SURA YA NNE II
"Umesema
u nani wewe?".
"Naitwa Joram
Kiango".
Inspekta
Mkwaju Kombora hakuyaamini masikio yake. Jina la Joram Kiango lilikuwa
maarufu kichwani mwake kama mbwa anavyoifahamu harufu ya chui. Mzee huyu
alimfahamu vyema Joram. Yule kijana machachari aliyefanya mengi dhidi ya
wahujumu uchumi na majasusi hatari ambao jeshi la polisi lilielekea kukata tamaa. Yule
kijana nadhifu sana, mpole sana, mwenye nguvu na akili. Si huyu mzee aliyesimama mbele
yake katika vazi la Kiarabu, akiwa amevaa kanzu nyeupe, kapiga kilemba, mwenye ndevu nyingi,
uso uliofunikwa na miwani na mkononi kashika fimbo ambayo
ilimsaidia katika mwendo wake wenye dalili zote za udhaifu wa kizee,
"Joram?", Inspekta Kombora akauliza tena.
"Naona
huniamini kwa vile hujanifahamu Inspekita", ilisema sauti ambayo Kombora alielekea kuifahamu
kwa mbali,lakini sura haikuwa ya Joram.
"Pengine
niondoe miwani na haya madevu ya bandia ili uweze kunitambua". Madevu
yakatolewa na miwani ikavuliwa, Uso ulisimama mbele yake ukitabasamu, Alikuwa
ni Joram Kiango halisi ambaye Inspekta Kombora alimfahamu vyema.
"Nini
sasa unafanya Joram?", alishangaa Inspekta Kombora. "Mchezo huu una
lengo gani?".
"Siyo
mchezo inspekta. Niko kazini. Unionavyo hapa mimi ni marehemu. wapo watu
wameniua. Nataka niendelee kuwa marehemu ili...
Inspekta
Kombora alimkatisha na kumwekea mkono begani huku akisema, "Sikia Joram.
Kama ni mzaha subiri nitakapokuwa huru ndipo utakapoufanya tena mchezo wako,
tucheke pamoja. Kwa sasa niko katika mkasa mzito ambao unaweza kuhatarisha
usalama wa jiji endapo mtu huyo mwenye roho ya kinyama hatapatikana".
Habari hiyo
ikamvutia Joram. "Mtu gani?", Joram alihoji mara moja.
"Hujasikia
tu? Nadhani wewe hupitwi na neno".
"Kusikia?".
"Kuhusu
msichana huyo aliyeuawa kikatili kuliko ilivyowahi kutokea. Polisi wamefanya
kuokota viungo vyake kimoja baada ya kingine ndipo ukapatikana mwili mzima wa
marehemu. Mtu aliyefanya mauaji hayo ni mnyama zaidi ya wanyama wengine wa
kawaida. Mtu mwenye kumchinja msichana mrembo kama yule".
"Sijakupata
Inspekta, yaani..." kisha Joram akapunguza kasi kuhoji kuhusu tukio hilo
kwa kituo. Inspekta Kombora akamweleza yote kuhusu tukio zima lilivyotokea
usiku huo huko Mburahati.
Hakukuwa na
sababun za kuupeleka mwili huo hospitali", Inspekta Kombora aliongeza.
"Viongo vyote vya marehemu vimeletwa hapa katika chumba cha maabara. Kama
utapenda kutazama vitu vya kutisha unaweza kwenda maabara, inatisha sana".
"Nitapenda
kumwona tafadhali".
Inspeta
Kombora akaiacha ofisi yake na kumuongoza Joram kuelekea maabara ambako
alifungua friji na kutoa kichwa cha msichana mrembo. Joram alikitambua kichwa
hicho kuwa cha Waridi. Kwa mara ya kwanza katika maisha yake, alihisi machozi
yakimdondoka. Aliyafukuza macho hayo kwa tabasamu huku akinong'ona kama mtu
anayesali. "Ni Waridi! Mungu akurehemu. Naamini ni mapenzi yako kwangu
ambayo yamekufanya ustahili adhabu hiyo ya kinyama. Naahidi nitakulipia
kisasi".
Sala hiyo
ilimfikia Inspekta Kombora. Akamgeukia Joram kwa mshangao na kusema,
"Kumbe unamfahamu msichana huyu? Tafadhali turejee ofisini ili unisimulie
kuhusu mkasa mzima ulivyotokea".
"Sijawa
na cha kusimulia", Joram alijitetea. Hata hivyo alilazimika kusimsimulia
Inspekta Kombora yote aliyoyajua. Alieleza jinsi alipomwona Waridi kwa mara ya
kwanza pale baa akiwa ametegwa kwa sumu iliyokusudiwa kumwua yeye. Akaeleza pia
yaliyotokea katika chumba ambacho waridi aliandaliwa kwa sumu ile ile ili
amnyweshe Joram kwa hila. Ambacho Joram hakueleza ni jinsi alipofika hapo kabla
ya wakati na kubahatisha, ingawa kwa taabu, kumwona mwuaji yule akitoa maelezo
kwa Waridi. Hilo aliliacha ili apambane nalo binafsi. Hakupenda kuwaachia
polisi ambao aliamini wangeweza kuharibu mapngo wake wa kumtia mikononi mwuaji.
"Ina
maana binti huyu marehemu ndiye yule msichana aliyetoroka hospitali baada ya
kuokotwa kando ya baa", Joram akatikisa kichwa kukubaliana na swali la
Inspekta Kombora.
"Ndiye.
Basi anastahili kifo cha aina hiyo. Kwa nini hakutoa taarifa polisi, tungeweza
kumsaidia. Alishirikiana na wahalifu kuandaa njama za kufanya uhalifu".
"Inawezekana
au isiwezekane", Joram alijibu kwa mkato. "Aweza kuwa alilazimika au
kulazimishwa. La muhimu sasa ni kumpata huyo mwuaji".
"Ndio...
apatikane haraka. Wewe humjui?".
Joram
alikanusha. "Angalia bwana mdogo. Ninavyookufahamu mimi bila shaka wajua
mwengi zaidi ya haya uliyonieleza. Nawe kama uonavyo hawa ni watu hatari kuliko
unavyofikiri. Usiwachukulie mzaha, Ucheze nao kama ilivyo kawaida yako".
"Kawaida
yangu sina mzaha wa mwuaji Inspekta", Joram alijibu. "Tena naamini
kuwa nitawafikisha mikononi mwako mapema zaidi. Ninayo nafasi nzuri sana. Sasa
hivi wao wanadhani kuwa nilikunywa ile dawa na sasa niko mahututi au marehemu
tayari. Imani hiyo itawafanya wapate jeuri ya kuendelea na mipango yao kama
walivyokusudia. Nataja kujua lengo lao, wanakusudia kufanya nini, na watu hawa
ni akina nani, baada ya kufahamu hivyo nitawaleta mikononi mwako.
"Kazi
hiyo ndiyo iliyonifanya nijibadili kuwa katika hali hii Inspekta. Nimeona nitoweke
machoni mwao. Kusudi langu kwako ni kukuomba uitangazie dunia kuwa nimefariki
ghafla. Nadhani watafurahi na kuendeleza mipango yao. Ndipo nitakapofufuka na
kuwashangaza kwa kuwatia mikononi.
Walijadiliana
kwa muda ofisini. Kombora akawa ameafikiana kwa taabu sana na Joram. Nia ya
Joram ilikuwa awaachie polisi kufanya kazi yao kwa makini. Lakini maelezo ya
Joram yalimtua Inspekta Kombora hata akakubali japo kwa shingo upande.
"Kumbuka ninavunja sheria zote za kushiriki katika uongo mkubwa kama huu.
Hivyo. usiniangushe kwa kushindwa kutimiza ahadi yako ya kuwatia watu hawa
mikononi mwa sheria", Inspekta Kombora alimwambia Joram.
"Wanifahamu
vizuri Inspekta. nakuhakikishia kuwa Siwezi kushindwa kamwe", Joram
alimjibu akiweka vyema ndevu zake za bandia na kuvaa miwani yake. Akautwaa
mkongojo wake na kuiacha ofisi ya Inspekta Kombora kwa mwendo ambao ulimfanya
Inspekta huyo ambaye hucheka kwa nadra sana aangue kicheko kipana.
Usiku huo
taarifa ya habari ya Radio Tanzania Dar es Salaam ilibeba habari ambazo
ziliwashitua wasikilizaji wengi kote nchini.
"...Joram
Kiango yule mpelelezi mashuhuri wa kujitegemea amefariki ghafla akiwa nyumbani
kwake kwa maladhi ambayo bado hayajathibitishwa. Madaktari wanaendelea na
uchunguzi watatoa taarifa za kifo hicho hivi karibuni baada ya
uchunguzi,,,"
Haikuwa
habari njema hata kidogo. Wala hakuna aliyetarajia kuisikia. Kila aliyemfahamu
Joram alitegemea kuwa kijana huyo angeuawa au kufa kwa risasi au madhara
mengine kutoka kwa adui zake. Kufa kwa maradhi! haiwezekani!.
Taarifa za
habari za sauti ya Kenya na Ujerumani ziliidaka habari hiyo haraka na kuitagaza
kwa mapana zaidi... "Yule kijana machachari"... Walisema wakenya,
"The Iron boy..." walimwita hivyo wajerumani... "Amefariki leo
ghafla. Yawezekana na njama za wahujumu ambao walimuogopa sana kijana huyu kama
moto".
Ndipo watu
walipolazimika kuamini. Wengi walisikitishwa na kifo hiki. Wengine walitoa
machozi. lakini Wachache walishangilia.
ITAENDELEA
0784296253
Comments
Post a Comment