NOTI BANDIA

SEHEMU YA TISA

Ilipofika saa tisa alasiri, Carlos Dimera, alikutana tena na kikosi chake cha kazi, muda mfupi uliopita alikuwa amepata ujumbe kutoka wakala wanaohusika na usafirishaji wa dawa za kulevya CCA ulioko Bogota, nchini Corombia, ujumbe ulimfahamisha kuwa ajiandae kupokea shehena kubwa ya dawa za kulevya.

Ujumbe huu ulimtatiza kidogo, Carlos Dimera, pamoja na kuwa na uzoefu mkubwa wa kupokea mizigo mikubwa zaidi, lakini safari hii alijiuliza maswali kadhaa wa kadha, alifikiria pia hali ya sasa ya usalama ilivyoimarishwa nchini Tanzania. Akapata hofu kidogo.

Kilichompa imani kidogo ni mabadiliko ya ghafla katika baraza la mawaziri, Waziri aliyekuwa mstari wa mbele kukamata wahalifu kiwanja cha ndege alikuwa amebadilishiwa Wizara. Carlos aliamini kuwa mabadiliko hayo ni kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa biashara hiyo. Akapiga moyo konde.

"Siku zote ndoto zangu ni kuwatafutia utajiri, naamini siku moja mtayakumbuka maneno yangu. Dakika kadhaa  zilizopita nimepata ujumbe wa maandishi kutoka wakala wanaohusika na usafirishaji wa mizigo, kutoka katika Jiji la Bogota, kuwa shehena kubwa ya dawa iko njiani kuelekea Dar es Salaam, Tatizo langu ni moja tu, tunaweza kuupokea mzigo huo kipindi hiki ambacho Serikali imekuwa macho kuangalia kila aina ya mizigo inaoingia na kutoka nchini?" alihoji Carlos.

Baada ya ukimya wa sekunde kadhaa, wajumbe wakiangaliana kila mmoja akitafakari hili na lile, Carlos akasimama. "Naomba tutafakari jambo hili kwa makini, naamini hakuna jambo linachoshindikana, mzigo utapita, lakini utapitaje? Hilo ndiyo swali langu".

"Sikilizeni", Nombo alirukia, kila mmoja akatega masikio kumsikiliza, "Dakika chache sana zilizopita, nilipokuwa nakuja kwenye kikao hiki, nimewasiliana na vijana wetu, wamenihakikishia kuwa mambo yanakwenda vizuri, adui yuko kwenye kikao, wameweza kudhibiti milango yote ya kuingia na kutoka katika jengo hilo, hivyo wamesema akitoka tu amekwisha, huyu mshenzi akitoweka, uhakika wa kuingiza huo mzigo ni asilimia mia".

"Asante kwa taarifa, nafarijika sana kuona kuwa mko makini katika jambo hili", alipongeza Carlos Dimera.

"Kama alivyosema Nombo, tunawasiliana na vijana karibu kila baada ya dakika tano, hatua waliyofikia ni ushindi, kifo cha mshenzi huyo kitawafanya viherehere wengine waogope, wakati taifa likiwa kwenye maombolezo ya msiba wa mbwa huyo sisi tutakuwa tunaingiza shehena nyingine wakati huo huo tunawapiga watu mapesa kwa kuwaachia noti bandia", Hawa Msimbazi alisema kwa kujiamini.

"Ninavyowajua vijana hawa, ninavyoijua shauku waliyonayo ni kupata maendeleo, bosi, naamini kabisa jua la kesho litakuwa kwa ajili ya watu wengine, mimi nahesabu kabisa kuwa Teacher ni marehemu, hii itawachanganya, wakati wao watakuwa wanafafuta namna nyingine ya kufanya wakati huo sisi tutakuwa tunachanja mbuga", Jackina alieleza huku akishangiliwa kwa makofi.

"Sioni sababu ya kupiga makofi, hili lifanyike baada ya kazi, sijawahi kumuona mtu amekwenda dukani kununua nepi za mtoto wakati mtoto mwenyewe hajazaliwa, tumalize kazi hii halafu tupongezane, kama nilivyosema hapo awali, pesa za matumizi zipo, akaunti yetu ina mapesa yanayosubiri matumizi tu", alionya Carlos Dimera.

Wakati huo, Simba, Nyati na Chui kama ambavyo wenyewe walivyojiita, walikuwa wameliweka eneo hilo chini ya himaya yao, walifuatilia kwa makini kufahamu kila mtu aliyeingia na kutoka ndani ya jengo hilo, na mtu huyo aliingia kwa kazi gani na alipotoka aielekea wapi?. 

Luteni Claud Mwita na Sajenti Julius Nyawaminza walikuwa hawafahamiani, kila mmoja alikuwa na jukumu lake binafsi. Hawakukaa kwa ajili ya kusoma magazeti tu, walifuatilia mwenendo wa kila mtu aliyeonekana kuwa katika eneo hilo. Hata wao wenyewe walitiliana mashaka, Claud akahisi jambo Nyawaminza akacheka, wakaonyeshana ishara. Walifahamiana kwa harufu.

Kikao kiliendelea kwa muda mrefu, wazee hawa walieleza kwa undani jinsi watu hao walivyofanikiwa kuwaibia mamilioni ya pesa. Kanali Emilly alikuwa amenyamaza kimya akiwasikiliza, huku mimi nikiuliza maswali pale ambapo sikuyaelewa vizuri maelezo yao.

"Tafadhali usilie mzee wangu, hii ndiyo mitihani ya dunia, cha msingi eleza kilichotokea ili mimi na Afande tuangalie njia rahisi ya kusaidia, kupata na kukosa yote yanawezekana", niliwaambia.

"Hakika", alisema kwa sauti ya mikwaruzo, akashindwa kujizuia akatoa machozi tena.

"Tutakesha sasa, maana ukilia hakuna kitakachofanyika", nilimwambia, akatingisha kichwa kukubaliana na maneno yangu, akatoa kitambaa akayafuta machozi yake.

"Samahani, jambo hili limenitia uchungu sana, maana baada ya watu hawa kufika nyumbani alfajiri, walinihimiza nitoe dawa iliyokuwa kwenye friji ili kazi ya kusafisha noti ianze mapema, nilifarijika sana kuwaona, lakini nilipofika kwenye friji, ilinishangaza chupa yenye dawa ilikuwa imepasuka na dawa yote imemwagika. Mama yangu hakika nilichanganyikiwa, niliwaita maofisa hawa waje kuona kilichotokea, walinilaumu kuwa sikuhifadhi dawa hiyo vizuri, nikabaki nimeduwaa".

"Aisee!, hiyo yote ni mbinu", nilisema kwa mshangao.

"Ilikuwa mbinu, kutokana na tatizo hilo, maofisa hawa walishauri dawa nyingine itafutwe haraka iwezekanavyo, tena walionekana kusikitishwa sana na kilichotokea, huku wakisema kuwa kazi hii ilitakiwa kuisha haraka ili kila mmoja afe na chake, kwani walihitaji sana pesa kwa ajili ya matumizi yao binafsi...".

"Haraka niliwasililiana na Profesa Davis Majigambo, baada ya kueleza kilichotokea, alionekana kutuhurumia, nilimuomba atusaidie dawa kidogo ili tusafishe kiasi cha dola ili tuweze kununua dawa nyingine, Profesa Majigambo alikataa, akieleza kuwa haiwezekani kwani hata yeye hana mamlaka ya kutoa dawa hiyo bila malipo, kwani inatolewa kwa siri kubwa...".

Wakati nikitafakari cha kufanya, maofisa hawa walinipigia simu, wakinihimiza nitafute dawa haraka, vinginevyo wao wamtafute mfadhili mwingine, nikalazimika kuuza nyumba yangu ili niweze kununua dawa hiyo, nikifahamu kuwa baada ya dola hizo kusafishwa, nitanunua kiwanja na kujenga jumba la kifahari zaidi ya niliyokuwa nikiishi, kumbe nilikuwa napotea", alisema huku akibubujikwa na machozi. 

"Ukauza nyumba?", nilimuuliza.

"Ndiyo, baada ya kupata pesa, nikanunua dawa nyingine kwa Profesa Majigambo. Lakini cha kushangaza baada ya kununua dawa hiyo, simu za maofisa hawa hazikupatikana tena, nilifika chuo kikuu, mahali ambapo nilikutana na Profesa Majigambo, sikufanikiwa kumuona, nilipouliza sehemu ya utawala, nilielezwa kuwa, chuo kikuu hakuna Profesa mwenye jina hilo, hapo ndipo nilichoka kabisa", alisema huku akifuta machozi.

"Hata ukilia haitasaidia, cha msingi ni kumuomba mungu", nilisimama nikatoka mahali nilipokuwa nimeketi, "Huu si mchezo wa kawaida, hii ni ngoma nzito. Hizi karatasi ndiyo uliambiwa kuwa dola?".

"Naam, ni pamoja na noti za mataifa mbalimbali", alisema.

Kwa kuwa nilikuwa nimeandika maelezo yake, nikayapitia na kuanza kumuuliza maswali. 

"Muda gani umepita baada ya tukio hili?".

"Ni siku ya saba sasa".

"Ulibainishaje kuwa umeibiwa?".

"Nimehaha kuwatafuta kwa simu bila mafanikio, tofauti na awali walipokuwa wakinihimiza nitafute dawa, lakini pia baada ya kupata ukweli kuwa mtu aliyetumia jina la Profesa Majigambo hafahamiki kabisa chuo kikuu, mara moja nikabaini kuwa nimeibiwa".

"Mbali na huyu Profesa Majigambo, ulifanikiwa kufahamu kwa majina hawa maofisa waliodai kutoka ubalozi?".

"Ndiyo, lakini nahisi yote yalikuwa ya bandia".

"Kwanini unadhani hivyo?".

"Walijitambulisha kwa majina ya Ramadhan Sharif, Mussa Abdallah na Josephat Stephan, ambayo sasa naamini kuwa si majina yao halisi, ni mataperi wazoefu, wameniacha katika hali ambayo sikuitarajia katika maisha yangu".

"Pole sana, mnaweza kwenda lakini kama mtapata wazo au jambo ambalo linaweza kutusaidia katika tukio hili tafadhali msisite kuwasiliana nasi, mimi pia nikitatizwa na jambo lolote nitaomba msaada wenu, cha msingi msizime simu zenu", niliwaambia halafu nikamgeukia Kanali Emilly, "Afande, mimi nimemaliza, huenda wewe una la nyongeza". 

"Hapana, nitauliza nini tena Teacher, cha msingi muwe wavumilivu wakati huu ambapo tunafuatilia jambo hili, nyie si wa kwanza", alishauri Kanali Emilly.

Baada ya watu hawa kuondoka, nilibaki ofisini kwa Kanali Emilly tukabadilishana maneno mawili, nikamweleza jinsi nilivyojipanga kufuatilia tukio hili. Kanali Emilly pia aligusia tatizo sugu la dawa za kulevya, na jinsi Rais alivyomfokea kuhusu hali mbali iliyopo nchini. Wakati najiandaa kutoka, simu yangu ya mkononi iliita.

Hallo", nilisema baada ya kupokea simu.

"Habari ya kazi molamu?", sauti kali ya shemeji yangu mpendwa Mama Feka ilisikika masikioni mwangu.

"Oh, molamu wane, uko salama?", nilimuuliza.

"Niko salama, lakini si salama kama unavyofikiria molamu, baada ya wewe kuondoka Nyamuswa ukiwa umepatwa na tatizo la kuunguliwa ofisi, nilisikia vibaya sana molamu, vipi umekuta hali gani, kumeteketea kabisa?".

"Hapana, bahati nzuri wahusika waliwahi kuzima, hakukuwa na madhara makubwa zaidi, maana mungu wetu aliingilia kati", nilimwambia.

"Unajua niko wapi?". aliuliza Mama Feka, shemeji yangu ambaye huko Nyamuswa wanamwita Cnthia Rothrock, akifananishwa na yule mwana mama mcheza sinema maarufu za mapigano.

"Nilikuacha Nyamuswa", nilimwambia.

"Molamu, shemeji yako niko njiani kuja Dar, nakuja kwenye mahafari ya chuo kikuu huria, mimi ni mmoja wa wahitimu wa sheria, nitakutafuta nikifika, baada ya Nyamuswa sasa ni Dar es Salaam", alisema Mama Feka.

"Karibu sana Dar es Salaam, utanifahamisha baada ya kufika", nilimwambia.

ITAENDELEA 0784296253

Comments

  1. Stories nzuri lakni inapoteza ladha na ufuatiriaji kwasababu inachukua muda mrefu sana kupost

    ReplyDelete

Post a Comment

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru