UCHU

KASHESHE

III

Willy aliangaliana na Bibiane. "Unasemaje tuwasaidie hawa ama vipi?", Bibiane aliuliza.

"Hapana tuendelee na mipango yetu. Hii imekuwa bahati nzuri kwetu, naamini Meja Kasubuga ana uwezo wa kuukabiri uvamizi huu, na nahisi walengwa wa uvamizi huu ni sisi tunatafutwa, huenda kikosi cha Col. Gatabazi kimesikia ama kuhisi kuwa tuko hapa. Wakati wao wanatusaka hii itatupa nafasi nzuri, kwanza kumtoroka Meja Kasubuga na pili kuendelea na mipango yetu. Panda gari twende zetu Kibumba tukawasake hawa majahiri", Willy alieleza huku wakipanda gari na kuondoka kwa kasi kuelekea Kibumba.

IV

Wakati kikosi cha Nkubana kikisonga mbele kuelekea hoteli Meridien-Izuda kilishitukiwa na askari mmoja wa doria ambaye baada ya kusikia nyayo za watu zisizo za kawaida akapanda juu ya mti na kuchungulia chini ya kjinjia kilichotelemka kutoka mlimani kuelekea hotelini. Akisaidiwa na mbalamwezi askari hjuyu aliweza kukiona kikundi cha askari kadhaa kikielekea hotelini hapo, baada ya kuthibitisha kuwa walikuwa askari wa adui na jinsi walivyokuwa wakisonga mbele kwa tahadhari kubwa huku silaha zao zikiwa zimewekwa tayari kwa mashambulizi.

Huyu askari wa doria alitelemka kwenye mti haraka haraka na kimya ili asiwagutue wale wavamizi waliokuwa hatua kumi tu karibu na ule mti na kwa kutumia uzoefu wa sehemu ile alikimbia kwa kutumia njia za mkato na kwenda kutoa taarifa kwa kikosi kilichokuwa kwenye maandalizi ya kuondoka kuelekea mpakani kisiondoke kwani kulikuwa na uvamizi.

"Kuna kikosi cha adui kinaweza kutushambulia sasa hivi, kimetumia kichochoro namba tatu na kitafika hapa sasa hivi, askari huyo alimweleza Mkuu wa kikosi hicho Sajenti Ibrahim.

"Oke, wewe kimbia kwa Afande Kasubuga umweleze wakati sisi tunaelekea huko kuwasimamisha mpaka tupate msaada", Sajenti Ibrahim aliamru na palepale akawaamru askari wake waweke silaha zao tayari na kusonga mbele kuelekea kichochoro namba tatu. Njia zote zilizokuwa zinaelekea kwenye hoteli hii zilipewa namba ili iwe rahisi kuzitambua kwani zilikuwa nyingi. Yule askari wa doria alikimbia mpaka ofisini kwa Meja Kasubuga lakini hakumkuta, kwani ndio wakati Meja Kasubuga alikuwa amewasimamisha Willy na Bibiane wasiondoke, na kabla hajajuwa ampate wapi na yeye alisikia milio ya bunduki akajuwa tayari mapambano yameanza.

Sajenti Ibrahim na kikosi chake walifanikiwa kuwaona wale askari wavamizi wakisonga mbele kuelekea hotelini na kwa vile hakujuwa walikuwa na nguvu kiasi gani aliamru askari wake waanze kushambulia hata bila kulenga shabaha kwa uhakika ili kuwatia kiwewe. Na kweli hii ilimshitua Nkubana kwani hakutegemea kukutana na upinzani haraka kiasi hicho kutokana na maelezo ya yule askari muasi.

"Luteni Nyamboma", Nkubana alimwita msaidizi wake, "Wewe endelea kukabiliana na hawa adui zetu ili mimi na askari watano tuweze kupata mwanya wa kwenda kumkamata Willy. Fanya mashambulizi makubwa ili askari wote wafikiri kuwa wanashambuliwa na kikosi kikubwa ili wote waje upande huu na sisi tupate urahisi pale Willy alipo".

"Sawa, nimekusoma Kamanda", Nyamboma alijibu.

Nkubana aliwachagua askari watano wazuri pamoja na yule kikaragosi wao. "Wewe tupeleke chumba cha yule mtu, tumia uzoefu wako wa hapa".

"Sawa afande, yule askari alijibu huku akitetemeka maana alistaajabu namna walivyokuwa wamebainika na kuonekana kwa adui mapema namna ile.

Mapigano makali yalianza na, kama Nkubana alivyotaka, askari wengi wa kambi ile walielekea upande wa mapigano kuongeza nguvu wakiongozwa na kiongozi wao Meja Kasubuga. Nkubana na askari wake hawakupata kikwazo mpaka walipofika kwenye chumba alichopangiwa Willy.

Baada ya Nkubana kushuhudia umahiri wa Willy Kigali, hakutaka kufanya makosa tena. Aliwapanga askari wake vizuri na kwa hadhari kubwa, walipofika kwenye chumba cha Willy na kwa amri moja wakaupiga mlango kwa nguvu zao zote na askari wawili wakaingia na mlango ndani ya kile chumba. Chumbani hawakumkuta mtu isipokuwa mikoba miwili iliyokuwa na nguo, Nkubana akautambua mkoba mmoja kuwa ulikuwa wa Bibiane, maana alipata kuuona pale sebuleni kwa Bibiane mjini Kigali.

"Watakuwa wapi hawa?", Nkubana alihoji, kisha akaendelea. "Wanaweza kuwa wamejiunga na askari wa hapa wanaopigana na kikosi chetu au wamevuka mpaka".

Yule askari kikaragosi alikuwa ametoka nje na akarudi na kusema. "Gari lao halipo, nafikiri wamekimbia mapigano".

Nkubana aliposikia hivyo woga ulimwingia kwani alijua mtu huyu amevuka mpaka. "Itatubini na sisi tuvuke mpaka sasa hivi. Wao wameondoka na gari sisi itabidi twende kwa miguu sasa", Nkubana aliamru huku ule upande wa mapigano makali yalikuwa yakiendelea.

"Itabidi turudi kuongeza nguvu", askari mmoja alishauri.

"Hapana, Luteni Nyambona ana ujuzi wa kutosha, akiona amezidiwa atarudi nyuma na kukimbilia mpakani. Huu ni wakati mzuri kwetu kuondoka kuwafuata hawa washenzi", Nkubana alijibu huku wakiondoka kuelekea mpakani.

V
Usiku ule Willy na Bibiane walipokuwa wakielekea kwenye mpaka wa Rwanda na Zaire, mbalamwezi iling'aa sana na kuyaonyesha mandhari safi ya milima ya Volkano ya Virunga.

Milima hii ilijulikana toka zama za kale, ambapo hata Wagiliki wa zamani waliizungumzia sana milima hii wakiita milima ya mwezi. "Sasa wewe mwenyewe unaweza kuona kwanini waliita hivyo", Willy alimsimulia Bibiane.

"Inaonekana wewe umesoma sana historia", Bibiane alieleza.

"Unajuwa kitu chochote hakiwezi kuwa kitu bila historia. Ili uijue dunia hii lazima ujue historia. Hata binadamu hawezi kuwa binadamu kama hana historia. Ndio maana mimi nikikwambia naitwa Willy, lazima utaniuliza Willy nani, nitakujibu Willy Gamba. Halafu utataka kujuwa baba yangu anatoka wapi halafu nitakwambia. Hii yote ni kutaka kujua historia yangu ili uweze kujua namna utakavyoniweka. Hata nchi. Nchi isiyokuwa na historia si nchi. Haiwezi kuwa na maendeleo. Sijui kama umenielewa vizuri mpaka hapo?", Willy alijibu na kuhoji.

"Nimekuelewa vizuri sana Willy. Kwa muda huu mfupi nitakaokuwa na wewe hakika nitajifunza mambo mengi", Bibiane alimwambia Willy.

"Sasa walikuwa wanakaribia sana mpakani, na Bibiane akasema.

"Tukivuka mpaka tu, lazima tutakutana na kikosi cha jeshi la Zaire, Unasemaje?".

"Unazijuwa njia nyingine tunazoweza kukwepa mambo ya mpakani?", Willy aliuliza.

"Ndiyo Willy, na ndio sababu nimesema hivyo, hapo mbele utakata kulia nitakuonyesha njia ya siri wanayotumia wapelelezi wa Akazu, lakini tuwe na tahadhari kubwa. Willy akakata kulia baada ya mwendo wa dakika kadhaa mara njia iliisha. Kukawa na njia ya majani tu. "Endelea tu. Ukikata tena kushoto. Tutakuwa tayari tuko Zaire. ni kilomita kama moja tu kutoka hapa", Bibiane alimwambia Willy, baada ya kutembea mwendo wa kilomita moja na baada ya kupita sehemu ya miti mingi walitokea mahali pa wazi na upande wa kushoto wakaona taa zinawaka.

"Pale ndio mpakani upande wa Zaire na ile ni kambi ya jeshi la Zaire", Bibiane alieleza.

"Tunaweza kupata magari ya jeshi pale?", Willy alimuuliza Bibiabe.

"Lazima. Unataka tukaibe gari moja la jeshi?", Bibiane alihoji.

"Unasoma sana mawazo yangu. Tusiibe, tukachukue tu?", Willy alijibu na kuendelea. "Ili tusije tukatia shirika la Msalaba Mwekundu dosari, yafaa tusiwe na gari lao kwenye uwanja wa mapambano. Hapa tutapata mahali pazuri pa kulificha halafu tukachukue gari la jeshi la Zaire. Itakuwa vilevile vigumu kusimamishwa na askari hovyohovyo".

"Je kuhusu nguo itakuwaje?", Bibiane alihoji tena kwa shauku.

"Kuhusu nguo tutawavua askari walioko mpakani". Willy alisema huku Bibiane akicheka sana.

"Wewe una mambo. Mbona naanza kusikia raha, usiku huu naona itakuwa kasheshe tupu", Bibiane alinena.

Walitafuta sehemu iliyokuwa na msitu wakalificha gari la Msalaba Mwekundu na kuitoa mizigo yao. Gari lilifichika vizuri sana kiasi kwamba ingekuwa vigumu mtu kuligundua mara moja.

"Tutalipitia kabla jua halijachomoza", Willy alinena.

"Kama tukiwa hai", Bibiane alijibu.

"Ili uweze kubaki hai fikiri kuwa utakuwa hai. Na ukiwa hai ukifikiri utakufa. Utakufa tu", Willy alifafanua.

"Sawa bosi. Tutarudi hapa kwenye gari letu tukiwa hai", Bibiane alisema.

"Mawazo safi kabisa", Willy aliongeza. Wakiwa wamebeba silaha zao na kila kitu walichohitaji kwa mapambano usiku ule walianza kuinyemelea ile kambi ya jeshi mpakani Zaire. Walipofika pale kituoni waliyaona magari matatu ya jeshi aina ya Landrover ya wazi nyuma yakiwa yameegeshwa. Walipoangalia vizuri waliwaona askari watatu. Kila mmoja akiwa ameegemea kwenye gari lake.

"Hao watakuwa madereva wa hayo magari", Bibiane alibobota kwa sauti ya chini.

"Hata mimi nafikiri hivyo, nahisi yalikuwa yamewachukua wale askari walioshambulia kule Meridiane hoteli, maana inaonekana hawa askari wanaosubiri watu", Willy alijibu.

Kwa vile yale magari yalikuwa karibu na ua wa michongoma na pale mahali. Willy alifikiri namna ya kuwashambulia bila ya kuwagutusha watu wengine pale kikosini. Mara akawaona askari wote wanakuja kuzungumza na yule askari aliyekuwa kwenye gari la mwisho karibu kabisa na ua.

"Bibiane kazi kwako, hapohapo wewe mshambulie yule wa kushoto. Mimi nitamalizana na wale wawili. Wa kati na kulia", Willy aliagiza huku hawa askari wakiwa sasa wameegemea kwenye magari yao huku wameipa visogo sehemu ile waliyokuwa wamejibanza akina Willy.

"Wale tutumie bastola zenye kizibo tusipoteze muda", Bibiane alishauri.

"Hapata, tunahitaji kila risasi tuliyonayo isipotee bure, pale ambapo tunaweza kulinda risasi nashauri tutumie njia nyingine, au unaogopa hutaweza kumkaba sawasawa?", Willy alimuuliza Bibiane.

"La, hasha! naweza sana Willy na wewe mwenyewe utanishuhudia leo; haya twende", Bibiane aliamru.

Huku wakitambaa chini kama nyoka, waliwanyemelea wale askari. walipofika usawa wa gari la kwanza Willy alisema. "Sasa", wote wawaili walirukia na bila kuwapa nafasi hata ya kushituka, Willy aliwapiga wawili karate kwenye vichwa akitumia mikono yake miwili na kupasua vichwa vyao palepale. Bibiane alimrukia yule wa kushoto na kumbana shingo na kisha kuikata kwa mikono yake. Hawa askari waliuawa kama kondoo. Hawakutoa upinzani wa aina yoyote, huenda kwa vile hawakutegemea kushambuliwa kama lile mahali pale. Kisha walizivuta maiti zao mpaka nyuma ya ua, wakawavua zile sare za jeshi na kuzivaa haraka haraka. Bibiane alichekelea sana maana zilikuwa kubwa. Hata hivyo akazifungafunga zikamwenea hivyohivyo.

"Utaweza kukimbia ama kupigana na adui ukiwa na magwanda haya?", Willy alimuuliza Bibiane huku akicheka.

"Tena ndio mazuri zaidi hasa kwa judo na karate", Bibiane alijibu.

Willy na Bibiane walibeba mizigo yao na kisha wakachungulia ndani ya magari na kukuta la gari la katikati likiwa na funguo. Waliweka mizigo yao ndani na kuliwasha na kisha kuondoka. Walipoangalia saa ilikuwa yapata saa nne na nusu usiku. Waliondoka bila mtu yeyote pale kuhisi kitu. "Moja kwa moja Kibumba", Bibiane alisema.

ITAENDELEA 0784296253...

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru