KIFO kaja
duniani kwa kazi moja tu. Akikukuta umekwisha... Akikusalimia umekwisha... Hana
mdhaha. Lakini sasa huyu anataka watu mashuhuri, watu wakubwa zaidi. Anataka
kuifanya Afrika nzima iangue kilio na maombolezo ambayo hayajapata kutokea
duniani. Na anataka hilo litokee siku moja, saa moja... "Bendera zote
duniani zipepee nusu mlingoti", anasema huku akichekelea. "Sijawahi
kushindwa..." Jasho linawatoka watu mashuhuri. Damu inamwagika kama
mchezo. Inspekta Kombora machozi yanamtoka. Joram Kiango anabaki kaduwaa.
SURA YA
KWANZA
"Bado
nasisitiza kuwa tusithubutu wala kujaribu kufanya lolote kabla ya kuhakikisha
kuwa Joram Kiango yu marehemu", ilidai sauti moja nzito.
"Naam,
lazima afe", sauti nyingine iliunga mkono. "Afe kabla hatujainua
mikono kufanya lolote tulilokusudia. Hakuna asiyefahamu jinsi kijana huyu
alivyo hatari anusaye shari na kuingilia kati kuharibu harakati zote.
Hajasahaulika alivyowakorofisha wale mashujaa waliotaka kuuangusha utawala wa
nchi ya Ngoko katika tukio lile lililoitwa Dimbwi la damu. Kadhalika bado
hatujasahau alivyosababisha vifo na kuharibu mipango ya majasusi waliotaka
kuiharibu nchi hii katika mkasa ambao mtu mmoja aliuandikia kitabu na kuuita
Najisikia kuua tena. Kwa kila hali Joram Kiango ni mtu hatari zaidi ya hatari
zote zinazoweza kutokea, Hana budi kufa".
Kicheko
kikavu kikasikika kidogo, kikafuatwa na sauti iliyokwaruza ikisema.
"Atakufa.
Lazima afe. Na atakufa kifo cha kisayansi kabisa. Mpango huu tumeuandaa kwa
uangalifu mkubwa, Na watekelezaji wake pia ni watu ambao wamehitimu vizuri
katika nyanja zote zinazohusika na kazi hii, Tuondoe shaka kabisa. Mpango huu
utafanikiwa kwa asilimia mia".
"Kwa
hiyo ndugu Mwemyekiti", ilisema sauti ya mtu wa kwanza. "Niwie radhi
kwa kukukata kauli. Ninachokuomba ni kuuahilisha mkutano huu na tusisubutu
kukutana tena hadi hapo Joram Kiango atakapokuwa kaburini, Pengine mtaniona
mwoga kupindukia, Lakni mimi sipedi kabisa kufanya jambo lolote wakati kijana
yule akiwa hai. Mnajua jinsi alivyo na miujiza. Anaweza kuwa hapa akisikiliza
mazungumzo yetu, kesho tukajikuta mahakamani bila kutegemea".
Ilizuka
minong'ono, sauti mbili tatu zilimuunga mkono msemaji aliyemaliza kusema. Jina
la Joram liliamsha hofu katika mioyo yao. Wakatazamana...
Walipenda
pia kumwona Mwenyekiti wao uso kwa uso. Kwa bahati mbaya, hawakuweza kuona uso
wake isipokuwa kiwiliwili tu, ambacho kilifunikwa kwa mavazi ya thamani kama
walivyokuwa wamevaa wao. Mwanga mkali uliotokana na taa ya umeme iliyowekwa kwa
namna iliwachoma macho kila walipotamani kumtazama Mwenyekiti usoni. Ni yeye tu
aliyekuwa na nafasi nzuri ya kuwatazama wote mmoja baada ya mwinginge
kikamilifu na kuwasoma nyuso zao. Wakati wa kumtambua Mwenyekiti ulikuwa bado
haujawadia hivyo hawakupaswa kumuona kabisa isipokuwa sauti yake tu.
Mkutano huo
ulifanyika katika chumba cha siri, chini ya ardhi katika mojawapo ya majumba ya
kifahari yaliyoko Jijini Dar es salaam.
Kila aina ya
tahadhari iliwekwa kuhakikisha usalama wa mkutano huu wa awali. Mkutano ambao
ulikuwa umeitishwa ghafla, kwa njia za kutatanisha, hata wajumbe hao walijikuta
wamefika kwenye mkutano bila kufahamu kilichowaleta hapo.
Mwenyekiti
akaufungua mkutano huo kwa maneno machache akisema: "Tunataka kuitetemesha
Afrika na kuishangaza dunia. Tunataka kuachia pigo ambalo halitafutika katika
historia ya Ulimwengu". Wajumbe wakaelewa kinachoendelea. Ndipo mjume
mmoja alipotoa rai ya kumaliza kikao hadi watakaposikia Joram Kiango amekuwa
marehemu.
Tahadhari
kubwa ilikuwa imechukuliwa wakati wa kuandaa mkutano huo. Wajumbe waliingia kwa
siri kubwa wakipita milango tofauti, katika eneo hilo vilitegwa vifaa vya
kisasa kwa ajili ya kuhakikisha kila mshiriki wa mkutano huo wa siri anahusika
kwa njia moja ama nyingine. Walihakikisha pia hakuna kifaa au chombo chochote
cha kunasa sauti ama kusikiliza maongezi hayo ya siri. Vinginevyo chumba hicho
kingeweza kutoweka kisayansi kisionekane mlango wowote zaidi ya kuta za
kawaida. Zaidi ya yote silaha za kisasa, hewa za sumu, buduki zisizotoa mlio,
madawa ya kulevya na mbinu zingine zilikuwa tayari kutumika endapo lolote
lingetokea. Kwa bahati mbaya, ni Mwenyekiti peke yake ndiye aliyejua mpango
mzima kuhusu mkanda huo.
Kulikuwa na
kila sababu ya kuweka tahadhari au uangalifu huo. Watu waliokutana katika
mkutano huu hawakuwa watu wenye njaa ya pesa wala kiu ya utajiri. Ni watu
mashuhuri walioshiba na kudhamiria kulinda shibe yao. Wote walikuwa na hadhi
mitaani, nyadhifa serikalini, na heshima katika chama. Waliokutana hapa wote
walikuwa na matarajio ya kuvuna matunda matamu. Matunda ambayo yangetokana na
mkutano huo. Hakuna mjumbe aliyependa kukosa utamu wa matunda hayo. Hivyo wote
walikuwa na dhamira moja.
"Inaonyesha
kuwa Joram ni tishio kwa kila mtu hapa", Sauti nzito ya Mwenyekiti
ilisema. "Hilo linanifanya nizidi kuwa na imani juu ya dhamira yenu. Joram
anaogopwa kuliko Polisi na jeshi zima la nchi hii, Kwanini? Wanajeshi mko hapa,
polisi mko hapa, Chama tawala kiko hapa. Serikali iko hapa. Anayekosekana hapa
ni mtu huyo anayejiita Joram Kiango. Mtu mtundu sana, ambaye utundu wake ni
madhara kwa watu wenye dhamira maalumu. Hakuna atakayeshuku kuwa kauawa.
Daktari atampima na kuona kafa kwa kansa ya moyo. Atauawa kitaalamu na kufa
kistaarabu. Msiwe na shaka".
Kimya kifupi
kikafuata. Wajumbe wakatazamana usoni. Kimya kilimezwa na sauti ya Mwenyekiti
alipoongeza maneno.
"Kwa
hiyo, naahirisha kikao hiki kama alivyoshauri mjumbe. Tutakutana tena hapa
baada ya wiki mbili, siku na saa kama za leo, kwa njia zetu zile zile, bila
kusahau kuwa joram Kiango hatakuwa Joram tena ila hayati Joram Kiango. Na
ifahamike kuwa kuitoa nje siri hii ni sawa na kujiwekea saini ya kifo chako
mwenyewe".
"Ni
kweli Mwenyekiti", sauti mbili tatu za wajumbe wenye hofu, ziliitikia.
ITAENDELEA
0784296253
Comments
Post a Comment