UCHUKASHESHE

IX

Mapigano makali kati ya kikosi cha Luteni Nyamboma na jeshi la Meja Kasubuga yaliendelea kwa kila upande kutumia mbinu kuukabiri upande mwingine. Kwa muda wa saa moja na nusu, Luteni Nyamboma hakurudi nyuma, lakini alikuwa amewapoteza askari wake wapatao kumi na watano, lakini nao pia walikuwa wamefanikiwa kuwaua askari zaidi ya arobaini wa jeshi la Meja Kasubuga. Luteni Nyamboma alipoona anaelemewa na risasi zinamwishia aliwaamru askari wake waliobaki kurudi nyuma ili wakimbilie mpakani ambako waliamini kuwa wangepata msaada zaidi.

Walirudi nyuma kwa hadhari na walipoona sasa wanaweza kukimbia ili kuwatoroka wanajeshi wa jeshi la Meja Kasubuga walifanya hivyo. Meja Kasubuga alimru jeshi lake liwafukuze na kuwakamata. yeye mwenyewe alirudi ofisini kwake ili aweze kupeleka habari Makao Makuu Kigali kueleza mambo yaliyokuwa yametokea. Col. Rwivanga ndiye aliyepokea simu na alipoangalia saa yake ilikuwa saa tano usiku.

"Afande, tumevamiwa hapa na jeshi la Intarahamwe na Wahutu wenye msimamo mkali, tumepoteza askari kama arobaini hivi, lakini tumefanikiwa kumrudisha adui nyuma, amekimbilia mpakani mwa zaire", Meja Kasubuga alimweleza Col. Rwivanga na kisha kueleza kwa kirefu mapigano yalivyokuwa.


"Hivyo, inaonekana hao ni askari wenye ujuzi mkubwa?", Col. Rwivanga aliuliza.

"Sana afande, mpaka mimi nimeshangaa, nafikiri fununu tulizonazo kuwa kuna kambi kubwa ya mafunzo yenye wakufunzi wenye utaalamu wa hali ya juu kuhusu mambo ya kijeshi ni kweli kabisa".

"Willy yuko wapi?".

"Katika prukushani hii Willy na mwenzake wamechomoka, naamini wamekwishavuka mpaka. Huyu mtu ataleta kasheshe kubwa, nadhani niruhusu sasa mimi na kikosi changu tuvuke mpaka ili tuwasaidie, maana alitaka kwenda Kibumba na huko ndiko kunasemekana kuna jeshi zima la Intarahamwe. Kwa vyovyote hawezi kurudi, kwani taarifa za siri tulizonazo kama ni kweli kuna askari zaidi ya elfu kumi katika kambi hiyo, na wakimbizi wote katika sehemu hiyo wamepewa mafunzo ya hali ya juu ya kijeshi. Kwani wale wakimbizi wanaokataa kushiriki mafunzo ya kijeshi wanauawa, elewa kuwa kuna wakimbizi zaidi ya laki moja wanaume, achilia mbali wanawake na watoto. Hivyo, Willy yuko katika hatari kubwa, huenda hakujua vizuri nguvu ya adui", Meja Kasubuga alimwambia Col. Rwivanga.

"Wewe fanya kazi moja kwanza, wafukuze hao wavamizi mpaka mpakani, wakivuka mpaka wewe na jeshi lako msivuke, mtusubiri hapo hapo mpakani. Mimi, Meja Tom Kabalisa wa Banyamlenge na Bwana Mpinda wa vikosi vya vyama vinavyopinga serikali ya Zaire tutakuja usiku huu kwa helkopita, naamini saa nane usiku tutakuwa tumefika hapo mpakani, msivuke mpaka tufike", Col. Rwivanga aliagiza.

"Sawa afande, mimi naendelea na mapambano, jeshi langu sasa linaelekea mpakani hivi sasa. Mkifika helkopita itue ile sehemu ya kawaida, tutakuwa tumeimalisha ulinzi eneo hilo, nitawasubiri", Meja Kasubuga alisema.

"Asante na kwaheri, msifanye chochote kwanza", Col. Rwivanga alisisitiza na palepale akajiweka tayari kisha akatoka kwenda kuwafuata akina Mpinda na Kabalisa kwa ajili ya kuelekea kwenye uwanja wa mapambano.

ITAENDELEA 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru