TUTARUDI NA ROHO ZETU?



Nchi zilizo msitari wa mbele katika Ukombozi Kusini mwa Afrika zimetendewa mambo mengi maovu na Utawala dhalimu wa Makaburu... Hata hivyo halikupata kutokea tishio zito la kutisha kama hili, ambalo linakaribia kutokea. Tukio la kutatanisha ambalo linawatoa machozi wananchi wa nchi mbalimbali za kiafrika. Wanajitokeza mashujaa na kwenda Afrika Kusini, ili kulikabiri tishio hilo lakini kila aendaye huko harudi na roho yake.

Inspekta Kombora nchini Tanzania jasho linamtoka. Anawatambua na kuwakumbuka mashujaa wengi lakini anamtambua shujaa mmoja. Joram Kiango. Jambo la kusikitisha ni kwamba sasa hivi Joram Kiango ni mtumiaji mzuri ambaye sasa anatembea kutoka jiji moja hadi lingine akiwa na yule msichana wake mzuri Nuru kwa ajili ya kustarehe. Juhudi za Kombora kumsihi Joram arejee kazini hazifui dafu. Badala yake Joram anafanya maajabu mengine ambayo yanalichafua jina lake hapa nchini Tanzania na kote duniani. Wakati huo siku ambayo utawala wa makaburu umeweka ili kuachia pigo lao la mwisho inazidi kukaribia. Sasa yamebaki masaa...
**********************************************************

HADITHI HII INAWAJIA KUFUATIA MAOMBI YA WASOMAJI WENGI WA BLOG YA MPIGANAJI, TUMELAZIMIKA KUWALETEA HADITHI HII KUTOKA KATIKA KITABU CHA 'TUTARUDI NA ROHO ZETU' KITABU KILICHOANDIKWA NA MTUNZI WA RIWAYA ZA KUSISIMUA ZA UPELEELZI, BEN R. MTOBWA. BAADA YA KUANDIKA KITABU HII BEN R. MTOBWA ALITOA KIDOKEZO KUWA 'IWE ZAWADI YAKE KWA KILA MWANAMAPINDUZI WA AFRIKA'. SASA ENDELEA.
*********************************************************

SURA YA KWANZA

Kama maji ya Bahari ya Hindi yangekuwa na hisia, basi yangejisikia fahari sana kupata fursa nyingine ya kuburudisha miili ya viumbe hawa wawili ambao walikuwa wakiogelea kando ya ufuko huu wakicheza na kucheka. Walifanya picha ya kuvutia sana hususan sura zao zuri zilipoibuka kutoka majini na kumezwa na tabasamu ambalo lilisababishwa na mizaha waliyokuwa wakifanyiana chini ya maji. Baada ya kuogelea kwa muda mrefu walirejea nchi kavu ambako walijitosa juu ya mchanga na kuruhusu joto likaushe maji miili yao. Ufuko pia ungekuwa na kila sababu ya kusherehekea fahari ya kulaliwa na viumbe kama hawa. Kwani walioana kimaumbile kama pacha, ilihali hawakuwa mtu na dada yake.

Walikuwa kama pea ya kiatu cha kiume kwa cha kike. Mwanamume hakuwa mwingine zaidi ya yule kijana mwenye umbo refu, mkakamavu, aliyekaa kiriadhariadha na sura nzuri, yenye dalili zote za hekima, ushujaa na ucheshi. Kwa jina anaitwa Joram Kiango.

Naye msichana alibahatika kupewa umbo lenye kila kitu ambacho msichana anahitajika kuwa nacho, wakati huohuo akiwa na kila ambacho mvulana legelege asingekuwa nacho, ni yule ambaye akutazamapo ungependa aendelee kukutazama, achekapo utafarijika, atembeapo unaburudika. Yule ambaye kuna madai kwamba alikuja duniani kwa makosa baada ya kuumbwa ili awe Malaika. Madai ambayo kama si ya kweli basi yako mbali sana na uongo. Hata jina lake halikutofautiana sana na sura yake. Wanamwita Nuru.

Baada ya kuhakikisha kuwa miili yao ilikuwa imekauka, walijifuta vizuri kisha wakazichukua taulo zao na kuondoka wakaifuata gari yao. Macho ya watu wengi, waswahili kwa watalii ambao walikuwa katika ufuko huo, hayakukoma kuwafuata. Kutazamwatazamwa, hasa wanapokuwa pamoja halikuwa jambo geni tena kwao. Mara kwa mara macho ya kiume yalikuwa ya yakimwandama Nuru huku macho ya kike yakimfuata Joram kila mahali walipopita. Walijifunza kuzoea hata wakaanza kusahau kuwa wanatazamwa. Hivyo, walipolifikia gari lao waliingia, Joram akalitia moto wakaondoka kwa mwendo usio wa haraka.

Hawakuwa na sababu yoyote ya kufanya haraka. Ratiba yao ya starehe ilikuwa ikielekea kwisha mapema zaidi ya walivyokusudia. Walikuwa wamekubaliana wakae katika miji yote mashuhuri hapa nchini kwa muda wa wiki nzima kwa kila mji. Lakini hii ilikuwa wiki ya pili tu na tayari walikuwa wameishi Zanzibar, Moshi, Arusha, Dodoma, Mwanza na kujikuta wamerejea Dar es Salaam. Kila mji waliuona unakinaisha baada ya siku mbili tu. Maisha ya mahotelini waliona yanawafaa watu wavivu, nazo mbuga za wanyama ziliwasisimua watalii, ilihali miji iliwaridhisha wenyeji, na safari za hapa na pale zilikinaisha.

Hivyo ingawa walirejea Dar es Salaam na kuendelea na starehe zao wakiishi katika hoteli ya Kilimanjaro, ingawa waliendelea kucheza na kucheka, ingawa hakuna aliyetamka neno lakini bado haikuwa siri tena kuwa maisha ya Kula, kulala...kula, tena, kulala tena", yalikuwa yameanza kuwachosha. Maisha hayo yalikuwa yameanza usiku ule ambao Joram Kiango asingeweza kusahau. Usiku hadi leo bado unamtia maumivu moyoni, kila anapokumbuka alivyozulumiwa haki na wajibu wake wa kuitia risasi katika kichwa cha Proper, yule katili ambaye pamoja na kuwaangamiza watu wengi ambao hawakuwa na hatia, alikuwa amemuua Neema Iddi kinyama. Ni siku hiyo ambayo Joram alitupa bastola yake na kuamua kuishi kivivu kama wanavyoishi watu wengine. Msichana huyu Nuru alikuwa amehusika sana katika mkasa huo ambao tayari mtu alikuwa ameuandikia kitabu na kukiita Salamu Toka Kuzimu. Kamwe Nuru alishindwa kuachana na Joram na asingeweza kusitahimili kumwona Joram akiteseka na msiba huo peke yake. Alimfuata na kumsihi hata kulipopambazuka wakajikuta wako pamoja juu ya kitanda kimoja.

Tangu hapo hawakuachana, Joram hakuwa mtu aliyeweza kuachwa kirahisi. Naye Nuru kadhalika alitofautiana sana na wale wanawake wazuri ambazo uzuri wao ni pindi wanapokuwa wamevaa nguo tu. Alikuwa na mengi ambayo alikuwa ameyatenda kwa nia moja tu - ya kumfariji Joram, naye Joram alijikuta akianza kujisamehe. Lakini asingeweza kusahau......

**********************************************************

Walipowasili chumbani katika hoteli ya Kilimanjaro, walijipumzisha vitandani mwao kwa muda huku wakilainisha koo zao kwa viwanyaji vitamu. Kisha walifuatana bafuni na kuyaondoa maji ya chumvi miilini mwao kwa kuoga vizuri kwa sabuni. Baada ya hapo waliekea kwenye chumba cha maakuli ambapo walikula na kujiburudisha kwa vinywaji vikali na maongezi laini.

Joram akiwa katika vazi lililomkaa vema, suti ya kijivu iliyooana na viatu vyeusi kama kawaida, alikuwa tishio kubwa kwa wanaume waliokuja na wasichana wao. Hata hivyo, walijifariji kwa kujua kuwa asingekuwa mwendawazimu wa kuvutwa na yeyote kwani aliyeketi nae hakuwa msichana wa kawaida.

"Kwanini wanaishi hapa bongo watu kama wale", mtu mmoja alimunong'oneza jirani yake.
"Tazama wanavyopendeza, wangeweza kwenda zao nje na kutajirika sana endapo wangecheza mchezo mmoja tu wa sinema", alidakia mwingine.

"Kweli kabisa", aliungwa mkono. "Hata maumbile yao yanafikiana. Yule dada anatosha kabisa kumtia mwanaume yeyote wazimu kiasi cha kumfanya auze hata nyumba yake.

Maongezi hayo hayakumfikia Joram wala Nuru. Lakini alikwisha zoea kuyasoma katika macho ya watazamaji wao. Hivyo, alitabasamu kidogo na kuagiza kinywaji kingine. Nuru alikuwa akiongea neno. Joram aliitika bila kumsikia. Waliendelea kunywa kwa muda hadi walipoamua kuwa wametosha ndipo walipofuatana katika ukumbi wa muziki ambapo walisikiliza muziki na kucheza kwa masaa kadhaa. Walipokinai walikiendea chumba chao ambacho kiliwalaki na kuwapa usiri. Katika usiri huo, kwa mara nyingine miili yao iliburudika na kusherehekea afya zao.

Kesho yake baada ya kufungua kinywa walitazamana katika hali ya kuulizana waitumie vipi siku hiyo. Nuru aliweza kuzisoma dalili za kuzikinai ratiba zao ambazo zilikuwemo katika macho ya Joram. Ingawa walikuwa wakistarehe na kujiburudisha furaha ilikuwa dhahiri kuwa burudani hizo zilikuwa zikiuburudisha mwili wa Joram kamwe hazikuwa zikiburudisha akili yake. Ingawa uso wake ulikuwa ukitabasamu mara kwa mara, roho yake ilikuwa ikiwaka kwa hasira kali dhidi ya adui zake. adui wa taifa na maendeleo ya jamii. Adui ambao walikuwa wamefanya maovu mengi yasiyokadilika na kumtia lile donda la rohoni kwa kumuua kikatili msiri wake mkuu Neema. Nuru kwa dhamila ya kumsahaurisha Joram na uchungu huo ndipo akajitoa kwake mwili na roho. Lakini ilikuwa dhahili kuwa jeraha hilo lilikuwa bichi katika roho ya Joram, na lisingepona kabisa isipokuwa kwa dawa moja tu kulipiza kisasi. Hayo alikuwa akiyaona wazi katika macho ya Joram ingawa alijisingizia kufurahia starehe zao. Iko siku Nuru aliwahi kumwambia. "Sikia Joram. Huonekani kufurahia lolote tunalofanya. Kwani usirudie ofisi yako na kuendeleza harakati zako, nitakuwa kama alivyokuwa Neema. Nitakusaidia kwa hali na mali. Joram alicheka na kumjibu Nuru. "Mara ngapi nikwambie kuwa nimeacha shughuli hizo. Nitaendelea kustarehe hadi nitakapoishiwa senti yangu ya mwisho. Ndipo nitakapotafuta kazi na kuifanya kwa utulivu kama vijana wenzangu".

"Kwanini lakini, kifo cha msichana mmoja tu kinakufanya usahau wajibu wako".

"Sivyo Nuru. Isieleweke kuwa nimechukia kwa kufiwa na Neema. Yeye ni mmoja tu kati ya wasichana wanaouawa kwa dhuluma na ukatili aina kwa aina ulioko duniani. Ni mmoja tu kati ya maelfu ya vijana wanaoteseka kwa shida ambazo wanazipata kwa makosa ya watu wengine. Ni mmoja tu kati ya mamilioni ya binadamu wanaoumia kwa umasikini ambao hawakuomba na dhiki ambazo hazina umuhimu wowote".

"Sidhani kama nimekuelewa Joram, unazungumza kama mshairi".

"Labda. Ninachotaka kusema ni kwamba bastola yangu haitoshi kukomesha maovu yote yanayotendeka hapa duniani. Kote Afrika na duniani binadamu hawako sawa kiuchumi. Wako wanaoshinda njaa na kuna wanaomwaga chakula. Kama kweli nakusudia kuondoa dhuluma na ukatili kwa nchi dhidi ya nchi nyingine, basi sina budi kuukomesha pia ukatili dhidi ya mwingine. Maadamu hayo yako nje ya uwezo wangu naona sina budi kusahau yaliyopita na kuanza kula na kunywa kama vijana wenzangu".

"Hasira hizo Joram. Upende usipende ukweli ni huo huo. bastola yako haiwezi kuwaelekea viongizi wazembe na wenye choyo ambao wanasababisha hali ngumu kwa wananchi. Lakini inawajibika kuwakomoa maadui ambao dhamila yao ni kuhakikisha hatulifikii lengo letu la kujenga taifa ambalo rais wake wanafaidi matunda ya uhuru wao. Unafahamu fika kuwa wanatunyima nafasi ya kufanya hayo"... Maongezi hayo yalikuwa yamefanyika siku chache zilizopita. Nuru alikuwa ameyakumbuka tena leo baada ya kuziona dalili za kukinai katika macho ya Joram. Alijua na kuamini kama wanavyoamini watu wote wanaomfahamu Joram kuwa starehe yake kuu ni pindi anapopambana na adui na burudani yake ni hapo anapowashinda. Vinginevyo Joram alikuwa akijisingizia starehe.

"Leo wapi mpenzi", Nuru aliona amchokoze Joram.

"Leo najisikia kulala tu".

"Kulala mchana, tangu lini umeanza tabia hiyo ya kulala mchana".

"Tangu nilipoacha kuwa Joram Kiango na kuwa kijana mtumiaji anaitwa Joram Kiango".

"Nilijuwa utachoka Joram. Kwanini usirudi ofisini na kuanzia leo?".

"Sikia Nuru. Usianzishe tena ubishi ambao siupendi. Kweli nitakuwa hapa nikiendelea kutumia tu na si vinginevyo".

"Sidhani kama unasema ukweli. Huonekani mtu wa kustarehe maishani". Joram hakumjibu. Alijilaza kitandani na kujisomea gazeti. kisha jirani yao chumba cha pili aliingia akiwa katokwa na macho. Hakujali kupiga hodi. Wala macho yake hayakuvutwa kuhusudu uzuri wa Nuru kama ilivyokuwa kawaida yake. badala yake alimwendea Joram kitandani akasema, "Hujasikia, Samora Machel amefariki, ndege yake imeanguka huko Afrika Kusini".

"Amekufa", Nuru alidakia na kuuliza kwa mshangao.

"Amekufa, na hii siyo bure. Iko namna haiwezi kuwa ajali ya kawaida".

"Afrika Kusini, alienda kufanya nini huko", Joram aliuliza kwa utulivu. Hata hivyo macho yake yalikuwa yakiwaka kwa hasira, ingawa hakupenda kujidhihilisha wazi kwa Nuru.

"Siku hizi hata taaifa za habari husikilizi Joram?", Nuru alimuuliza.

"Samora hakwenda Afrika Kusini. Alikuwa akitokea nchini Zambia ambako alikutana na rais Mobutu Seseseko wa Zaire na Waziri Mkuu wa Zimbabwe, Robert Mugabe kutafuta suruhisho na mbinu za kuiwekea Afrika Kusini vikwazo zaidi vya uchumi".

"Wanasema chanzo cha ajali hakijapatikana. Bila shaka watakuwa waliosababisha ajali hiyo kwa njia moja ama nyingie", alisema kwa masikitiko.

"Nadhani wamezoea kutuangamiza wapendavyo. Kwao sisi ni sawa na vifaranga wanaofugwa. Yeyote ambaye hawampendi wanamponda kwa urahisi. Jambo la kusikitisha ni kwamba sisi hatuwezi kufanya lolote baya dhahiri ni kwamba tutaendelea kuuawa mpaka lini. Kwanza walimuua Mondalane. Sasa wamemuua mrithi wake Samora na siyo hao tu. Viongozi wengi wa Afrika wamekuwa kama mifugo yao. Tunaorodha ndefu ya viongozi wetu wanaouawa ama kupinduliwa kwa matakwa yao. Tutaendelea kuvumilia mpaka lini", Nuru alikuwa akizungumza kama peke yake. Lakini macho yake yalikuwa yakimtazama Joram. Alitamani aone kitu katika macho yake. Hakukiona. Jambo ambalo lilimfanya ainame chini na kuruhusu matone kadhaa ya machozi yamdondoke. Yalikuwa machozi ya hasira zaidi ya hudhuni.

***********************************************************

Kifo hiki cha kijana shujaa aliyeheshimiwa kote dunia, aliyependwa na wapenzi wake na kuogopwa na adui zake, kilifuatiwa na minong'ono mingi kote dunia. Watu walisema hili na lile, wakipingana na kuafikiana.

"Walimuua au...".

"Bila shaka".

..."Njama za Afrika Kusini".

"Na vibaraka vyao".

Siku chache baadae maongezi yalibadilika.

"Umesikia Makaburu wanadai kuwa wataendelea kuwaadhibu viongozi na wananchi wa nchi zote za mstari wa mbele ambao wanajifanya vichwa ngumu?".

"kweli?, washenzi sana wale. Wanaweza kufanya lolote".

Na baada ya siku chache mambo yakaanza kutokea. Magazeti na vyombo mbalimbali vya habari duniani viliandika habari za kusikitisha.

Watu mia nne wamefariki dunia, mia tisa kujeruhiwa vibaya na wengine maelfu kuponea chupuchupu kufuatia ajali isiyokuwa ya kawaida iliyotokea katika jiji la Lagos Nigeria. Watu hao walikuwa katika uwanja wa mpira wakati wa mchezo kati ya timu ya taifa ya nchi hiyo na Zaire. Dakika chache kabla ya mchezo huo kwisha, moto mkali umelipuka na kubomoa uwanja na kusababisha maafa hayo. Wachunguzi wa mambo wanahisi kuwa huenda utawala wa Afrika Kusini unahusika.

Kabla watu hawajasahau habari hiyo, ilifuatia taarifa nyingine ya kutisha vilevile.

Harare, Zimbabwe
Maghala manane ya serikali yaliyokuwa yakihifadhi chakula yameungua moto kwa pamoja. Chanzo cha moto huo hakijajulikana. Jambo la kushangaza ni jinsi maghala hayo yalivyoungua kwa pamoja wakati yako katika wilaya mbalimbali za nchi hiyo. Kuna mashaka kuwa tukio hili kwa njia moja ama nyingine linahusiana na maafa ya Nigeria.

Na baada ya siku chache

Dar es Salaam, Tanzania
Katika matukio ya kutisha na kushangaza yanayoendelea kutokea katika nchi zenye msimamo wa kimapinduzi za Afrika leo asubuhi, Tanzania imepata pigo kubwa la kusikitisha. Jengo la Benki kuu ambalo lilikuwa likikamilisha marekebisho baada ya ule moto wa awali limeungua tena. Safari hii haielekei kuwa kutakuwa na matengenezo yoyote yanayoweza kulilekebisha zaidi ya kujengwa upya. Chanzo cha mto huo hakijafahamika.

Habari hizi zilitisha Afrika na kuishangaza dunia. Kila mtu aliyezisikia radioni na kuzisoma magazetini alishangazwa na matukio haya ambayo mfano wake haukupata kutokea katika historia ya Afrika na dunia.

Ajali ni jambo la kawaida. Kadhalika kuna watu wanaoamini kuwa kuna kitu kinachoitwa mkosi, na bahati mbaya, lakini mikosi mingi kiasi hiki na bahati mbaya kuziandama nchi chache za Afrika zenye msimamo mmoja katika suala la ukombozi ni jambo ambalo lilisababisha nyongeza katika fikra za wasomaji na wasikilizaji wa vyombo vya habari. Kitu kinachoitwa roho mbaya, kilipenya katika fikra hizo, ingawa hakukuwa na hakika katika mawazo hayo. Baadhi hata waliwahi kutamka hadharani kuwa kuna mkono wa mtu katika matukio hayo. Mawazo hayo yalifuatiwa na hofu katika mioyo ya wananchi na serikali zao walipojiuliza. Kipi kingefuata, "Joram, tutakaa kimya kusubiri maafa zaidi", Nuru alikuwa akimuuliza Joram baada ya kusoma habari za tukio la benki kuu katika gazeti. Alikuwa amejitahidi kustahamili kutosema lolote aliposoma matukio ya Lagos na Harare. Lakini hili la nyumbani lilimgusa zaidi Nuru. "Aibu iliyoje", aliendelea Nuru. Tuendelee kustarehe kwa vinywaji na muziki huku tukisubiri maafa mengine yatatokea, haiwezekani Joram. Lazima tufanye jambo".

Ndio habari hizo hazikuwa zimempendeza Joram. Hata hivyo alikuwa amezisoma kama raia wengine bila kudhihilisha dalili yoyote ya nia ya kufanya lolote kama alivyokuwa awali. Jambo ambalo lilimfanya Nuru atokwe na machozi.

"Serikali inao polisi na wapelelezi wake, ambao inawalipa pesa nyingi", Joram alisema. "Mimi ambae nimeacha shughuli hizo nitasaidia nini?".

"Huwezi kusema hivyo Joram. Siamini kama moyo wako wa uzalendo umedidimia kiasi hicho".

"Haujadidimia, uko palepale kama ilivyo mioyo ya wazalendo wengine".

"Lakini wewe si mzalendo wa kawaida Joram. Taifa linakuthamini na kukutegemea. Huwezi kulisalti kiasi hicho bila sababu ya kuridhisha.  Lazima ufanye jambo.

"Ndio. Nitafanya jambo. Nitastarehe na kuendelea kustarehe kama wanavyofanya vijana wenzangu. "Njoo kitandani Nuru. Tafadhali. Njoo tustarehe acha wenye shibe waendelee kulinda shibe yao. Wewe na mimi tuna nini katika nchi hii".

"Joram...".

"Nuru njoo tafadhali. Na kama umenichoka sema nimtafute Nuru mwingine ambaye hachoshwi na starehe. Nuru angependa kukataa. Lakini asingeweza. Akamfuata Joram kitandani na akajilaza kando yake kitandani huku machozi yakimtoka kama kondoo anayesubiri kuchunwa.

**********************************************************

ITAENDELEA 0784296253

Comments

Post a Comment

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU