IKWIRIRI WALAANI MATUSI NA KEEJELI ZA TANROD

 Mzee Iddi Rashid

Wakaazi wa mji wa Ikwiriri, Rufiji, mkoani Pwani wamelaani vikali vitendo vya ubabe, lugha za matusi na kejeli zilizofanywa na baadhi ya maofisa kutoka Wakala wa Barabara nchini (TANROD) wakati wa zoezi la bomoabomoa linaloendelea nchini Tanzania.

Wakizungumza na waandishi wa habari, waliotembelea eneo la tukio, Ikwiriri jana, wananchi hao wameeleza kusikitishwa na kitendo cha maofisa hao kuvunja nyumba zao bila kujali zuio lililowekwa na Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi.

Mmoja waathirika hao, Mzee Iddi Rashid (80), ambaye nyumba yake ya ghorofa moja ilivunjwa, ameeleza kusikitishwa na kauli iliyotolewa na maofisa kutoka Tanrod wakati akiwaonyesha notisi ya kuzuia kubomoa nyumba yake mpaka kesi ya msingi ya madai itakapoisha.

Anasema, alipoonyesha notisi hiyo kwa maofisa wa Tanrod, alielezwa kuwa hawafanyi kazi kwa makaratasi yaliyotoka chooni, wakimaanisha kuwa notisi hiyo ni sawa na karatasi za Toilet Paper.

Mzee Rashid anasema, aliambiwa maneno hayo ya fedheha mbele ya watoto na wajukuu zake. "Hakika sikutegemea maofisa kutoka serikalini kutoa matusi na lugha chafu kiasi hiki, noti ya Mahakama Kuu kufananishwa na karatasi ya chooni, wanyonge watapata wapi haki", anahoji.

Amesema nchi hii inaongozwa kwa sheria na kanuni, ndiyo maana baada ya kuona nyumba zao zimewekewa alama za kuvunjwa waliamua kukimbilia mahakamani kwa vile barabara hiyo iliwakuta.


    Akizungumza huku machozi yakimtoka, Mzee Rashid anasema si kusudi lake kupingana na serilkali juu ya upanuzi wa barabara kwani suala hilo ni maendeleo, lakini maofisa hao wametumia ubabe kutekeleza majukumu yao bila kujali sheria.

Alionyesha notisi ya zuio namba 159/2016 iliyosainiwa Machi 7, na Jaji B.R. Mtungi kuwataka Wakala wa Barabara, Mwanasheria Mkuu wa serikali kusitisha bomoabomoa hiyo, ndipo maofisa hao wakatoa lugha za kejeli.

Anaeleza kuwa juhudi zaidi zilifanyika ikiwa pamoja na kutoa taarifa kituo cha Polisi Ikwiriri, lakini hakupata msaada na nyumba hiyo ilivunjwa na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali.

Waathirika wengine katika bomoabomoa hiyo, ambao pia wameeleza kusikitishwa na kauli za kejeli, Mzee Mohamed Ngasinga, Mzee Abdallah Mohamed Ngwali, Mzee Bakari Machela, Saidi Mlawa, Fatuma Ali, Safia Ali Abdallah na Ali Mohamed, wamemtaka Rais John Magufuli kuwa makini na baadhi ya watumishi wa serikali.

Wazee hao wamesifu jitihada zinazofanywa na Rais Magufuli, lakini wakatoa rai juu ya maofisa wa Tanrod kuheshimu sheria za nchi kama Rais anavyosisitiza kila siku anapozungumza na wananchi.

Maofisa hao wa Tanrod walifika eneo la tukio majira ya saa nne asubuhi, April 3, mwaka huu wakitumia gari namba STK 8385 na Greda namba CW 5192 ambalo lilitumika kubomoa nyumba hizo.

Meneja wa Tanrod Mkoa wa Pwani, Tumaini Sarakikya, ameeleza kusikitishwa na kauli za zilizotolewa na maofisa hao kwa waathirika na kuahidi kulifuatilia suala hilo haraka iwezekanavyo.

Alifafanua kuwa sheria inaelekeza kuwa nyumba yenye zuio la mahakama hairuhusiwi kuvunjwa. Anabaisha kuwa maofisa hao walieleza kuwa hawakuona zuio la mahakama walipofika eneo la tukio kitu ambacho kinapingana na maelezo ya waathirika.

Mzee Iddi Rashid, akionyesha alama ya mita 30, zilizowekwa kisheria na Wakala wa Barabara TANROAD
Sehemu ya nyumba ya Mzee Rashid ilityovunjwa.

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru