UCHU

KASHESHE

XV

Meja Kasubuga alipigana vikali na jeshi la Luteni Nyamboma na kufanikiwa kuwazidi nguvu na hivyo askari wa jeshi hilo walilazimika kukimbilia mpakani. Luteni Nyamboma alikuwa amepoteza askari wengi sana, walipfika mpakani wakitegemea kumkuta Nkubana ili awaongezee nguvu ya askari warudi kuendeza mapambano, lakini hakumkuta Nkubana. Hivyo, Luteni Nyamboma akaamua kuelekea Kibumba na masalia ya askari wa kikosi chake waliobaki. Luteni Nyamboma alipoangalia saa yake ilikuwa saa nane usiku. Walitumia magari waliyoyakuta pale mpakani, Luteni Nyambona na askari wake waliondoka kuelekea Kibumba.

Hata hivyo, Luteni Nyamboma alilazimika kuwaacha askari wa jeshi la Zaire pale mpakani kwa ajili ya ulinzi ili baada ya kazi ya Gisenyi Luteni Nyamboma awafuiate Kibumba.

Meja Kasubuga alipofika mpakani aliyaona magari yanaondoka kasi eneo la mpakani. Meja Kasubuga akagundua kuwa magari yale yalikuwa yakielekea Kibumba. Asingekuwa ameamriwa na Col. Rwivanga awasubiri pale mpakani hakika Meja Kasubuga angeyafuata magari yaliyoondoka na kikosi kile. Baada ya kufika mpakani, jeshi la Meja Kasubuga lilifanikiwa kukitwaa kikosi cha jeshi la Zaire kilichokuwa kikiwasaida wanajeshi la Intarahamwe na hii ikawa ngome ya jeshi lake kwa muda.

Kikosi hiki kilichokuwa mpakani mwa Zaire na Rwanda kilikuwa kimejijenga vizuri kivita, kikiwasaidia wanajeshi wa Intarahamwe na kundi la Akazu lililokuwa likifanya jitihada ya kuivamia serikali ya RPF ili kutwaa madaraka ya kuiongoza Rwanda kijeshi.

Baada ya kuhakikisha usalama wa eneo hili, Meja Kasubuga alielekea sehemu iliyoandaliwa, ambayo Col. Rwivanga alimweleza kuwa angetua hapo kwa Helikopta akiwa na kiongozi wa kikundi cha Banyamulenge na kiongozi wa vikosi vya vyama vinavyoipinga serikali ya Zaire. Meja Kasubuga alipoangalia saa yake ilikuwa saa nane na dakika kumi. Muda ambao Col. Rwivanga aliahidi kuwa atafika Gisenyi. Hivyo, Meja Kasubuga na kikosi chake wakaamua kusubiri.

Col. Rwivanga alikuwa na matumaini makubwa na kikosi cha Meja Kasubuga, hivyo baada ya kuondoka Kigali kwa Helikopta ya jeshi, walisafiri moja kwa moja usiku huo kuelekea Gisenyi. Col. Rwivanga hakuwa na papala wakati wote alikuwa akitafakari jambo kabla ya kulifanyia kazi. Alikuwa mmoja wa maofisa wa jeshi walioheshimiwa na kutegemewa sana na serikali ya Rwanda. Alikuwa mtu mwadilifu asiyependa kuisalti nchi yake, kutokana na msimamo wake dhabiti aliogopwa sana na vibaraka hususan wanaotaka kuigawa Afrika.


Alikuwa akijitosheleza kiulinzi, kutokana na hali hiyo nyumba yake haikuwekewa ulinzi kutoka jeshini, kama ilivyo kwa maofisa wengine wa ngazi za juu kama yeye. Alikuwa mmoja wa makomandoo wa jeshi waliofuzu vizuri mafunzo yake, lakini kutokana na cheo chake jeshini alibaki kuwa ofisa wa jeshi aliyeheshimiwa sana. Alikuwa mpole asiyependa makuu, alikuwa na subira, hata ukimchoma kidole machoni hatakufanya kitu. Lakini akilazimika kuchukuzwa na upuuzi alifanya kitu ambacho hakuna awezaye kuamini, hakuwa na mchezo tena. Huyo ndiye Col. Thomas Rwivanga, Afisa wa jeshi mwandamizi.

ITAENDELEA 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU