SALAMU KUTOKA KUZIMU

SURA YA NNE

Kama kuna wanawake ambao husimbua mioyo ya wanaume mara tu watokeapo mbele yao hata wanaume hao wakajisahau na kuzisahau shughuli zao, basi ni dhahiri pia wapo wanaume ambao huisumbua mioyo ya wanawake kwa kiwango kile kile. Na kama kweli wapo, miongoni mwao yumo Joram Kiango. Hayo yalijidhihirisha baada ya Waridi kumtia machoni Joram alipoingia chumbani.

Moyo wake ulipoteza mapigo kwa sekunde kadhaa. Roho yake ilihisi kupaa nje ya mwili wake. Kadhalika, damu ilimsisimka kiasi cha kumfanya ahisi ganzi mwili mzima. Hivyo, hakuweza kuyaondoa macho yake juu ya umbo la Joram ambaye alimsogelea polepole. Nusura wazimu umpande Waridi alipoona uso na tabasamu la Joram, lililotosha kuwa tiba kwa maradhi yake. Maradhi aliyoamini kuwa hayangeweza kutibika.

Kwa bahati mbaya, Waridi hakuwahi kupenda mwanaume katika maisha yake. Hivyo hakujua mapenzi ni nini. Hakuwahi kuyaonja. Kama angejua, angefahamu nini kitatokea. Badala yake alihisi maumivu moyoni na huzuni kubwa akilini mwake. Akanusurika kutokwa na machozi. Hakujua nini kinamtokea. Isipokuwa kitu kimoja tu alikifahamu, Joram hakuwa mtu wa kufa, Hakuona sababu ya kumwua, Asingeweza...

Tazama alivyosimama mbele yake kwa upendo na utulivu kama malaika asiye na hatia. Tazama anavyochekelea kwa furaha kama nuru, Mtazame. La, huyu kijana si mtu wa kufa. Waridi akawa ameamua hivyo.

"Nadhani mimi ni mgeni wako, mpenzi, Joram alisema tena, akinyoosha mkono wake kumgusa Waridi kwenye bega lake la kuume.

Joram alikuwa ameshangazwa na uzuri wa msicha huyu. Vipi wengine waumbwe kwa upendeleo kiasi hiki wakati wengine wasitofautiane sana na vinyago? alijiuliza. Mavazi mazuri ya msichana huyu pia yalimchanganya Joram; yalikuwa mavazi mapya ya thamani kubwa, kisha ya kihuni kama yalivyondaliwa mahususi kwa ajili ya kumtongoza! Hicho hakikumshangaza Joram, Lakini alishangazwa na uso mzuri wa msichana huyu ukiwa katika dimbwi la majonzi, mashaka, hofu na msiba. Hilo halikumshangaza hata kidogo.

"Ndio...ka... karibu kaka", waridi alianza kusema huku akibabaika,

Joram alimvuta mkono na kumwongoza hadi kitandani, ambako alimketisha kisha naye akaketi kando yake huku akiendelea kuushika mkono wa Waridi.

"Nilikwambia kuwa sauti yako ni tamu kama ilivyo sura yako? Naamini sikukosea. Ama kweli umeumbika bibie. Ulimhonga nini muumba hata akakupendelea?"

Sauti ya Joram, tabasamu lake likasindikiza kila neno, hali hiyo ikamfanya Waridi aanze kuchangamka. Akasahau yote yaliyokuwa mbele yake na kujikuta kazama katika maongezi na Joram. Katika kipindi hicho kifupi bila kujifahamu Waridi alijikuta tayari akiwa ameufunua moyo wake wote kwa Joram, akimsimulia matatizo yake yote. Alipotanabahi alikuwa akisema: "Najisikia kutoweka nje ya nchi hii".

"Kwanini?".

Swahili hilo lilimzindia Waridi. Hakujua yapi alikuwa tayari kuyatamka ambayo hayakustahili kuiacha milki ya kinywa chake, Hofu ikamrejea. Akalikumbua jukumu lililokuwa mbele yake: kumfanya kijana huyu kuwa marehemu. Ama ni yeye atajayefanywa marehemu.

Hofu hiyo, ilizidi baada ya Joram kuinuka na kuiendea meza iliyokuwa na chupa mbili za pombe huku akisema: "Bia hii? Unaonaje nikianza kuimimina tumboni mwangu ili kupoza joto la Dar es Salaam kabla hujanieleza sababu za kuniita hapa? Siamini kwama kweli umeniita kwa ajili ya kunishukuru tu, yaani hilo likusukume kunitafuta..."

"Usinywe hiyo pombe", Waridi alifoka.

"Kwanini mpenzi? Nilidhani umeiandaa kwa ajili yangu", Joram alifuatwa na tabasamu la kukata na shoka.

Waridi alikuwa akitetemeka. Lakini asingeweza kusahau maneno ya yule mtu katili Proper alipomwambia: "Nitakuwa chumba cha pili... Ukishindwa tena nitakuua papa hapa..." Waridi hakupenda kufa, lakini pia hakuwa tayari kumuona kijana huyu asiye na hatia, afe. Afanye nini? Kwa kutojua la kufanya akaanza kulia. Mikono ya Joram ilitua tena mabegani kwa Waridi akimfariji na kumkumbatia huku akisema.

"Kama hutaki ninywe hii bia ni wazi kwamba kuna zawadi kubwa na tamu zaidi ya bia uliyoiandaa kwa ajili yangu. Kwa bahati mbaya nina mazoea ya kunywa pombe kabla ya yote. Kwa maana hiyo niruhusu ninywe bia moja tafadhali".

"Usi..." Waridi alijaribu kufoka tena. Joram alimzuia kwa kuuziba mdomo wake kwa kiganja cha mkono wake huku akiweka kinywa chakr karibu na sikio la Waridi, akamnong'oneza.

"Najua kitakachotokea. Sinywi pombe hiyo. Acha nijifanye kama nakunywa ili nimpumbaze huyu anayetaka kuniua. Nitakuomba wewe uwe msiri wangu. Mwache aamini kuwa ameniua. Mwache kila mtu aamini kuwa nimekufa. Nataka kufahamu hawa waliokusudia kuniua jambo gani wanakusudia kutenda".

waridi aliduaa. "Ume... umewezaje kujua? aliuliza kwa kunong'ona.

"Niliwahi kufika eneo hili mapema na kumsikia alivyokuwa akikuamru. Nawe pia lazima ufahamu kuwa uko hatarini. Huyu ni mtu hatari. Mara tuu utakapotoka hapa, toroka uende kokote asikoweza kukufikia. Sasa acha nijifanye nainywa pombe yake". Joram akaongeza sauti kusema. "Glasi? Acha ninywe kihuni".

Joram aliifungua chumpa moja na kuingia nayo msalani ambako aliimimina nusu kwenye tundu la choo, Akarudi na kuitua mezani huku akiendelea kuongea na Warid, mazungumzo yao yalifanyika taratibu kwa sauti ya chini. Mara kadhaa Joram alimshika waridi na kumtomasa hapa na pale kwa ajili ya kumtoa hofu.

"sasa mpenzi sikia", aliongeza. "Ninaye mgeni ambaye atakuja ofisini kwangu baada ya nusu saa kuanzia sasa. Baada ya kumalizana na mgeni huyo, leo kutwa nzima nitakuwa huru. Waonaje niende ofisini mara moja na kurudi sasa hivi? Naamini leo tutashinda pamoja kwa furaha sana. Naamini itakuwa siku njema twetu".

"Sawa", Waridi alijikongoja kujibu.

"Tafadhali nikukute, ukiwa kama ulivyozaliwa. Ikiwezekana, kitandani, sawa?"

"Bila shaka".

Mara tu Joram alipotoweka machoni mwake, Waridi alijikuta akirejewa na hofu. Ile hakika na ushujaa ambao alikuwa ameuhisi kwa kusikia sauti ya Joram na kuyaona macho yake yang'aavyo sasa ilikuwa kama ndoto tu. Ndoto ya kale. Hakujua lipi afanye. Akaendelea kuduwaa kimya, akitazama huku na huku kama aliyetegemea kumwona Zibril akimjia kwa lengo ka kutwa roho yake.

Waridi angetimua mbio Proper alivyoingia ghafla huku akimtazama Waridi kwa macho ya kutisha. Waridi angeweza kukimbia kama ukuta usingekuwa umemtenga na dunia ya nje. Alichofanya ni kurudi nyuma hatua kadhaa hadi alipoegemea ukuta, macho yenye hofu kayatoa kama kondoo aliyekuwa juu ya madhabahu, akisubiri kutolewa kafara.

"Mwanakharamu... malaya mkubwa, mwana wa malaya mkubwa...", Proper alifoka. "Umekosa walau ushujaa wa kunidanganya kuwa hawara yako amekunywa pombe niliyomwandalia? Mara hii umesahau kuwa mmekubaliana naye adai kuwa ameinywa ili asingizie kuwa kafa. Nakusikitikia Bi. mdogo. Namsikitikia pia huyo hawara yako. Hajui afanyalo. Anadhani kuwa anacheza na watoto wadogo kama alivyozowea. Nilikuwa nimemfanyia hisani kubwa ili afe kistaarabu hakutaka. Kajitia ujanja. Sasa atakufa kifo cha kusikitisha zaidi".

Jodor Proper aligeuka kama anataka kutoka. Mara kama aliyekumbuka jambo alimgeukia tena Waridi na kusema. "Nawe malaya mwovu hufai kuishi zaidi. Huna faida duniani wala haki ya kuishi tena. Utamfuata mpenzi wako Bomba akhera. Mpe salamu zangu, mwambie hongera kwa hila zake zisizo na ila". Akageuka na kutoka.

Machozi yalikuwa yamenyauka machoni mwa Waridi. Sasa aliiona dunia kama kitu ambacho kilikuwa kando yake. Naam, maisha yake yalikuwa ukingoni. Asingeweza kutilia mashaka sauti ile ya Proper yenye uhakika. Sauti ambayo masikioni mwake ilikuwa kama saut ya mauti yenyewe.

Kwanini aendelee kusubiri? alijiuliza. Kwanini asubiri kifo cha mateso na kashfa? Akajiuliza kwanini asitangulie? Sasa macho yake yalikuwa yakitambaa kila mahali kutafuta silaha yoyote ambayo ingefaa kumtoa roho. Mara macho ya waridi yakatua kwenye ile chupa yenye pombe yenye sumu iliyoandaliwa kwa ajili ya Joram, bila kufikiri kwa mara ya pili aliiendea ile chupa yenye pombe akajimiminia tumboni mwake.

Mara Waridi akapata faraja kubwa ambayo ilimfanya asahau hofu na kudharau vitisho vyote vilivyokuwa mbele yake. Alijiona yu njiani hatua chache tu kufika katika milki mpya. Milki ambayo itampa uhuru kamili.

Furaha hiyo ikamuongoza Waridi, alitoka ndani ya chumba hicho na kuiendea lifti. Akatelemka hadi chini. Aliiacha hoteli na kuanza safari ya kuelekea kituo cha mabasi. Mavazi yake yakiwa kama yalivyokuwa, umbo lake likiwa kama lilivyo, na sura yake nzuri ikiwa imepambwa na tabasamu, viliyafanya macho ya wanaume kumtazama kwa mshangao wenye tamaa. Baadhi waliguna walipomuona, wawili walimkonyeza na mmoja alidiriki hata kumfuata. Wote walipata tuzo kwa tamaa zao. Tuzo ambalo lilikuwa tabasamu pana zaidi ambalo liliwafanya wabaki wameduwaa nyuma yake hoi bin taabani.

Waridi akaendelea na safari yake. Mwendo wake ukiwa nyongeza nyingine ya maneno kwa watazamaji. Akiwa kajaza nyuma, kakatika kati na kunyooka alivyonyokeana, ilikuwa kana kwamba hatembei bali anafanya maonyesho ya miondoko kama wanavyofanya warembo katika mashindano ya miss. Mwenyewe akiwa hana habari hizo, aliendelea na msafara wake hadi alipokifikia kituo na kujiunga na umati wa watu waliokuwa wakisubiri usafiri wa umma.

"Gari hii hapa dada", mtu mmoja alimwambia Waridi. Ilikuwa teksi. Waridi hakufanya hiana, akajitosa ndani ya teksi hiyo huku akisema. "Nipeleke Mburahati",

"Vizuri, lakini waonaje kama tukipitia hapa Embassy Hoteli tukapate walau bia mbili mbili baridi?", dereva alitupa ndoano yake.

"Samahani, leo nina haraka, nitafute siku nyingine".

"Kesho".

"Sawa..." waridi alilaghai. Rohoni akiamini kuwa kesho hatakuwa Dar es Salaam. Hatakuwepo hapa nchini, wala popote Afrika. Atakuwa nje. Nje ya dunia. Aliendelea kuwaza kwa furaha huku akimwitikia dereva huyo, "Ndio", kwa kila dereva huyo alilosema wakati hata hamsikii. Walipofika mbele yavijumba vayo, Waridi alimtaka dereva asimame. "Ni hapa, asante kaka", dereva hakuyaamini masikio yake, "Yaani uaishi hapa. Katika vijumba hivi? Na unaishi hapa dada?", dereva alishawishika kuuliza.

"Hapa ndio kwangu", Waridi alijibu wakati akitelemka kutoka ndani ya gari.

"Hapa?", dereva aliuliza tena kwa mshangao. Hakutia neno lingine. Badala yake aligeuza gari lake na kurudi alikotoka kwa mwendo wa kasi.

Walidi akapokelewa na wenzake waliojawa na mshangao. "Iwe", alisema mmoja wao. "Ulikuwa wapi".

"Na ilitokea nini hata ukaondoka bila kuaga?", alihiji mwingine. Maswali yalikuwa mengi mno. Waridi hakuwa na muda wa kuyajibu yote. Wala hakukumbuka ajibu maswali gani. Alichokumbuka ni jinsi alivyoingia chumbani kwake na kujilaza kitandani akisubiri kifo. Usingizi mzito ukamchukua.

Alipoamka ilikuwa usiku wa saa tatu. Chumba cha pili kitanda cha mwenzake kilikuwa kikilalamika kwa uzito wa viumbe waliokuwa wakikitumia. Naye alikuwa akigongewa mlango. Mteja akainuka na kumwendea. Alikuwa mtu mwenye umbo la mwili wa mtoto na uso wa mzee. Alikuwa na pesa zake mkononi tayari. "Leo sifanyi kazi", Waridi alimwambia mteja huyo na kufunga mlango wake. Hakujali malalamiko ya mteja huyo. Alikuja mwingine. Na mwingine tena. Wote Waridi aliwakatalia. Nao wakaondoka shingo upande.

Halafu akaja huyu mteja ambaye hakukubali kuondoka. Alikuwa kavaa kofia kubwa iliyofunika uso wake na koti kubwa lililofunika hadi miguuni. Aliingia kwa kujlazimisha na kufunga mlango nyuma yake huku akisema, "Lazima".

"Leo sitaki".

"Hata kwa bei kubwa?".

"Hata ukitoa milioni".

Mtu huyo alicheka kidogo. "Mimi wanitaka. Umekuwa ukinisumbua muda wote huu", Alitupa koti lake chini na kubaki katika suruali na shati. Akaivua kofia yake na kuitupa juu ya koti. Ni hapo Waridi alipomtambua. Macho yenye hofu kubwa yakamtoka.

"Bila shaka utakuwa umenikumbuka ", alisema polepole. "Unadhani nilikusudia ufe kistaarabu kwa ile sumu?, Ile ilikuwa maalumu kwa ajili ya Joram Kiango peke yake. Wewe ni mwovu mwenye dhambi nyingi. Unastahili kufa kishenzi".

Kabla Waridi hajafahamu kama ilimpasa kufanya nini, alijikuta tayari kadakwa ghafla kwa mkono kwa mkono wenye nguvu, ambao uliibana mikono yake yote miwili. Haraka kamba zikapita mikononi mwake. Alipotanabahi kupiga kelele, alijikuta katupiwa dude fulani kinywani ambalo lilimziba kinywa. Mara akatupwa chini na kudungwa sindano ambayo ilimlegeza hata asiweze kutapatapa.

Kisha kisu kikali kilichomolewa kutoka ubavuni na kuanza kupita juu ya mwili wake. Maumivu yalikuwa makali ajabu, lakini hakuwa na uwezo wa kulalamika. Alichoweza kufanya ni kuendeleo kukodoa macho yenye dalili zote za hofu na maumivu. Macho hayo yalishuhudia mikono yake ikikatwa mmoja baada ya mwingine na kuwekwa juu ya kitanda. Kisha tumbo la waridi likafumuliwa na utumbo kumiminika katika sinia lililokuwa mezani. Baada ya sekunde kadhaa alikuwa tayari amekata roho pindi kichwa chake kilipokatwa na kuwekwa juu ya debe, kando ya kitanda.

Baada ya kuridhika na kazi yake. Proper alizivua nguo zake zenye damu na kuzifunika katika mifuko ya koti lake ambalo alilivaa na kisha kutoroka zake nje polepole kama wateja wengine. Hapo nje aliwakuta wateja kadhaa ambao walisimama kwa namna ya mstari wakisubiri zamu zao. Akafanya haraka kuiendea sehemu aliyoficha gari yake.

Mteja aliyeingia baada ya Proper aliduwaa kwa kutokumuona Waridi. Kisha alishangaa kuiona mikono ya mwanamke huyo iliyolala peke yake juu ya kitanda. Halafu akakiona kichwa kilicholowa damu, kimelala chali. Hakuyaamini macho yake. Na ilipomtokea kuamini alihisi akili yake ikipaa. Alipiga kelele kwa nguvu na kuanza mbio akielekea barabarani, Alianguuka, akainuka na kuendelea kukimbia.

Mtewa mwingine alichungulia tu na kugeuka akianza safari ya kurudi zake alikotoka kimya kimya.


Ni mteja wa tatu aliyetoa taarifa kwa majirani na wenzake kuhusu kilichomtokea Waridi. Yeye pia alitoweka. Majirani walichanganyikiwa kwa muda mrefu. Mmoja wao alitapika. Wawili wakalia kwa nguvu. Umati mkubwa wa watu ulifika. Polisi pia hawakuchelewa.

ITAENDELEA 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU