SURA YA TATU II
Kesho yake
ilikuwa asubuhi yenye mawingu kiasu cha kuvunja nguvu ya jua kali ambalo
lilikuwa likitishia kutawala. Mmoja kati ya wale askari waliomchukua Waridi
pale baa alikuwa tayari kawasili kazini kwake. Mkuu wake wa kazi alihitaji
ripoti kamili ya "Kushambuliwa kwa yule msichana malaya" Akamtaka pia
kujitahidi waliotenda tukio hilo watafutwe na kupatikaba haraka iwezekanavyo
kwani mchezo wao wa kubaka wasichana si mzuri kimaadili hususan mchezo wa
hatari.
Askari huyo
akalazimika kumsubiri mwenzake kwa muda mrefu, hakutokea. Ikamshangaza. Kwa
kuwa makazi yake hayakuwa mbali na kituo cha polisi cha Magomeni, askari huyo
aliamua kumfuata nyumbani, Alimkuta! Lakini alimkuta katika hali ambayo haikuwa
ya kawaida, Kwani haikuwa jambo la kawaida mtu aanze kuvaa suruali kabla
haijafunika matako, aache kazi hiyo ba kuanza kuinamia sakafu hadi kichwa
kigonge chini mfano wa mtu anayeswali. Na zaidi ya hayo mgeni aingie baada ya
kupiga hodi mara kadhaa bila kuitikiwa, lakini akukute ukiendelea kuinama kimya
kimya. Dakika mbili, tatu hadi tano.
"Bobi",
askari huyo alimwita mwenzake kwa mshangao, akijiuliza huu ni mzaha wa aina
gani, na umeanza lini! "Bobi", aliita tena askari huyo huku
akimtazama tena kwa makini zaidi askari huyo. Ndipo alipoanza kuona povu lenye
damu damu likimdondoka mwenzake mdomoni na puani. Akaruka nyuma, kisha
akakusanya nguvu na kumsogelea ili amchunguze vizuri zaidi. Akayaona macho yake
yalivyoduaa, akauona ulimi ulivyotoka na kutembea nje ya meno, akaona... Hofu
ikamkumbuka ghafla. alikuwa akitazama maiti ya askari mwenzake. Hima akarudi
kituo cha polisi kutoa taarifa.
Marehemu
alipelekwa hosptali ambako daktari hakuchelewa kutoa taarifa kuhusu ugonjwa uliosababisha kifo hicho.
"Ugonjwa wa moyo", daktari alidai. Kwamba alikutwa na ugonjwa huo
ghafla wakati akivaa nguo zake, ikabainishwa kuwa kifo cha askari huyo
kilitokana na shinikizo la damu.
Hakuna
aliyeshuku kuwa asakri huyo amekufa kwa sumu ile, ya aina yake, ambayo aliigusa
kutoka kwa Waridi, na kuifikisha sehemu iliyokusudiwa kufika, mwilini mwake,
bila askari huyo kujua.
Sumu hiyo
iliandawaliwa kwa ajili ya Joram Kiango peke yake
ITAENDELEA
0784296253
Comments
Post a Comment