ameelezwa na Col. Rwivanga. Badala ya kubisha hodi langoni aliamua kupita kwenye uchochoro, akapanda ukuta kisha akatumbukia ndani. Alitambaa chini kwa chini mpaka akaufikia ukuta wa nyumba hii. Dirisha la nyuma lilikuwa limefungwa, hivyo aliendelea kuambaa na ukuta. Ndipo aliposikia sauti za watu wakizungumza na kucheka. Alichungulia dirishani na kuwaona watu watatu. Wanaume wawili na mwanamke mmoja. Mazungumzo yao yalikuwa kwa lugha ya Kifaransa, ambayo Willy aliielewa vizuri sana, mazungumzo yao ndiyo yaliyomshitua na kumweka chonjo.

"Kazi mimi nimeifanya kwa ustadi mkubwa. Hiyo pesa kweli iko kwenye akaunti yangu Nairobi?", mmoja wa wale vijana alimwuliza yule mwanamke.

"Siyo wewe tu, nyote kesho pigeni simu kwenye benki zenu. Mambo safi. Nimeelezwa na wakala wa mlipaji kuwa pesa zimetumwa kwa njia ya 'swift' na tayari ziko kwenye akaunti zenu", yule mwanamke alijibu.

"Mimi nilihitaji kulipwa dola laki moja. Ndizo zilizotumwa na kuwekwa kwenye akaunti yangu?", yule mwanaume wa pili aliuliza.

"Ndio. Sasa kwenye akaunti yako kuna dola laki tatu. Zimeingia pamoja na zile za malipo ya kuwatorosha wale makamanda wa Intarahamwe kwenda Zaire", yule mwanamke alijibu.

"Kama kesho nikijuwa pesa yangu yote hiyo iko benki, basi mimi nitatoroka kwenda Kenya. Halafu Afrika Kusini. Sitaki kukaa hapa tena, tusije tukabainika kuwa tuko kwenye upinzani", mwanaume wa pili alisema.

Hapa Willy aliamini kuwa wakati wa kukabiliana ana kwa ana na watu hawa ulikuwa umefika kwani walionekana kana kwamba wanataka kuondoka. Mawazo na akili ya Willy yalivutika sana kwa yule mwanamke kuliko hata kwa wale wanaume wawili ambao alihisi ni Luteni Silasi Biniga na Juvinali Mukama. Alipogeuka tu kutaka kwenda kubisha hodi kwenye mlango wa mbele, alijikuta akiuangalia mtutu wa bunduku kubwa aina ya 'Sub Machine Gun'.

"Usisogee hata hatua moja. Hapohapo ulipo weka mikono yako juu, geuka nyuma na utembee kuelekea mlango wa mbele ya nyumba hii", Willy alimrishwa na yule askari na kutii amri kama alivyokuwa ameamriwa.

"Nani huyo tena", Silasi Biniga aliuliza katika hali ya mshangao.

"Nini Ananie", Juvinali naye aliuliza.

"Inkotanyi", Ananie alijibu.

"Bibiane wewe nenda. Sisi ngoja tujuwe huyu mtu ni nani?", Juvenali alimweleza yule mwanamke huku yeye na Luteni Biniga wakichukuwa bastola zao na kutoka nje kwenda kumkabiri mtu huyu aliyekuja kuwapeleleza ili kabla hawajamuua wajuwe ni nani na anajuwa nini kuhusu wao. Wakati Bibiane anatoka ndani alikutana na Willy pamoja na mtu aliyemkamata, wakiwa wamefika mbele ya nyumba, kwenye mlango wa mbele.

"Simama hapo", Ananie alimwamru Willy huku akiwa bado ameweka mikono yake kichwani. Bibiane alipotoka nje alimwangalia Willy. Willy naye akamtazama. Kulikuwa na mwanga wa kutosha kuweza kumtambua mtu. Bibiane alimwemweseka kwa Willy kisha akalekea kwenye lango kubwa la kutokea nje na kutokomea gizani.

"Luteni Biniga..., lazima mtu huyu ni Inkotanyi, amekuja kupeleleza kuhusu tukio la leo", Ananie alimwambia Luteni Biniga walipotoka nje pamoja na Juvinali. Luteni Biniga alimwangalia Willy na kwa sura yake akabaini kuwa mtu huyu hakuwa Mnyarwanda. Bila kuchelewa Luteni Biniga alimpiga Willy kwa kitako cha bastola kwenye paji la uso na Willy akaanguka chini. Alipoanguka Juvinali naye alimpiga teke la tumboni. Willy alipotaka kuinuka alipigwa teke la ubavuni. Ni hapa ambapo mambo yaligeuka. Baada ya Juvinali kutupa teke kali lililompata Willy vilivyo ubavuni. Willy akahisi amevunjika mbavu, kama sumaku.

Willy aliunasa mguu wa Juvinali kabla haujarudi na kuupinda, kisha akauvuta upande wake, haraka sana akamlalia juu. Hii yote ilitokea kwa haraka mno kiasi cha kuwatatanisha Luteni Biniga na Ananie wasijuwe wafanye nini kwani wangefyatua risasi wangemuua Juvinali. Bastola ya Juvinali ilianguka chini karibu yao. Tena kwa kutumia nguvu zote alizokuwa nazo Willy alimrusha Juvinali kwa Ananie aliyekuwa kama hatua mbili kutoka pale walipokuwa. Juvinali akamkumba Ananie, wakaanguka huku bunduki ya Ananie ikitema risasi zilizomwingia Juvinali na kumwua hapohapo.

Wakati Willy alipomrusha Juvinali kwa Ananie. Haraka aliirukia ile bastola na kumpiga risasi kadhaa Luteni Biniga. Kabla hajafyatua bastola yake, risasi zikampata Luteni Biniga kwenye paja la uso na kumwua pale pale. Ananie naye kwa kutumia nguvu zake zote. Alijaribu kuitoa maiti ya Juvinali ili aichukuwe tena bunduki yake. Lakini hakuwahi. Willy alimpiga tena teke la kichwa na kumtoa fahamu. Willy akaivuta maiti ya Juvinali na kuitoa juu ya Ananie na kuanza kumvuta Ananie ili aweze kumuuliza maswali. Mara akasikia mlio kama wa king'ola. Akajuwa ama yule mwanamke ameripoti au ule mlio wa bunduki na bastola umesikika. Hivyo akajuwa angekutwa pale, kwa hasira aliivunja shingo ya Ananie na kumtupa chini. Akakimbilia ukutani. Akauparamia ukuta na kuangukia kwenye uchochoro wa mtaa wa pili; akakimbilia kwa Col. Rwivanga.

Alipoingia nyumba ya Col. Rwivanga. Ndipo Col. Rwivanga alipojuwa kuwa alipokuwa ameumia sana. Col. Rwivanga alikuwa ameusikia mlio wa bunduki lakini kwa Kigali halikuwa jambo la ajabu, ingawa alikuwa na wasiwasi. Lango la ua wake lilipofunguliwa tu alikuwa nje na ndipo alipomwona Willy akiingia huku akipepesuka. Col. Rwivanga alimsaidia wakaingia ndani. Willy alikuwa anatoka damu puani, Col. Rwivanga akajuwa kuwa alikuwa ameumia sana maana alipoonekana kama ana nyuso mbili kwa vile paji lake lilikuwa limevimba vibaya sana.

"Utadhani umekanyagwa na trekta", Col. Rwivanga alisema baada ya kumwona Willy.

"Nakwambia ni zaidi ya trekta. Sijawahi kupigwa teke lenye nguvu kama lile", Willy alijibu.

Dkt. Daniel Robinson alikuwa daktari mkuu wa Hospitali ya King Faisal mjini Kigali na alikuwa rafiki mkubwa wa Col. Rwivanga kabla Dkt. Robinson hajaja Rwanda alikuwa daktari katika Hospitali ya Mulago mjini Kampala, ambako alikuwa akiishi karibu na Col. Rwivanga. Na kwa muda wote walipokuwa Kampala walikuwa marafiki wa karibu sana.

Kwa hivyo wakati RPF walipoingia tu Kigali, Col. Rwivanga ndiye aliyekuwa kiongozi wa kikosi cha kwanza kabisa kilichoongoza mapambano dhidi ya majeshi ya serikali. Na kituo cha kwanza kabisa ni kuwaokoa watu waliokuwa Hospitali ya King Faisal ambako kuliwa na maelfu ya watu wakiwa pamoja na rafiki yake Dkt. Robinson. walikuwa wamejisalimisha ndani ya Hospita, lakini baada ya Intalahamwe kuwa wamewaua watu wengi Hospitali hapo pamoja na wagonjwa.

Baada ya Col. Rwivanga kuingia na kikosi cha kulinda usalama, watu wengi walipona. Siku zilizofuata majeruhi na wengineo aliponea katika Hospitali hiyo, hivyo Col. Rwivanga alimpigia simu Daktari Robinson ambaye ni Mzungu Mwingereza na kumweleza juu ya Willy kujeruhiwa.

"Niko njiani!", Dkt. Robinson alimweleza Col. Rwivangga, wakati walipokuwa wanamsubiri Daktari, Willy alimweleza Col. Rwivanga yote yaliyotokea nyumbani kwa Luteni Silas Biniga.

"Nini maana ya Inkontanyi?, maana waliniita hivyo", Willy aliuliza baada ya kumaliza maelezo yake.

"Inkontanyi huwa ina maana ya RPF. Maana yake hasa ni mpiganaji mkali na maarufu katika Kinyarwanda. Lilikuwa ni jina lililopewa kikosi kimoja cha Mfalme wa Bugiri katika karne ya kumi na tisa hivyo. Walihisi kuwa wewe utakuwa ni mpelelezi wa RPF", Col. Rwivanga alieleza.

"Kwa hiyo. Inamaana wao siyo RPF", Willy aliuliza.

"Bila shaka, kama ulivyosikia na hili limenitia wasiwasi sana kutambua kuwa katika uongozi wa katikati. Na bila shaka wa juu wa RPF tumeingiliwa na wasalti. Kinachoonekana wazi ni kuwa hawa waliopambana nawe nao ni watu wanaofanya hivi vitendo ni wapenda pesa. Sasa mtu au kikundi hatari ni kile kinachotoa pesa hicho ndicho yafaa tukijuwe na kukiangamiza ili Rwanda iweze kurudi hali yake ya amani", Col. Rwivanga alijibu.

"Basi mtafute yule mwanamke niliyesikia wakimwita Bibiane na jibu lako utakuwa umelipata", Willy alijibu huku akionekana kuwa maumivu yalikuwa yamezidi. Mara akasikia honi ya gari.

"Daktari huyo rafiki yangu, ngoja utubiwe usife maana kazi sasa ndiyo imeaanza", Col. Rwivanga alimtia moyo Willy.

ITANDELEA 0784296253
   

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru