WAPENDWA WASOMAJI WA BLOG YA MPIGANAJI, TUNAWAOMBA RADHI KWA KUKOSA HADITHI HII, KULITOKANA NA SEHEMU HII KUWA NDEFU NA HIVYO KUHITAJI MAANDALIZI YA MUDA MREFU. SASA ENDELENA KUPATA UHONDO JINSI WILLY ALIVYOINGIA KIGALI.
CENTRE
CHRISTUS
Ilikuwa
yapata saa moja ya usiku wakati Willy alipofika kwenye kituo cha kidini cha
Centre Christus. Alikuwa bado anasikia maumivu ya ubavuni yaliyotokana na
mapambano ya juzi yake. Hata hivyo, aliamua kuendelea na kazi kwa vile muda
ulikuwa hamruhusu kungoja apone kabisa.
Langoni mwa
kituo hiku alimkuta mtawa mmoja aliyemwuliza jina, na baada ya kujitambulisha
mtawa huyu alimchukuwa Willy na kumpeleka kwenye nyumba ya Padri Marcel
Karangwa ambaye alimkuta akimsubiri.
"Karibu
sana Willy Gamba, karibu Kigali. Kigali inanuka mauti; hata nyumba ya Mungu
inanuka mauti", Padri Karangwa alimkaribisha sebuleni mwa nyumba yake.
"Nashukuru
sana Padri hasa kwa kukubali mimi nije nikuone mara tu baada ya maafa
yaliyotokea kwenye kituo chako hiki, nashukuru sana", Willy alijibu.
"Unakaribishwa
sana, Bwana Musoke amenieleza kila kitu, nasi tunafarijika sana kukutana na
watu kama nyinyi ambao mnaweza kuleta matumaini ya amani ya nchi kama hii.
Kweli, tuko tayari kukupa maelezo yoyote unayohitaji kwa shughuli yako",
Padri Karangwa alimweleza Willy.
"Asante
Padri, mimi nisingependa nichukuwe muda wako mwingi kwa vile una majukumu
makubwa ya kukijenga upya kituo hiki na kurudisha imani ya watu katika nyumba
ya Mungu", Willy alijibu wakati mmoja wa watawa akileta chai na kahawa.
"Utakunywa
chai au kahawa", Padri Karangwa alimuuliza Willy.
"Chai
ya rangi", Willy alijibu na kupewa chai ya rangi na kipande cha mkate na
Padri Karangwa akapewa kahawa.
"Bwana
Musoke alisema ungependa kujuwa kwa kifupi hasa ni nini kiini cha chuki
iliyokithiri kati ya makabila haya ya Kitutsi na Kihutu".
"Sawa
kabisa", Willy alijibu.
"Kwanza
kabisa mimi ni Mtutsi...". Alipoanza kuongea akaingia Padri mwingine.
Padri Karangwa alimkaribisha na kumjulisha kwa Willy Gamba. "Huyu Padri
Boniface Sibomana na ni mmoja wa watu waliopona mauaji". Kisha akamjulisha
Willy Gamba. "Na huyu ni Willy Gamba, mwandishi wa habari kutoka Tanzania,
ambaye pia amekuja kama wengine wengi waliomtangulia kutupa pole na kutaka
kuelewa vipi watu wa nchi moja wanaweza kugeukiana na kuuana kikatili namna
hii.
Willy na
Padri Sibomana walipeana mikono na wakaketi chini kuendelea na mazungumzo.
"Kama
nilivyokueleza mimi ni Mtutsi, lakini Padri Sibomana ni Mhutu, sasa sema
tofauti yetu sisi kimaumbile ni nini?", Padri Karangwa alimwuliza Willy.
Willy aliwaangalia wote wawili. kweli kimaumbile kati ya hawa wawili hasa
hakukuwa na tofauti.
"Hakuna",
Willy alijibu huku mapadri hawa wawili wakitabasamu.
"Kama
hakuna jibu la swala zima la mauaji ya Watutsi na Wahutu wenye msimamo wa
wastani, basi mauaji haya yalishinikizwa kisiasa na kikundi cha watu wachache
wenye madaraka makubwa katika Serikali ya Rwanda. Mara nyingi vita ya wenyewe
kwa wenyewe katika Rwanda ikisingiziwa kuwa ni vita ya kikabila. Hii si kweli
na inapotosha ukweli, ila yanapotokea mauaji kama haya ndipo ujenzi wa chuki wa
kikabila unajengwa. Wahutu na Watutsi wameishi pamoja kwa karne nyingi na
tofauti zao si hizi tunazoziona leo, kwani hakukuwa na chuki kati ya makabila
haya. Ni utawala wa kikoloni wa kugawa nitawale na baadaye. Serikali zetu
zilizoongozwa na ubinafsi na uchu wa madaraka uliohubiri kuwepo tofauti kati ya
wahutu na Watutsi, tofauti ambazo awali hazikuwepo. Kwa kifupi ni kwamba ili
mbinu za kisasa za kuyatumia makabila haya mawili ili watawala wabaki kwenye
madaraka ambayo yamesababisha mauaji haya ya kikatili ambayo
tumeyashuhudia", Padri Karangwa alinyamaza kidogo ili anywe kahawa yake
wakati Willy na Padri Sibomana wakimsikiliza kwa makini.
Kisha Padri
Karangwa aliendelea. "Kama nilivyosema mwanzo, mauaji ya kikatili Rwanda
hayakutokea ghafla tu kiwendawazimu eti kwa sababu kabila moja lilikuwa
likilichukia kabila lingine. Mauaji ya Rwanda yalikuwa yamepangwa siku nyingi
na kwa ufasaha kabisa na watawala wa nchi yetu. Ili kulielewa hili na ili mtu
asisingizie kuwa mauaji haya yametokana na ukabila inabidi kwa kifupi tuangalie
historia ya Rwanda kwa maana ya makabila haya mawili ya Watutsi na
wahutu", Padri Karangwa alieleza.
"Nafikiri
kweli ni vizuri tupate historia fupi ya jinsi chuki ilivyojengeka maana mauaji
haya ya Watutsi na Wahutu wenye siasa kali ni ya kinyama yaani binadamu ameweza
kuwa mharibifu na mkatili kiasi hiki", Willy alisema kwa kusikitika.
"Historia
ya Rwanda inaonyesha kwamba watu wa kwanza kuishi Rwanda walikuwa wawindaji
ambao ni kizazi cha kabila dogo la Watwa. Inasemekana kuwa wakulima, ambao ni
Wahutu, ndio waliofuatia na kisha wafugaji ambao ni Watutsi, ndio walikuwa wa
mwisho kufika, na wote waliishi pamoja kila ukoo ukiwa na utawala wake wa
kichifu. Kusema kuwa Watutsi walikuja kama wavamizi na kutaka kutawala kwa
nguvu makabila mengine si kweli, kwani wana historia wengi wameupinga usemi
huo, ila kitu ambacho kilitokea ni kwamba karibu vizazi ishirini vilivyopita
ukoo mmoja wa Kitutsi ulioitwa Nyinginya ulipata sifa katikati ya Rwanda na
kuanzisha utawala wa kifalme ambao ulitawanyika kwenda kusini mwa Rwanda ya
sasa.
Lakini
historia inaonyesha kwa bunge lao la wakati huo lilikuwa linaitwa 'abini', nalo
liliwashirikisha Wahutu na Watutsi pamoja. Na kwa vile utawala wa Wanyinginya
ulikuwa na nguvu, machifu wa Kihutu katikati ya kusini mwa Rwanda walimezwa na
kukubalika kama Wanyinginya. Hapa ndipo swala la ukabila wa Kihutu na Kitutsi
ulipotambuliwa, si kutokana na ukoo wa Kihutu au Kitutsi bali kwa kutokana na
hadhi mtu aliyokuwa nayo. Ukiwa mtawala, hata ukiwa Mhutu uliitwa Mtutsi. Kama
huna mali uliitwa Mhutu, na hivyo hii hali iliashiria kuoana kwingi kati ya
Wahutu na Watutsi. Ndiyo sababu hata wewe umeshindwa kututoa tofauti,"
Padri Karangwa alinena.
"Kama
si vitambulisho hivi mara nyingi kweli huwezi kujua Mhutu ni yupi na Mtutsi ni
yupi maana vile vile tunazungumza lugha moja, tofauti na nyinyi," Padri
Sibomana alidakia.
"Huko
ndiko ninakokwenda," Padri Karangwa alisema na kisha kuendelea,
"Kusema kweli tofauti halisi ambayo ilibaki ilikuwa kwa wahutu wa
kaskazini ambao waliendelea na utawala wao mpaka hapo wakoloni walipofika.
Pamoja na kwamba utawala wa Wahutu wa kaskazini haukumezwa na utawala wa ukoo
wa Nyiginya, bado wahutu hawa na watutsi waliishi bila matatizo."
"Matatizo
yalianza lini? Willy aliuliza.
"Usiwe
na haraka, mimi taaluma yangu ni ualimu nakupeleka taratibu uelewe na huko
tutafika," Padri Karangwa alimjibu na kisha kuendelea, "Tatizo hasa
lilianza wakati wakoloni walipofika Rwanda mwishoni mwa karne ya kumi na tisa.
Wamisionari wa Kijerumani na kisha askari wa Kijerumani walipofika Rwanda
walikuta utawala uliojengeka wa ukoo wa Nyinginya ambao kama nilivyosema ulikuwa
ukoo wa Kitutsi. Kama walivyokuwa wakoloni wote walitumia tawala walizozikuta
kuwasaidia kutawala. Hivyo, Wajerumani na kisha Wabelgiji baada ya kukuta
utawala wenye nguvu ulikuwa wa kitutsi wakaamua kuutumia huu utawala na
kuubadilisha uwe wa kinyanyasaji ili ile sera yao ya gawa utawale iweze
kufanikiwa. Kwa kusaidiwa na wakoloni sasa watutsi walifuta nafasi yoyote
waliyokuwa nayo wahutu kabla ya wakoloni na kuwanyang'anya mali na madaraka, na
hii yote ilichochewa na wakoloni ili kuwagawa watu wa nchi hii. Na, kwa vile
ilikuwa vigumu kuwatofautisha wahutu na watutsi kwa urahisi mnamo mwaka wa
1933-34 vitambulisho vilianzishwa na wakoloni kwa wananchi wote wa Rwanda
vikiwatambulisha kikabila yaani Wahutu, Watutsi au Watwa na vitambulisho hivi
hivi ndivyo vilivyotumika katika mauaji haya na mengine mengi yaliyokwisha
tokea.
"Kwa
kutumia vitambulisho hivi basi maendeleo ya Wahutu na Watwa yalizimwa
kabisa?", Willy aliuliza.
"Ndiyo,
yalizimwa na hata shule nafasi zote zilitolewa kwa Watutsi, kanisani nako baada
ya Omwami kubatizwa kuwa mkatoliki hata kanisa liliwabagua Wahutu. Kanisa
Katoliki wakati huo ndilo lilikuwa linamiliki karibu shule zote katika Rwanda.
Hivyo liliwasomesha Watutsi na kuhakikisha Wahutu hawapati nafasi ya kusoma ila
walibaki na haki ya kuhubiriwa tu", Padri Karangwa alijibu.
"Kwa
hiyo vitambulisho vilikuwa moja ya mambo yaliyojenga ukabila ndani ya
Rwanda?", Willy aliuliza tena.
"Ndiyo,
kabla ya vitambulisho ilikuwa vigumu kujuwa huyu ni kabila gani na vitambulisho
kama nilivyosema hapo mwanzo, vilianzishwa na wakoloni wa Kibelgiji ili kujenga
ukabila ili wautumie huu ukabila kuwagawa Wanyarwanda kwa faida yao ili iwe
rahisi kuwatawala. Baada ya kupewa vitambulisho watu wote waliotambuliwa kama
Wahutu walinyanyaswa na kunyimwa hazi zozote na elimu na vilevile mali na hata
Wahutu wa Kaskazini ambao walikuwa wakijitawala wenyewe, wakoloni mnamo mwaka
1912 walimshinikiza na kumsaidia Omwami atwae madaraka katika sehemu hizi.
Kutwaa madaraka Kaskazini mwa Rwanda kwa Watutsi kulikataliwa na Wahutu wa
sehemu hii na mapigano makali yalitokea yakiongozwa na Mhutu aitwae Ndugutse.
Kwa vile Watutsi walikuwa wakisaidiana na wakoloni, Wahutu walishindwa na
wakatawaliwa na Watutsi. Wahutu wengi waliuawa na huo ndio ukawa mwanza wa
uhasama na chuki kati ya Wahutu wa Kaskazini na Watutsi. Sasa, ukiangalia
mwanzo mwa hii vita ulikuwa umechochewa na wakoloni maana, kama nilivyosema
hapo mwanzo, wakoloni walipofika walikuta makabila haya yakiishi kwa
amani", Padri Karangwa alijibu.
"Ilikuwaje
sasa baadaye Wahutu kuja kutawala Rwanda", Willy aliuliza.
"Baada
ya vita kuu vya pili Watutsi walianza kuomba uhuru kama ilivyokuwa katika nchi
zingine za kiafrika. Wakoloni wa Kibelgiji kuona hivi, na jinsi Watutsi
walivyokuwa na nguvu na walivyokuwa wamesoma, wakaingiwa na wasiwasi, wakajuwa
Watutsi wasingewahitaji iwapo watapata uhuru. Hivyo Wakoloni wa Kibalgiji
wakaamua kuwageuka na kuwasaidia Wahutu kuwaunga mkono. Viongozi wa Kihutu
walikuwa wachache na wote walikuwa na kisomo kidogo walichopata kwa Wamisionari.
Hivyo, kwa vile hawakuwa na nguvu zozote za kiutawala, walipoanza siasa, siasa
yao ikawa ya kikabila. Hivyo mwaka 1957 chama cha kupigania haki za Wahutu,
kikiongozwa na Gregoire Kayibanda, kilianzishwa kikiitwa Permehutu. Na Wakoloni
wa Kibelgiji, wakiwa sasa wamewageuka Watutsi, walianza kukisaidia chama cha
Permehutu, huku wakikitafutia nafasi ya kuuangusha utawala wa Watutsi. Nia yao
ikiwa kuwaingia kwenye madaraka Wahutu ambao hawakuwa na nguvu ili waendelee
kuwategemea kama wangepata uhuru. Hii ingewasaidia wakoloni kuendeleza maslahi
yao kwani Wahutu wangewategemea sana kuwalinda dhidi ya Watutsi waliokuwa na
nguvu za kijeshi na utawala. Kwa hiyo wakoloni ndio wangeendelea kutawala
kiaina kwani watawala wa Kihutu wangekuwepo kama mfano tu.
"Je,
viongozi wa Kitutsi hawakushituka?", Willy aliuliza.
"Walianza
kushituka lakini mambo yalitokea kwa ghafla sana wakati Omwami Rudahigwa
alipofariki kiajabu mjini Bujumbwe mwaka 1959. Jeshi la Ubelgiji lilisimamia
kuangushwa kwa utawala wa Kitutsi ambao ulikuwa na umwagaji wa damu vibaya
sana. Jeshi la Ubelgiji lililowasaidia Watutsi kuanzia mwaka 1912 sasa
liliwasaidia Wahutu na ile chuki ya mwaka 1912 ya Wahutu wa kaskazini
ilijitokeza na inasadikiwa kuwa Watutsi wapatao elfu kumi waliuawa na wengi wao
wakakimbilia nchi jirani. Hivyo, Wahutu ndio wakawa watawala chini ya Kayibanda
baada ya kusaidiwa na wakoloni wa Kibalgiji kuwaweka madarakani", Padri
Karangwa alieleza.
"Kwa
nini baada ya hapo vitambulisho viliendelea, si Wahutu wangeachana navyo sasa
maana vilikuwa vinawabagua?", Willy alitaka kujua.
"Hapana,
mambo sasa yaligeuka; Wahutu sasa ndio walikuwa watawala. Hivyo, wakaanza
kuwanyanyasa Watutsi. Na vitambulisho hivyo hivyo vilivyowasaidia Wahutu
kuwatambua Watutsi na kuwabagua, hata Watutsi wengine wakabadili vitambulisho
vyao na kujiita Wahutu maana sasa kibao kilikuwa kimewageukia. Ingawaje Watutsi
ndio waliokuwa wamesoma lakini sasa walibaguliwa na Wahutu waliokuwa hawana
kisomo maana ndio waliochukua madaraka serikalini. Elimju yote sasa ilitolewa
kwa wahutu na Watutsi wakabaki kuangaika na kunyanyaswa. Wengi wao wakaanza
kukimbia. Kwa vile jeshi asilimia kubwa lilibaki la Kibelgiji hivyo hakuna kitu
ambacho Watutsi wangefanya. Ingawaje Watutsi waliokimbia walijaribu
kuishambulia Rwanda kwa kuunda jeshi la msituni lakini hawakufua dafu. Jeshi
zaidi la kuongeza nguvu liliitwa mara moja toka Ubelgiji kuja kutokomeza maasi
mara uvamizi wa kitutsi ulipoanza. Kwa hiyo, katika miaka yote ya sitini hali
iliendelea kuwa ya wasiwasi nchini Rwanda huku watutsi wakiendelea kuuwawa na
kunyanyaswa",
"Ilikuwaje
Habyarimana akafanya mapinduzi, maana yeye ni Mhutu na utawala ulikuwa
Wakihutu? " Willy aliuliza.
"Swali
zuri," Padri Karangwa alijibu na kisha akaendelea, "Serikali ya
Kayibanda ilianza kuishiwa mbinu na Wabelgiji wakaanza kuichoka maana sasa
ilikuwa inakuwepo kwa sababu ya ukabila tu. Mnamo mwaka 1973 Kayibanda akafanya
makosa. Kwa vile Watutsi walikuwa wamenyimwa nafasi yoyote katika serikali,
kibiashara na sehemu zingine zozote, sehemu waloyokimbilia ilikuwa ni ndani ya
kanisa. Hivyo, Seminari nyingi zilijaa Watutsi pamoja na vyuo vikuu ambavyo
viliitwa vyuo vya Watutsi. Kwa hiyo, mwaka 1973 ili kuwaondoa Watutsi katika
vyombo vyote vya elimu, serikali ilianza kushambulia seminari, shule na vyuo
vikuu. Kwa vile vyombo vyote vya elimu vilikuwa mikononi mwa kanisa katoliki
Askofun wa kanisa katoliki akaanza kupiga makelele na kulaani serikali. Hata
hivyo, huyu Kayibanda kabla ya kushika madaraka alikuwa katibu wa Askofu huyu na alikuwa akiwaunga mkono
wahutu. Hapo ndipo Wabelgiji tena wakapata nafasi na kumtumia Meja Generali
Habyarimana kufanya mapinduzi na kumtoa rais Kayibanda.Haybarimana alikuwa
Mhutu wa kaskazini na Kayibanda wa kusini. Utawala wake ulipokelewa kwa shangwa
na Watutsi na Wahutu ukifikiriwa utakuwa utawala wa haki na usawa lakini hali
haikuwa hivyo, badala ya kuwa na mgawanyiko wa Watutsi na Wahutu mambo
yalizidi. Sasa kukawa na upendeleo kwa Wahutu wa kaskazini na kuwabagua Watutsi
na Wahutu wa kati na kusini. Ndiyo sababu Wahutu wenye siasa ya wastani
waliuawa katika mauaji ya aprili wakiwamo wanasiasa, wafanyakazi wa serikali na
wafanyabiashara, wote walikuwa wa kusini. hivyo, kufika wakati wa sasa sera ya
gawa nitawale iliendelea katika Rwanda."
"Maelezo
yako toka mwanzo yameonyesha kuwa Wahutu na Watutsi kama watu hawakuwa na
tatizo kati yao. Wamekuwa wakitumiwa na watawala wa kikoloni na watawala wa
kizalendo ambao wamekuwa wakiwachonganisha ili wakosane na kwa kukosana kwao
wao wafaidike," Willy alieleza.
"Haswa,
ndiyo sababu nimeeleza yote haya uweze kulielewa tatizo la Rwanda. Tatizo letu
si ukabila, tatizo letu ni uongozi."
"Sasa
nini kilifanya hali ifikie mauaji, kama ni tatizo la uongozi nchi nyingi za
Kiafrika zina tatizo hilo. Na kama ni kutumiwa na mataifa ya nje nchi nyingi
zinatumiwa hivyohivyo, mauaji kama haya ni ya pekee katika dunia, hayana
mfano," Willy alimuuliza Padri Sibomana ambaye alikuwa akisikiliza kwa
muda mrefu bila kusema kitu.
"Nafikiri
hilo swali lako ndilo kila mtu anajiuliza, maana mauaji haya tuliyo yashuudia
hayana mfano, hata ya Hitler yalichukua muda mrefu maana vita vilipiganwa kwa
miaka, lakini mauaji haya yanashinda fikra kwani yalianza dakika chache tu
baada ya kufa Rais na kusambaa nchi nzima utafikiri moto wa petroli,"
Padri Sibomana alisema.
"Wakati
wa Habyarimana kulijitokeza kikundi kidogo cha watu kilichomzunguka ambacho
ndicho kilichokuwa kinafaidika na utawala wake. Kikundi hiki kilikuwa cha watu
wa kaskazini kutoka sehemu za Gisenyi na Ruhengeri nacho kilijulikana kwa jina
la Akazu. Kikundi hiki kilijilimbikizia mali na madaraka, kilijenga ngome ya
kukizunguka na hakuna kikundi kingine kilichoweza kupenya ngome hiyo. Hivyo,
ili Rais na kikundi hiki waweze kuendelea kujilimbikizia mali na madaraka
kilihakikisha kuwa hakuna biashara wala nafasi ya uongozi inayoweza kupatikana
mahali popote bila kikundi hicho kutoa ruksa. Kikundi hiki kilikuwa cha Wahutu.
Hivyo, uhalali wa serikali ulipoanza kushitukiwa, kwa vile kikundi hiki cha
Akazu kilikuwa kimejilimbikizia mali nyingi, kilianza kuitumia mali hii na ya
serikali kujenga jeshi lake, redio yake, magazeti na kutumia vyombo hivi
kuwachochea Wahutu, ambao ndio wengi, wawachukie Watutsi ambao sasa walikuwa
wanausaili uhalali wa serikali hii wakiwemo Wahutu wapendao amani na usawa ambao
waliitwa Wahutu wenye msimamo wa wastani. Kufikia mwaka 1990 kulikuwa hakuna
Mtutsi mwenye madaraka katika serikali, kwa mfano kati ya wakuu wa mikoa kumi
na moja hakukuwa na Mtutsi hata mmoja; kati ya vyeo 143 vya juu serikalini
hakukuwa na Mtutsi hata mmoja; kati ya mabalozi wote walioteuliwa kwenda nje
Mtutsi alikuwa mmoja tu. Na kati ya wabunge sabini, ni watutsi wawili tu
waliokuwa wabunge. Katika jeshi walihakikisha hakuna Mtutsi na hasa jeshi la
kumlinda Rais lote lilikuwa na Wahutu na Wahutu hao vilevile walikuwa ni ama
ndugu za Rais au wa mkewe", Padri Karangwa alieleza.
"Sijaelewa
vizuri jinsi hali hii ilivyoashiria kufikia mauaiji yaliyotokea", Willy
alisema huku akionyesha sasa kuwa makini zaidi.
"Huku
ndiko ninakokwenda. Hawa Akazu pamoja na familia ya Rais walifikia kujiita
miungu wadogo. Walifanya kila walichotaka. Kuna habari za kuaminika kuwa kuna
Mzungu mmoja rafiki yake sana na Rais ambaye alikuwa anawatengenezea fedha kwa
maana ya kuchapisha na wao wanamlipa mazao kama kahawa kwa bei yake, na mazao
mengine yoyote aliyohitaji; na pia kuna tetesi kuwa hata bangi ililimwa na watu
hawa na kusambazwa na huyu Mzungu. Kusema kweli, hawa watu walitajirika kuzidi
kiasi na wakajisahau kabisa. Ili kubaki katika hali hii kama nilivyosema
mwanzo, ilibidi sasa wachochee ukabila. Walikuwa wameshafilisika kisiasa, uhali
wa utawala ulikuwa hauna msimamo tena. Hivyo, kimbilio lilikuwa ni ukabila na
kuhakikisha Wahutu wananufaika na utawala, na ilikuwa ni rahisi sana
kuwachochea na kufanya lolote ambalo viongozi wao wa Kihutu walitaka wafanye.
Uchochezi wa Wahutu ulizidi kuanzia mwaka 1988 baada ya kongamano la Watutsi
lililofanyika Washington D.C Marekani na kuamua kuiondoa serikali tawala
madarakani. Mkutano huo pia ulihuhudhuliwa na Wahutu ambao walikuwa wakipinga
mwenendo wa serikali tawala. Haja ya wakimbizi wa Kitutsi kurudi nyumbani kwa
njia yoyote ile ndiyo ilikuwa msukumo wa kongamano hili huku Marekani, kwani
Rais alikuwa akieleza kuwa wakimbizi hawana haki tena ya kurudi Rwanda kwa kuwa
nchi ilikuwa ndogo mno na isingeweza kuwapokea tena". Padri Karangwa
alinyamaza kidogo na kuchukua glasi ya maji.
Padri
Sibomana akatumia wakati huu kumkata kauli kidogo. akasema, "Padri
alilisahau swala la wakimbizi wa Kibanyarwanda Uganda, maana hili lina uhusiano
mkubwa mno na hali hii yote anayoieleza".
"Bila
shaka Padri Sibomana, nilikuwa bado niendelee huko ila kwanza nilitaka
kuonyesha mshikamano wa Wahutu ulikuwaje", Padri Karangwa alijibu.
"Sawa
Padri, endelea", Padri Sibomana aliafiki.
"Kama
alivyo kumbusha Padri Sibomana, wakimbizi wengi walijiunga na jeshi la NRA la
Uganda katika miaka ya themanini. Hao walimsaidia Rais wa sasa wa Uganda
kuchukua madaraka. Kwa kawaida, wakimbizi mara kwa mara hujiingiza kiurahisi
jeshini kuliko kukaa bure na hii vile vile huwapa tamaa ya kutafuta njia za
kijeshi kurudi kwao. Na hivi ndivyo ilivyokuwa kwa wakimbizi wa Kibanyarwanda
waliokuwa Uganda, wengi wao wakiwa Watutsi na Wahutu wachache. Makamanda wengi
wan NRA walikuwa wakimbizi wa Kibanyarwanda. Baada ya kushika madaraka Uganda
ubaguzi ulianza wa wakimbizi wa Kinyarwanda Uganda. Waliwapinga hasa waliokuwa
wapinzani wa serikali na raia wa kawaida wa Kiganda waliona hawa wakimbizi kama wanaokuja kuwanyang`anya
haki zao kwa vile walikuwa wakishika vyeo vya juu katika jeshi la NRA ambali
sasa ndilo lililokuwa likitawala Uganda. Ilikuwa ni hali hii na nia ya kurudi
kwao kwa hali yoyote sasa, iliyo ashiria kuzaliwa kwa RPF. Hivyo makamanda wa
Kinyarwanda walikuwa NRA sasa waliamia RPF.
"Inasemekana
Rais wa Uganda, ili asiwe na matatizo nyumbani kwake kwa sababu nilizozisema
hapo juu, alikuwa msukumo mkubwa wa kuisaidia RPF ili wakimbizi hawa
walazimishe kurudi kwao kwa kutumia nguvu za kijeshi. Kutokana na hali hii
mnamo tarehe 1 oktoba 1990 watoto wa wakimbizi wa Kinyarwanda, ambao walikuwa
wapiganaji wa NRA, walikusanyika kusini- magharibi mwa Uganda na siku hiyo ya
tarehe moja wakaivamia Rwanda. Ingawa hawakufanikiwa, lakini nguvu yao
ilifahamika na kusababisha kiwewe kwa utawala wa Rwanda, na hapa ndipo mipigano
ya kuwaangamiza Watutsi wote na Wahutu waliokuwa wanaunga mkono jitihada za
Watutsi ilipoanza kupangwa na Akazu. Kama nilivyosema hapo mwanzo ili uchochezi
kwa Wahutu dhidi ya Watutsi upate kufanikiwa, kundi lililokuwa linafaidika na
utawala huu liliunda jeshi lake lililoitwa Interahamwe. Interahamwe maana yake
ni "wale wanaovamia na kupigana pamoja". Jeshi hili liliundwa toka
sehemu mbali mbali nchi nzima na kufundishwa na kikosi maalumu cha Rais kataka
kambi za Gabiro na Bigongwe, na wote waliochaguliwa walikuwa Wahutu isipokuwa
kamanda wao alikuwa Mtutsi ambaye baba yake alikuwa amechukua kitambulisho cha
Kihutu. Wengi wa Interahamwe walikuwa ni vijana ambao walikuwa hawana kazi,
Wakipewa vinywaji na pesa wakifundishwa kuwachukia Watutsi na kufanya maasi ya
aina yoyote ile tokea kubaka, kunyang`anya mpaka kuua. Wizara ya ulinzi ndiyo
iliyotoa silaha na kutoa sehemu za kufanyia mafunzo ingawa Interahamwe ilibaki
mali ya Akazu na cha tawala. Vilevile wakimbizi wa Kirundi nao walichukuliwa na
kuingizwa katika jeshi hili Iterahamwe. Inasemekana kuwa hawa wakimbizi wa
Kirundi, ambao ni Wahutu, walikuwa wakatili zaidi kuliko hata wenzao wa Rwanda.
Wakuu wa Interahamwe hawakuishia hapo tu bali walienda mpaka Goma, Zaire,
ambako nako walichukua askari wa kujiunga na Interahamwe. Wazaire
waliochukuliwa ni wale wenye asili ya Kihutu lakini Wazaire wanye asili ya
kitutsi kwa jina la Wabanyamulenge, wao walikataa kwani wao walikuwa wanaunga
mkono harakati za RPF.
"Hawa
Interahamwe walikuwa wengi kiasi gani?" Willy aliuliza.
"Hata
kufikia tarehe 6 aprili na baada ya kifo cha Rais na mauaji kuanza inasemekana
kwamba kila Mhutu sasa alikuwa Interahamwe, lakini Interahamwe waliochukua
mafunzo haswa walikuwa wamefikia kiasi cha elfu kumi."
"Inasemekana
yalifanyika mauaji mengi kwa silaha hafifu kama rungu, panga na kadhalika.Hii
ni kwasababu haya marungu yaliweza kutengenezwa kienyeji na kwa urahisi au
vipi?" Willy aliuliza.
"Hapana,
marungu na mapanga haya yaliagizwa na kundi la Akazu kutoka China. marungu haya
yalipendekezwa na Akazu kwani kila yalipotumiwa yalitoa maumivu ya ajabu kwa
adui. Na inasemekana kuwa watu wengi walitoa pesa kununua kuuawa na risasi
kuliko kustaimili kifo cha rungu. Marungu haya, kwa mfano yalianza kuingia
Rwanda tokea januari 1993 yakipakuliwa toka Mombasa kupitia Nairobi na
kuhifadhiwa kwenye maghala Kigali na Kibungo. Lakini, pamoja na marungu haya
serikali ya Rwanda, kati ya mwaka 1992 na 1994, iliagiza silaha kubwa kubwa
toka Ufaransa. Vile vile silaha zingine zilitoka Ulaya ya mashariki kupitia
Zaire. Ufaransa, hata hivyo, ndiyo iliyokuwa mfadhili mkubwa wa siliha kwa
serikali ya Rwanda. Inasemekana yule mzungu rafiki wa Rais na Akazu ndiye
alipanga mipango yote ya uuzaji wa silaha kati ya Ufaransa na Rwanda.
Inasemekanaq kuwa Mfaransa huyu ambaye pia alikuwa na uhusiano wa karibu na
Ikulu ya Ufaransa alifikia kuwa mshauri mkuu wa Rais na ndiye aliyekuwa
anamshauri Rais afanye nini, aseme nini na hata mauaji mengi inasemekana
yalitokana na ushauri wake. Na kwa vile Rais na watu wake walitaka kutawala
maisha, huyu mtu ambaye alikuwa akiwapa silaha za hali ya juu ili RPF isiweze
kufurukuta, walimwonja kama Mungu, hata ndege ya Rais inasemekana ilitolewa
kama zawadi nja mtu maarufu wa huko Ufaransa kwa mipango ya huyu mtu,"
Padri Karangwa alieleza.
"Kwa
hiyo mauaji haya ya Rwanda yalipangwa, na siyo kwamba yalitokea tu kwa bahati
mbaya, kwa kuchukizwa na kifo cha Rais?" Willy aliendelea kumdadisi Padri.
"Bila
shaka. Hili kundi la Akazu lilikuwa na vyombo vya propaganda vingi ambavyo
vilisaidia kuingiza chuki kati ya Wahutu na Watutsi ili iwe rahisi kuwatumia
Wahutu katika mpango wao wa kuwamaliza Watutsi ili waweze kutawala milele.
Magazeti kama Kangura na Stesheni ya Redio ya RTLM vilikuwa vinamilikiwa na
kundi hili. Gazeti hili lilianzishwa katikati ya mwaka 1990 na liliungwa mkono
na chama tawala pamoja na Rais na familia yake huku likiongozwa na rafiki wa
Rais. Vilevile lilikuwa likifadhiliwa na huyo Mfaransa. Kazi kubwa, kama
nilivyo sema hapo awali , ilikuwa ni kuchochea chuki kati ya Wahutu na Watutsi,
huku radio hiyo na gazeti hilo vikiwahamasisha Wahutu wajiweke tayari
kuwashambulia na kuwavamia Watutsi ambao kila wakati liliwasema kuwa wanataka
kurudisha utawala wao wa kifalme, kila Mhutu amwue Mtutsi aliye karibu nae. Maneno
makali kama haya ambayo yaliyotokea kila siku katika vyombo hivi yalikuwa ni
chanzo kikubwa kwa mambo yaliyotokea kwanzia tarehe 6 Aprili alipouawa
Rais," Padri Karangwa alieleza.
"Naona
saa zimeenda, tumezungumza sana maana sasa yapata saa tatu na nusu usiku.
Lakini kabla hatujamaliza Padri hasa nani alimuua Rais?" Willy aliuliza.
Sura ya
Padri alibadilika na kisha akauliza, "Unataka maoni yangu binafsi?"
"Ndiyo
kwani kwa maoni yako kutokana na ulivyonieleza unaweza kuhisi, na hisia zako
zinaweza kuwa sahihi,willy alijibu.
"Maoni
yangu binafsi ni kwamba Rais aliuawa na Akazu. Ilipoonekana kuwa Rais alikuwa
ameamua kutia sahihi ya makubaliano ya Arusha, hiki kikundi chake cha Akazu
kikajua huu ndio utakuwa mwisho wao kufaidika. Hivyo wakaamua kumuua Rais ili
katika machafuko hayo, waweze kupanga serikali mpya na kusimika utawala wao
mpya ambao ungewahakikishia kuendelea kufaidi. Ukweli kuwa watu wake ndio
waliomuua kwa kuogopa utawala wa kidemokrasia ambao ungefuata baada kutia saini
makubaliano ya Arusha, ulijitokeza katika gazeti lao la Kangura, katika gazeti
hilo ilitabiriwa kuwa Rais angeuawa na askari wa jeshi la Rwanda mnamo mwezi wa
machi 1994 kufuatia kukubali kwake kusaini makubaliano ya Arusha. Gazeti hilo
ambalo lilichapishwa mnamo mwezi wa Januari 1994 liliendelea kusema kuwa
atakayemwua Rais atakuwa ni Mhutu. Na likasema kuwa waandishi wa gazeti hilo na
rafiki zake na Rais huyo walimuasa asiweke saini makubaliano ya Arusha lakini
ilionekana kuwa Rais alikuwa amebanwa sana na serikali zilizokuwa zikisuluisha
mgogoro kiasi kuwa alikuwa hana msimamo. Hivyo, gazeti hilo katika toleo hilo,
lilisema kuwa Rais atauawa na hapo ndipo vitatokea vita na damu nyingi
itamwagika na jeshi la UNAMIR lisingeweza kufanya kitu. Lilizidi kumshauri Rais
akatae kutia saini makubaliano hayo vinginevyo kifo chake hakitaepukika. Na
yote yaliyoandikwa kwenye toleo hilo ndiyo yaliyotokea. Rais alipokubali tu
kutia sahihi makubaliano ya Arusha basi hawa watu wake wakatimizi ahadi yao kwani wao ndio
walioshika hatamu zote za serikali kuanzia utawala mpaka jeshini. Kwa hiyo, baada
ya kusikia amekubali makubaliano ya Arusha basi walikiamurisha kikosi cha
mizinga cha Kanombe, na ndege ya Rais ilipokuwa inakaribia kutua makombora
matatu yalipigwa, mawili yakaipiga ndege; Rais na watu wote waliokuwemo, ikiwa
pamoja na Rais wa Burundi, wakauawa. Akazu walipanga kuwa baada tu ya Rais
kuuawa basi jeshi lao la Interahamwa lingeanza mauaji mara moja ya kuakikisha
kuwa Watutsi wote pamoja na yeyote aliyekuwa anawaunga mkono anauawa. Mbinu hii
ilikuwan ni kutaka RPF kukosa watu wa kuwaunga mkono ndani ya nchi hiyo na
hivyo kushindwa vita. Lakina ya mungu mengi, mambo hayakwenda moja kwa moja
kama walivyotarajia," Padri Karangwa alieleza na kuchukua glasi ya maji na
kunywa.
"Lo
maelezo yako yameniingia vizuri na nafkiri kutokana na ulivyoeleza kweli Rais
aliuawa na mfumo wake mwenyewe wa kung`ang`ania madaraka kwani hata wakati
alipokuwa amefikia kubadili mawazo yake, mfumo wake aliokuwa ameuweka haukumpa nafasi. Hivyo,
ilibidi ummalize ili ubinafsi wa watu wake waliomzunguka uendelee,"m Willy
alisema huku akiwa kama anajisemea mwenyewe.
"Watu
ka nyinyi basi ndio mnaotakiwa mueneze habari hizi ili viongozi wengine wajue
kuwa utawala wa mabavu, na wakung`ang`ania madaraka ili wewe tu ndio ufaidike
una mwisho wake, na mwisho wake ni mbaya ata ufanyeje,"Padri Sibomana
alidakia.
"Tutajitahidi
kueleza ukweli huu," Willy alijibu.
"Nafikiri
itakuwa vizuri kesho kama ukipata nafasi uje nikuonyeshe mauaji yalivyo
fanyika, uone ukatili usio kifani,"Padri karangwa alimweleza Willy.
"Nitajitahidi,
lakini kwa vile nina shughuli nyingi inabidi nirudi haraka Arusha. Kama
sitaweza kufika maelezo yako yanatosha. Na kabla basi sijaondoka nikuulize
swali."
"Uliza
usiwe na wasiwasi, sisi tumefurahi kuwa nawe hapa wala hatuoni kama muda
unaenda" Padri Karangwa alijibu.
"Unafikiri
baada ya RPF kuchukua madaraka kutakuwa na maana na uelewano Rwanda? au niulize
tena vingine baada ya haya mauaji ya kikatili dhidi ya Watutsi yalivyofanywa na
Wahutu, unafikiri kutakuwa na uelewano kati ya makabila haya hata kama RPF
itaweka utawala wa demokrasia?"
"Hilo
swali gumu lakini nafikiri ndilo swali lenye maana kubwa sana. Uelewano kwa
sasa utakuwa mgumu. Vidonda vya mauaji ya ndugu zao Kitutsi bado vibichi na
kama binadamu lazima kutakuwa na kisasi, kwa hili tusijidanganye. Pili, baada ya RPF kuchukua madaraka maelfu ya
Wahutu wamekimbia ni wakimbizi huko Tanzania, Zaire, na nchi zinginezo. Kati ya
hawa waliokimbia na hasa waliokimbilia Zaire, ni wale Interahamwe na wanajeshi
wa serikali ya zamani. Kwa vyovyote, hawa nao wataanza kujikusanya na kuunda
tena jeshi la kuja kuvamia tena Rwanda, na Serikali ya sasa haita kubali.
Hivyo, vita vitaendelea na itaendelea kwa muda mrefu kama jumuiya ya kimataifa
itaendelea kulipa kisogo swala hili la Rwanda. Tatu, miongoni mwa wakimbizi
wanaoumia ni wanawake na watoto, na watoto hawa taabu watakazozipata huko
watakuwa wanaelezwa kuwa ni sababu ya Watutsi ambao wamewafukuza nchini mwao na
hivyo kujenga chuki tena. Watoto wa Kitutsi vilevile watakuwa wanaelezwa ndugu
yako fulani aliuawa na Wahutu; na kwa vile kila familia iliathirika chuki hii
itazidi kujengeka maradufu. Mimi maoni yangu ni kwa serikali ya RPF isilipize
kisasi. Wakimbizi wote warudishwe nyumbani. Wale ambao wanajulikana kabisa ndio
waliusika na kuongoza mauaji haya ya kikatili, wakamatwe kokote duniani waliko
na wafikishwe maakamani. Kama dunia hii isivyokuwa na usawa, wale wote
walioongoza mauaji haya kwa vile wana pesa tayari wapo nchi za nje wanakula starehe.
Wanaohangaika sasa ni wanawake na watoto; hii si sawa. Lazima hawa watu
wakamatwe hasa kundi la Akazu, wote wakamatwe wafikishwe maakamani,"Padri
Karangwa alimalizia huku sasa machozi yakimlengalenga.
"Kwa
kweli, hali ya nchi yetu hii itayumba kwa muda mrefu. Wote wanachotegemea sasa
ni serikali ya RPF iweze kuwahamasisha wananchi waweze kusameheana ili tujenge
taifa jipya. Nakubaliana na Padri Karangwa kuwa ili tukio kama hili lisitokee
tena, wote waliohusika na kitendo hiki wafikishwe mbele ya maakama wahukumiwe
na adhabu kali itolewe ili kitu kama hiki kisitokee tena popote duniani, maana
ni kitu cha kutisha ambacho kinafanya akili isikubali kuwa binadamu anaweza
kuwa katili na mharibifu namna hii kama ilivyotutokea sisi hapa. Hapa Willy,
dunia isinyamaze mpaka hapo wote waliohusika wameadhibiwa," Padri Sibomana
alitoa maoni yake.
Huku
akiinuka, Willy alishukuru na kusema, "kusema kweli sina maneno ya kuweza
kueleza jinsi ninavyo shukuru kwani naweza kurudi Arusha kesho maana yote
nimepata niliyotaka kujua kwenu na nimejifunza mengi, asante sana. Nipatapo
nafasi nitawatembelea tena. Nikishindwa kuja kesho mara nyingine nitakuja kwa
mapumziko. Asanteni sana, tena sana."
"Nasi
tunashukuru sana kwani kuja kwako kumetufariji kumbe kuwa huko duniani kuna
watu wanaoyajali matatizo yetu yaliyotupata. Asante sana," Padri Karangwa
alimalizia, kisha wakamsindikiza Willy mpaka kwenye gari lake; akaondoka.
ITAENDELEA 0784296253
Comments
Post a Comment