SALAMU KUTOKA KUZIMU

SURA YA TATU III

Wakati huo huo Joram Kiango alikuwa akipokea simu iliyopigwa ofisini mwake.

"Sauti yako i tamu mno masikioni sister, yaelekea nawe u kiumbe mzuri sana. Siwezi kuukataa kamwe mwaliko wa mtu mwenye sauti nzuri kama hiyo, Baada ya saa moja nadhani nitafika... Haya... Ahsante... Umesema wapi vile... Heh... Light Lodge?... Hapo siyo?. Nitafika baada ya saa moja...", akaweka simu chini na kuukunja uso wake akimtazama Neema Iddy, katibu wake ambaye pia alikuwa akumtazama.

"Nani?", Neema alihoji kwa shauku.

"Anajiita waridi".

"Waridi? Anataka nini?" Joram alipochelewa kujibu. Neema aliongeza. "Sikujua Joram kama nawe u mroho wa wanawake kiasi hicho. Sauti tu unaridhika na kuahidi kumfuata? Angalia Joram. Utaingia katika mtego. Una maadui wengi katika nchi hii".

"Nalijua hilo", Joram alisema. "Siendi kwa sababu ya sura wala sauti yake kama nilivyosema. Kilichonivutia ni maelezo yake. Anasema yeye ni yule msichana ambaye alipigwa pale baa ya Forest of Flowers. Anadai kuwa nia yake ni kunishukru pamoja na kunipa habari fulani ambayo inasisimua".

"Malaya kama yule! Hana habari yoyote. Anachotaka ni kukupata wewe tu".

"Hapana", Joram alimkatisha. Sauti yake ndiyo iliyonifanya nivutiwe hata kumwahidi kuwa nitakwenda. Inavyoonyesha kuna kitu zaidi ya anachosema. Nahitaji kujua ni nini. Zaidi ya sauti, nadhani utakumbuka kuwa jana binti huyo alilia sana akilitaja jina langu. Sijui alivyonijua".

"Ni mimi niliyekutaja kwanza".

"Ni kweli, lakini hiyo siyo sababu ya kumfanya aniite jina langu mara nyigi tena kwa ufasaha kiasi kile. Ni kama mtu aliyekuwa akinifahamu kitambo".

"Wewe si mtu unayefafamika Joram?".

"Pamoja na hilo", Joram aliongeza. "Ni wapi alikopata namba yangu ya simu? Tuseme kwenye vitabu vya simu. Kwa nini ahangaike kiasi hicho? Na kwa nini iwe mapema hivyo? Neema, huoni ni mwujiza huu? Jana tu alikuwa hoi. Leo anazungumza kwa uchangamfu kabisa na yuko logi badala ya hospitali! Huoni kama kuna jambo hapo? Yaonyesha kuwa ananitafuta. Yawezekana hata jana alikuwa akinihitaji mimi tu hakuwa majeruhi wala mgonjwa!" Akasita kidogo kabla hajaongeza kwa sauti ya chini akisema: Na atanipata. Kwa muda mrefu nimekuwa sina kazi ya kufanya".

Wakati huo Joram alikuwa wima akivuta droo hii na ile, akiweka hiki mifukoni na hiki kiunoni. Mara akaanza hatua za haraka kuelekea mlangoni.

"Yaani unakwenda Joram, mara hii!", Neema aliuliza kwa mshangao.

"Naam".

"Mapema namna hiyo? Si umemwambia baada ya saa moja?".

"Niliamua kumdanganya. Siamini kama yeye ananieleza ukweli mtupu, hivyo nami sioni ubaya wa kumweleza uongo kidogo. Nataka kufika mapema kidogo nione anachofanya".

"Lakini ujihadhari", Neema alimwambia wakati akivuka kizingiti cha mlango.

"Usijali Neema", Joram akamjibu bila kugeuka nyuma. 

ITAENDELEA 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU