SURA YA KUMI
III
Wakiwa
angani ndani ya Helikopta, Nuru aliweza kuona vizuri baadhi ya maiti za
makachero wa makaburu waliouawa huku wakiwa wamevalia sare pamoja na silaha zao
mikononi. Walikuwa wamelazwa sakafuni mbele ya lango kubwa la kuingia katika
mojawapo ya vyumba ndani ya jingo hilo lililozungukwa na ua wa seng'enge.
Halikopta ililizunguka jumba hilo mara tatu. Von alikuwa akitumia darubuni
kuona huku na huko. Aliporidhika na hali ya usalama, alimwamru rubani wa
Helikopta hiyo kutua kando ya ua huo karibu na kichaka mahali ambapo mtambo huo
ulikuwa kando ya mji.
Ilikuwa
safari ya dakika mbili tatu tu, kutoka mjini hadi kufika kwenye mtambo huo.
kabla ya kuanza safari hiyo Von alikuwa ametupiana maneno yasiyofaa na msaidizi
wake ambaye alikuwa ameshangazwa na maamzi ya Von kuambatana na Nuru ndani ya
Helikopta.
"Sikubaliani
kabisa na uamzi huo. Nadhani ni wewe ndiye uliyetunga sheria hizi, kumpiga
risasi mtu yeyote atakayeonekana akiusogelea mtambo ule, awe raia wa nchi hii
ama mgeni. Vipi leo aende huyu mhalifu ambaye bado tunawatuhumu yeye pamoja na
mwenzake ambaye yawezekana kuwa yuko huko akifanya mauaji ya siri kwa makachero
wetu".
"Huyu
ni mateka wangu", Von alimjibu. "Bado nina mengi ya kumsaili. Zaidi
ya hayo kama kweli Joram yuko huko tutamtumia huyu kumfanya Joram asithubutu
kuendelea na chochote anachowaza kichwani mwake", Von alitetea msimamo
wake.
"Bado
sikubali", Msaidizi huyo alisimamia hoja yake. "Nimeandaa kikosi cha
askari wanne ambao ulipaswa kufuatana nao huko. Kadhalika nilikuwa nikisubiri amri
yako ili nitume askari wengine zaidi ya hamsini kwa njia ya magari. Inaonekana yote ninayofanya
ni kazi bure".
"Ni
bure kabisa", Von alimjibu. "Unajua kabisa kuwa mtambo ule unalindwa
katika hali isiyo na shaka kabisa. Hata kama mtu atafanikiwa kuingia ndani hawezi
kabisa kufanya uhalibifu wa aina yoyote. Pamoja na juhudi zake zote bado
ataambulia kufa tu. Hivyo nakushauri urudi na hao askari wako uliowaandaa.
Nitakwenda mimi, huyu mateka na rubani tu. Sawa", Von alieleza kwa
msisitizo.
Msaidizi
huyo alimtazama Von kwa hasira na mshangao. Von hakuwa na kawaida hiyo. Alikuwa
amezithamini sana hekima zake hususan katika masuala yote ya kiusalama katika
nchi hii kwa kipindi chote, miaka yote walipokuwa wakifanya kazi ya kuilinda
nchi yao. Lakini vitendo vyake masaa machache yaliyopita vilimchanganya kabisa.
Vilikuwa vitendo ambavyo havikubaliki. Yeye kama mtu wa pili katika suala zima
la usalama wa utawala huo hakuona kama kuna sababu ya kumtii Von hata kwa hilo.
Hivyo alimtupia jicho la hasira na kumwambia, "Kwa mara ya kwanza
nitafanya kinyume cha matakwa yako".
"Na kwa
mara ya kwanza nakwambia kuwa... kuwa... Hufai kufanya kazi chini yangu. Baada
ya suala hili nitaangalia suala lako", Von alisema huku akimsukumiza Nuru
ndani ya Helikopta akamwamru rubani kuondoka haraka.
Hata hivyo
moyoni Von alikuwa na mashaka kuhusu maamzi yake hayo. Alijua kabisa kuwa
alikuwa akifanya kosa kubwa sana kufuatana na Nuru huko aendako. Lakini pia
aliamini kuwa hiyo ilikuwa nafasi yake ya pekee kufanya mapenzi na msichana
huyo na kisha amuue. Ndani ya jumba hilo la mitambo kulikuwa na vyumba kadhaa
kikiwepo chumba maalumu kwa ajili ya faragha za wakubwa tu. Chumba hicho
kilikuwa na mtambo wa televisheni inayotumia nguvu ya setilaiti iliyoko angani
inayotumika kuitazama miji mbalimbali ya Afrika kwa umakini mkubwa. Vilevile
kulikuwa na chombo maalumu ambacho kiliwawezesha makaburu kutazama shughuli zote
zinazofanyika katika kila chumba ndani ya jumba hilo.
Ilikuwa
kawaida kwa Von kujifungia ndani ya chumba hicho mara kwa mara kwa ajili ya
kutazama utendaji kazi wa mitambo hiyo na jinsi wahandisi wanavyofanya kazi
bila wao kujua. Mhandisi mmoja katika jumba hilo aliwahi kupoteza kazi na uhai
wake baada ya kushukiwa na Von kuwa alikuwa na dhamila mbaya ya kuhujumu mtambo
huo. Hata hivyo kifo cha mhandisi huyo machoni mwa watu ilionekana kama ajali
iliyosababishwa na dereva aliyelewa na kumgonga mtu aliyekuwa akitembea kando
ya barabara katikati ya mitaa ya Johannesburg. Leo Von alikusudia kukitumia
chumba hicho kujistarehesha na mwili wa Nuru kabla ya kutulia na kuanza
kuangalia kwa furaha watu wanavyoteketea kwa moto katika miji ya Dar es Salaam,
Lagos, Lusaka, Harare na kwingineko.
Furaha
iliyokuwa ikichemka katika fikra za Von iliingia nyongo baada ya Helikopta yake
kupita juu ya jengo hilo na kushuhudia jinsi walinzi wa eneo hilo walivyolala
hovyo wakiwa maiti baada ya kuuawa. Kutokana na hali hiyo, Von aliingiwa na
hofu, akamtupia Nuru jicho la chuki. Tamaa aliyokuwanayo dhidi ya Nuru ikaanza
kuyeyuka taratibu na nafasi yake kuchukuliwa na hasira kali. Von alitamani
ammalize Nuru papo hapo ili kusahau yote aliyokuwa akihitaji kwake. Wazo
jingine likamjia akilini kuwa. Kwa vile Nuru anaonekana katili sana asiyeogopa
kifo kama walivyo wanawake wengine anaowafahamu. Hata hivyo Von akajipa moyo
kuwa Nuru anaweza kufa baada ya kutaabika sana. Akaamini kuwa hakuna mateso
yatakayomtaabisha zaidi ya kushuhudia kifo cha mpenzi wake Joram Kiango. Von akiwa na uhakika asilimia mia kuwa Joram
alikuwa mahali fulani katika jengo hilo akilia na kusubiri kifo, Von alitoa
bastola yake na kuigongagonga kwenye kisogo cha Nuru. Baada ya Helikopta kutua,
Von alimwamru Nuru.
"Twende",
Von alisema kwa hasira mara baada ya kushuka kutoka ndani ya Helikopta huku
akimwamru rubani awe makini wakati akimsubiri.
Nuru
alitelemka na kufuata maelekezo ya Von. Kila walikopita kulikuwa na miili
kadhaa ya marehemu waliouawa hovyo, baadhi wakitokwa na damu baada ya
kujeruhiwa kwa risasi zilizoingia miilini mwao.
Kiasi fulani
ilimshangaza Von kuona jinsi mtu mmoja Joram Kiango peke yake alivyofanikiwa
kuwaangamiza askari wengi kiasi kile bila wao kujitetea. Lakini hali hiyo
haikumshangaza Nuru hata kidogo. Wala hakuhitaji kusimuliwa. Nuru akiwa mtu
anayemfahamu vizuri Joram na hila zake nyingi alijua kuwa Komando huyo alitumia
njia moja ama nyingine kuwafikia askari hao wa makaburu na kuwashikisha adabu
pamoja na kujiamnini kwa kuwa na silaha za kisasa na bunduki aina ya sub
machine gun.
Baada ya kufanya kazi yake ipasavyo Joram, akitoka kona moja
kwenda kona nyingine katika ngome ya adui, Joram alifanikiwa kutoa hati zake za
bandia na kuwaonyesha askari wa makaburu. Hati ambazo zilifungwa kwa namna
fulani kiasi cha kuhifadhi hewa ya sumu ambayo bila shaka iliwafanya askari wa
makaburu kulewa ghafla. Hivyo akawa na nafasi nzuri ya kuwaua mmoja baada ya
mwingine bila kutumia silaha nzito.
Kilichomshangaza
Nuru ni kutokufahamu Joram alikuwa wapi na akifanya nini muda wote huo tana
katika eneo la hatari kama hilo. Nuru alikuwa amekadilia kuwa dakika tano
zingetosha kabisa kuuteketeza mtambo huo na kutoweka. Na kwa mjibu wa ramani
yao ndani ya jumba hilo hakukuwa na ulinzi wowote zaidi. Nuru akajiuliza vipi
Joram asitokee na kummalizia Von. Mtu mnene, ambaye hakuwa na uwezo wowote wa
kupambana na Joram. Nuru akaamini kuwa
ndoto yao unakaribia kuwa kweli, akamuomba Mungu moyoni mwake ili wamalize kazi
na kuondoka kurudi Tanzania.
Von hakumpa
Nuru nafasi ya kuwaza zaidi. Alikuwa akimsukumasukuma kwa mtutu wa bastola yake
haraka haraka. Nuru hakuwa mzito, mara moja alielewa kuwa Von alimtanguliza ili
amfanye kuwa ngao yake endapo lolote lingewatokea tofauti na mategemeo yake.
Baada ya Von kukagua baadhi ya vyumba vya jengo hilo, akiwa amemtanguliza Nuru
kama kawaida, walifika katika chumba maalumu ambacho Von na viongozi wengine hukitumia
kwa ajili ya mapumziko.
Ukiondoa
makochi na kabati lililojengwa ukutani, chumba hicho hakikutofautiana na
maabara au studio ya aina yake katika macho ya Nuru. Mashine na mitambo kadhaa
ilikuwa imepangwa kwa tafasiri fulani, kutani kukiwa na screen zilizopangwa
katika hali ya kupokea habari mbalimbali. Von aliiendea mashine moja ambayo
machoni mwa Nuru ilionekana kama komputa, akaanza kubonyeza swich aina kwa aina
mara kioo katika ukuta mmoja kilipata uhai na kuanza kuonyesha mambo ya ajabu.
Baada ya hali kutulia Nuru aliweza kuona teknolojia hiyo inavyofanya kazi,
waliweza kuona chumba baada ya kingine katika jengo hilo. Kupitia screen hiyo
kilionekana chumba kilichokuwa na mitambo ya aina mbalimbali ya kutisha.
Nuru
aliweza kuwaona wahandisi watatu waliokuwa makini wakifanyakazi ya kuongoza
mitambo hiyo huku wakiwa hawana dalili zozote kuwa mambo yalikuwa yakienda
mrama. Kitendo cha wahandisi hao kuwa makini na kazi yao kilimfurahisha sana
Von, akaangua kicheko cha furaha. Ni yeye aliyependekeza kuwa ishara ya hatari
kwa usalama wa mitambo hiyo zisiwafikie wahandisi hao wasije wakapatwa na hofu
na kusababisha setilaiti iliyoko angani kukosa mawasiliano kutoka ardhini,
jambo ambalo lingeweza kusababisha maafa na hasara isiyokadiliwa.
Kwa jinsi jengo
hilo lilivyoandaliwa Von alikuwa na hakika kabisa kuwa ingemhitaji binadamu
mwenye moyo wa malaika kuwafikia wahandisi hao na kufanikiwa kuuharibu mtambo
huo. Aliamini kuwa Joram hakuwa na moyo huo. Ni hilo tu lililokuwa likimtia
nguvu Von. Sasa akaamini kuwa hakuwa amekosea. Kwa muda aliwatazama tena
wahandisi hao wanavyowajibika. Wakiamini kuwa leo ilikuwa siku maalumu ya kazi
kubwa hivyo walifanyakazi zao kwa umakini na juhudi ya hali ya juu. Kisha Von
alibonyeza kuona sehemu nyingine. Chumba hicho kikahama na vyumba vingine
vikaanza kuonekana katika kioo.
"Nataka
umuone mpenzi wako atakavyokufa ama mahali alikofia", Von alimwambia Nuru
huku akimwelekezea tabasamu la kifedhuli lililoyasindikiza maneno yake,
"Keti tafadhali. Keti hapa ili uweze kuona kwa starehe jinsi Afrika
inavyoteketezwa kwa mioto ya ajabu".
ITAENDELEA
0784296253
Comments
Post a Comment